Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nani kumrithi Gianni Infantino ikiwa ataondoka FIFA?
Inaonekana shinikizo linaendelea kuongezeka dhidi ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino.
Raia huyo wa Uswisi amejikuta katika wakati mgumu baada ya kufuta mpango wake wenye utata wa kuuza sehemu ya hisa za mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi.
Kwa sasa, Infantino bado anatarajiwa kugombea tena urais wa FIFA mwezi Machi 2027, akilenga muhula wa nne na wa mwisho wa uongozi wake.
Ili ashinde uchaguzi huo, atahitaji kupata angalau kura 106 kati ya wanachama 211 wa FIFA.
Hata hivyo, mashirikisho kadhaa ya soka ya kitaifa, yakiwemo yale ya England na Wales, tayari yameanza kuondoa barua zao za kumuunga mkono kugombea tena.
Aidha, kuna uwezekano kwamba Baraza la FIFA linaweza kuitisha kikao cha dharura na kujaribu kumlazimisha Infantino kujiuzulu.
Iwapo huu utakuwa mwanzo wa mwisho wa uongozi wake, swali kubwa linalobaki ni nani atakayekuwa na nafasi ya kumrithi katika kiti cha urais wa FIFA.
Victor Montagliani
Victor Montagliani ni rais wa Concacaf, shirikisho linalosimamia soka Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati na Karibiani.
Kama ilivyokuwa kwa Gianni Infantino, Montagliani alichaguliwa mwaka 2016 akiwa na ahadi ya kuimarisha utawala bora na kufanya mageuzi ndani ya soka.
Akiwa rais wa zamani wa Canada Soccer, alichangia kwa kiasi kikubwa maandalizi na uandaaji wa Kombe la Dunia la 2026, ambalo kwa mara ya kwanza linaandaliwa kwa pamoja na nchi tatu: Canada, Marekani na Mexico.
Montagliani anazungumza kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kiitaliano na Kihispania.
Akieleza sababu za kugombea urais wa Concacaf, aliwahi kusema katika mahojiano na tovuti ya BC Business:
"Mimi ninapoamua kufanya jambo, nalifanya kwa dhati. Niligharamia kampeni yangu kwa fedha zangu mwenyewe kwa miezi mitatu, nikitembelea nchi zote 41 wanachama, kuanzia Marekani hadi Bonaire, kisiwa kidogo karibu na Venezuela."
Montagliani pia aliongoza maandalizi ya Copa América 2024 iliyopanuliwa na kuandaliwa na Concacaf.
Katika mahojiano na BBC Sport, alipinga wazo la kufanya mashindano hayo kuwa ya kudumu.
Kisiasa, anatajwa kuwa na ushawishi mkubwa. Alihusika katika kupunguza mvutano uliotokana na juhudi za aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsène Wenger, za kushawishi Kombe la Dunia lifanyike kila baada ya miaka miwili.
Pia hajawahi kuunga mkono kikamilifu pendekezo la kupanua Kombe la Dunia hadi timu 64.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi mwaka 2025, Montagliani alisema mchezo wa soka una nguvu za kustahimili changamoto za kisiasa.
"Soka ni kubwa kuliko viongozi wa sasa wa dunia. Mchezo huu utaendelea kuwepo licha ya mabadiliko ya tawala. Je, hali hiyo inaleta changamoto? Bila shaka. Lakini uzuri wa soka ni kwamba ni mkubwa kuliko mtu yeyote au nchi yoyote."
Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa
Sheikh Salman bin Ibrahim Al Khalifa, rais wa Shirikisho la Soka la Asia (AFC), alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2013 na baadaye akachaguliwa bila kupingwa kwa muhula wa nne, ambao unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Raia huyo wa Bahrain ameongoza kipindi cha ukuaji mkubwa wa soka la Asia. Chini ya uongozi wake, AFC imeanzisha na kuimarisha mashindano mapya, yakiwemo AFC Champions League Elite, AFC Champions League Two, AFC Challenge League, pamoja na Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya Asia, iliyoanzishwa msimu wa 2024/25.
