Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani haijasema lolote baada ya mkutano wa kuamua 'hatma' ya Iran

Mkutano wa Ijumaa ulifanyika katika Ikulu ya White House, katika sehemu inayotumika kushughulikia migogoro mikubwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Maambukizi 906 yanayoshukiwa kutokana na aina ya Bundibugyo ya Ebola - WHO

    Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuna visa 906 vinavyoshukiwa vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ikiwa ni pamoja na vifo 223 vinavyoshukiwa ambavyo vinachunguzwa.

    Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni anasafiri kuelekea katikati mwa mlipuko wa sasa wa Ebola - mkoa wa Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Tedros Adhanom Ghebreyesus anazuru nchi hiyo ili kuimarisha juhudi za kudhibiti kuenea kwa virusi hatari.

    Ameonya kuwa kuna changamoto nyingi - kwa sababu ni virusi adimu na hadi kufikia sasa bado hakuna chanjo na eneo lenyewe linakabiliwa na migogoro na watu wengi kuhama makazi yao, na kuchangia kueneza ugonjwa huo.

    WHO inasema uwezo wa kufanya vipimo umeimarika.

    Mlipuko wa aina adimu ya virusi vya Bundibugyo mashariki mwa nchi hiyo unatishia kulemea mamlaka za afya, huku visa vikiripotiwa pia nchini Uganda.

    Kumekuwa na visa 125 vilivyothibitishwa vya Ebola nchini DRC, ikiwa ni pamoja na vifo 17 vilivyothibitishwa huko Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, tangu mlipuko huo ulipoanza takriban miezi miwili iliyopita.

    Pia kumekuwa na visa tisa vilivyothibitishwa vya Ebola nchini Uganda, karibia vitatu kati ya hivyo chanzo chake ni DRC, na kifo kimoja. Hata hivyo, hakuna maambukizi ya jamii yaliyoripotiwa, WHO ilisema.

    Soma zaidi:

  2. Bunge Ghana lapitisha muswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja

    Bunge nchini Ghana limeidhinisha muswada mpya unaoharamisha mapenzi ya jinsia moja na uendelezaji wa shughuli za LGBTQ+.

    Kujitambulisha kama mpenzi wa jinsia moja, mtu aliyebadili jinsia au mpenzi wa jinsia zote mbili kunaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela.

    Muswada huo pia unaanzisha "wajibu wa kuripoti" vitendo vilivyopigwa marufuku kwa polisi.

    Viongozi wa kidini wamemshinikiza Rais John Dramani Mahama, ambaye bado anahitaji kuidhinisha sheria hiyo, kuimarisha sheria zinazopinga mapenzi ya jinsia moja tangu alipoingia madarakani mwaka jana.

    Marufuku hiyo imekosolewa vikali na mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch, ambayo ilisema inaweka maisha ya watu wa LGBTQ+ hatarini huku pia "ikiwahimiza raia kufuatiliana na kusemana".

    Mahusiano ya jinsia moja yamepigwa marufuku nchini Ghana chini ya sheria zilizoanzia enzi ya ukoloni wa Uingereza.

    Katika hotuba yake kwa Bunge, aliyeleta muswada huo Mchungaji John Ntim Fordjour alisema unalinda familia na maadili ya kitamaduni ya Ghana.

    Aliongeza kuwa marufuku hiyo mpya itafanya sheria zilizopo kuwa "imara zaidi, zenye kujumuisha mengi zaidi, na masharti magumu zaidi katika kukabiliana na desturi za LGBTQ+".

    Mtu yeyote anayejitambulisha kama "mshirika", wa neno la jumla linalomaanisha mfuasi wa watu wa LGBTQ+, anaweza pia kukabiliwa na kifungo jela.

    Soma zaidi:

  3. 'Muuzaji wa sumu' mtandaoni aliyekiri kusaidia wengi kujiua

    Mwanamume mmoja amekiri mashtaka 14 ya kusaidia wengine kujiua nchini Canada baada ya kuuza sumu mtandaoni.

    Kenneth Law, mwenye umri wa miaka 60, alikiri kosa hilo katika mahakama ya Ontario siku ya Ijumaa, kama sehemu ya makubaliano na waendesha mashtaka, ambao waliondoa mashtaka makubwa zaidi ya mauaji.

