Moja kwa moja, Trump asema makubaliano ya Marekani na Iran kutiwa saini leo, lakini Tehran yatilia shaka muda uliopangwa

Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, Trump amesema Mlango wa bahari wa Hormuz, njia kuu ya meli, itakuwa "wazi kwa wote" mara tu makubaliano hayo yatakapokubaliwa.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Guyana yampendekeza balozi wake kuwania ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa

    Carolyn Rodrigues-Birkett amekuwa mwakilishi wa Guyana katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2020.

    Chanzo cha picha, Wizara ya mambo ya kigeni ya Guyana

    Maelezo ya picha, Carolyn Rodrigues-Birkett amekuwa mwakilishi wa Guyana katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2020.

    Guyana imemteua balozi wake katika Umoja wa Mataifa kugombea wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja huo wa kimataifa, jambo lililotangazwa na Rais wa taifa hilo la Amerika Kusini, Irfaan Ali, usiku wa Ijumaa.

    Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa, António Guterres wa Ureno, anatarajiwa kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka huu baada ya kuhudumu kwa mihula miwili tangu mwaka 2017.

    Carolyn Rodrigues-Birkett amekuwa mwakilishi wa Guyana katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2020.

    Guyana ni taifa la pwani ya Bahari ya Atlantiki lililopo kati ya Venezuela na Brazil, lenye idadi ya watu isiyofikia milioni moja.

    Akizungumza katika hotuba yake, Rais Ali alisema maono ya Rodrigues Birkett kwa Umoja wa Mataifa yanajikita katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuongeza ufanisi na mwitikio wa taasisi hiyo, kukuza utawala jumuishi wa dunia na kuhakikisha Umoja wa Mataifa una uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisasa.

    Ali pia alisifu uongozi wa balozi huyo mwenye umri wa miaka 52 wakati Guyana ilipohudumu kwa muhula wa miaka miwili kama mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 2024 na 2025.

    “Uchaguzi wetu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wenye mafanikio wa muhula wetu wa 2024 hadi 2025 umeonyesha kwa dunia kuwa Guyana inaweza kutoa uongozi katika ngazi mbalimbali za mfumo wa kimataifa,” alisema Ali.

    Rodrigues Birkett aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Guyana kati ya mwaka 2008 na 2015 kabla ya kujiunga na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kama Mratibu Maalumu wa Ushirikiano na Mabunge.

    Mwaka 2017 aliteuliwa kuwa mkuu wa Ofisi ya Mawasiliano ya FAO mjini Geneva, Uswisi, ambako alihudumu hadi mwaka 2020.

    Hadi sasa, hakuna mwanamke aliyewahi kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

    Mataifa mengi yanaendelea kushinikiza mwanamke achaguliwe kwa mara ya kwanza kuongoza taasisi hiyo, huku nchi za Amerika ya Kusini zikidai ni zamu yao kwa kuzingatia utamaduni wa mzunguko wa kijiografia katika uteuzi wa nafasi hiyo, ingawa si mara zote kanuni hiyo imekuwa ikifuatwa kikamilifu.

    Miongoni mwa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Michelle Bachelet, aliyewahi kuwa Rais wa Chile na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Rebeca Grynspan wa Costa Rica, pamoja na María Fernanda Espinosa.

    Wagombea wengine waliotangaza nia ni Rafael Grossi kutoka Argentina na aliyekuwa rais wa Senegal Macky Sall.

    Soma zaidi:

  2. Siku ya kuzaliwa ya Trump yaambatana na kutiwa saini kwa makubaliano ya Iran na Marekani

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, anatimiza miaka 80 Jumapili ya leo Juni 14, siku ambayo amesema pia itashuhudia kutiwa saini kwa makubaliano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu kati ya Marekani na Iran.

    Trump amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo kunaweza kufungua kwa haraka Mlango wa Bahari wa Hormuz na kuanzisha mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ingawa viongozi wa Iran wameendelea kuonyesha tahadhari na mashaka kuhusu muda wa kutiwa saini kwake.

    Kwa majuma kadhaa, Trump amekuwa akisema kuwa makubaliano hayo yako karibu kufikiwa.

    Wakati huo huo, anasherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa hafla kubwa ya mashindano ya UFC katika ikulu ya White House.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Tunachojua kuhusu makubaliano yatakayotiwa saini na Marekani na Iran

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani na Iran, kwa upatanishi wa Pakistan, Qatar na mataifa mengine kadhaa, zinatarajiwa kutia saini hati ya maelewano leo.

    Chini ya makubaliano hayo, usitishaji wa mapigano utaongezwa kwa siku 60, Mlango wa Bahari wa Hormuz utafunguliwa tena, na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yataanzishwa.

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesema pande hizo mbili zimekaribia kufikia makubaliano ambayo hayajawahi kushuhudiwa hapo awali, huku maandalizi ya kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki yakiendelea.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, pia amesema kuwa makubaliano hayo yatatiwa saini leo na kwamba Mlango wa Bahari wa Hormuz utafunguliwa mara moja kwa meli zote za biashara na usafirishaji.

