Jinsi Gen Z wanavyopania kubadili mwelekeo wa uchaguzi wa Kenya 2027

    • Author, Barbara Plett Usher
    • Nafasi, Mwandishi wa Afrika
    • Akiripoti kutoka, Nairobi, Kangema & Meru
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Ademba Allans anafanya siasa, na hasa usajili wa wapiga kura, kuwa jambo la kisasa na linalovutia vijana nchini Kenya.

Mwanafunzi huyo, ambaye pia ni mwanahabari na mhamasishaji wa masuala ya kiraia, alianzisha kampeni ya usajili wa wapiga kura kupitia mitandao ya kijamii mapema mwaka huu. Akitumia picha za selfie, muziki na vichekesho, alilenga kuwahamasisha vijana kujisajili na kushiriki katika mchakato wa uchaguzi.

Matokeo yake yalizidi matarajio ya wengi. Kufikia mwisho wa zoezi la usajili, watu milioni 2.6 walikuwa wamejiandikisha kuwa wapiga kura wapya nchini kote. Sasa analenga kuwahamasisha wengine milioni 2.3 kujiandikisha katika awamu inayofuata.

"Ilikuwa ni mtindo wa siasa wa Gen Z ," anasema. "Ilihusisha ubunifu, mvuto na matumizi ya mitandao ya kijamii. Tulifanikiwa kuibua hamasa kubwa kiasi kwamba watu walihisi hawakupaswa kubaki nyuma. Kila mtu alitaka kuwa sehemu yake."

Kizazi cha Gen Z, kinachowajumuisha waliozaliwa mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, kilijitokeza kwa nguvu katika ulingo wa kisiasa miaka miwili iliyopita. Maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana yaliishinikiza serikali kuondoa mswada wa kodi uliokuwa umepingwa vikali. Hata hivyo, mafanikio hayo yalifuatiwa na ukandamizaji mkali wa polisi, uliosababisha vifo na majeraha kwa baadhi ya waandamanaji.

Sasa vijana nchini Kenya wanataka kuhamisha mapambano yao kutoka mitaani hadi kwenye sanduku la kura, wakichochewa na hasira dhidi ya mfumo wa kisiasa wanaouona kuwa umegubikwa na ufisadi na ukiukwaji wa haki unaotekelezwa na baadhi ya vyombo vya usalama.

Kwa kuwa ni kundi kubwa la wapiga kura, vijana wanaamini wana uwezo wa kuathiri mwelekeo wa siasa za nchi. Zaidi ya asilimia 30 ya Wakenya wenye sifa ya kupiga kura wana umri wa chini ya miaka 35, hali inayowapa ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa kitaifa na kuwafanya kuwa nguvu muhimu katika kuamua matokeo ya kisiasa.

za maoni zinaonyesha Rais William Ruto yuko katika mazingira magumu kisiasa, huku kiwango chake cha uungwaji mkono kikionekana kuyumba.

Lakini swali linaloibuka ni ikiwa kizaza cha Gen Z kinaweza kugeuza harakati zake zilizoanzia mitandaoni na zisizo na uongozi wa moja kwa moja kuwa nguvu ya kisiasa inayoweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.

"Harakati hizi zinazoongozwa na vijana ni vigumu kutabiri zinakoelekea," anasema mchambuzi wa siasa Tom Mboya.

"Hazihitaji rasilimali nyingi na zinaweza kujitokeza wakati wowote. Maandamano ya Muswada wa Fedha yalikuwa ya kisiasa kwa kiasi kikubwa, lakini harakati hizi bado hazijajaribiwa kwenye siasa za uchaguzi. Ikiwa zitaamua kumuunga mkono mgombea fulani, basi mgombea huyo anaweza kunufaika pakubwa," anaongeza.

Moja ya nguvu za Gen Z ni uwezo wake wa kuhamasisha vijana nje ya miundo ya vyama vya siasa na bila kutegemea ukabila, ambao kwa muda mrefu umekuwa msingi muhimu wa siasa za Kenya.

Allans anasema harakati hizo zimekuwa makini kutounga mkono mgombea au chama chochote. Kile wanachosisitiza, anasema, ni umuhimu wa kuchagua viongozi bora badala ya kufuata misimamo ya kisiasa au kikabila.

"Hatujawahi kushuhudia kundi kubwa la wapiga kura ambalo halijafungamana na chama au mwanasiasa fulani. Sisi tunataka watu wawachague viongozi wanaowaamini," anasema.

"Kwa sasa, sisi ni kura zinazoweza kuelekea upande wowote kwa sababu hakuna anayejua tutamuunga mkono nani."

Wakati huohuo, Rais William Ruto na chama chake cha UDA wanakabiliwa na changamoto za kisiasa huku uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 ukikaribia.

