Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi katika
maeneo maalum nchini Iran baada ya Rais Donald Trump kuishutumu Iran kwa
"ukiukaji wa kijinga" wa makubaliano yake ya kusitisha mapigano
kufuatia shambulio dhidi ya meli ya mizigo katika Mlango wa bahari wa Hormuz.
Kamandi Kuu ya Marekani au Centcom ilisema
ilishambulia vituo vya kuhifadhia makombora na ndege zisizo na rubani na sehemu
za rada za pwani siku ya Ijumaa.
Ilisema hatua hiyo ilikuwa kujibu shambulio la
ndege isiyo na rubani dhidi ya meli ya mizigo siku ya Alhamisi, tukio ambalo
lilisimamisha mpango wa kuwahamisha maelfu ya mabaharia waliokwama katika eneo
hilo.
Tehran ilisema meli hiyo ya mizigo ilishambuliwa
kwa sababu ilikuwa ikitumia njia ambayo ahaijaidhinishwa kupita kwenye maji ya
Ghuba.
Centcom - ilielezea mashambulio hayo kama
"jibu kubwa" la kulipiza kisasi shambulio la ndege zisizo na rubani
za Iran.
"Uchokozi usio na msingi dhidi ya meli za
kibiashara uliofanywa na vikosi vya Iran ulikiuka wazi makubaliano ya usitishaji
mapigano," ilisema katika taarifa.
Centcom inasema jeshi la Marekani "litaendelea
kutoa uratibu wa njia salama na usaidizi kwa meli za kibiashara zinazopita
kwenye mlango wa bahari wa Hormuz".
Hata hivyo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya
Kiislamu ya Iran (IRGC) lililaumu "serikali ya Marekani kwa kukiuka mkataba".
Katika taarifa yake IRGC ilisemaMarekani ilifanya
mashambulizi ya anga katika ufuo wa Iran "kwa visingizio mbalimbali vya
meli inayokiuka utaratibu wa usafiri katika Mlango wa bahari wa Hormuz".
IRGC ilisema jeshi lake la majini lililipiza kisasi
kwa kushambulia ngome kadhaa za kijeshi za Marekani katika eneo hilo, bila
kutoa maelezo zaidi. BBC imewasiliana na Pentagon kuthibitisha hilo.
"Wakiendelea kufanya uchokozi majibu yetu
yatakuwa makubwa zaidi kuliko haya," IRGC iliongeza.
Tehran ilifunga mkondo huo baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya
Iran kuanza mwishoni mwa mwezi Februari.