Duka la Pombe Saudia: Je! Mwanamfalme wa Saudia anaiondoa nchi hiyo kwenye utambulisho wa Kiislamu?

.

Chanzo cha picha, Getty images

Maelezo ya picha, Mwanamfalme wa Saudia Muhammad bin Salman

Saudi Arabia imesema itafungua duka mjini Riyadh ili kuuza pombe kwa watu maalumu wasiokuwa Waislamu kutoka nje ya nchi.

Hii itakuwa mara ya kwanza baada ya miaka 70 kwa pombe kuuzwa nchini Saudi Arabia. Wateja wa duka hili la pombe Riyadh watakuwa wafanyikazi wa kidiplomasia.

Wafanyakazi hawa wa kidiplomasia wamekuwa wakiagiza vifurushi vya pombe vilivyotiwa muhuri wa diplomasia kwa miaka mingi.

Maafisa wa Saudia wanasema duka hili litakomesha biashara haramu ya vileo. Pombe imepigwa marufuku nchini Saudi Arabia tangu 1952, wakati mtoto wa Mfalme Abdul Aziz alipompiga risasi na kumuua mwanadiplomasia wa Uingereza akiwa amelewa.

Kulingana na hati zilizoonekana na mashirika ya habari ya AFP na Reuters, duka hili jipya la pombe litakuwa katika majengo ya Kidiplomasia ya Riyadh.

Hivi sasa, kuna sheria nchini Saudi Arabia inayoadhibu kunywa au kumiliki pombe; kifungo gerezani, kuchapwa viboko hadharani na kufukuza wageni wasioidhinishwa.

Kulingana na hati mpya zinazohusiana na sera ya pombe, utawala wa Saudi unafanyia kazi sheria mpya. Chini ya sheria mpya, kiasi maalum cha pombe kitaruhusiwa kuletwa. Hii itasimamisha shughuli za pombe zisizodhibitiwa.

Kulegeza Sheria

fcv

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa miaka mingi, wafanyakazi wa kidiplomasia wamekuwa wakitumia mizigo yao wenyewe kuingiza pombe na utawala wa Saudi hauingilii suala hilo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waziri Mkuu wa Saudi Arabia na Mwanamfalme Mohammed bin Salman analegeza baadhi ya sheria. Nchi nyingine za Ghuba pia zina sera kama hiyo kuhusu pombe.

UAE na Qatar, wasio Waislamu wenye umri wa zaidi ya miaka 21 wanaruhusiwa kuuza pombe katika hoteli, vilabu na baa. Bado haijatajwa katika waraka wa Saudi Arabia ikiwa pia itafanya sawa na UAE na Qatar.

Pombe ni marufuku katika Uislamu. Saudi Arabia ilikuwa na aina fulani sheria nyepesi kuhusu pombe hadi 1952.

Lakini 1951, Mwanamfalme Mishari bin Abdul Aziz al-Saud alimpiga risasi mwanadiplomasia wa Uingereza Cyril Osman huko Jeddah. Alifanya hivyo kwenye hafla na baada ya kukataa kumtilia pombe.

Mwaka mmoja baada ya tukio hili, Mfalme Abdul Aziz alipiga marufuku kabisa pombe. Mishari alihukumiwa katika kesi hiyo ya mauaji.

Mwaka 2018, mchakato wa kutoa leseni kwa wanawake ulianzishwa kwa mara ya kwanza nchini Saudi Arabia. Juni 2018, leseni zilitolewa kwa wanawake 10 kwa mara ya kwanza.

o

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman alichukua uamuzi wa kihistoria wa kuondoa marufuku ya kuendesha gari kwa wanawake.

Kuanzia Juni 24 mwaka 2018, wanawake walionekana wakiendesha magari barabarani nchini Saudi Arabia.

Hatua hii ya kuwapa wanawake haki ya kuendesha gari inachukuliwa kama sehemu ya kampeni ya Mwanamfalme Muhammad bin Salman kuifanya nchi hiyo ya kihafidhina kuwa ya kisasa.

Licha ya hatua hizi, bado anakabiliwa na ukosoaji. Wanaharakati wa haki za wanawake wa Saudia, ambao walifanya kampeni ya wanawake kuendesha gari, wamezuiliwa na serikali ya Saudia, wakituhumiwa kuwa na uhusiano na mashirika ya nje.

Dira ya 2030 ilitangazwa 2016-17. Lengo kuu la mpango huu ni kuleta mseto wa uchumi wa Saudi Arabia kwa kupunguza utegemezi wake wa mauzo ya mafuta.

Kwa kuendeleza viwanda vingine, kukuza sekta ya utalii na kukuza viwanda binafsi ili viweze kuzalisha ajira nyingi nchini na kuipunguzia serikali mzigo.

Je! anaiondoka Saudia kwenye utambulisho wa Kiislamu?

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Mohammed bin Salman mwenye umri wa miaka 38 ndiye anaeiongoza nchi hiyo kwa miaka saba sasa.

Chini ya uongozi wake, Mwanamfalme alichukua maamuzi mengi ambayo yalisifiwa na ikasemwa anaibadilisha Saudi Arabia kutoka nchi ya kihafidhina ya Kiislamu hadi nchi ya kisasa.

Miongoni mwa mambo mengine, ameondoa marufuku ya sinema na matamasha. Wasanii wa hip-hop walialikwa. Na uliberali pia ulionekana kwenye mavazi ya wanawake.

Mfalme alipunguza majukumu kwa wanazuoni wenye msimamo mkali. Polisi wa kidini walifutwa. Pamoja na haya, Mwanamfalme pia alianzisha mazungumzo ya kuboresha uhusiano na Israel.

kk

Chanzo cha picha, Getty Images

Jarida la Marekani la The Atlantic lilimuuliza Mwanamfalme wa Saudia 2022, ikiwa anataka kuifanya Saudi Arabia kuwa ya kisasa kiasi cha kudhoofisha utambulisho wake wa Kiislamu?

Kujibu swali hili alisema, "kila nchi ulimwenguni imejengwa kwa misingi ya mitazamo na maadili tofauti. Kwa mfano, Marekani imejengwa juu ya maadili ya demokrasia, uhuru na uchumi huria.

Watu hubaki wamoja chini ya misingi hiyo. Lakini je, demokrasia zote ni nzuri? Je, demokrasia zote zinafanya kazi ipasavyo? Hakika sivyo.

"Nchi yetu imejengwa kwa misingi wa maadili ya Uislamu. Kuna tamaduni za kikabila na tamaduni za Kiarabu. Pia kuna utamaduni na imani za Saudia. Hii ni nafsi yetu. Tukiiacha nchi itaharibika.

“Swali kwetu ni jinsi ya kuifikisha Saudi Arabia kwenye njia sahihi ya maendeleo ya kisasa. Kuna maswali sawa kwa Marekani kuhusu jinsi ya kuiweka demokrasia, soko huria na uhuru kwenye njia sahihi. Swali hili ni muhimu kwa sababu wanaweza kwenda kwenye njia mbaya.

"Kwa hivyo, hatutaondoka kwenye maadili yetu kwa sababu hii ni roho yetu. Kuna misikiti mitakatifu Saudi Arabia na hakuna mtu anayeweza kuiondoa.

“Ni jukumu letu kuhakikisha misikiti hii mitakatifu inabaki na tunataka kuiweka nchi katika njia sahihi kwa watu wa Saudia na kikanda. Tunataka kuyaunganisha mambo na ulimwengu wote kwa misingi ya amani na kuishi pamoja.”

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah