Je, wanawake huwa na huruma kuliko wanaume?

Chanzo cha picha, Getty Images/ Javier Hirschfeld/ BBC
Utafiti wa sayansi umeweza kumaliza dhana potofu kuhusu huruma, na kuleta fikra mpya kuhusu uume.
Wanawake wanapofanikiwa kupiga hatua, mara nyingi hupuuziliwa na kusemwa "sio wanawake ndio waliweza kufanya hivyo, ni wanaume waliokuwa wamevalia shimizi" Mwanafalsafa Mary Astel aliandika mwaka wa 1705.
Kuna wakati Malkia Elizabeth I, alisema ataiongoza Uingereza kama mfalme, licha ya kuwa na mwili "dhaifu wa mwanamke."
Ingawa hizi ni hadithi za kale, bado kuna ubaguzi ikija katika kufafanua ufanisi.
Bado tunafafanua kuwa na hulka ya huruma kama suala linalokuja kiasili kwa mwanamke, ila sifa ya kutaka kutawala na kuwa na ujasiri huja kiasili kwa wanaume.
Hata wakidhibitisha tabia sawa, wanaume huonekana kuwa na ujasiri na kujituma zaidi kuliko wanawake.
Moja ya tabia inayoonekana kuwa ya wanawake ni kuwa na huruma.
Wanawake huonekana kama watu walio na huruma na hisia, ila wanaume ambao huonyesha huruma huonekana kuwa wadhaifu.
Lakini mbona iko hivi? Je ni kweli wanawake wanahuruma zaidi kuliko wanaume, ama hivyo ndivyo tumeaminishwa?
Dhana za kijinsia kama hizi huathiri jinsi tunavyolea watoto wetu, utamaduni wa sehemu yetu ya kazi na uongozi. Ila kile ambacho hatukioni ni jinsi ubaguzi huu huanza mapema katika maisha ya mtu na kusisitizwa hadi kubadilisha matarajio ya mtu na kuathiri jinsi tunatarajia watu wengine kuendesha maisha yao.
Homoni zinazochangia kuwa na huruma
Huruma inahusisha uwezo wa kuelewa fikra za mtu na hisia zake na hutusaidia kutoa usaidizi unaofaa.
Pia inaweza kueleweka kwa mtazamo wa kuweza kutambua hisia na kuzingatia mitazamo ya wengine ya kihisia.
Wanasayansi hutumia njia tofauti kupima uwezo wa mtu kuwa na hisia kupitia kuwapa kazi au wajaze hojaji.
Na imegunduliwa kuwa wanawake hurekodi viwango vya juu kuliko wanaume.
Simon Baron-Cohen, mwanasaikolojia kutoka chuo kikuu cha Cambridge anasema kuwa "akili ya mwanamke imeumbwa kiasilia kuwa na huruma" na hii huwafanya wanawake kufanya vyema katika majukumu ya malezi ila akili ya mwanaume "imeumbwa kuelewa na kujenga mifumo"

