Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Saini kabla ya kusali: Sheria mpya ya ubadili dini inavyowaathiri waumini India
- Author, Janhavee Moole
- Nafasi, BBC Marathi, Mumbai
- Author, Zoya Mateen
- Nafasi, BBC News, Delhi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Baadhi ya makanisa ndani na pembezoni mwa jiji la Mumbai, mji mkuu wa kifedha wa India, yameanza kuwaomba waumini kutoa tamko kwa maandishi linalosema: "Nimekuja hapa kusali kwa hiari yangu mwenyewe."
Wageni huandika majina yao, wakati mwingine huongeza namba ya kitambulisho, na kusaini kuthibitisha kuwa hakuna aliyewalazimisha au kuwashawishi kwa kuwapa kitu ili wahudhurie kanisani. Fomu hizo, ambazo BBC imeziona, hazina hadhi rasmi kisheria. Makanisa huzihifadhi iwapo mkutano wa ibada utapingwa na waandaaji wake wakatuhumiwa kwa kosa la kujaribu kuwabadili dini waliohudhuria.
Utaratibu huo ulianza katika baadhi ya makanisa mwishoni mwa Agosti, muda mfupi kabla ya sheria mpya inayopiga marufuku ubadili dini kuanza kutumika katika jimbo la Maharashtra, ambalo Mumbai ni mji mkuu wake.
Sheria hiyo inakataza ubadili dini unaofanywa kwa kutumia nguvu, udanganyifu, shinikizo au vishawishi. Pia inawataka watu wanaotaka kubadili dini kwa hiari kuwajulisha mamlaka mapema.
Ubadili dini unaokiuka sheria unaweza kusababisha kifungo cha hadi miaka saba, na adhabu hiyo inaweza kufikia miaka 10 kwa anayekiuka sheria mara ya pili.
Serikali ya Maharashtra inasema sheria hiyo inalenga kuwalinda watu, hasa walio katika mazingira magumu kijamii au kiuchumi, dhidi ya kulazimishwa au kudanganywa kubadili dini.
Lakini wakosoaji wanasema tafsiri pana ya sheria hiyo, adhabu kali na kuchunguzwa hata kwa ubadili dini wa hiari kunaweza kuifanya serikali na polisi kuingilia mojawapo ya maamuzi binafsi zaidi ambayo mtu anaweza kufanya. Serikali ya jimbo hilo haikujibu maombi ya BBC ya kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Ingawa sheria hiyo inahusu dini zote, wasiwasi mkubwa unaonekana katika maeneo yanayohudhuriwa na watu wa dini za wachache, hasa Wakristo.
Kiini cha mjadala huo ni mvutano wa muda mrefu kuhusu madai, ambayo mara nyingi hutolewa na makundi ya mrengo wa kulia, kwamba baadhi ya watu hulazimishwa au kushawishiwa kubadili dini kwa kupewa manufaa.
Devdan Tribhuvan ameshuhudia baadhi ya wasiwasi huo kwa karibu.
Tribhuvan, ambaye ni Mkristo wa kizazi cha nne kutoka Vasai, kitongoji cha Mumbai, ni mwanachama wa shirika linalotoa msaada wa kisheria kwa Wakristo ndani na pembezoni mwa jiji hilo.
Katika miezi ya hivi karibuni, anasema, watu wamezidi kumfikia si kwa ajili ya kesi mahakamani, bali kuelezea jinsi mikutano ya ibada ilivyovurugwa na kuuliza kuhusu mambo ambayo bado wana uhuru wa kufanya.
Baadhi wameeleza kuhusu watu wasiowafahamu kuingia makanisani na kuwauliza waliohudhuria:
"Jina lako nani? Kwa nini uko hapa? Kuna mtu amekuahidi kitu?"
Tribhuvan anasema maswali hayo yanaweza kuwa makali zaidi pale muumini anapokuwa na jina ambalo halisikiki kama la Mkristo:
"Kuna mtu amekulazimisha kuja? Kuna mtu amekupa kitu ili uje?"
