Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Dharau na kiburi' vilivyomfukuzisha Nchimbi CCM
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mohammed Kawaida, amesema aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, alionyeshwa hatua za kinidhamu baada ya kudharau maelekezo ya chama na kushindwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili.
Hii ni kauli ya kwanza kutoka kwa kiongozi wa CCM kueleza hadharani mazingira na uamuzi wa kumfukuza Nchimbi katika chama hicho.
Nchimbi alijiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais Agosti 25, 2026 na pia kutangaza kustaafu siasa na utumishi wa umma. Agosti 26, CCM ilitangaza kumfukuza uanachama kwa sababu za kinidhamu, bila kueleza kwa undani sababu zilizochukuliwa dhidi yake.
Akizungumza leo, Agosti 29, 2026, Chamwino, Dodoma, wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais, Kawaida amesema Kamati Kuu kwa kushirikiana na Halmashauri Kuu ya CCM ilikuwa imetoa maelekezo kwa Nchimbi kufika mbele ya Kamati ya Maadili.
Amesema Nchimbi hakufika mbele ya kamati hiyo, akieleza kuwa sababu zilikuwa "kiburi" na kutouona umuhimu wa kufuata maelekezo ya chama.
"Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ikishirikiana na NEC ndiyo iliyotoa maelekezo ya kiongozi aliyepita kuitwa katika Kamati ya Maadili, naye kwa sababu ya kiburi, kwa sababu ya kutouona umuhimu na kudharau maelekezo ya chama akasita kufika hapo," amesema Kawaida.
Amesema baada ya Nchimbi kushindwa kufika, Kamati Kuu pamoja na Halmashauri Kuu zilifanya uamuzi kuhusu uanachama wake.
Kawaida amesema tukio hilo linapaswa kuwa funzo kwa vijana wa CCM kuhusu umuhimu wa kuheshimu chama, Katiba, kanuni na taratibu zake.
"Lakini hili ni funzo la kwanza tunalolipata vijana kuendelea kuheshimu chama, kuheshimu Katiba, kuheshimu kanuni na taratibu za Chama cha Mapinduzi," amesema.
Amesema funzo lingine ni umuhimu wa kuwa na nidhamu, kufanya kazi kwa weledi na kuwa mtu wa kuaminika pale anapoaminiwa.
Pia kauli hiyo ya Kawaida imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani na Makamu wa Kwanza wa Rais, Joseph Warioba, kusema Nchimbi "si chawa wa aina yoyote", akieleza kuwa misimamo yake ya kisiasa ilikuwa sehemu ya kile alichoamini.
Ingawa hakumtaja yeyote kwa jina, Kawaida amesema viongozi wastaafu wanaopinga au kutoa maoni kuhusu mwenendo wa viongozi waliopo madarakani wanapaswa kuheshimiwa kutokana na nafasi walizowahi kushikilia, lakini wasiwaelekeze viongozi waliopo namna ya kutekeleza majukumu yao.
"Si kwamba hatuna kuwajibu, si kwamba hatuna hoja za kuwaambia, tunazo, lakini tunaheshimu nafasi walizotumikia katika taifa letu, tunaheshimu kazi walizozifanya katika taifa letu, tunaheshimu muda wao walioutumia katika kulitumikia taifa letu," amesema.
"Kama wao walivyoachwa kufanya kazi zao, wasitupangie na sisi watuache tufanye majukumu yetu."
Amesema CCM inaongozwa na Katiba, kanuni na taratibu zake na kwamba viongozi wake hawawezi kufuata matakwa au mawazo ya watu wengine yanapokwenda kinyume na utaratibu wa chama.