Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Kim Jong-un huwa hamzungumzii mama yake?
Katika mambo mengi fiche kuhusu kiongozi wa Korea kaskazini, Kim Jong Un, suala la mama yake mzazi limesalia fiche.
Tangu kuchukua madaraka miaka 15 iliyopita, Kim hajawahi kumtaja mamake waziwazi.
Tofauti na viongozi wawili wa awali wa Korea Kaskazini Kang pan sook mamake Kim il-Sung na Kim Jong-Sook mamake Kim Jong-Il, walikuwa wanaitwa "mama wa Korea".
Ila mamake Kim jong Un, Ko Yong-hui, hajaonekana hadharani wala hakuna majengo yaliyopewa jina lake kama njia ya heshima.
Kufichwa kwa Ko Yong-hui, kunaonekana kutokana na alikotoka na pia kuwa hawara, mambo ambayo wachambuzi wanasema huenda ikaathiri utawala wa kiongozi huyo.
Kulingana na waandika wasifu, Ko alizaliwa Osaka Japan mwaka wa 1952, kutoka kwa wazazi waliokuwa wakaazi wa kisiwa cha Jeju ambayo kwa sasa inamilikiwa na Korea kusini.
Kwasababu familia yake iliishi Japan, Ko alikuwa "zainishi mkorea" jina walilopewa wakorea walioishi eneo hilo wakati wa ukoloni wa Japan kati ya mwaka 1910-1945.
Wakorea wengi waliwaonea wivu wale waliokuwa wakirejea kutoka Japan kipindi hicho, kwani walirejea na pesa nyingi pamoja na vifaa vya nyumba.
Ila pia waliitwa "jaebo" jina la kudunisha kwa kudai watu waliotoka Japan walikuwa na mawazo mabaya ya kigeni.
Nchini Korea kaskazini, kuna matabaka ya watu na Wakorea Zainichi wanatajwa kuwa watu wasiokuwa na tabaka halisi na wanaweza kusababisha uhasama.
Watu kutoka kundi hili, hufuatiliwa kwa karibu na serikali na mara nyingi wananyimwa nafasi katika vyuo vikuu au ajira.
Korea kaskazini ni jamii yenye ngazi tofauti ambayo si rahisi kubadilisha tabaka lako.
Dkt Jung Young-tae kutoka chuo kikuu cha Dongyang, anasema jamii hiyo pia imeundwa kwa mfumo wa "mtu kuwa na hatia sababu ya undungu" ambapo raia wanaweza kuadhibiwa kwa matendo yaliyofanywa na wanafamilia wao.
Hadithi ya Cinderella
Ko alipokuwa na umri wa miaka 10, familia yake ilirejea Korea Kaskazini.
Familia yake ilikuwa miongoni mwa wakorea 93,000 waliohama kutoka Japan na kurejea katika taifa hilo la kikomunisti, kupitia mpango wa kuwapa maisha bora wanaorejea Korea Kaskazini ikiwemo kazi na elimu ya bure.
Ila Ko alibahatika kuepuka maisha ya umaskini na kuteseka ambayo ilikuwa inawasubiria wakorea zainichi wengi, baada ya kupendwa na kiongozi wa wakati huo Kim Jong-il.
Ingawa hakutambulishwa rasmi kama mke wa kiongozi huyo, inasemekana rais huyo tayari alikuwa amemuoa Kim Yong-Suk, binti ya mwanajeshi mmoja mkuu, ndoa amabyo ilikuwa imepangwa na babake.
Ko alikuwa miongoni mwa kundi la densi, na alimvutia kiongozi huyo kutokana na urembo wake na ujuzi wake wa densi.Hii ni kulingana na kitabu alichochapisha mwanahabari wa Japan Yuji Gomi.
Ingawa hakuoleka rasmi na kiongozi wa taifa hilo wala kutambuliwa rasmi, Ko aliishi maisha ambayo Gomi aliita "hadithi ya Cinderella"
Ripoti zinaashiria kuwa Kim Jong-il alimpenda sana Ko, licha kuwa alikuwa amemuoa Kim yong-suk aliyekuwa anaishi mjini Pyongyang huku Ko na wanawe watatu wakiishi mji wa pwani wa Wonsan.
Kulingana na Kim Hyung-soo kutoka shirika la North Studies Association, anasema "Kim Jong-un si mtoto wa mke wa kwanza, ni mwanaharamu wa Ko Yong-hui"
Ukoo wa uongozi wa taifa hilo unasemekana kuwa takatifu, kwa hivyo wazo kuwa Kim ni mzaliwa wa mama "jaebo" haikubaliki.
Watoto wanaozaliwa nje ya ndoa nchini Korea kaskazini, hukumbwa na unyanyapaa
Kulingana na Gomi, Ko alikuwa anatamani sana maisha yake ya Japan na hata kuwafunza watoto wake ikiwemo Kim jong-un kuzungumza kijapani.
Kenji Fujimoto ambaye alikuwa mpishi wa Kim Jong-il kutoka mwaka wa 1988 hadi 2001 anasema Kim Jong Un alikuwa anaimba sana nyimbo za Kijapani, na alikuwa anatamani sana taifa hilo kutokana na uchumi wake uliostawi.
Ingawa babake Kim Jong-il hakuwahi kumtambua Ko kama bibi ya rais, Ko mara nyingi alionekana akitembea na Jong-il na hata kukagua gwaride, na mara nyingi Jong-il alikuwa amemuamini na hata angemshauri katika masuala ya kisiasa.
Ila ni vipi kijana wa pili wa Jong-il alichukuwa madaraka licha ya kuwa mwanaharamu?
Waandika wasifu wengi wanasema, Ko alimuandaa sana Jong-un kumrithi babake.
Kim Jong-nam kijana wa kwanza wa Kim jong-il, walikuwa wamekosana baada ya kijana huyo kutilia shaka mfumo wa uongozi wa taifa hilo akitaka kuwe na mabadiliko.
Mawazo ya Jong-nam yalitokana na masomo yake katika mataifa ya nje na aliweza kuzungumza kiingereza na kifaransa. Pia alikuwa amejizolea sifa ya mtu anayependa starehe kutokana na kutembelea sehemu za starehe kama Casino na kuishi Maisha ghali.
Kijana mkubwa wa Ko yong-hui, Jong Chol, hakuchukuwa madaraka kutokana na uraibu wake wa kutumia madawa ya opium.
Kim jong-un baadaye alikuwa kipenzi cha babake kutokana na uwezo aliouonyesha wa kuwa kiongozi.
Dadake Ko alitwika jukumu la kumlinda Jong-un na dadake wakati wanasoma Uswizi, ila walitorokea Marekani baada ya Ko kupatikana na saratani ya matiti wakihofia maisha yao.
Ingawa Kim alimrithi babake, walichohofia kilitokea. Baada ya kuingia madarakani, alimuua mjomba wake huku Jong-nam akipatikana amefariki nchini Malaysia.
Kifo cha Ko
Ko alifariki kabla ya Kim Jong-il, ila kifo chake katika hospitali moja mjini Paris hakikutajwa na vyombo vya habari vya Korea kaskazini.
Ukoo fiche wa Kim Jong-un unasemekana ndio maana siku yake ya kuzaliwa si siku ya mapumziko ya kitaifa kama ilivyokuwa kwa viongozi wa awali. Kwani kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kunaweza kuzua maswali kuhusu mamake mzazi.
Kutokana na ukoo wake fiche, wachambuzi wanasema ndiyo maana Kim Jong-un alimtambulisha mkewe mapema hadharani, ili kutoa nafasi kwa binti yake Jo ae Ki kumrithi siku za usoni