Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, "Singewaacha wengine wafe" - Rubani aliyedungwa kisu asimulia dakika za hofu angani

Ndege ya Flydubai (FZ1073) iliyokuwa ikielekea Tel Aviv kutoka Dubai ilishuka ghafla kwa zaidi ya futi 17,000 takribani saa mbili na nusu baada ya kuanza safari.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Mke wa zamani wa Chivayo afika nyumbani kwa familia

    Sonja Madzikanda, aliyekuwa mke wa mfanyabiashara wa Zimbabwe Wicknell Chivayo, amejitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu kifo chake baada ya kufika nyumbani kwa familia mjini Harare kutoa heshima zake za mwisho.

    Sonja aliwasili siku ya Ijumaa akiwa ameandamana na mama yake katika makazi ya familia ya Chivayo huko Gletwin, ambapo ndugu, marafiki na waombolezaji wamekuwa wakikusanyika tangu mfanyabiashara huyo afariki katika ajali ya helikopta.

    Ujio wake umevutia umakini mkubwa kutokana na historia yake na Chivayo. Wawili hao walikuwa katika ndoa iliyojaliwa watoto wawili kabla ya kuachana na baadaye kuhusika katika mgogoro wa kisheria uliohusisha watoto na mali.

    Picha na video zilizosambazwa na vyombo vya habari vya Zimbabwe zilimuonyesha Sonja akiwa amevaa mavazi meusi ya maombolezo alipokuwa akiungana na wanafamilia na waombolezaji wengine.

    Kifo cha Chivayo, mke wake Lucy Muteke na watu wengine watatu katika ajali ya helikopta wiki hii kimezua majonzi makubwa nchini Zimbabwe na nje ya nchi, huku viongozi wa kisiasa na watu mashuhuri wakituma salamu za rambirambi.

  2. Christa Pike hajitambui baada ya hukumu ya kifo kushindikana

    Tahadhari: Makala hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuyapata ya kushtua

    Mfungwa wa kunyongwa nchini Marekani, Christa Pike, alikuwa hajitambui na alikuwa amewekewa mashine ya kumsaidia kupumua siku ya Alhamisi usiku, baada ya jaribio la kutekeleza hukumu yake kifo kwa sindano ya sumu kushindikana, kwa mujibu wa mawakili wake.

    Pike, mwenye umri wa miaka 50, alidungwa dozi mbili za dawa ya pentobarbital siku ya Jumatano katika jaribio la kutekeleza hukumu yake ya kifo. Hata hivyo, aliendelea kuwa hai na baadaye alikimbizwa hospitalini kwa gari la wagonjwa.

    Hali yake bado ni mbaya na anaendelea kupata matibabu katika hospitali moja eneo la Nashville, Tennessee.

    Mawakili wake sasa wanataka hukumu yake ya kifo ibadilishwe, wakisema jaribio hilo lililoshindikana linaibua maswali makubwa kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo. Pike alihukumiwa kifo mwaka 1996 kwa mauaji ya Colleen Slemmer.

    Ijumaa, mawakili wake waliwasilisha ombi la dharura mahakamani wakitaka ushahidi wote unaohusiana na tukio hilo uhifadhiwe. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, madaktari walikuwa wakijaribu kuokoa maisha yake huku wakifanya jitihada za kuondoa dawa hiyo mwilini mwake.

    ‘Sindano moja ilipinda kabisa’

    Mawakili wa Pike wanasema wakati wa maandalizi ya utekelezaji wa hukumu, maafisa wa gereza walijaribu mara kadhaa kupata mshipa wa kumdunga dawa hiyo.

    Walisema takriban sindano saba zilitumika, na wakati mmoja Pike mwenyewe alielekeza sehemu ambazo zingeweza kutumika kupata mshipa.

    Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa mahakamani, sindano moja ilitolewa ikiwa imejipinda kabisa baada ya jaribio hilo kushindikana.

