Simba v Yanga: Mambo 7 kutoka dabi ya 'jeshini'

Muda wa kusoma: Dakika 5

Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga nchini Tanzania imeendelea kuthibitisha ukubwa wake, safari hii ikichezwa katika mazingira ya kipekee, kwenye uwanja wa kambini ama jeshini, Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Sare ya mabao 2-2 haikuwa tu matokeo, bali ilikuwa picha halisi ya ushindani, ubora na presha ya mechi kubwa. Simba walianza kwa kasi na dhamira ya wazi ya kutawala mchezo mapema. Mabao ya Libasse Gueye na Clatous Chama yaliwapa faida ya mapema na kuonyesha mpango wao wa kushambulia kwa nguvu.

Lakini Yanga walirejea kwa utulivu na uzoefu. Kupitia Prince Dube na nahodha Bakari Mwamnyeto, walionyesha uthabiti na kupambana hadi dakika ya mwisho, japo matokeo yalisalia kuwa sare.

Sare hiyo inaacha pengo la alama tano likiendelea kuwepo, lakini zaidi ya hilo, imeacha mjadala mpana kuhusu kiwango cha dabi, mazingira ya mchezo na mchango wa wachezaji binafsi. Haya hapa mambo saba yaliyojitokeza.

1. Ubora wa dabi ya kariakoo unarejea?

Kwa muda mrefu, dabi ya Kariakoo ilikuwa imeanza kupoteza ladha yake kwa kuwa ya upande mmoja na inayotabirika. Lakini kilichoonekana Isamuhyo ni taswira tofauti kabisa.

Mchezo ulikuwa wazi, wenye mashambulizi ya kasi na nafasi nyingi za kufunga kutoka pande zote mbili. Hakukuwa na timu iliyokuja kulinda, kila mmoja alitaka kushinda.

Uliona ufundi, ubora, kujituma na kujiachia kwa wachezaji kuonyesha walichonacho. Kama wangekuwa kwneye uwanja bora zaidi zaidi kama taifa pengine ladha na ubora ungeongezeka zaidi.

Kwa urahisi kabisa, matokeo yangekuwa makubwa zaidi kama nafasi za wazi zingetumika vyema. Wachezaji kama Elie Mpanzu na Prince Dube walikuwa na nafasi za kuongeza mabao lakini hawakuzitumia.

"Bonge moja la game (mchezo), ufundi, maarifa vimetawala hapa" , kauli hii ilielezea kila kitu kuhusu ubora wa mchezo.

Kwa ujumla, ilikuwa ni dabi ya burudani, mabao na viwango vya juu.

3. Wiki ya kipekee, dabi mbili ndani ya siku 5

Katika hali isiyo ya kawaida, mashabiki wameshuhudia dabi mbili ndani ya siku tano. Aprili 29, 2026, Simba waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga katika Kombe la Muungano kule Zanzibar. Kisha Mei 3 wakakutana tena kwenye ligi kuu.

Pengine kwa kizazi hiki wanashuhudia kwa mara ya kwanza dabi mbili ndani ya siku 5, na pengine itawachukua muda kushuhudia tena dabi mbili ndani ya wiki moja kwenye uhai wao.

Mfululizo huu umeongeza ushindani na presha kwa wachezaji, lakini pia umeongeza ladha na burudani ya kipekee kwa mashabiki.

Ni aina ya ratiba inayohitaji uimara wa hali ya juu kimwili na kisaikolojia, lakini kwa mashabiki pia inaleta burudani mara mbili kwa muda mfupi. Na kwa upande mwingine inaleta presha.

Wapo waliolala vizuri, na wapo waliolala kwa usingizi wa mang'amng'am. Matokeo yaliyopita kule Zanzibar hawakuyataka, na walioyataka hawakutaka matokeo tofauti.

3. Uamuzi wa kiwango cha juu

Waamuzi kutoka Morocco wakiongozwa na Hamza El Fareq walionesha utulivu na umakini mkubwa katika kuchezesha mchezo huu.

Katika dabi nyingi, maamuzi ya waamuzi huwa sehemu ya mjadala mkubwa. Lakini safari hii, hakukuwa na matukio makubwa ya utata yaliyotawala baada ya mechi.

Maamuzi yao yalionekana kuwa sahihi kwa kiwango kikubwa, na yalisaidia kuipa mechi utulivu mzuri. Hii iliruhusu wachezaji kuonyesha ubora wao bila kuvurugwa na kelele za nje.