Tafiti za maoni zinaonyesha kuwa Wakenya wengi hawaridhishwi na mwelekeo wa nchi, huku wengi wakisema hali yao ya kiuchumi imezorota tangu Ruto alipoingia madarakani mwaka 2022.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema umaarufu wa rais pekee hauwezi kuamua matokeo ya uchaguzi. Wanaeleza kwamba Ruto ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa wa kupanga kampeni za uchaguzi na ana faida ya kuwa mgombea anayetoka katika serikali iliyo madarakani.

Kwa upande mwingine, wapinzani wake bado wanaonekana kugawanyika, na bado haijulikani iwapo watafanikiwa kuunda muungano imara wa kumpa changamoto kubwa katika uchaguzi ujao.

Mmoja wa wanasiasa waliovutia hisia za vijana wengi wa kizazi cha 'Gen Z' ni Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Amejitokeza kama kiongozi wa vuguvugu linaloitwa 'Linda Mwananchi', ambalo linapata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana ambao hawajaridhishwa na hali ya mambo.

Sifuna alianza kuvutia hisia zao alipojaribu kuwazuia polisi kuwapiga risasi waandamanaji waliokuwa wakivamia jengo la Bunge wakati wa maandamano ya mwaka 2024.

Sasa anaongoza vuguvugu analolitaja kuwa la "wananchi kwa wananchi", linalotetea haki za binadamu, utawala wa sheria na utekelezaji wa katiba.

Ingawa bado hajatangaza rasmi nia ya kuwania urais, tayari ameanza kampeni za kujijengea uungwaji mkono katika maeneo mbalimbali nchini. BBC ilikutana naye wakati wa ziara yake ya hivi karibuni katika Kaunti ya Meru, eneo la kati mwa Kenya ambalo lilikuwa miongoni mwa ngome muhimu za Rais William Ruto katika uchaguzi uliopita.

"Vijana wanataka kuona mazingira ambayo kila mtu ana nafasi sawa ya kushindana na kufanikiwa," aliiambia BBC kabla ya kuanza mkutano wake wa hadhara ulioambatana na shamrashamra na umati wa wafuasi.

"Tunahitaji kubadilisha mfumo uliopo ili kila mtu apate fursa sawa, iwe ni katika elimu, ajira au maendeleo ya kiuchumi. Hakuna anayepaswa kuachwa nyuma kwa sababu ya alikotoka au hali yake ya maisha," alisema.

Kwa mtazamo wake, uchaguzi wa mwaka 2027 utakuwa jaribio muhimu la kupima nguvu ya mawazo yanayohamasishwa na vijana.

"Uchaguzi wa 2027 utatuonyesha kama ujumbe huu unaoungwa mkono na vijana unaweza kubadilika kuwa nguvu ya kisiasa. Wajibu wetu kama viongozi ni kutoa dira inayowavutia wananchi na kuwafanya waamini kwamba mabadiliko yanawezekana," alisema.

Ruto mwenyewe aliingia madarakani mwaka 2022 akiwa na ujumbe wa mabadiliko ulioavutia wapigakura wengi. Aliahidi kujenga uchumi unaowanufaisha wananchi wa kawaida na kuinua makundi yaliyokuwa yakihisi kutengwa katika maendeleo ya nchi.

Tangu wakati huo, serikali yake imeanzisha mageuzi kadhaa, yakiwemo mabadiliko makubwa katika mfumo wa huduma za afya. Hata hivyo, baadhi ya vijana wanasema walikatishwa tamaa na sera za kuongeza kodi na hatua za kubana matumizi, ambazo wamezihisi moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.

"Nimekuja hapa kwa sababu nataka kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa. Tunahitaji viongozi wapya wanaoelewa changamoto halisi zinazowakabili vijana wa Kenya," Brandon Muremi, mwenye umri wa miaka 23, aliiambia BBC.

BBC ilikutana naye katika moja ya vituo vya mwisho vya ziara hiyo ya kisiasa iliyokuwa na shughuli nyingi. Msafara huo ulitembelea maeneo manne tofauti, huku wakati mwingine ukisababisha msongamano wa magari, viongozi wakisimama juu ya magari yao na kuhutubia umati wa watu kwa hotuba za hamasa katika kila kituo walichosimama.

"Tunahitaji viongozi wanaotekeleza ahadi zao, si wale wanaobaki kwenye maneno pekee," anasema Conrad Mutangili, mwanafunzi wa uhandisi wa mitambo mwenye umri wa miaka 19, ambaye alihudhuria mkutano huo kwa kutaka kujionea kilichokuwa kikiendelea.

"Tunatafuta mtu ambaye anaweza kutimiza ahadi zake na kuwaletea wananchi matokeo wanayoahidi. Wanasiasa wengi huahidi mambo mazuri sana, lakini mwisho wa siku wananchi hawaoni matokeo yake," anaongeza.

Kwa Yvonne Kileme, mwanafunzi wa sayansi ya kompyuta mwenye umri wa miaka 22, suala kuu ni ajira.

"Tunataka kuona matokeo haraka," anasema, ingawa anakiri kwamba baadhi ya miradi ya serikali huchukua muda kabla ya kuanza kuleta mabadiliko yanayoonekana. "Jambo kubwa tunalolitaka sisi vijana ni ajira, ajira, ajira."

