Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yaweka masharti kabla ya kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz

Marekani, kwa upande wake, inaendelea kusisitiza kuwa Mlango wa Hormuz uko wazi na kwamba mabomu ya baharini yameondolewa, huku ikisema hakuna mazungumzo yaliyopangwa kwa sasa na Iran.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Araqchi: Uwezekano wa kurejea kwenye mkondo wa diplomasia ungalipo

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anasema uwezekano wa "kurejea katika mazungumzo ya kidiplomasia upo, lakini Marekani inastahili kuelewa kwamba kutumia nguvu hakufanyi kazi."

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, Abbas Araqchi alielezea mazungumzo yake na Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, kuwa yenye "tija," na kusema: "Shinikizo halifanyi kazi.

    Marekani lazima ijenge imani, izungumze kwa heshima, itambue haki za Iran, na itimize ahadi zake."

    Waziri Mkuu wa Qatar alisafiri hadi Tehran jana akiongoza ujumbe, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi ya juu, akiwemo Masoud Pezeshkian na Mohammad Baqer Qalibaf, Rais na Spika wa Bunge la Iran.

    Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ilisema kuwa mkutano huo ulijadili "hali ya hivi karibuni katika eneo hilo" na "kuandaa mazingira mwafaka ya mazungumzo yatakayosaidia kuimarisha usalama na utulivu katika eneo hilo."

    Maelezo zaidi:

  2. Saudi Arabia yawakamata makumi ya Waethiopia kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya

    Mamlaka ya Saudi Arabia imewakamata takribani raia 60 wa Ethiopia mwezi huu kwa tuhuma zinazohusiana na dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kusafirisha mirungi, bashish, na vidonge vilivyodhibitiwa.

    Mnamo Agosti 27, Jumatano, maafisa waliripoti kukamatwa kwa Waethiopia 15 wakiwa wamebeba kilo 290 za mirungi.

    Kurugenzi Kuu ya Walinzi wa Mipaka ya Saudi Arabia ilisema watu wengine 12 walikamatwa katika operesheni tatu tofauti katika majimbo ya Jazan na Asir, kwa mujibu wa Gazeti la Saudi Arabia.

    Al-Riyadh iliripoti kwamba wengine watatu walikamatwa katika jimbo la Riyadh wakiwa na vidonge 29,430.

    Mamlaka zilisema washukiwa wamekamilisha "michakato ya awali ya kisheria" na kukabidhiwa kwa mamlaka husika, huku wengine wakipelekwa katika ofisi ya mwendesha mashtaka.

    Kukamatwa huku kunakuja huku Saudi Arabia ikiendelea kutoa adhabu ya kifo kwa hatia zinazohusiana na dawa za kulevya.

    Human Rights Watch iliripoti mnamo Julai kwamba takribani Waethiopia 17 walikuwa wamenyongwa tangu Januari, huku mauaji yakifanywa kwa siku tofauti mwezi Juni na Julai.

    Vyanzo viliiambia BBC kwamba takriban Waethiopia 200 kwa sasa wako kwenye foleni ya kifo.

    Kulingana na vyombo vya habari vya Saudi Arabia, Waethiopia waliokamatwa katika operesheni za hivi karibuni wanatuhumiwa kwa kujaribu kuingiza kilo 290 za mirungi, kilo 33 za bangi, na zaidi ya vidonge 72,000 vya bangi vilivyodhibitiwa nchini.

    Bado haijulikani ni adhabu gani wafungwa hao watakabiliwa nazo. Hata hivyo, data rasmi inaonyesha kwamba kati ya watu 365 waliouawa nchini Saudi Arabia mwaka jana, asilimia 68 kati yao walihukumiwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

    Makundi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch na Amnesty International yamelaani matumizi ya adhabu ya kifo kwa Saudi Arabia, hasa kwa makosa yasiyo ya kuua ya dawa za kulevya, na kuhoji haki ya mchakato wa kisheria.

    Soma:

  3. Mfalme wa Norway aaga dunia

    Mfalme wa Norway, Harald V, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 89, baada ya kulazwa hospitalini wiki iliyopita. Mfalme huyo alikuwa anaugua ugonjwa adimu wa damu.

    Ikulu ya mfalme mjini Oslo imesema alifariki kwa amani mwendo wa saa kumi na mbili na nusu za asubuhi hii leo, katika hospitali ya taifa mjini Oslo. Bendera ya kifalme ya ikulu imeshushwa hadi nusu mlingoti.

    Nafasi yake imechukuliwa na mwanawe Haakon mwenye umri wa miaka 53.

    Baada ya miaka 35 kwenye kiti cha ufalme, Harald atakumbukwa kama mfalme aliyependwa na aliyefanya mageuzi makubwa, kwa kufanya taasisi ya kifalme kuwa ya kisasa, akavunja mila za kifalme kwa kumuoa mtu wa kawaida, na kuwa mtu wa kuwaunganisha wananchi wakati wa nyakati ngumu nchini Norway.

    Soma pia:

  4. Sudan yaondoa amri ya kutotoka nje usiku na hali ya dharura Khartoum

    Mamlaka nchini Sudan, zimeondoa amri ya kutotoka nje usiku, iliyodumu kwa miaka miwili na kumaliza hali ya dharura katika mji mkuu wa Khartoum.

    Kamati ya Usalama ya Jimbo la Khartoum imesema wakazi wa mji huo sasa watakuwa huru kusafiri na kufanya kazi wakati wowote, ingawa polisi wataendelea kushika doria na vituo vya ukaguzi vitaendelea kuwepo.

    Amri hiyo ya kutotoka nje iliwekwa mwezi Mei mwaka wa 2024, ikizuia watu kusafiri kati ya saa kumi na moja jioni hadi saa kumi na moja alfajiri, huku pia ikiweka vikwazo kwa baadhi ya shughuli za biashara na shughuli nyingine.

    Mamlaka pia zimeweka vikwazo vipya kwa wageni wanaoingia katika Jimbo la Khartoum. Chini ya kanuni hizo mpya, wageni wanaosafiri kwa mabasi ya masafa marefu, magari ya umma au binafsi, au treni wataruhusiwa kuingia katika jimbo hilo ikiwa tu wana vibali halali vya kuingia au vibali vinavyohitajika.

    Mabadiliko hayo yanakuja wakati mamlaka za Sudan zinajaribu kurejesha maisha ya kawaida mjini Khartoum, mji ambao uliharibiwa vibaya wakati wa mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF).

    Serikali kuu ya Sudan imekuwa ikirejesha taasisi za serikali katika mji mkuu, baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa mji huo.

    Hata hivyo, mapigano kati ya jeshi na RSF bado yanaendelea katika maeneo kadhaa, ikiwemo majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kaskazini, hali ambayo imesababisha watu wengi kuyahama makazi yao.

    Soma pia:

  5. Spika wa bunge apokea jina la Makamu wa Rais mteule

    Sasa ni zamu ya Bunge la Tanzania kuamua kuhusu jina la Makamu wa Rais mteule, Deogratius John Ndejembi.

    Spika wa Bunge, Mussa Zungu, leo amepokea rasmi jina la Ndejembi lililopendekezwa na Chama cha Mapinduzi, CCM, kwa ajili ya kuwasilishwa kwa wabunge.

    Jina hilo limewasilishwa na Katibu wa Rais, Balozi Ali Jabir Mwadini, akiwa ameambatana na Mpambe wa Rais, ADC, Brigedia Jenerali Nyamburi Mashauri.

    Baada ya kupokelewa kwa jina hilo, hatua inayofuata ni kura ya wabunge, ambao wataamua iwapo Ndejembi anafaa kuidhinishwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

    Ndejembi alipokelewa kwa shangwe na wabunge alipowasili bungeni.

    Bunge linatarajiwa kumpigia kura leo, katika hatua muhimu kuelekea kujaza nafasi hiyo baada ya kujiuzulu kwa Emmanuel Nchimbi.

  6. Kiongozi wa upinzani Zambia, Brian Mundubile anazuiliwa na polisi

    Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, ambaye amekuwa mafichoni baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa urais, amekamatwa kwa tuhuma za uhaini.

    Katika uchaguzi uliofanyika tarehe 13 mwezi Agosti, Rais Hakainde Hichilema alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata asilimia 60 ya kura zilizopigwa dhidi ya asilimia 38 alizopata Mundubile.

    Siku moja baada ya uchaguzi huo, vikosi vya usalama vilivamia nyumba moja katika mji mkuu, Lusaka, inayohusishwa na Mundubile. Katika uvamizi huo, waziri mmoja wa zamani wa serikali aliuawa na wanasiasa wengine kadhaa walikamatwa.

    Mamlaka ziliishtumu upinzani kwa kupanga uasi na kutaka kuipindua serikali, madai ambayo upinzani umekanusha.

