Vita vya Iran vilivyochochea madai ya uongo kuhusu 'wizi wa mawingu'

f
    • Author, Marco Silva na Lamis Talebi Job
    • Nafasi, BBC Verify and BBC Arabic
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Madai yasiyo na msingi yameenea kwenye mitandao ya kijamii yakidai kuwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimevuruga kile kinachoitwa operesheni ya "wizi wa mawingu" Mashariki ya Kati.

Zaidi ya wiki moja iliyopita, mbunge wa Iraq Abdullah Khaikani alidai katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Rashid kwamba Uturuki na Iran zimekuwa zikilalamikia kile alichodai ni juhudi za Marekani za "kutawanya" na "kuiba mawingu" kwa kutumia ndege.

Bila kuwasilisha ushahidi wowote, alisema mvua zimerejea Iraq katika siku na miezi ya karibuni kwa sababu Marekani ilikuwa imeelekeza nguvu zake katika vita vya Iran na hivyo haikuwa tena na nafasi ya kufanya vitendo hivyo.

Hata hivyo, wanasayansi wanasema hakuna teknolojia inayojulikana inayoweza kuwawezesha binadamu "kuiba" mawingu.

Amer Jaberi, msemaji wa Shirika la Hali ya Hewa la Iraq, alisema madai hayo "hayana msingi wa kisayansi wala mantiki." Aliongeza kuwa hata kabla ya vita kuanza Februari 28, 2026, Iraq ilikuwa tayari imetabiriwa kupata msimu wa mvua.

Akijibu swali la BBC, Khaikani alirudia madai yake kwamba "silaha za mabadiliko ya tabianchi" zilitumiwa kwa makusudi kusababisha ukame nchini Iraq, lakini hakuwasilisha ushahidi wowote.

Mwezi Machi, mvua kubwa ilisababisha mafuriko katika mji wa Mosul nchini Iraq.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwezi Machi, mvua kubwa ilisababisha mafuriko katika mji wa Mosul nchini Iraq.

Kauli zake zinaakisi madai ambayo yamesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii katika wiki za karibuni.

Nchini Uturuki, baadhi ya watumiaji wa mitandao wamehusisha vita vya Iran na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni nchini humo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mazingira, Mipango Miji na Mabadiliko ya Tabianchi ya Uturuki, Februari 2026 ulikuwa mwezi wa Februari wenye mvua nyingi zaidi katika kipindi cha miaka 66.

Katika moja ya machapisho yaliyotazamwa zaidi ya milioni, mtumiaji mmoja wa mitandao alidai kuwa kufungwa kwa anga ya Uturuki baada ya vita kuanza kulisababisha mvua kuendelea kunyesha kwa sababu Marekani haikuweza tena "kuiba" mawingu.

Wengine pia walidai kwa uongo kuwa ukame mkubwa uliokuwa ukiikumba Iran uliisha siku tano tu baada ya Iran kushambulia maeneo ya Marekani Mashariki ya Kati.

Kaveh Madani, mkurugenzi wa Taasisi ya Maji, Mazingira na Afya ya Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa, anasema ''sehemu kubwa ya imani hizi inatokana na kutoaminiana kwa umma na uelewa mdogo wa mzunguko wa maji na mfumo wa tabianchi''.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Watu wanaoeneza madai haya hudai chanzo cha tatizo ni mchakato unaoitwa "uchavushaji wa mawingu", ambao wanasema umetumiwa kama silaha ya kisiasa.

Uchavushaji wa mawingu ni mbinu ya kuchochea mabadiliko madogo ya hali ya hewa kwa kutumia mawingu yaliyopo ili kusaidia kuzalisha mvua au theluji zaidi.

Kwa kawaida, mbinu hiyo hutumia ndege kusambaza chembechembe kama 'silver iodide' ndani ya mawingu ili kusaidia kutengeneza matone ya maji na kusababisha mvua.

Mwaka uliopita, Iran ilipokumbwa na upungufu mkubwa wa mvua na mabwawa kukauka, mamlaka zake ziliamua kutumia mbinu hiyo katika bonde la Ziwa Urmia, ambalo lilikuwa limekauka kwa kiasi kikubwa.

Ingawa mbinu hiyo imetumika katika nchi nyingi, zikiwemo Marekani, China na Falme za Kiarabu, wanasayansi wanasema athari yake ni ndogo sana, na inaweza kuongeza mvua kwa kiwango kisichozidi asilimia 15 kutoka kwa mawingu yaliyopo tayari.

Diana Francis, mkuu wa Maabara ya Sayansi ya Mazingira na Jiografia katika Chuo Kikuu cha Khalifa, Abu Dhabi, anasema uchavushaji wa mawingu unapaswa kueleweka kama "marekebisho madogo kwa wingu lililopo tayari, si chombo cha kudhibiti hali ya hewa."

Baadhi ya wanaounga mkono nadharia ya "wizi wa mawingu" hudai kuwa uchavushaji wa mawingu katika eneo moja hunyima maeneo jirani mvua, lakini wataalamu wanasema tafiti zinaonyesha madai hayo si ya kweli.

Jeff French, profesa wa sayansi ya anga katika Chuo Kikuu cha Wyoming, anasema ushahidi uliopo unaonyesha kuwa hata kama athari hiyo ipo, ni ndogo sana kiasi kwamba haiwezi kutofautishwa na mabadiliko ya kawaida ya mvua.

Wanasayansi wanasisitiza kuwa hakuna teknolojia ya kudhibiti moja kwa moja mwelekeo au nguvu ya mifumo ya hali ya hewa.

Wanachosema kimebadilika ni athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zimeongeza uwezekano na ukali wa matukio ya hali mbaya ya hewa Mashariki ya Kati.

Wakati Iran ikikabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 60, watu wa Tehran waliomba mvua msimu uliopita.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati Iran ikikabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 60, watu wa Tehran waliomba mvua msimu uliopita.

Shughuli za binadamu, hasa uchomaji wa mafuta ya kisukuku kama makaa ya mawe, gesi na mafuta, zimechangia kupanda kwa joto duniani.

Shirika la Hali ya Hewa Duniani linasema kasi ya ongezeko la joto Mashariki ya Kati katika miongo ya karibuni imekuwa mara mbili ya wastani wa dunia.

Jopo la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi pia limeonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu yanafanya vipindi vya joto kuwa virefu na vikali zaidi, hali inayoongeza shinikizo kwa rasilimali chache za maji katika eneo hilo.

Wakati huohuo, mvua zimekuwa zisizotabirika zaidi. Hii ina maana kuwa mvua hunyesha mara chache zaidi, lakini zinaponyesha mara nyingine huwa za ghafla na kubwa kiasi cha kusababisha mafuriko ya haraka.

Israa Tarawneh, profesa wa uhandisi wa maji na mazingira katika Chuo Kikuu cha Mota nchini Jordan, anasema hali kama hiyo huongeza hofu ya umma kuhusu usalama wa maji.

Wataalamu wanasema katika mazingira kama haya, madai ya uongo kuhusu udhibiti wa tabianchi au wizi wa rasilimali za maji husambaa kwa urahisi.

Dkt Sarah Smith, mtafiti wa fizikia ya tabianchi katika Chuo Kikuu cha Oxford, anasema hali ya sintofahamu na kutokuwa na uhakika huwafanya watu kuvutiwa na nadharia za njama.

Anasema watu hujaza mapengo ya uelewa wao kwa maelezo mepesi yanayoonekana kushawishi, lakini kwa kufanya hivyo hukosa kuelewa chanzo halisi cha tatizo.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid