Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mamia wakamatwa Ufaransa katika machafuko yaliyofutia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
Maelfu ya maafisa walijaribu kudhibiti ghasia huku umati wa mashabiki - baadhi wakiwasha moto mitaani- kushangilia ushindi wa PSG dhidi ya Arsenal.
Muhtasari
- Shule Kenya zahimizwa kuimarisha usalama kufuatia janga la moto shuleni
- Jenerali mstaafu wa Nigeria atekwa pamoja na mkewe kaskazini-magharibi
- Kombe la Dunia 2026: Afrika Kusini yalalamikia kucheleweshwa kwa viza ya wachezaji wake
- Israel yatangaza kudhibiti Kasri la Beaufort nchini Lebanon
- Ebola inasambaa kwa kiwango cha 'kutisha sana' DR Congo, MSF yaonya
- Kenya yathibitisha kushirikiana na Marekani katika ujenzi wa kituo cha Ebola
- Mamia wakamatwa Ufaransa katika machafuko yaliyofutia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi
Shule Kenya zahimizwa kuimarisha usalama kufuatia janga la moto Utumishi
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen amewataka wakuu wa shule na bodi za usimamizi kuchukua hatua madhubuti katika kutekeleza kanuni za usalama zilizowekwa ili kuwalinda wanafunzi.
Murkomen alisisitiza haja ya shule kuhakikisha hakuna msongamano wa wanafunzi katika mabweni na kuhakikisha kuna vifaa vya kutosha kukabiliana na hali ya dharura.
"Lazima mchukue hatua kuhakikisha kuwa mabweni yetu hayana msongamano na yana njia za dharura," alisema.
Waziri Murkomen pia alizitaka taasisi za mafunzo kuimarisha miundombinu ya ufuatiliaji, ikiwa ni pamoja na kuweka kamera za CCTV katika maeneo ya kimkakati.
"Tunahitaji kuhakikisha kuwa shule zote zimeweka i kamera za CCTV katika maeneo muhimu, hata katika chumba kikuu cha ufuatiliaji wa matukio," alisema.
Pia aliwahimiza walimu kudumisha uhusiano mzuri na wanafunzi, akisema mawasiliano ya wazi yanaweza kusaidia kutambua na kushughulikia maswala yanayoibuka kabla ya hajageuka kuwa matukio makubwa.
Maelezo zaidi:
Jenerali mstaafu wa Nigeria atekwa pamoja na mkewe kaskazini-magharibi
Afisa mkuu mstaafu wa jeshi la Nigeria na mke wake wametekwa nyara na watu wenye silaha kaskazini-magharibi mwa Nigeria, jeshi limethibitisha.
Meja Jenerali Rabe Abubakar, ambaye alikuwa na hadhi ya juu katika jeshi la Nigeria kati ya 2015 na 2017, alitekwa kutoka kwa gari lake siku ya Jumamosi alipokuwa akisafiri katika jimbo la Katsina.
Juhudi za kuwaokoa wanandoa hao na kuwasaka watekaji wao zinaendelea, msemaji wa jeshi Jenerali Michael Onoja aliambia BBC.
Tukio hilo linaangazia changamoto za kiusalama zinazokabili baadhi ya maeneo ya kaskazini-magharibi mwa Nigeria, ambapo magenge ya wahalifu yanayojulikana kama "majambazi" mara kwa mara huwateka ili kujipatia fidia, na kufanya mashambulizi katika maeneo ya vijijini.
Baadhi ya wanamgambo wa kijihadi pia wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika eneo hilo.
Kambi inayodaiwa kuwa ya wanamgambo katika jimbo la Sokoto ndiyo ililengwa na mashambulizi ya anga ya Marekani tarehe 25 Disemba mwaka jana.
Katsina imekuwa mojawapo ya majimbo yaliyoathiriwa zaidi na ghasia hizo.
Jimbo la Zamfara, ambalo linapakana na Katsina na Sokoto, limekabiliwa na ghasia kama hizokwa miaka mingi, huku baadhi ya jwakaazi wakijaribu kufanya amani na makundi yenye silaha, juhudi ambazo kwa kiasi kikubwa zimeshindwa kuleta utulivu wa kudumu.
Serikali imeongeza juhudi za kuzuia utekaji nyara, ikiwa ni pamoja na kuanzisha hatua zinazolenga kuzuia malipo ya fidia lakini, mashambulizi yameendelea.
Soma pia:
Kombe la Dunia 2026: Afrika Kusini yalalamikia kucheleweshwa kwa viza ya wachezaji wake
Waziri wa michezo wa Afrika Kusini amekerwa na tukio la kucheleweshwa kwa hati ya usafiri ya timu ya soka ya nchi hiyo kuelekea Mexico kabla ya michuano ya Kombe la Dunia .
Shirika la utangazaji la taifa SABC lilisema hali hiyo imewafanya baadhi ya wachezaji kunyimwa viza. Hakuna maelezo mengine yaliyotolewa.
Akijibu, waziri wa michezo Gayton McKenzie alisema aliambia Shirikisho la Soka la Afrika Kusini (Safa) "Nimeomba kupewa maelezo na lazima hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika na sintofahamu hii".
"Tunafanywa kuonekana kama wapumbavu," aliongeza kwenye X. Safa bado haijatoa tamko lolote kuhusiana na suala hilo.
Timu hiyo maarufu Bafana Bafana, inatarajiwaa kumenyana na Jamaica katika mechi ya kirafiki nchini Mexico siku ya Ijumaa.
Kisha watacheza mechi ya ufunguzi wa Kombe la Dunia dhidi ya Mexico, ambayo ni mwenyeji wa mashindano hayo pamoja na Marekani na Canada, tarehe 11 Juni.
Afrika Kusini ni mojawapo ya mataifa 10 ya Afrika yanayoshiriki katika Kombe la Dunia litakalojumuisha timu 48.
Pia unaweza kusoma:
Israel yatangaza kudhibiti Kasri la Beaufort nchini Lebanon
Jeshi la Israel leo (Jumapili) limetangaza kuwa limekuwa likipanua operesheni zake za ardhini kusini mwa Lebanon, baada ya kuvuka Mto Litani, na kuashiria kuwa limechukua udhibiti wa Kasri ya Beaufort.
Msemaji wa jeshi Avichai Adraee aliandika kupitia jukwaa la X kwamba majeshi ya Israel yalivuka Mto Litani na kupanua mashambulizi yao dhidi ya Hezbollah kaskazini mwa mto huo, huku operesheni zikijumuisha maeneo ya ziada.
Adraee alisema kwamba alianzisha "operesheni kubwa katika Milima ya Shaqif na eneo la Wadi Saluki siku kadhaa zilizopita," kama sehemu ya "kuimarisha udhibiti wa operesheni kusini mwa Lebanon na kuondoa tishio la moja kwa moja dhidi ya Galilee Panhandle na mji wa Metula."
Amedokeza kuwa idadi kubwa ya wanajeshi wake wameanza mashambulizi "ili kupanua safu ya mbele ya ulinzi," na kuongeza kuwa vikosi vyake vinafanya kazi "karibu na Nabatieh, ambayo ni moja ya ngome kuu za kundi la kigaidi la Hezbollah kusini mwa Lebanon, na yuko tayari kuendelea na mashambulio akilazimika kufanya hivyo."
Wakati huo huo jeshi la Israel limetangaza kuwa limeshambulia miundo mbinu ya Hezbollah katika mji wa Tiro na maeneo mengine kusini mwa Lebanon.
Soma zaidi:
Ebola inasambaa kwa kiwango cha 'kutisha sana' DR Congo, MSF yaonya
Kuenea kwa kasi kwa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumezua hali ya "wasiwasi", shirika la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) limeonya.
Akiongea wiki mbili baada ya mlipuko huo kutangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), naibu mkurugenzi wa MSF Dk Alan Gonzales alisema kamwe "kesi nyingi" hazijawahi kurekodiwa hivi karibuni.
Kauli yake inakuja wakati mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, alipotembelea mkoa wa Ituri mashariki mwa Congo - eneo lililoathiriwa zaidi - kuongoza harakati za kudhibiti virusi.