Chanzo cha picha, Alamy/ Javier Hirschfeld/ BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baron Cohen anasema kwamba ingawa sababu za kijamii zinaathiri huruma, utafiti wake unaashiria kuwa mfichuo wa homoni kwa mtoto akiwa tumboni una mchango katika ukuaji wake katika jamii.
Utafiti wake wa mwaka 2006 uliowahusisha zaidi ya watoto 200 wenye umri wa miaka 6 hadi 9 uligundua kwamba viwango vya homoni ya testosterone katika maji ya uzazi (amniotic fluid) wakati wa ujauzito ambavyo huwa juu zaidi kwa wavulana kuliko wasichana, vina uhusiano wa moja kwa moja katika vipimo vilivyofanywa vya kuweza kuchambua kanuni au mifumo.
Mfichuo wa homoni ya testosterone kwa mtoto akiwa tumboni ulikuwa kigezo chenye cha kutabiri kiwango cha huruma cha mtoto kuliko jinsia yake.
Utafiti mwingine wa mwaka 2007 pia ulionyesha kuwa mfichuo wa kijusi kwa homoni ya testosterone ulikuwa na uhusiano wa kinyume na vipimo vya huruma.
Baron-Cohen anasema,"Kilicho wazi ni kwamba mambo kama huruma au uelewa wa mifumo ni mchanganyiko changamano wa sababu za kibiolojia na za kijamii."
Je, huruma hupatikana kwenye vinasaba?
Katika utafiti uliogundua kuwa utofauti wa kijinsia katika kazi zilizohitaji huruma haukuwa mkubwa; Wanawake wanahuruma zaidi katika mataifa 36 kati ya 57 ambako utafiti huu ulifanyika, ila matokeo katika mataifa 21 yalikuwa sawa, na watafiti wanasema hawakuweza kupata sababu ya hilo.
Wanawake hurekodi matokeo ya juu katika vipimo vya huruma ikilinganishwa na wanaume.
Katika utafiti wa vinasaba uliohusisha watu zaidi ya 46,000 mwaka wa 2018, ambao walijaza hojaji na kutoa sampuli ya DNA, utafiti huo uligundua kuwa vinasaba havichangii popote kwa mtu kuwa na huruma. Mazingira ambayo mtu anakulia na kuishi huchangia viwango vya huruma mtu huyo atakuwa nayo
Hisia za huruma katika jamii
Wanawake huonyesha zaidi sifa za huruma si kwa sababu wanazaliwa nazo kama wanasayansi wengi wanavyodai, bali kwa sababu wasichana na wanawake hulelewa kijamii kuzingatia hisia zao na kutanguliza mahitaji ya wengine tangu wakiwa wadogo.
Wasichana pia mara nyingi hupewa vitu za kuchezea kama mwanasesere wanazozitumia kujifunza malezi, ilhali wavulana huhamasishwa kucheza na vifaa vya kazi na magari ya kuchezea.
"Wasichana wadogo huambiwa wawe wema na wasiwe wakorofi, na baada ya muda, hiyo inakuwa sehemu ya utambulisho wao," anasema Gina Rippon mtaalam wa sayansi ya neva.
Katika kitabu cha Breadwinners, kinaeleza hoja kuwa kihistoria wanaume wamekuwa na mamlaka zaidi kuliko wanawake na bado wanaendelea kuwa nayo katika biashara na siasa, na hii huchangia wao kuwa na kiwango cha chini cha huruma.
Kwa upande mwingine, watu wasio na uwezo mkubwa kifedha huonekana kuweza kugundua haraka hisia za wengine.
Utafiti mmoja uligundua kuwa watu waliojihisi kuwa na "hadhi ya chini kijamii, kipato cha chini au wanaotoka tabaka la chini" wanauwezo wa kugundua haraka hisia za watu wengine.
Huruma ni hulka ambayo hubadilika
Huruma ni hisia mtu anaweza kujifunza kulingana na Nathan Spreng, daktari wa magonjwa ya neva katika chuo kikuu cha McGill, Canada.
"Mara tunapoelewa wazo hili la kihisia, tunaweza kulizingatia na kujifunza hisia za watu wengine, na kuboresha viwango vyetu vya huruma," alisema Spreng kwenye chapisho la BBC la The Documentary Podcast.

Chanzo cha picha, Alamy/ Javier Hirschfeld/ BBC
Utafiti mmoja uligundua kuwa wanawake waliwashinda wanaume katika kubaini hisia za mtu mwingine.
Madhara ya kuwa na huruma
Wanawake mara nyingi huhukumiwa kwa kuwa na uwezekano mdogo wa kuwa viongozi kuliko wanaume, kwa sababu viongozi huonekana kama watu walio na mamlaka, uthubutu na msimamo thabiti, sifa ambazo kwa kawaida huhusishwa na wanaume.
Lakini linapokuja suala la upweke, wanawake huwa na uwezekano mkubwa wa kutafuta msaada kutoka kwa mitandao ya kijamii kuliko wanaume. Kutengwa katika jamii ni sababu inayojulikana kuongeza hatari ya mtu kujitoa uhai na kiwango cha kujiua mionngoni mwa wanaume ipo juu.

Chanzo cha picha, Alamy/ Javier Hirschfeld/ BBC
Simulizi ya umuhimu wa kutambua hisia miongoni mwa wanaume na wanawake inaendelea kubadilika, ikijumuisha umuhimu wa huruma kwa wengine na majukumu ya malezi, hii ni kulingana na Niall Hanlon, mwanasosholojia kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia Dublin nchini Ireland.
"Kwa ujumla, wanaume na wavulana hulelewa kuona malezi katika mtazamo tofauti ikilinganishwa na wanawake na wasichana. Wanajiona kuwa baba lakini hawatarajii kuchukua majukumu ya malezi"
Lakini jamii tayari imebadilika na kuwa na mazingira yanayowawezesha wanaume wengi kukumbatia majukumu ya malezi na kuonyesha huruma waziwazi.
Wanaume sikuhizi hutumia muda wao mwingi na watoto wao ikilinganishwa na zamani, ingawa wanawake bado wanawajibika pakubwa kuwalea watoto.