    Mamlaka zilisema mpishi huyo wa zamani aliuza takriban vifurushi 1,200 vya sumu kwa wateja - ambao alikutana nao katika mijadala ya kujiua mtandaoni - katika nchi 40, takriban robo ya vifurushi hivyo vikitumwa Uingereza.

    Mashtaka yote yanahusiana na waathiriwa wa Canada - lakini familia za waathiriwa wa Uingereza zimesema zimekasirika kwamba waendesha mashtaka wa Uingereza hawangemshtaki Law kuhusiana na vifo vya Waingereza 79, ambavyo mamlaka inasema vinahusiana na bidhaa alizouza eneo hilo.

    Barua kutoka Huduma ya Mashtaka ya Kifalme, iliyoonekana na BBC, ilisema Law hatakabiliwa na mashtaka nchini Uingereza kwa sababu anaweza kupinga kupelekwa kwake baada ya kupatikana na hatia ya makosa kama hayo nchini Canada.

    Law alikamatwa mnamo mwezi Mei 2023, kufuatia uchunguzi tata uliofanywa na takriban mashirika 11 ya kutekeleza sheria na kuwahusisha wachunguzi kutoka takriban nchi kumi na mbili, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Italia na Marekani.

    Kukamatwa kwake kulikuja wiki moja baada ya uchunguzi wa Times kudai alikuwa akiwauzia vijana sumu, baada ya mwandishi wa habari kujifanya mteja na kuzungumza na Law moja kwa moja.

    Inasemekana Law alimshauri mwandishi wa habari jinsi ya kutumia bidhaa zake ili "kuhakikisha anakufa".

    Makachero wa Canada waliiambia BBC mnamo 2023 kwamba Law aliendesha tovuti nyingi zinazotoa vifaa na sumu ili kuwasaidia watu kujiua.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Marekani haijasema lolote baada ya mkutano wa kuamua 'hatma' ya Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa na mkutano na wasaidizi wake wakuu ili kufanya "maamuzi ya mwisho" kuhusu mfumo wa kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran, lakini ulihitimishwa bila ufafanuzi kuhusu hatua zinazofuata.

    Trump alisema Iran lazima ikubali kwamba haitawahi kuwa na silaha ya nyuklia au bomu, ili Mlango-Bahari wa Hormuz ufunguliwe tena kwa ajili ya "usafiri wa meli bila vikwazo kwa pande zote mbili", na mabomu yoyote katika njia ya maji "yaharibiwe".

    Mkutano wa Ijumaa ulifanyika katika Ikulu ya White House, katika sehemu inayotumika kushughulikia migogoro mikubwa. Iran awali ilisema haikuwa ikijadili kuhusu mpango wake wa nyuklia.

    Siku ya Alhamisi, nchi hizo mbili zilikubaliana kuhusu mfumo wa makubaliano - unaojulikana kama mkataba wa makubaliano - ukisubiri idhini ya Trump na uongozi wa Iran, kulingana na maafisa wa Marekani.

    Inaripotiwa kwamba makubaliano hayo yangeongeza muda wa kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuanzisha mazungumzo kuhusu mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran.

    "Rais Trump atafanya tu makubaliano ambayo ni mazuri kwa Marekani na yanayoangazia masuala yenye kuleta utata. Iran haiwezi kamwe kumiliki silaha ya nyuklia," afisa mmoja wa Ikulu ya White House aliambia CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani.

    Tangu kuanzishwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano tarehe 8 Aprili, Trump amependekeza mara kwa mara kwamba Marekani na Iran ziko karibu kufikia makubaliano na mazungumzo yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna matokeo yoyote ya msingi yaliyopatikana.

    Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii mapema Ijumaa, Trump alisema alikuwa tayari kuondoa kizuizi cha Marekani kwenye utumiaji wa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kuruhusu meli zilizokamatwa kwenye njia ya maji "kuanza mchakato wa 'kuelekea nyumbani!'"

    Soma zaidi:

  5. Hujambo na karibu katika taarifa zetu mubashara kukujuza yanayoendelea duniani. Leo ni tarehe 30/05/2026.