Takribani watu 246 wamefariki kutokana na ebola huku wengine zaidi ya 1,000 wakishukiwa kuwa na virusi ugonjwa huo.
Nchi jirani ya Uganda imeripoti kifo kimoja na kuthibitisha watu wameambukizwa.
"Wiki mbili baada ya kutangazwa kwa ugonjwa wa Ebola katika Mkoa wa Ituri, hali inazidi kuwa mbaya," Gonzalez alisema katika taarifa siku ya Jumamosi.
Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi.
Virusi vya Ebola kwa kawaida huwapata wanyama, hasa popo, lakini binadamu huambukizwa wakati pale watu wanapokula au kushika wanyama walioambukizwa.
Huchukua siku mbili hadi 21 kwa dalili kujitokeza. Dalili huanza ghafla na kufanana na mafua, kama vile homa, maumivu ya kichwa, na uchovu.
Maelez zaidi:
Kenya yathibitisha kushirikiana na Marekani katika ujenzi wa kituo cha Ebola
Serikali ya Kenya imethibitisha kuwa inaanzisha kituo cha karantini ya Ebola kwa ushirikiano na Marekani katika katika kambi ya kijeshi iliyopo Kaunti ya Laikipia.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Waziri wa Afya wa Kenya alisema kuanzishwa kwa kituo hicho kutaimarisha ufuatiliaji, kuwatenga walioambukizwa, na uwezo wa kukabiliana na hali ya dharura.
"Uwekezaji huu utaimarisha usalama wa afya ya Kenya kwa kuboresha uwezo wa maabara, miundombinu ya afya, ufuatiliaji wa magonjwa, mifumo ya kukabiliana na dharura, na utayari wa wafanyikazi zaidi ya tishio la sasa la Ebola," wizara ilisema.
Tangazo hilo linakuja siku kadhaa baada ya mahakama ya Kenya kuzuia kwa muda mpango ya kuanzisha kituo cha karantini cha Ebola kinachohusishwa na Marekani nchini humo, wakati ambapo kituo hicho kilitarajiwa kuanza kazi.
Chini ya makubaliano na Kenya, Marekani ilikuwa imepanga kutumia kituo hicho chenye vitanda 50 kuwatibu Wamarekani walioathiriwa na Ebola katika eneo hilo.
Soma zaidi:
Mamia wakamatwa Ufaransa katika machafuko yaliyofutia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
Zaidi ya watu 400 wamekamatwa kote nchini Ufaransa kufuatia ushindi wa Paris Saint-Germain (PSG) kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Arsenal usiku wa jana huko Budapast, Hungary.
Maelfu ya maafisa walitumwa kudhiditi machafuko yaliyotatiza huduma za mabasi, treni na reli katika mji mkuu Paris.
Polisi walirusha vitoa machozi kutawanya umati wa watu katikati mwa jiji huku baadhi yao wakijeruhiwa katika vurumai hilo
Video zilizonaswa jijini Paris na kusambazwa mitandaoni zinaonyesha miali ya moto ikizimwa, baiskeli zikiwaka barabarani na waltu waliokuwa wapiga kelele wakivunja vioo mbele ya duka moja.
Eneo maarufu la Champs-Élysées lilifurika na mashabiki muda mfupi baada ya timu ya Ufaransa kuinyuka Arsenal kupitia mikwaju ya penalti. Mapema Jumamosi kulikuwa na makabiliano kati ya polisi na mashabikii waliojitokeza kutazama fainali kwenye skrini kubwa katika uwanja wa PSG wa Parc des Princes.
Polisi wanasema magari sita, biashara kadhaa na maeneo la kuegesha mabasi yaliharibiwa wakati wa machafuko hayo..
Vurugu sawa na hizo zilishuhudiwa wakati PSG iliposhinda kombe hilo mwaka jana, ambapo sherehe za ushindi ziligeuka kuwa machafuko.
Waziri wa Mambo ya Ndani Laurent Nuñez amasema mwaka huu, mamlaka ilikuwa imejiandaa vilivyo kudhibiti tukio kama hili likijitokweza.
Karibu wa Matangazo ya moja kwa moja.