    Aidha, Trump ameonya kuwa iwapo makubaliano hayo hayataanza kutekelezwa haraka na kikamilifu, kuna uwezekano wa kurejelewa kwa matumizi ya nguvu za kijeshi.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Uingereza yaunga mkono juhudi za Trump kumaliza mzozo wa Iran

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza imetangaza kuwa Waziri Mkuu Keir Starmer amejadili juhudi za kumaliza mzozo unaohusisha Iran katika mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani, Donald Trump.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Starmer amekaribisha hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo na kusisitiza kuwa Uingereza iko tayari kuunga mkono utekelezaji wa makubaliano yoyote ya amani yatakayofikiwa, pamoja na kushirikiana na washirika wa kimataifa kuhakikisha yanafanikiwa.

    Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kuhusu umuhimu wa kurejesha uhuru wa usafiri na usafirishaji ili kupunguza athari hasi za mkwamo wa kiuchumi duniani.

    Katika maendeleo mengine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Muhammad Ishaq Dar, na mwenzake wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud, walifanya mazungumzo kwa njia ya simu kuhusu mwafaka unaojadiliwa kati ya Marekani na Iran.

    Pakistan inaendelea na juhudi za upatanishi kati ya Iran na Marekani, ikisaidia kufanikisha usitishaji wa mapigano na kuwezesha mazungumzo yanayolenga kufikiwa kwa makubaliano ya amani kati ya mataifa hayo mawili.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Trump asema makubaliano ya Marekani na Iran kutiwa saini leo, lakini Tehran yatilia shaka muda uliopangwa

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa makubaliano ya kumaliza mapigano kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kutiwa saini Jumapili, baada ya Tehran kuonyesha mashaka kuhusu muda wa kufikiwa kwa makubaliano hayo.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa bidhaa kwa meli, utakuwa "wazi kwa wote" mara tu makubaliano hayo yatakapokubaliwa.

    Pakistan, ambayo imekuwa mpatanishi muhimu katika mazungumzo hayo, pia ilisema makubaliano hayo yanatarajiwa kukamilishwa ndani ya saa 24 zijazo na kwamba maandalizi ya kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki yanaendelea.

    Kabla ya matamshi ya Trump, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alionyesha tahadhari kuhusu ratiba hiyo akisema:

    "Tutalazimika kusubiri na kuona tarehe kamili ya kutiwa saini kwa hati ya maelewano, ingawa haitakuwa kesho."

    Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump aliandika:

    "Makubaliano hayo yamepangwa kutiwa saini kesho(akirejelea leo), na mara tu yatakapotiwa saini, Mlango wa Hormuz utakuwa WAZI KWA WOTE."

    Akirejelea kile kinachoaminika kuwa akiba ya urani iliyoboreshwa ya Iran, Trump alisema kwamba "wakati mwafaka, hali ikiwa imetulia kabisa, tutaingia na kuchukua mabaki ya nyuklia," akiongeza kuwa baadaye yataharibiwa.

    Kwa miongo kadhaa, Iran imekuwa ikituhumiwa na mataifa ya Magharibi kwa kujaribu kutengeneza silaha za nyuklia. Tehran imekuwa ikikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani, ikiwemo uzalishaji wa umeme na shughuli za utafiti.

    Trump pia alionya kwamba iwapo mambo hayataenda "haraka, kwa urahisi na kwa utulivu", Washington ina "njia mbadala ya mwisho kabisa", ambayo alieleza kuwa anatumaini haitalazimika kutumiwa tena.

    Mapema Jumamosi, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema kuwa "tuko karibu zaidi kuliko wakati wowote kufikia makubaliano ya amani."

    "Tukiwa na matarajio ya kukamilisha makubaliano hayo ndani ya saa 24 zijazo, Pakistan inajiandaa kwa kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki mara tu yatakapokamilika, kabla ya mazungumzo ya kiufundi kuanza wiki ijayo," Sharif aliandika kwenye mtandao wa X.

    Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Seyed Abbas Araghchi, alisema kuwa makubaliano kati ya Iran na Marekani yako karibu kufikiwa.

    Alisema makubaliano hayo yanatarajiwa kujumuisha kusitishwa kwa mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah nchini Lebanon.

    Araghchi aliiambia televisheni ya taifa ya Iran kuwa makubaliano hayo pia yanajumuisha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz pamoja na kuondolewa kwa vizuizi vya Marekani dhidi ya bandari za Iran.

    Hata hivyo, alisema mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yataanza katika hatua ya baadaye.

    Maafisa wa Marekani wamethibitisha baadhi ya vipengele vya makubaliano hayo, wakisema kuwa manufaa ya kiuchumi kwa Iran yatategemea uwezo wa Tehran kutekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo.

    Ripoti za awali kutoka Marekani zilidokeza kuwa Lebanon huenda isiwe sehemu ya makubaliano hayo, huku Iran ikiripotiwa kusisitiza suala hilo lijumuishwe katika mazungumzo.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya taarifa zinazochipuka. Tutakuletea matukio ya mkataba wa makubaliano ya Iran na Marekani unaotiwa saini Jumapili ya tarehe 14 Juni 2026.