Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran: Masharti yetu saba lazima yatimizwe kabla ya kufungua Mlango wa Hormuz

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema Marekani hivi karibuni imeiwasilisha Iran mapendekezo kadhaa ya kumaliza mzozo kupitia wapatanishi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Jeshi la Sudan na RSF zatuhumiana mauaji ya raia Kordofan

    Jeshi la Sudan limelishutumu kundi la (RSF) kwa kuwaua takriban raia 23 katika eneo la Umm Badr, jimbo la Kordofan Kaskazini, katikati-kusini mwa nchi hiyo, huku mapigano yakiendelea kati ya pande hizo kwa ajili ya kudhibiti eneo hilo.

    Taarifa hiyo ilichapishwa na shirika la habari la serikali ya Sudan, Suna News Agency, Oktoba 3.

    Joint Force, ambayo ni mshirika wa jeshi la Sudan, imesema RSF ilifanya “uhalifu wa kikatili” huko Umm Badr kwa kuwaua raia wasio na silaha.

    Msemaji wa Joint Force, Meja Mutawakkil Ali Wakil Abuja, amesema: “Video inayosambaa pamoja na taarifa za eneo hilo inaonyesha kuwa wapiganaji wa RSF waliwaua raia, jambo ambalo ni ukiukaji wa misingi yote ya kibinadamu na sheria za kimataifa.”

    Kwa upande mwingine, Sudan Founding Alliance (Tasses), inayoongozwa na RSF, imelishutumu jeshi la Sudan na vikosi washirika kwa kuwaua angalau watu 23 katika mji wa Sodari, jimbo la North Kordofan, baada ya kutwaa eneo hilo kutoka kwa RSF.

  2. Marekani yataka pande zote za mzozo wa Tigray kujizuia

    Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani imezitaka pande zote zinazohusika katika mzozo wa Tigray kujizuia, huku vikosi vya serikali ya Ethiopia vikiendelea kuimarisha udhibiti wao katika mji mkuu wa eneo hilo, Mekelle.

    Msemaji wa Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tommy Pigott, amesema Marekani inazihimiza kwa nguvu Ethiopia na Eritrea kuheshimu mamlaka na uadilifu wa maeneo ya nchi jirani, kujiepusha na hatua zinazoweza kuzidisha mzozo, na kurejea katika mazungumzo na ushirikiano.

    “Pembe ya Afrika haiwezi kumudu mzozo mwingine wa kijeshi na janga la kibinadamu,” alisema.

    “Mgogoro wowote unaweza kuhatarisha ushirikiano unaoendelea kati ya Marekani na nchi hizo mbili, pamoja na maslahi yao ya pamoja.”

    Hayo yakijiri, Serikali ya Ethiopia imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Eritrea wiki hii, ikiishutumu kwa kuunga mkono muungano wa waasi unaodaiwa kuhusisha Sudan na Misri.

    Nchi zote tatu zimekanusha mara kwa mara madai hayo.

    Eritrea nayo imetangaza kuwa imekatiza kabisa uhusiano wa kidiplomasia na Ethiopia, baada ya wanadiplomasia wake kuamriwa kuondoka nchini Ethiopia ndani ya saa 48.

    Viongozi kutoka baadhi ya nchi jirani za Ethiopia wanatarajiwa kukutana nchini Misri baadaye leo, Jumapili.

    Addis Ababa imeishutumu Cairo pamoja na Eritrea kwa kuunga mkono waasi wa Tigray, ambao walianzisha shambulio siku 11 zilizopita.

    Kwa sasa, wapiganaji hao wamejiondoa katika maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti na kuanza kuendesha mapambano ya siri.

    Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuongezeka kwa mvutano kati ya Ethiopia na Eritrea kunaweza kusababisha kuyumba kwa usalama wa eneo lote.

  3. Iran: Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi masharti saba yatimizwe

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema Marekani hivi karibuni imeiwasilisha Iran mapendekezo kadhaa kupitia wapatanishi, huku Tehran ikisisitiza kuwa Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi masharti saba yaliyowekwa katika Mkataba wa Maelewano wa Islamabad yatimizwe.

    Akizungumza katika kikao cha Bunge leo, Qalibaf hakutoa maelezo kuhusu mapendekezo ya Marekani, lakini alisema “enzi za kupoteza muda na kulazimisha masharti ya upande mmoja zimekwisha.”