    Mundubile na naibu wake Zulu walikuwa wamejificha katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Lusaka.

    Wawili hao wamekamatwa baada ya Rais Hakainde Hichilema kuishinikiza Umoja wa Mataifa kuwakabidhi kwa mamlaka za Zambia.

    Hapo jana, shirika la habari la taifa la Zambia,ZNBC, liliripoti kuwa wawili hao walikuwa wakihojiwa na maafisa wa usalama wakiwa na mawakili wao, baada ya polisi kudai kuwa, walikuwa wanajishughulisha na shughuli zinazoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

    Soma pia:

  7. Congo yaanza kutoa chanjo dhidi ya Ebola

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza kutoa chanjo dhidi ya Ebola, katika juhudi za kudhibiti mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa huo kuwahi kurekodiwa nchini humo.

    Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi mjini Kisangani, makao makuu ya mkoa wa Tshopo, mashariki mwa nchi.

    Wahudumu wa afya na watu wengine walio mstari wa mbele katika kukabiliana na Ebola ni miongoni mwa watakaopewa chanjo kwanza.

    Waziri wa Afya, Roger Kamba, amesema chanjo ya Ervebo itatolewa kwanza kwa wahudumu wa afya pamoja na watu waliowasiliana na wagonjwa.

    Mlipuko huo umeenea katika mikoa sita, huku takwimu za serikali zikionyesha kuwa hadi Jumanne kulikuwa na visa 5,713 vilivyothibitishwa na vifo 2,744.

    Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema mlipuko huo bado haujadhibitiwa na huenda ukazidi ukubwa wa mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016, uliosababisha zaidi ya vifo 11,000.

    Hata hivyo, kuna changamoto kuhusu chanjo hiyo. Ebola inayosababisha mlipuko wa sasa ni aina ya Bundibugyo, wakati Ervebo imeidhinishwa dhidi ya aina nyingine, Zaire ebolavirus.

    Kwa sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa mahsusi dhidi ya Ebola ya Bundibugyo. Chanjo ya Ervebo inatumika chini ya mpango wa matumizi ya huruma, huku wataalamu wakikusanya data ili kubaini iwapo inaweza kutoa kinga dhidi ya aina hiyo ya virusi.

    Kampeni hiyo inatarajiwa kuwafikia watu katika maeneo 14 ya afya katika mikoa ya Tshopo, Bas Uele na Haut Uele.

    Soma Pia:

  8. Trump aagiza Ziwa Ontario kuitwa Ziwa Amerika

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo la kiutendaji linalolenga kubadili jina la Ziwa Ontario na kuliita Ziwa Amerika.

    Hatua hiyo inakuja baada ya mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na Canada kuvunjika wiki iliyopita, huku Marekani ikiweka ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa za Canada zenye thamani ya dola bilioni 20.

    Trump amekuwa akitishia mara kadhaa kubadili jina la ziwa hilo, ambalo ni miongoni mwa maziwa makuu matano yanayopatikana katika eneo la Marekani na Canada.

    Kwa mujibu wa agizo hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani imepewa siku 30 kusasisha jina hilo katika hifadhidata rasmi ya majina ya maeneo ya kijiografia nchini humo.

    Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, amepinga hatua hiyo, akisema jina Ziwa Ontario lina historia ya zaidi ya miaka 400.

    Carney amesema ziwa hilo linaitwa Ontario na litaendelea kuitwa hivyo.

    Hii si mara ya kwanza kwa Trump kujaribu kubadili jina la eneo linaloshirikisha nchi nyingine. Mwaka 2025, alisaini agizo la kubadili jina la Ghuba ya Mexico kuwa Ghuba ya America, hatua ambayo Mexico imeikataa.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Vyombo vya habari Marekani: Mkuu wa CIA aishinikiza Urusi kutoshirikisha Iran taarifa za kijasusi

    Vyanzo vilivyo na ufahamu kuhusu suala hilo vimeviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, John Ratcliffe, aliiomba idara za ujasusi za Urusi kutoshirikisha Tehran taarifa ambazo zinaweza kuisaidia Iran, wakati wa ziara yake ya siri mjini Moscow.

    Inadaiwa pia kuwa suala la msaada wa Urusi kwa Iran lilikuwa miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa katika mazungumzo yake na maafisa wa Urusi.