Rais William Ruto amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake inaendelea kuunda nafasi za kazi, akisema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana lilikuwepo hata kabla ya kuingia madarakani mwaka 2022.

Pia amejaribu kuwafikia vijana wa Kizazi Z kupitia programu za mikopo na ruzuku kwa biashara ndogo ndogo, pamoja na uwekezaji katika teknolojia na ajira za kidijitali.

Kiongozi wa kitaifa wa vijana wa chama cha UDA, Kariuki Ngunjiri, aliiambia BBC kuwa ana imani chama hicho kitashinda uchaguzi wa 2027 kwa kishindo.

"Rais anasikiliza wananchi, amekuwa karibu na vijana na anaelewa changamoto zao. Serikali imeweka mikakati ya kuwasaidia kupata ajira, na hilo limetupa nguvu kubwa kama chama," alisema.

Kwa mujibu wake, mjadala unaotawala mitandaoni hauonyeshi kwa lazima hali halisi ya kisiasa nchini.

"Hatuna wasiwasi na kelele za mitandaoni. Sisi tunajikita katika masuala ya maendeleo yanayogusa maisha ya vijana moja kwa moja. Mitindo ya mijadala ya mtandaoni na lebo maarufu mara nyingi si kigezo cha kuamua matokeo ya uchaguzi," alisema.

Alisema hayo wakati wa mkutano wa UDA uliofanyika Kangema, takriban kilomita 100 kaskazini mwa Nairobi, ambako viongozi wa chama walikuwa wakieleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.

Miongoni mwa waliohudhuria alikuwa Shintah Mutahi, mwenye umri wa miaka 23, ambaye bado anatafuta ajira.

"Nilikuja kusikia kile wanachosema. Labda kuna fursa ya kazi inaweza kujitokeza. Ninaamini wanaweza kusaidia, lakini wanahitaji kupewa muda wa kutekeleza ahadi zao," alisema.

John Kiragu, kiongozi wa vijana wa UDA katika eneo hilo, anasema anaelewa sababu zilizowasukuma vijana wengi kushiriki maandamano ya mwaka jana.

"Kumekuwa na changamoto nyingi, hilo halina mjadala," alisema. "Lakini sasa serikali inajaribu kuwashirikisha vijana zaidi na kutekeleza mipango ambayo, kwa mtazamo wake, inaweza kuboresha maisha yao katika siku zijazo."

Kiragu alisema pia anajishughulisha mpango unaolenga kupambana na matumizi ya pombe miongoni mwa vijana, tatizo ambalo linaendelea kuathiri sehemu kubwa ya eneo hilo. Wakati wa mkutano huo wa hadhara, baadhi ya vijana waliohudhuria walionekana kuwa tayari wametumia pombe za kienyeji za bei nafuu tangu mapema asubuhi.

Miongoni mwa waliofika kusikiliza ahadi za viongozi alikuwa Calvin Ware, nahodha wa timu ya soka ya eneo hilo. Hata hivyo, alisema hakuwa na matarajio makubwa kutokana na ahadi hizo, akieleza kuwa amesikia kauli kama hizo mara nyingi, hasa wakati wa kampeni za uchaguzi.

"Tayari tumeamua tunachotaka," alisema. "Tunataka mabadiliko. Tunataka kuona kizazi kipya cha viongozi na mawazo mapya kutoka kila pembe ya nchi. Hatutaki siasa zinazojengwa juu ya ukabila au maslahi ya makundi fulani. Tunataka mabadiliko, na hilo ndilo jambo muhimu kwetu."

Tulipokuwa tukizungumza, shangwe zilianza kusikika kutoka uwanjani. Mkutano ulikuwa umefikia mwisho na watu walikuwa wakijipanga foleni kupokea kiasi cha fedha taslimu kilichotolewa kwa wahudhuriaji. Kila mmoja alikuwa akipewa shilingi 350 za Kenya, sawa na takriban dola tatu za Marekani.

Nchini Kenya, si jambo la ajabu kwa baadhi ya wanasiasa kutoa fedha ili kuwahamasisha watu kuhudhuria mikutano ya kisiasa. Katika baadhi ya kampeni, kiasi kikubwa cha fedha hutumika katika juhudi za kuwavutia wapigakura.

"Kuliko ilivyo katika sehemu nyingi duniani, fedha bado zina nafasi kubwa katika siasa za Kenya," anasema mchambuzi wa siasa Tom Mboya. "Gharama ya kushiriki na kushindana katika siasa za Kenya ni kubwa sana."

Huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukizidi kukaribia, kuna dalili zinazoonyesha kwamba mazingira ya kisiasa nchini yanaweza kuwa yanabadilika. Hisia za kutoridhishwa miongoni mwa vijana zimeibua mjadala mpya kuhusu mustakabali wa siasa za Kenya na uwezo wa kizazi kipya kuleta mabadiliko.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi