Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Moja kwa moja, Marekani yachukua udhibiti wa mapipa ya mafuta nchini Venezuela
Rais wa Marekani Donald Trump, ametangaza kuwa Marekani imefikia makubaliano na Venezuela ya kudhibiti zaidi ya mapipa bilioni 65 ya mafuta nchini humo.
Muhtasari
- Mke wa Besigye aomba aruhusiwe kumpeleka mumewe Geneva kwa matibabu
- Raia wawili wa Nigeria wapelekwa Marekani kujibu mashtaka ya uhalifu wa mtandaoni
- Watu 27 wafariki katika shambulio la Urusi mjini Kyiv
- Zaidi ya watu 600 wameaga dunia kutokana na mafuriko yaliyotokea Nepal - Tibet
- Niger: Uwanja mkuu wa ndege walengwa huku milio ya risasi ikiripotiwa mjini Niamey
- Ndejembi kuapishwa rasmi kuwa Makamu mpya wa Rais nchini Tanzania
- Iran yalaani vikwazo vya kiuchumi vya Marekani, huku uchumi wa taifa hilo ukiendelea kudorora
- Marekani yachukua udhibiti wa mapipa ya mafuta ya Venezuela
Moja kwa moja
Na Beldeen Waliaula
Mke wa Besigye aomba aruhusiwe kumpeleka mumewe Geneva kwa matibabu
Winnie Byanyima, mke wa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Dkt. Kizza Besigye, ametoa wito kwa mamlaka za Uganda kumruhusu mumewe kusafiri kwenda Geneva, Uswizi, kwa ajili ya kupata matibabu maalumu.
Byanyima ametoa ombi hilo baada ya kusemakana kuwa Besigye alihamishwa kutoka Gereza la Luzira na kupelekwa katika Hospitali ya Joint Clinical Research Centre (JCRC) jana usiku, hali yake ya afya ikiwa dhaifu.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X, Byanyima alisema hali ya afya ya Besigye inaendelea kudorora, huku akipata ugumu kufanya shughuli za kawaida.
“Baada ya giza kuingia, Dkt. Kizza Besigye alihamishwa kutoka Gereza la Luzira na kupelekwa Hospitali ya JCRC . Bado ni mdhaifu sana. Anapata shida kutembea, kuzungumza, kuandika au hata kushikilia kitu kwa uthabiti,” aliandika Byanyima
Byanyima amezitaka mamlaka kumruhusu kumpeleka Besigye Geneva, ambako amesema anaweza kupata matibabu yanayofaa akijumuika na familia yake.
“Ninaomba jambo moja tu mruhusu nimpeleke Geneva kwa ajili ya kupata matibabu yanayofaa, akiwa amezungukwa na familia yake.”
Besigye amekuwa kizuizini tangu alipokamatwa mwezi Novemba mwaka wa 2024 nchini Kenya na anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Hali yake ya afya ilizorota mwezi Julai baada ya kuanguka wakati wa kesi yake ilikuwa inasikilizwa katika Mahakama moja mjini Kampala.
Soma pia:
Raia wawili wa Nigeria wapelekwa Marekani kujibu mashtaka ya uhalifu wa mtandaoni
Wanaume wawili kutoka Nigeria wamesafirishwa hadi nchini Marekani, kujibu mashtaka ya ulaghai wa kingono mtandaoni, katika sakata inayohusisha kifo cha kijana mmoja wa Marekani, kulingana na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X ,kwamba wanaume hao raia wa Nigeria, walikamatwa baada ya uchunguzi kufanywa.
Shirika la Nigeria la Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kifedha (EFCC) liliwataja wanaume hao wawili kuwa Mudashiru Afeez Olawale na Adebola Festus Adekunle.
EFCC ilisema wawili hao walikabidhiwa kwa mamlaka za Marekani kufuatia uchunguzi wa FBI kuhusu madai ya kuwalaghai watoto.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X, shirika hilo lilisema washukiwa hao wanadaiwa kuwalenga wavulana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 17, wakitumia picha zao za uchi kuwalazimisha kutoa pesa kupitia kadi za zawadi, kuwatumia kwa benki na sarafu za kidijitali.
Kwa mujibu wa EFCC, kesi moja ilihusisha mvulana mwenye umri wa miaka 13 ambaye aliwasiliana na wawili hao kwenye mtandao wa Instagram na kubadilishana picha za uchi.