    Pia walidai kuwa Pike alikuwa akilia, akigugumia na kupumua kwa nguvu wakati akidungwa dozi hizo mbili.

    Kufuatia tukio hilo, Gavana wa Tennessee, Bill Lee, ameagiza uchunguzi huru kufanyika na kusitisha utekelezaji wote wa adhabu za kifo katika jimbo hilo kwa kipindi kilichosalia cha mwaka.

    Hata hivyo, Idara ya Magereza ya Tennessee imetetea utaratibu uliotumika, ikisema ulifuatwa kulingana na kanuni zilizopo.

    Mamlaka bado hazijaeleza kwa nini utekelezaji huo ulishindikana wala kama zitajaribu tena kutekeleza hukumu ya Pike.

    Soma Zaidi:

  3. "Singewaacha wengine wafe" - Rubani aliyedungwa kisu asimulia dakika za hofu angani

    Rubani Mhindi wa ndege ya Flydubai aliyedungwa kisu na rubani mwenzake akiwa angani amesema alikuwa amedhamiria kupambana hadi mwisho kwa sababu hakuwa tayari kuwaacha abiria wengine wapoteze maisha.

    Kapteni Smit Machchhar alisema alikuwa ameanguka sakafuni akiwa amejeruhiwa na bado akishambuliwa alipogundua kuwa ndege iliyokuwa imewabeba zaidi ya abiria 170 ilikuwa ikipoteza mwelekeo na kushuka kwa kasi.

    "Nikiwa nimeanguka sakafuni na kujeruhiwa, nilijiambia nijaribu kwa mara ya mwisho kufungua mlango kutoka ndani," alisema wakati wa mazungumzo ya video na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

    "Wengine waliingia na pia walisaidia kudhibiti hali. Nilikuwa napigania maisha yangu mwenyewe, lakini wakati huo huo nilijua kwamba singewaacha wengine wafe," aliongeza.

    Ndege ya Flydubai, safari namba FZ1073, iliyokuwa ikielekea Tel Aviv kutoka Dubai mapema Jumatano, ilishuka kwa zaidi ya futi 17,000 (mita 5,200) takribani saa mbili na nusu baada ya kuanza safari.

    Awali ilituma ishara ya dharura kwa waongozaji wa trafiki wa anga kabla ya kutumia msimbo wa 7500, ambao hutumika kuashiria utekaji wa ndege.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema baadaye kuwa rubani mmoja alimshambulia mwenzake kwa kisu na "inaonekana alijaribu kuangusha ndege".

    Baada ya abiria na wahudumu kumdhibiti mshambuliaji, marubani wawili wa akiba waliokuwa ndani ya ndege waliweza kuitua salama katika Uwanja wa Ndege wa Tabuk, kaskazini-magharibi mwa Saudi Arabia, saa 06:58 kwa saa za huko.

    Machchhar, ambaye amesifiwa kama "shujaa wa kweli", alipelekwa hospitalini Tabuk kabla ya kuhamishiwa Abu Dhabi kwa matibabu zaidi. Inaripotiwa kuwa hali yake ni nzuri na anaendelea kupata nafuu.

    Serikali ya India imemsifu kwa ujasiri wake, huku mitandao ya kijamii nchini humo ikijaa ujumbe wa pongezi tangu utambulisho wake ujulikane.

    Machchhar alisema amekuwa rubani kwa miaka 17 na anaweza kutambua kinachoendelea kwenye ndege hata akiwa amefumba macho.

    Akizungumza kuhusu majeraha yake, alisema: "Sioni jeraha hili kama jeraha. Nikifanya hivyo, itakuwa ngumu zaidi kupona. Ninaliona kama safari ambayo itachukua muda, lakini nina imani nitapona na kurejea katika afya njema."

    Soma Zaidi Hapa:

  4. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu ya leo. Tarehe ni 03/10/2026. Mimi ni Asha Juma.