    Ziara hiyo ni ya kwanza kwa mkuu wa CIA kwenda Moscow ambayo imefahamika hadharani tangu mwaka 2021. Kremlin imethibitisha kuwa Ratcliffe alikutana na maafisa wa ujasusi wa Urusi, lakini si Rais Vladimir Putin.

    Mbali na suala la Iran, Ratcliffe anaripotiwa kujadili pia wasiwasi wa Marekani kuhusu usalama wa wanachama wa NATO katika mazungumzo hayo.

    Hata hivyo, Marekani na Urusi hazijatoa maelezo rasmi kuhusu yaliyomo katika mazungumzo hayo, huku CIA ikikataa kutoa maoni kuhusu ziara hiyo.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, aliielezea ziara hiyo kuwa ya "kawaida kwa kiasi" na kusema mawasiliano hayo yanaweza kusaidia kusukuma mbele baadhi ya masuala, likiwemo suala la kumaliza vita nchini Ukraine. Hakutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo hayo.

    Ripoti kuhusu msaada wa kijasusi kutoka China na Urusi kwa Iran wakati wa vita kati ya Marekani, Israel na Iran zimeibuliwa mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni.

    Moscow nayo imekuwa ikiishutumu Marekani na washirika wake wa Ulaya kwa kuipatia Ukraine taarifa za kijasusi na imekuwa ikiitaka Washington kusitisha msaada huo.

    Maelezo zaidi:

  10. Idadi ya watu waliofariki Nepal na Tibet yafikia 469 huku kukiwa na hofu ya mafuriko zaidi

    Takriban watu 469 wamefariki dunia nchini Nepal na mamia hawajulikani walipo baada ya mafuriko makubwa ya ghafla yaliyokumba eneo la milimani mpakani mwa Nepal na Tibet Jumatano.

    Nchini Tibet, watu watatu wamefariki na zaidi ya 550 hawajulikani walipo. Haijafahamika iwapo baadhi ya watu hao wamehesabiwa pia katika takwimu za Nepal.

    Waokoaji wanaendelea kuwasaka manusura, lakini wanakabiliwa na hofu ya kutokea kwa mafuriko mengine katika eneo lililoharibiwa.

    Shirika la Msalaba Mwekundu limeiambia BBC kuwa waokoaji wako katika hali ya tahadhari kutokana na ripoti kwamba wimbi jingine la mafuriko linaweza kulikumba eneo hilo.

    Ziwa lenye maji yanayoongezeka limejitokeza karibu na mpaka wa China na Nepal, hali inayozua hofu kwamba huenda kingo zake zikapasuka na kusababisha mafuriko mengine.

    Maafisa wa eneo hilo wameiambia BBC kuwa kuporomoka kwa barafu ya mlima kulisababisha wimbi kubwa la maji lililosomba nyumba na barabara, pamoja na kuharibu kituo muhimu cha mpakani kinachounganisha Nepal na Tibet.

    Eneo hilo hutembelewa na makumi ya maelfu ya watalii kila mwaka.

    BBC imezungumza na ndugu za baadhi ya watu ambao bado hawajulikani walipo.

    Dada wawili ambao wazazi wao hawajulikani walipo wameeleza matumaini yao ya kuwaona tena, wakisema: "Tunawapenda sana na tunataka warudi nyumbani."

    Soma Zaidi hapa:

  11. Iran yaweka masharti kabla ya kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz

    Mkuu wa usalama wa Iran, Mohsen Rezaei, amesema Tehran inaandaa orodha ya masharti ambayo Marekani inapaswa kutimiza kabla ya Iran kuruhusu tena usafirishaji kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia maombi kutoka kwa wapatanishi wanaojaribu kupunguza mvutano kati ya Iran na Marekani.

    Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema utawala wa Rais Donald Trump unafanya maamuzi yasiyo sahihi kwa kutegemea taarifa potofu.

    Ghalibaf amesema Washington lazima itekeleze ahadi zake chini ya MOU kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

    Waziri Mkuu wa Qatar yuko Tehran katika juhudi za upatanishi, huku akijadili pamoja na viongozi wa Iran masuala muhimu, likiwemo suala la Mlango wa Hormuz na uwezekano wa kuanza tena kwa mazungumzo kati ya Tehran na Washington.

    Marekani, hata hivyo, inaendelea kusisitiza kuwa Mlango wa Hormuz uko wazi na kwamba mabomu ya baharini yameondolewa, huku ikisema hakuna mazungumzo yaliyopangwa kwa sasa na Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  12. Hujambo, natumai umzima na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya leo Ijumaa.