Shirika hilo lilisema baadaye mvulana huyo alitishiwa kuwa picha hizo zitasambazwa kwa watu wake wa karibu iwapo hangewatumia pesa.
“Vitisho hivyo viliendelea hata baada ya kijana huyo kusema kwamba alikuwa na nia ya kujiua,” EFCC ilisema.
Mitandao hiyo ya kuwalaghai watoto kwa kuwatishia kuvujisha picha zao za uchi zilichochea kifo cha mtoto mmoja, na uchunguzi ukapelekea kukamatwa kwa raia hao wawili wa Nigeria.
Soma pia:
Watu 27 wafariki katika shambulio la Urusi mjini Kyiv
Takriban watu 27 wameuawa baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani ya Urusi kushambulia ghala moja mjini Kyiv, nchini Ukraine.
Watu wengine 42 wamejeruhiwa, huku zaidi ya 380 wakihamishwa kutoka eneo lililoshambuliwa katika wilaya ya Bucha.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa shambulio hilo dhidi ya ghala lilisababisha mlipuko, huku miundombinu iliyoko karibu ikiharibiwa, ikiwemo majengo ya makazi ya watu na kituo kinachotoa huduma ya uangalizi kwa wazee.
Soma pia:
Zaidi ya watu 600 wameaga dunia kutokana na mafuriko yaliyotokea Nepal - Tibet
Operesheni ya kuwatafuta manusura wa mafuriko nchini Nepal, imeingia siku ya nne baada ya mafuriko hayo kusababisha maafa katika mpaka wa Nepal na Tibet siku ya Jumatano.
Idadi ya waliofariki nchini Nepal imeongezeka na kufikia watu 626, kwa mujibu wa mamlaka za taifa hilo.
Watu 2,426 wanaripotiwa kutojulikana walipo.
Katika eneo la Tibet, idadi rasmi ya waliofariki imefikia saba, huku watu 554 wakiripotiwa kutojulikana walipo kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China.
Kupata taarifa kutoka Tibet imekuwa vigumu, lakini China sasa imetoa baadhi ya picha za tukio hilo.
Nchini Nepal, angalau raia 517 wa kigeni wameripotiwa kutoweka, wakiwemo mahujaji na watalii waliokuwa wakifanya safari za milimani.
Waziri wa Fedha wa Nepal amekadiria kuwa nchi hiyo itahitaji kati ya dola bilioni 4 au 5, kwa ajili ya kujenga upya taifa hilo baada ya mafuriko hayo makubwa.
“Haya ni makadirio tu. Tathmini ya hasara na uharibifu bado inaendelea,” Swarnim Wagle aliiambia shirika la habari la Reuters.
Soma pia:
Niger: Uwanja mkuu wa ndege walengwa huku milio ya risasi ikiripotiwa mjini Niamey
Milio ya risasi na milipuko imeripotiwa katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Niger, Niamey, karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa, na kambi ya kijeshi iliyo karibu na ikulu ya rais.
Chanzo kimoja kimeiambia shirika la habari la Reuters kwamba washambuliaji walilenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani na kujaribu kuvuka ukuta unaozunguka ikulu ya rais.
Inasemekana vikosi vya usalama vimefanikiwa kurejesha udhibiti wa Kambi ya Anga ya 101, iliyoko karibu na uwanja wa ndege, ingawa taarifa hiyo haijathibitishwa.
Serikali ya Niger bado haijatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo, na hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo. Bado haijulikani ni nani waliotekeleza shambulio hilo au iwapo kuna watu waliojeruhiwa au kuuawa.
Uwanja huo wa ndege na maeneo ya kijeshi yaliyo karibu, tayari yamelengwa mara mbili mwaka huu na makundi yenye itikadi kali.
Wanamgambo wa Islamic State walishambulia eneo hilo mwezi Januari, huku kundi la JNIM lenye uhusiano na al-Qaeda likitekeleza shambulio jingine mwezi Juni.
Jeshi lilichukua mamlaka nchini Niger mwaka wa 2023, na kuipundua serikali ya kiraia iliyokuwepo, na kuahidi kukabiliana na uasi ambao ulikuwa umeongezeka nchini humo.
Mamlaka za kijeshi nchini Niger zimewataka wananchi katika mji mkuu, Niamey, kuwa watulivu baada ya milio ya risasi na milipuko kuripotiwa katika maeneo kadhaa ya mji huo.
Soma pia:
Ndejembi aapishwa rasmi kuwa Makamu mpya wa Rais nchini Tanzania
Deogratius John Ndejembi,ameapishwa rasmi kuwa Makamu mpya wa rais nchini Tanzania, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi.
"Usiwe samaki, mwanetu nenda ukakue, tumekupa majukumu makubwa na ni imani yangu utaweza" alisema Rais Samia Suluhu akimpongeza makamu huyo mpya.
Hafla hiyo ya uapisho imefanyika katika ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Ndejembi mwenye umri wa miaka 43, atakuwa Makamu wa rais wa 13 tangu Tanzania ipate uhuru, akiwa miongoni mwa Makamu wa rais vijana zaidi kuwahi kushika nafasi hiyo.
Soma pia:
Iran yalaani vikwazo vya kiuchumi vya Marekani, huku uchumi wa taifa hilo ukiendelea kudorora
Iran imelaani vikwazo vipya vya kiuchumi villivyotangazwa na Marekani, ikiviita 'ugaidi dhidi ya serikali yake' huku Kiongozi Mkuu wa Iran akipiga marufuku vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri 'mshikamano wa kijamii.'
Kuna hofu kuwa kuongezeka kwa changamoto za kifedha kunaweza kusababisha machafuko nchini humo.
Vita vya Marekani na Iran sasa vimetimiza miezi sita, huku mazungumzo ya kutafuta suluhu yakiwa yamekwama.
Utawala wa Rais Donald Trump umeongeza juhudi za kuiadhibu Iran kifedha kupitia mpango uliouita “ Economic D-Day.” Vikwazo hivyo vinaongeza madhara ya vita kwa uchumi wa Iran, ambako mfumuko wa bei umefikia asilimia 66 mwezi uliopita.
Washington imeonya nchi mbalimbali zipunguze uhusiano wao wa kibiashara na Iran au zikabiliwe na vikwazo vya kiuchumi, ingawa Wizara ya Fedha ya Marekani bado haijatekeleza adhabu hizo.
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Iran imesema katika taarifa iliyotolewa hapo jana kuwa nchi zote zina wajibu chini ya sheria za kimataifa kukataa kutekeleza vikwazo vya Marekani dhidi ya Tehran.
Iran imetaja hatua mpya za Marekani kuwa “uhalifu dhidi ya ubinadamu”, ikisema zinaweka afya na maisha ya mamilioni ya raia katika hatari kubwa.
Soma pia:
Marekani yachukuckua udhibiti wa mafuta ya Venezuela
Rais wa Marekani Donald Trump, ametangaza kuwa Marekani imefikia makubaliano na Venezuela ya kudhibiti zaidi ya mapipa bilioni 65 ya mafuta nchini humo.
“Makubaliano haya ya kihistoria yatazidisha zaidi ya mara mbili akiba ya mafuta ya Marekani, utaongeza kwa kiasi kikubwa usambazaji wetu wa mafuta na kupunguza bei ya petroli kwa Wamarekani wote,” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii.
Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez, amepongeza makubaliano hayo, akisema yatasaidia kufufua uchumi wa taifa lake.
Trump alikuwa ameahidi kutumia akiba ya mafuta ya Venezuela, ambayo ni kubwa zaidi duniani, baada ya Marekani kumkamata rais wa taifa hilo Nicolás Maduro, mapema mwaka huu.
Hivi karibuni, Trump amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kupunguza bei za mafuta nchini Marekani, ambazo zimepanda kutokana na mzozo wa Iran.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, alitaja makubaliano hayo ya mafuta kuwa “ushindi mkubwa kwa wananchi wa Marekani na Venezuela.” Hata hivyo, maelezo machache kuhusu makubaliano hayo yametolewa.
“Kwa wananchi wa Venezuela, makubaliano haya yataleta karibu dola bilioni 100 za uwekezaji kutoka sekta binafsi, na kutengeneza ajira zenye mishahara mizuri na kuimarisha uchumi wa Venezuela,” Rubio alichapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Maelezo zaidi kuhusu makubaliano hayo hayajatolewa. Trump alidai kuwa makubaliano hayo yalifikiwa “bila gharama yoyote kwa walipa kodi wa Marekani.”
Soma pia:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumamosi ya leo