    Amesema, “Hadi masharti yetu saba, kwa mujibu wa Mkataba wa Maelewano wa Islamabad, yatimizwe, Mlango wa Hormuz hautafunguliwa.”

    Qalibaf, ambaye alikuwa mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo yaliyofanyika Islamabad, amesema Iran “haijafurahi kupita kiasi wala haiogopi,” bali “inapigana upande mmoja huku ikiendelea na mazungumzo upande mwingine.”

    Kwa mujibu wa Qalibaf, Iran inaendelea kuwa katika medani ya kijeshi kwa nguvu zake zote na itakabiliana na adui kupitia “hatua mpya za kushtukiza,” huku ikiendelea na juhudi za “kuimarisha nafasi yake ya juu katika uwanja wa kijeshi” na kutetea haki za wananchi wa Iran kupitia diplomasia.

    Akizungumzia kauli “zinazokinzana” kutoka kwa viongozi wa Marekani, Qalibaf amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haifanyi maamuzi yake ya kisera na usalama wa taifa kwa kuzingatia machapisho ya mitandao ya kijamii au mahojiano ya kila siku ya viongozi wa Marekani.

    Amesema, “Iran huamua hatua zake kwa kuzingatia mwenendo na vitendo halisi vya adui, si kauli zinazotolewa kwenye vyombo vya habari.”

    Soma Zaidi Hapa:

  4. Waziri wa Iran: Vita wala vikwazo si suluhisho la mzozo na Marekani

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mzozo kati ya Iran na Marekani hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi wala kwa kuongeza vikwazo.

    Araghchi amesema Marekani tayari “imeshindwa katika vita na diplomasia,” na kwamba kujaribu kuweka vikwazo zaidi hakutakuwa na manufaa.

    Akizungumza katika mkutano na mabalozi na mabalozi wanaokaimu wa nchi mbalimbali walioko Iran, Araghchi amesema suluhisho pekee linaloweza kuleta matokeo ni mazungumzo ya kidiplomasia yenye haki, usawa na heshima, yatakayolenga kumaliza vita na kile alichokiita uchokozi dhidi ya Iran.

    Kuhusu maandalizi ya Iran kukabiliana na uwezekano wa shambulio jipya la kijeshi kutoka Marekani, Araghchi amesema Iran iko tayari zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

    Amesema Iran inatumai Marekani itachagua “busara na hekima,” lakini iwapo Washington itaamua tena kutumia nguvu za kijeshi, Iran itachukua hatua zozote itakazoona muhimu kwa ajili ya kujilinda.

  5. Ufaransa kuongeza ufadhili wa kukabiliana na Ebola nchini DRC

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, amesema Ufaransa itaongeza ufadhili kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

    Barrot alitembelea Bunia siku ya Jumamosi, mji ambako kisa cha kwanza cha Ebola kilithibitishwa na ambao ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi katika mashariki mwa DRC. Aliwahimiza viongozi kuendelea kuwa waangalifu ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

    Ufaransa tayari ilikuwa imetenga dola milioni 15.1 kusaidia mapambano dhidi ya Ebola kati ya Januari na Julai mwaka huu.

    Tangu Rais Emmanuel Macron alipotembelea DRC mwaka 2023, Ufaransa imeendelea kutoa msaada wa kibinadamu na kusaidia tafiti za kitabibu, pamoja na misaada mingine. Paris inatarajiwa kujadili suala la Ebola katika mkutano ujao wa kibinadamu utakaofanyika nchini humo.

    “Ebola inaweza kuonekana kuwa tatizo lililo mbali kwa baadhi ya watu au viongozi wa kisiasa, lakini inaweza kurejea kwa haraka sana. Wajibu wetu ni kuzuia kurejea kwa milipuko hiyo,” Barrot alisema.

    Alipunguza hofu kuhusu uwezekano wa virusi hivyo kuenea baada ya kisa kimoja kuripotiwa nchini Ufaransa, na kuwashukuru wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu pamoja na wahudumu wa afya kwa juhudi zao za kudhibiti mlipuko huo.

    Wakati huohuo, mamlaka katika kaskazini-mashariki mwa DRC zilionya Jumatano kwamba baadhi ya wakazi wanaendelea kupuuza vikwazo vilivyowekwa kwa lengo la kudhibiti mlipuko wa Ebola. Hatua hiyo imechukuliwa huku hospitali na shule moja katika mji wa Kisangani zikiendelea kufungwa baada ya maambukizi kuthibitishwa miongoni mwa wafanyakazi.