Wengi wanaomtafuta hawalengi kuchukua hatua za kisheria. Wanataka kujua iwapo kukusanyika tu kwa ajili ya kusali kunaweza kuwafanya wawe katika hatari ya kutuhumiwa kwa ubadili dini.
Mwezi Julai, uchunguzi uliofanywa na gazeti la The Indian Express uliandika kuhusu matukio matano ya kuvurugwa kwa mikutano ya maombi ya Kikristo katika maeneo mbalimbali ya Mumbai kati ya Aprili na Julai.
Kesi tisa za polisi zilifunguliwa baadaye - saba dhidi ya waumini au waandaaji wa mikutano ya maombi, na mbili dhidi ya wanachama wa kundi la kitaifa la Kihindu, Bajrang Dal. Polisi hawakujibu maswali ya kina kuhusu kesi hizo au hatua zilizochukuliwa.
"Je, kukusanyika kwa ajili ya kusali pekee ni ubadili dini?" anauliza Tribhuvan.
Huko Mumbai, swali la Tribhuvan lina uzito wa pekee.
Jiji hilo limekua kwa kuvutia watu kutoka maeneo mbalimbali ya India na nje ya nchi, huku kila kundi likija na miungu na mila zake.
Kengele ya kanisa inaweza kusikika umbali mfupi kutoka kwenye mwito wa sala kutoka msikitini; huku hekalu au madhabahu ya dini moja ikiwavutia waumini wa dini nyingine.
Watu wa dini mbalimbali huelekea kwenye eneo la ibada la Waislamu la Haji Ali. Wahindu huwasha mishumaa katika kanisa katoliki la Mount Mary linalotazama jiji hilo.
Umati mkubwa hujaa mitaa ya Lalbaug wakati wa sherehe ya Kihindu ya Ganesh Chaturthi na kutembelea hekalu la Siddhivinayak mwaka mzima.
Maharashtra ni jimbo la hivi karibuni miongoni mwa zaidi ya majimbo kadhaa ya India yaliyochukua hatua za kuzuia ubadili dini.
Sheria hizo hutofautiana, lakini wigo wake umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, hasa katika majimbo yanayoongozwa na chama cha Bharatiya Janata Party (BJP) cha Waziri Mkuu Narendra Modi.
Baadhi ya sheria hizo zinapingwa katika Mahakama ya Juu ya India.
Nyuma ya kuongezeka kwa sheria hizo kuna madai ambayo yamekuwa yakitolewa kwa muda mrefu na makundi ya kitaifa ya Kihindu kwamba Wakristo hutumia fedha, elimu au huduma za afya kuwavutia watu maskini na jamii za makabila kuachana na Uhindu.
Pia kuna madai kwamba wanaume Waislamu huwafuata wanawake Wahindu kwa lengo la kuwabadilisha dini - njama inayodaiwa kuitwa "jihad ya mapenzi" (love jihad).
Wakosoaji wanasema madai hayo yamechangia unyanyasaji dhidi ya mikutano ya ibada ya Kikristo na wapenzi wa dini tofauti, na kwamba sheria hizo zinawapa wanaotoa tuhuma hizo njia ya kuhusisha polisi katika masuala ya sala, ndoa na imani.
Serikali ya Maharashtra inasema sheria mpya inawaacha watu huru kubadili dini kwa hiari, huku ikishughulikia kile inachodai kuwa ni ongezeko la ubadili dini wa kulazimishwa ambalo sheria zilizokuwepo hazijaweza kukomesha.
Wakosoaji wanahoji mipaka kati ya kulazimishwa na kufanya uamuzi kwa hiari.
"Hatuungi mkono ubadili dini wa kulazimishwa, ikiwa upo," alisema Samsuddin Tamboli, rais wa Muslim Satyashodhak Mandal, shirika linalopigania mageuzi miongoni mwa Waislamu.
Wasiwasi wake unahusu kile ambacho sheria inakitambua kama kishawishi.
Sheria hiyo inafafanua "kishawishi" ni kama ajira, elimu ya bure katika taasisi ya kidini, ahadi ya ndoa, "maisha bora" na "uponyaji wa kiungu."
