Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Trump anaishinikiza Uturuki kujiunga na Mkataba wa Abraham?
Rais wa Marekani Donald Trump anasema ili kufikia makubaliano na Iran, baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Uturuki, zinahitajika kujiunga na Mkataba ya Abraham.
Trump alisisitiza umuhimu wa Saudi Arabia, Qatar, Pakistan, Uturuki, Misri na Jordan kutia saini Mkataba wa Abraham.
Makubaliano ya Abraham yaliandaliwa mwishoni mwa muhula wa kwanza wa Trump ili kurekebisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na baadhi ya mataifa ya Kiarabu, na upatanishi wa Marekani.
Mikataba ya pande mbili ilitiwa saini kwa mara ya kwanza kati ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain mnamo Septemba 2020.
Kufuatia hatua hiyo, Sudan ilitangaza nia yake ya kurejesha uhusiano na Israel mnamo Oktoba 2020, lakini mchakato wa utiaji saini haukufikiwa kutokana na kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Morocco ilifuata mkondo huo mnamo Desemba 2020, na hivyo kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Israel.
Kazakhstan, ambayo imekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Israel tangu 1992, pia ilijiunga na Mkataba wa Abraham mnamo Novemba 2025.
Somaliland, ambayo Israel iliitambua rasmi kama taifa huru mwezi Desemba 2025, pia imetangaza nia yake ya kujiunga na Mkataba wa Abraham..
Israel ndio nchi pekee inayoitambua rasmi Somaliland, ambayo ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia. Hata hivyo, Somaliland inadumisha uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia na nchi nyingine kadhaa.
Makubaliano hayo yanasema nini?
Azimio la Mkataba wa Abraham, lililochapishwa kwenye tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, linasisitiza "kuhifadhi na kuimarishwa kwa amani" katika eneo la Mashariki ya Kati.
Wahusika katika makubaliano haya wanajitolea "kukuza mazungumzo ya kidini na kitamaduni" na "kukuza uhusiano wa kirafiki" kati ya nchi zilizotia saini.
Azimio hilo linasema, "Tunataka uvumilivu na heshima kwa watu wote ili kuifanya dunia hii kuwa mahali ambapo kila mtu, bila kujali rangi, imani, au kabila, anaweza kuishi kwa heshima."
Pia inasema, "Tunafuata maono ya amani, usalama, na ustawi kwa Mashariki ya Kati na dunia nzima."
Jina "Maagano ya Abraham" lilichaguliwa ili kusisitiza asili ya kawaida ya Uyahudi, Ukristo, na Uislamu, inayojulikana kama "dini za Abraham."
Nchi nyingi zilizotia saini mkataba huo ziko katika eneo ambalo dini hizo tatu zilianzia na kuenea.
Makubaliano ya Abraham yanaonekana kama muendelezo wa hatua zilizochukuliwa na Marekani kurejesha uhusiano kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu.
Baadhi ya wataalamu wanaeleza kuwa Israel na mataifa ya Kiarabu yanayoegemea dhehebu la Kisunni, yaliyotia saini Mkataba wa Abraham, yako katika ushindani wa kikanda na Iran, ambayo ina waumini wengi wa Kishia.
Athari yake ni gani?
Ingawa azimio lilichangia kufikiwa kwa Mkataba wa Abraham linazingatia ushirikiano wa kidini na kitamaduni, ushirikiano wa kisiasa pia ni kipengele muhimu cha mpango huu.
Moja ya vikwazo vikubwa vinavokabili uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu ni mtazamo wake dhidi ya Wapalestina.
Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao ulitia saini makubaliano hayo kabla ya mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023, ilisema wazi kuwa hata ikirejesha uhusiano wake na Israel lakini haiungi mkono mpango wa Israel kuchukua Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu.
Katika muktadha huo, ilisisitizwa kuwa suluhu la mataifa mawili katika suala la Israel na Palestina linapaswa kuzingatiwa.
Hata hivyo mashambulizi ya Hamas na operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza yameongeza hali ya wasiwasi kati ya Israel na majirani zake.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema kuwa kulitambua rasmi Taifa la Palestina baada ya shambulio kama hilo "itakuwa kutuza ugaidi."
Saudi Arabia, ambayo Marekani imekuwa ikishinikiza kujiunga na Mkataba wa Abraham tangu 2020, pia inajikokota katika kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kutokana na mtazamo wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Jordan, ambayo inapakana na Ukingo wa Magharibi, pia bado haijajiunga na Mkataba wa Abraham.
Hata hivyo, Jordan ilitia saini mkataba wa amani na Israel mwaka 1994.
Misri, ambayo ni jirani mwingine wa Israel, sio sehemu ya Mkataba wa Abraham.
Cairo ina mkataba tofauti wa amani na Israel, uliotiwa saini mwaka 1979.
Majirani wa kaskazini wa Israel, Lebanon na Syria, pia hawajajumuishwa katika makubaliano hayo. Sehemu za mikoa ya kusini ya nchi zote mbili zinakabiliwa na uvamizi wa Israel.