    Zaidi ya kesi 8,000 za Ebola zimethibitishwa na zaidi ya watu 4,000 wamefariki tangu mlipuko huo ulipoanza mwezi Mei mwaka huu.

    Maelezo zaidi:

  6. Kiongozi wa Ujerumani atoa wito wa kuizuia Urusi mapema

    Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, amewasili katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, akisema Rais Volodymyr Zelenskiy anaweza kutegemea uungwaji mkono wa Ujerumani, huku mashambulizi ya Urusi yakizidi.

    Merz, pamoja na wakuu wa kampuni kadhaa za ulinzi, amesema mashine ya vita ya Urusi itaelekeza nguvu zake kwa nchi nyingine iwapo haitazuiwa.

    Ujerumani inaipatia Ukraine msaada wa kijeshi wenye thamani ya hadi euro bilioni moja, ukiwemo mifumo ya ulinzi ya kukabiliana na ndege mpya zisizo na rubani zinazotumia injini za ndege, zinazotumiwa na Urusi.

    Rais Zelenskiy amesema Vladimir Putin anaidhinisha mashambulizi yanayolenga raia, baada ya kushindwa kupata ushindi wa kijeshi.

    Soma Pia:

  7. Australia yachunguza uhusiano wa rubani msaidizi wa Flydubai na nchi hiyo

    Mamlaka za Australia zinafanya uchunguzi kuhusu uhusiano wa nchi hiyo na rubani msaidizi wa shirika la ndege la Flydubai, ambaye anadaiwa kujaribu kutwaa udhibiti wa ndege iliyokuwa ikielekea Israel.

    Rubani huyo msaidizi anadaiwa kumshambulia rubani mkuu kwa kutumia shoka la dharura wakati wa safari ya ndege kutoka Dubai kuelekea Tel Aviv, kabla ya abiria kumzidi nguvu na kufanikiwa kurejesha udhibiti wa ndege hiyo.

    Mamlaka za Australia hazijamtaja rasmi rubani huyo msaidizi, ambaye ametajwa na vyombo kadhaa vya habari, vikiwemo Reuters, CNN na The New York Times, kuwa ni Hamam al-Hammami.

    Mwendesha mashtaka nchini Umoja wa Falme za Kiarabu amesema uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo pamoja na sababu zinazoweza kuwa nyuma ya kitendo hicho.

    Katika taarifa yake kwa BBC, Polisi wa Shirikisho la Australia (AFP) wamethibitisha kuwa wanafanya uchunguzi kuhusu “uhusiano wa mtu huyo na Australia.”

    AFP imesema uchunguzi huo unahusisha polisi wa majimbo pamoja na chombo cha usalama cha taifa, na kuongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa “kwa wakati mwafaka.”

    Vyanzo vinavyofahamu suala hilo, vilivyozungumza na vyombo vya habari vya Australia, vimesema rubani huyo msaidizi alipewa viza ya mwanafunzi mwaka 2014 na kusoma nchini Australia kati ya mwaka 2015 na 2017, kabla ya kuondoka nchini humo.

    Shirika la Utangazaji la Australia (ABC) limeripoti kuwa visa yake ya mwanafunzi ilifutwa mwaka 2019 baada ya kutokuwa tena amejiandikisha katika kozi, hali iliyomfanya asistahili kuendelea kuwa na visa hiyo.

    Soma Zaidi Hapa:

  8. Meli ya kivita ya Marekani yatia nanga Thailand huku mvutano na Iran ukiendelea

    Meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, USS George H.W. Bush, imewasili Phuket, Thailand, siku ya Jumapili, huku takriban wanajeshi 4,800 wa kikosi chake wakipewa mapumziko.

    Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, meli hiyo imekuwa ikishiriki katika operesheni za Marekani kwa miezi kadhaa, wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukizidi.

    Reuters, ikinukuu vyombo vya habari vya eneo hilo, imeripoti kuwa meli hiyo itatia nanga katika maji ya pwani, huku wanajeshi wake wakitarajiwa kushuka na kutumia siku tano katika kisiwa hicho.

