Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Mariam na safari ya kufua nguo kusaka $15,000 kupandikizwa figo
"Kama siku zingerudi nyuma, kabla sijapata ugonjwa wa figo, ningekuwa nafanya vipimo vya afya mara kwa mara."
Haya ni maneno ya Mariam Ali, msichana wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 26 ambaye maisha yake yalibadilika ghafla baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa figo.
Miaka miwili tu baada ya kuhitimu shahada ya Elimu katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Mariam alianza safari ngumu ya matibabu, hofu na matumaini.
Mariam ni miongoni mwa vijana wengi nchini Tanzania wanaokabiliwa na magonjwa sugu kama ugonjwa wa figo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, idadi ya vijana walio chini ya miaka 50 wanaopata ugonjwa huo inaongezeka kwa kasi, hali inayotia wasiwasi mkubwa kwa jamii.
Baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo, Mariam anasema maisha yake yalibadilika kabisa. Anakumbuka siku aliyopokea majibu ya vipimo kutoka kwa daktari kuwa ni siku yenye maumivu makubwa moyoni mwake.
"Siku daktari aliponiambia nina tatizo la figo nililia sana. Nilikuwa naogopa na kujiuliza, kwa nini mimi? Nilikuwa hata sielewi vizuri alichokuwa ananieleza kwa sababu akili yangu ilikuwa imechanganyikiwa," anasimulia Mariam.
Mbali na hofu ya ugonjwa wenyewe, Mariam alianza kuwaza kuhusu ndoto zake za maisha. Alijiuliza kama bado angeweza kuolewa, kupata watoto na kuishi maisha ya kawaida kama wanawake wengine.
"Nilimuuliza daktari maswali mengi. Nilijiuliza nitapata mume kweli? Nitazaa? Maisha yangu yatakuwaje?" anasema.
Hata hivyo, anasema madaktari walimpa moyo . Walimueleza kuwa watu wengi waliowahi kupitia hali kama yake waliweza kuendelea na maisha yao baada ya matibabu ya kuchuja damu kitaalamu dialysis na hatimaye kupandikiza figo.
'Mama yupo tayari kunitolea figo, tatizo ni gharama ya upandikizaji'
Mariam anasema kwamba mama yake yuko tayari wakati wowote kujitolea figo ili kuokoa maisha yake,lakini hadi sasa hajafanikiwa kupata kiasi cha pesa kinachotakiwa ili kufanikisha upandikizaji huo.
"Kupandikiza figo hapa nyumbani Tanzania ni takriban milioni 40" huku kuchuja damu ni milioni moja kila mwezi. Kwa biashara ya usafi wa majumbani nitahitaji muda mrefu sana kukusanya kiasi cha kukidhi matibabu na upandikizaji.
"Daktari alinieleza kuwa nikifuata matibabu ninaweza kuendelea kuishi kawaida. Alinipa mifano ya watu waliopitia hali kama yangu na wakapona na kuendelea na maisha yao vizuri lakini pia wanawake kuweza kupata Watoto baadae," anasema.
Kwa sasa Mariam anafanya kazi mbalimbali za usafi wa majumbani ili kujisitiri na kupata fedha za matibabu. Licha ya uchovu na changamoto za kiafya, amesema hana uchaguzi mwingine zaidi ya kupambana.
"Watu wengine wananishangaa kwanini nafanya kazi wakati ninaumwa. Ukweli ni kwamba gharama za matibabu ni kubwa sana. Nisipojituma, nitazimudu vipi?" anaeleza.
Anasema wakati mwingine mawazo kuhusu gharama za kuchuja damu na upandikizaji figo humchosha sana kiakili. Lakini aliamua kutokukata tamaa.
"Tatizo limeshanifika, siwezi kulikimbia. Lazima nitafute namna ya kukabiliana nalo," anasema kwa sauti ya matumaini.
Mitandao inapokeaje elimu ya afya mtandaoni?
Mbali na matibabu, Mariam amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kueleza safari yake na kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa kufanya vipimo vya afya mapema. Kupitia mitandao hiyo, amekutana na watu wengi wenye changamoto kama yake, jambo lililompa faraja kubwa.
"Nimegundua kuwa sipo peke yangu. Watu wengi wamepitia hali kama yangu na bado wanaendelea kupambana. Hilo limenipa nguvu," anasema.
Mariam anatumia sauti yake kuiasa jamii kuhusu umuhimu wa kuchunguza afya mara kwa mara na kutokupuuzia dalili za magonjwa.
Huku akihimiza ujasiri, matumaini na nguvu ya kupambana hata pale maisha yanapobadilika ghafla.