Aidha, Kombe la Mataifa ya Asia (Asian Cup) limepanuliwa na kushirikisha timu 24.
Al Khalifa pia aliidhinisha tamko kali la AFC lililoukosoa mfumo wa uongozi wa FIFA chini ya Gianni Infantino kufuatia sakata la mpango wa FIFA Forward Enterprise (FFE).
Katika msimamo huo, aliungwa mkono na mashirikisho yote 46 wanachama wa AFC, licha ya ukweli kwamba mengi yalikuwa yakifahamu kuwa fedha zilizokuwa zimeahidiwa kupitia mpango wa Infantino zilikuwa nyingi na zingeweza kuwa na mchango muhimu katika bajeti zao za maendeleo ya soka.
Msimamo wa Al Khalifa umeongeza uzito wa sauti za viongozi wanaotaka uwazi zaidi na mageuzi ya utawala ndani ya FIFA, jambo linalomfanya kutajwa miongoni mwa watu wanaoweza kuwa wagombea wenye nguvu iwapo nafasi ya urais wa FIFA itakuwa wazi.
Nasser Al-Khelaifi
Rais wa Paris Saint-Germain (PSG), Nasser Al-Khelaifi, alichukua uenyekiti wa European Clubs' Association (ECA) baada ya tukio kubwa lililotikisa soka la Ulaya mwaka 2021, wakati mradi wa European Super League ulipoporomoka ndani ya saa 48 tangu kutangazwa kwake.
Chini ya uongozi wake, ECA ilibadilisha jina na kuwa European Football Clubs (EFC).
Muhimu zaidi, Al-Khelaifi alipanua uanachama wa chombo hicho hadi kufikia zaidi ya klabu 800. Miongoni mwa klabu kubwa za Ulaya, ni Real Madrid pekee iliyobaki nje ya umoja huo.
Kwa mtazamo wa wengi, raia huyo wa Qatar atakuwa mpinzani mwenye nguvu dhidi ya Gianni Infantino ikiwa ataamua kugombea urais wa FIFA.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa mtu wa karibu naye zinaonesha kuwa hana nia ya kuwania nafasi hiyo.
Akizungumzia uwezekano huo siku ya Alhamisi, chanzo hicho kilisema:
"Kwa kweli kabisa, kabisa, kabisa hana hamu ya kazi hiyo."
Kauli hiyo inaashiria kuwa, licha ya ushawishi wake mkubwa katika soka la kimataifa, Al-Khelaifi hana mpango wa kuwania urais wa FIFA kwa sasa.ndilo lilikuwa jibu la mtu wa karibu na kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 52 alipoulizwa Alhamisi kuhusu uwezekano huo."
Mattias Grafstrom
Mattias Grafström aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa FIFA mwezi Mei 2024 na tangu wakati huo amekuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya uongozi wa shirikisho hilo.
Baada ya Gianni Infantino kuchaguliwa kuwa rais wa FIFA mwaka 2016, Grafström alihudumu kama Mkuu wa Ofisi ya Rais (Chief of Staff), nafasi iliyomfanya kuwa mmoja wa washauri wa karibu zaidi wa Infantino.
Grafström pia alionekana mara kwa mara katika matukio ya Kombe la Dunia, jambo lililoonesha nafasi yake muhimu ndani ya FIFA.
Hata hivyo, ukaribu wake mkubwa na Infantino unaweza kuwa changamoto ikiwa ataamua kugombea urais wa FIFA. Aidha, kuna mtazamo miongoni mwa baadhi ya wadau wa soka kwamba rais ajaye wa FIFA anapaswa kutoka nje ya Ulaya, jambo ambalo linaweza kupunguza uwezekano wa kutwaa nafasi.
Rais mpya wa FIFA anatarajiwa kuthibitishwa katika Mkutano Mkuu wa 77 wa FIFA utakaofanyika nchini Morocco mwezi Machi 2027.
Wanaotaka kugombea urais huo wanapaswa kuwasilisha majina yao ifikapo 18 Novemba.