Hata kusifu dini moja kuliko nyingine kunaweza kuchukuliwa kuwa kishawishi chini ya sheria hiyo.
"Ufafanuzi huo umewekwa kwa namna isiyoeleweka kiasi kwamba karibu manufaa yoyote anayopata mtu yanaweza kuchukuliwa au kudaiwa kuwa ni kishawishi," alisema Abhay Thipsay, jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Bombay.
"Ikiwa mtu anapata manufaa fulani na kwa uamuzi wake mwenyewe anaamua kubadili dini kwa sababu hiyo, kwa nini ichukuliwe kuwa ni kosa?"
Sheria hiyo pia inawaruhusu wazazi, ndugu na jamaa wengine kutoa malalamiko kwa polisi kuhusu ubadili dini unaodaiwa kuwa kinyume cha sheria.
Katika hali hiyo, mtu anayeshtakiwa kwa kusababisha au kusaidia ubadili dini anatakiwa kuthibitisha kuwa mchakato huo ulikuwa halali.
Wakosoaji wanasema kifungu hicho kinaweza kuongeza changamoto kwa wapenzi wa dini tofauti, ambao tayari wakati mwingine hukumbana na upinzani kutoka kwa familia zao.
Sheria za India zinawaruhusu watu wa dini tofauti kuoana bila mmoja wao kubadili dini, lakini wanatakiwa kutoa taarifa ya ndoa hiyo mwezi mmoja kabla.
Lara Jesani, wakili ambaye amewasaidia baadhi ya wapenzi wa dini tofauti kupata ulinzi wa mahakama, anasema taarifa kuhusu ndoa zilizopangwa wakati mwingine huwafikia ndugu na makundi ya kitaifa ya Kihindu yanayopinga ndoa hizo ndani ya kipindi hicho cha mwezi mmoja.
Katika baadhi ya kesi alizoshughulikia, anasema, familia zimewapeleka wanawake kwa nguvu, hata kutoka katika ofisi za wasajili wa ndoa.
Sasa ana hofu kuwa sheria mpya inaweza kuwapa familia au makundi ya mrengo wa kulia njia nyingine ya kuwaandama wapenzi hao pekee.
"Hata pale ambapo hakuna hata mmoja wao anayelenga kubadili dini, wanandoa hao wana hofu kwamba ndugu anaweza kumshutumu mmoja wao kwa kujaribu kumbadilisha dini mwenzake."
Serikali ya Maharashtra haikujibu maswali ya kina ya BBC kuhusu wasiwasi huo.
Hata hivyo, wakati sheria hiyo ilipopitishwa, Waziri wa Jimbo Pankaj Bhoyar alisema haikiuki haki ya mtu kubadili dini.
Alisema hitaji la kutoa taarifa lililenga kubaini iwapo ubadili dini ulifanyika kwa hiari, huku serikali ikiendelea kuwa na uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya ubadili dini unaofanywa kwa udanganyifu, shinikizo au vishawishi.
Lakini Tribhuvan bado ana wasiwasi.
Anasema hali hiyo ya hofu imefika hata kwenye mikutano midogo ya ibada inayofanyika karibu na maeneo wanayoishi waumini, pale kanisa linapokuwa mbali.
Watu 50 wanaweza kuhudhuria, anasema, na wakati mwingine idadi hiyo hufikia 100 - huku mtu ambaye si Mkristo pia akijiunga.
"Ikiwa mtu mwingine anatamani kuja kusali, hatuwezi kumzuia," alisema.
"Hiyo ndiyo tunaita haki ya kuchagua."
Kwa Thipsay, jaji mstaafu, tahadhari hiyo inaibua swali pana zaidi.
"Ikiwa mtu mzima ana uwezo wa kufanya maamuzi makubwa - kama vile kuchagua mtu wa kumuoa au kuolewa naye - na amepewa haki ya kupiga kura," alisema, "kwa nini asiwe na uwezo wa kufanya uamuzi huu pia?"
Imetafsiriwa na Faidha Ngaga