Ni ushahidi kuwa matumizi ya waamuzi wa kimataifa yanaweza kuongeza ubora wa mechi kubwa. Juni 25 mwaka jana, mechi ya ligi baina ya timu hizo ilichezeshwa na waamuzi kutoka nchini Misri, Amin Mohammed Omar aliyekuwa mwamuzi wa kati alisaidiwa na waaamuzi wa pembeni Mahmoud Ahmed na Samir Gamal wote ni kutoka Misri.

Wiki hii pia mwamuzi mkenya Dickes Mimisa Nyagrowa, alichezesha fainali ya Kombe la Muungano ya timu hizi katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Mechi zote hizi kelele na lawama kuhusu maamuzi hayakusikika kwa kiwango kilichozoeleka wanapochezesha waamuzi wa ndani.

4. Goli la msimu limepatikana?

Kiungo wa Simba, Clatous Chama aligunga moja ya mabao bora kabisa ya msimu katika mchezo huu.

Akipokea pasi ya kupenyeza na Mpanzu, akiwa ameupa mgongo lango, alipika tiktaka ya upande kwa ujanja wa haraka na kufunga kwa ustadi.

Ni bao la kiwango cha juu, la nadra na lenye ubunifu wa kipekee, hasa likizingatiwa ukubwa wa mechi yenyewe.

Tayari limeanza kusambaa kwenye mitandao na kuingia kwenye mjadala wa bao bora la msimu.

5. Chama amerudi kiwango chake?

Mbali na kufunga bao zuri, Chama anaendelea kuonyesha dalili za kurejea kwenye ubora wake wa zamani.

Katika dabi ya Kombe la Muungano, alisababisha penati ya ushindi. Katika mchezo huu wa ligi, amefunga bao moja na kutoa pasi ya bao kwa Libasse Gueye.

Hii inaonyesha wazi mchango wake katika mechi kubwa na uwezo wake wa kuamua matokeo.

"Chama atabaki mbantu wa ajabu kuwahi kucheza soka ukiacha Samuel Et'oo", anasema theutdcode kupitia mtandao wa X.

Naye Ayubu Madenge anaongeza:

"Kwenye jumba la makumbusho na historia ya soka Tanzania, jezi ya Clatous Chama itapambwa na madini ya dhahabu na almasi. Mwamba kutoka Lusaka amedhihirisha kuwa yeye ni mchezaji wa daraja la juu sana".

Kwa kiwango hiki, Chama anaendelea kuthibitisha hadhi yake kama mchezaji wa mechi kubwa. Anazeeka na ubora wake.

6. Isamuhyo na mjadala wa hadhi ya uwanja

Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ulikuwa sehemu kubwa ya mjadala kabla, wakati na baada ya mchezo. Dabi kupigwa 'jeshini' kukaifanya wengine kuhoji, "dabi jeshini?' na inaondoa hadhi yake ya dabi ya Kariakoo.

Licha ya kuwa na vipimo vikubwa vya kuchezea, bado kulikuwa na maswali kuhusu kama unakidhi hadhi ya dabi ya Kariakoo. Malalamiko yalihusu ubora wa sehemu ya kuchezea na miundombinu kwa ujumla.

"Kariakoo dabi kuchezwa Isamuhyo ni aibu ya kitaifa" anasema The 6th Estate kupitia mtandao wa X, akiongeza kuwa "haipaswi kuchezwa kwenye mazingira ya mitaani. Inapaswa kuchezwa kwenye uwanja wenye hadhi, usalama, parking, matangazo, VIP, sehemu za vyombo vya habari na uwezo wa kubeba thamani yake ya kibiashara".

Hata hivyo, pamoja na mjadala huo, uwanja haukuzuia burudani iliyopatikana ndani ya dakika 90.

7. Utulivu wa nje ya uwanja

Tofauti kubwa na dabi nyingi zilizopita imeonekana nje ya uwanja.

Hakukuwa na vurugu wala misongamano mikubwa kama ilivyozoeleka katika viwanja kama Benjamin Mkapa au ule wa Uhuru, Jijini Dar es Salaaam. Mashabiki waliingia na kutoka kwa utaratibu mzuri. Uchache wao pia ulisaidia utaratibu huo.

Hali hii inafanana kwa kiasi fulani na ilivyozoeleka Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan, ambapo mara nyingi utulivu hujitokeza zaidi.

Hata hivyo, utani wa jadi haukukosekana. Baadhi ya mashabiki wa Simba waliwazodoa wenzao wa Yanga wakidai wachezaji wa timu hiyo wamebadilishia nguo kwenye nyumba jirani badala ya vyumba rasmi.

Kwa ujumla, ulikuwa ni mchanganyiko wa utulivu na utani wa soka, hali inayoweza kuwa funzo kwa maandalizi ya mechi zijazo.