    Ziara hiyo inakuja mwezi mmoja baada ya meli nyingine ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, USS Abraham Lincoln, kutia nanga katika bandari ya Laem Chabang, ambako takriban wanajeshi 5,000 wa kikosi chake walipata muda wa mapumziko.

    Soma pia:

  9. Argentina yaitandika Burkina Faso 7-0 katika mechi ya kirafiki

    Argentina imeifunga Burkina Faso mabao 7-0 katika Uwanja wa Monumental usiku wa Jumamosi, katika mchezo wa kwanza kati ya miwili ya kirafiki dhidi ya timu za Afrika.

    Hii ilikuwa mechi ya kwanza kabisa kwa ngazi ya timu za taifa za wakubwa kukutanisha Argentina na Burkina Faso, huku timu hizo zikitenganishwa na nafasi 60 katika viwango vya hivi karibuni vya FIFA.

    Argentina ilikuwa ikicheza mchezo wake wa kwanza tangu Lionel Messi alipotangaza mwezi Agosti kuwa anaacha kuichezea timu ya taifa.

    Messi hakuitwa katika kikosi kilichocheza dhidi ya Burkina Faso, lakini anatarajiwa kurejea kwenye kikosi cha Argentina kwa mchezo wake wa kuaga dhidi ya timu nyingine ya Afrika, Benin, utakaochezwa Jumanne.

    Lautaro Martínez aliifungia Argentina bao la kwanza dakika ya nne, akianza safari ya ushindi mkubwa kwa wenyeji.

    Argentina ilifunga mabao matano katika kipindi cha kwanza kabla ya kuongeza mengine mawili baada ya mapumziko na kukamilisha ushindi huo wa mabao saba.

    Mchezo huo ulichezwa mbele ya mashabiki wachache katika Uwanja wa Monumental kufuatia adhabu zilizowekwa na FIFA dhidi ya Argentina baada ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Hispania.

    Burkina Faso ilipata nafasi tatu za kulenga lango, lakini ni moja pekee iliyolenga lango. Kipa Abdoul Guira alikuwa na kazi kubwa usiku huo mjini Buenos Aires, akifanya sevu 11.

    The Stallions waliwasili kwa kuchelewa katika mji mkuu wa Argentina baada ya kukumbwa na ucheleweshaji nchini Morocco, hali iliyovuruga maandalizi yao kwa mchezo huo.

    Kabla ya mchezo huo, Burkina Faso ilikuwa imetoka sare ya 1-1 dhidi ya Benin na kuifunga Jamhuri ya Afrika ya Kati 1-0 katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika.

    Kikosi hicho kilikuwa pia kimefeli kufunga katika michezo sita kati ya saba iliyopita iliyopoteza, na matokeo ya Jumamosi yameendeleza mwenendo huo.

    Kwa upande wa Argentina, uhusiano wa soka la taifa hilo na Afrika una historia ndefu. Hivyo, ni jambo la kipekee kuona timu za Afrika zikipewa nafasi katika wiki ya kuaga kwa Messi.

    Messi amekutana na Nigeria katika baadhi ya nyakati muhimu za safari yake ya kimataifa, kuanzia fainali ya Kombe la Dunia la FIFA la vijana chini ya miaka 20 mwaka 2005 hadi fainali ya soka ya Olimpiki mwaka 2008, michezo yote miwili ambayo Argentina ilishinda.

    Pia amekutana na Super Eagles katika Kombe la Dunia mara tatu na kufunga mabao matatu dhidi ya Nigeria katika michuano ya mwaka 2014 na 2018.

  10. Trump: Iran ichague, kutatua mzozo kwa njia ngumu au rahisi

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema mzozo kati ya Iran na Marekani unaweza kutatuliwa kwa “njia ngumu au njia rahisi.”

    “Nina uamuzi wa kufanya kuhusu Iran,” Trump aliwaambia waandishi wa habari alipokuwa akiondoka katika Ikulu ya White House kuelekea katika mkutano wa hadhara huko Vandalia, Ohio.

    Trump pia alisema Iran “imedhoofishwa kwa kiasi kikubwa” kutokana na hatua na operesheni za Marekani, na kwamba nchi hiyo “imekaribia kabisa kuachana na mipango yoyote ya kujipatia silaha za nyuklia.”

    Hata hivyo, Iran imeendelea kukanusha mara kwa mara madai kwamba inajaribu kujipatia silaha za nyuklia.

  11. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 04/10/2026.