Rwanda yazindua mfumo mpya wa mirahaba kwa wasanii, kuipiku Tanzania?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Wasanii na wabunifu nchini Rwanda wamekaribisha Agizo jipya la Waziri linaloanzisha mfumo rasmi wa ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha (royalty fees), wakisema litasaidia kurekebisha changamoto za muda mrefu za malipo yasiyo rasmi na matumizi ya kazi zao bila idhini.

Miongoni mwa wanaopongeza hatua hiyo ni mchoraji na mwanamuziki mkongwe Pascal Bushayija, ambaye anasema mfumo huo unaweza kuwa ni mabadiliko muhimu kwa maisha ya wasanii waliokuwa wakipoteza mapato yao kwa miaka mingi.

"Nyimbo zangu zinachezwa, lakini sijalipwa"

Katika studio yake tulivu iliyojaa rangi na kazi za sanaa, Bushayija anaendelea kuchora huku akirejea safari yake ya zaidi ya miongo mitatu katika muziki na uchoraji.

Wimbo wake maarufu "Elina", uliotolewa miaka ya 1980, bado unachezwa kwenye redio, hoteli na maeneo mbalimbali nchini Rwanda, lakini anasema hakuwahi kunufaika ipasavyo na matumizi hayo.

"Inaniumiza sana kusikia nyimbo zangu kila mahali, hoteli, baa na redioni, bila idhini yangu au kupata chochote. Haki miliki zetu zimepuuzwa kwa miaka mingi. Wakati umewadia wasanii kupata haki zao," anasema Bushayija.

Tanzania wamekuwa wakitoa mirahaba kwa wasanii, lakini kiwango kinachotolewa mara nyingi kimekuwa kikihojiwa na wadau pamoja na wasanii wenyewe.

Mfumo mpya wa kudhibiti mirabaha

Kwa mujibu wa wataalamu wa sheria, agizo hilo jipya linatarajiwa kuweka mfumo wa lazima wa kufuatilia na kukusanya mirabaha kutoka kwa watu na taasisi zinazotumia kazi za ubunifu.

Wanasema matumizi ya teknolojia yataongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato hayo.

"Agizo hili linahakikisha kuwa yoyote anayetumia kazi za sanaa lazima alipe au awe na idhini. Teknolojia itasaidia kufuatilia matumizi ya maudhui kwa haraka na kwa uwazi," anasema mwanasheria, Jean Paul Ibambe.

Wasanii wasema ni hatua ya mabadiliko

Kwa wasanii wengi, mageuzi hayo yamepokelewa kama hatua ya muda mrefu iliyokuwa ikisubiriwa.

"Tumefurahi kupita kiasi. Hii ni kama ngao kwa wasanii. Kazi zetu sasa zitaheshimiwa na tutaanza kuishi kutokana na kazi zetu kama ilivyo sehemu nyingine duniani," anasema Intore Tuyisenge.

Usajili wa kazi za sanaa

Kwa mujibu wa mpango huo mpya, wasanii watahitajika kusajili kazi zao kwa mamlaka husika ili zitambuliwe rasmi na kulindwa chini ya mfumo wa mirabaha.

Hata hivyo, baadhi ya wasanii wanasema utekelezaji wake utahitaji ufuatiliaji makini ili kuhakikisha unawanufaisha watendaji wadogo na wakubwa kwa usawa.

Wito wa uwiano mpya katika sekta ya ubunifu

Kwa wasanii wa jukwaani kama Sabrina Mwerere, mabadiliko haya ni ishara ya mwanzo mpya kwa sekta ya ubunifu nchini Rwanda.

Huku matumaini yakiongezeka, wengi wanatazamia kuona kama mfumo huo utaweza kutatua changamoto za muda mrefu za upotevu wa mapato na kuhakikisha kazi za sanaa zinathaminiwa ipasavyo.

Mageuzi haya yanaashiria mwelekeo mpya wa uchumi wa ubunifu nchini Rwanda, ambapo kazi za wasanii hazitathaminiwa tu kwa umaarufu wake, bali pia kwa thamani ya kiuchumi inayopaswa kulipiwa ipasavyo.