Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Infantino aomba radhi kwa makosa aliyoyafanya, lakini ataendelea kuwa rais wa FIFA
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, ameomba radhi kwa "makosa" aliyofanya katika mpango wenye utata wa kuuza hisa za baadhi ya mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi. Hata hivyo, ataendelea kuwa rais wa FIFA baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wakuu wa shirikisho hilo katika mkutano uliofanyika nchini Morocco.
Infantino aliitisha mkutano wa bodi ya usimamizi katika ofisi ya FIFA ya Afrika mjini Rabat siku ya Jumatano, kufuatia kuongezeka kwa ukosoaji dhidi ya pendekezo lake ambalo hatimaye lilisitishwa.
Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) lilisema mwishoni mwa wiki kuwa limepoteza imani kwa Infantino, likielezea pendekezo la FIFA Forward Enterprise (FFE) kama "makubaliano yasiyo wazi, ya siri, na yasiyofuata taratibu."
Ukosoaji pia ulitoka ndani ya FIFA yenyewe, ukiwemo kutoka kwa Katibu Mkuu Mattias Grafstrom, ambaye alihudhuria mkutano huo. Katika mawasiliano ya ndani aliyotuma kwa wafanyakazi wa FIFA siku ya Jumanne, Grafstrom alisema hali hiyo ni "mlolongo wa matukio ya kusikitisha na yasiyokubalika."
Hata hivyo, baada ya mkutano huo, Grafstrom pamoja na bodi ya usimamizi walitoa taarifa wakithibitisha tena kuwa wanaunga mkono kikamilifu uongozi wa Infantino kama rais wa FIFA.
Infantino na Grafstrom pia walituma barua iliyosainiwa kwa makamu wa marais wa FIFA, wajumbe wa Baraza la FIFA na mashirikisho yote 211 wanachama wa FIFA, wakisema kuwa "wanaomba msamaha kwa dhati" kwa makosa yaliyofanyika na kuahidi kuwa hayatajirudia.
Baada ya mkutano huo, wawili hao walionekana pamoja wakitazama mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mjini Rabat.
Infantino alikuwa amependekeza kila shirikisho mwanachama lipatiwe dola milioni 40 za Marekani iwapo lingeunga mkono mpango wa kuruhusu uwekezaji binafsi katika mashindano ya FIFA, yakiwemo Kombe la Dunia la wanaume na wanawake, kupitia kampuni tanzu mpya iitwayo FIFA Forward Enterprise (FFE).
FIFA ilisema kuwa katika mkutano huo ilikiri kuwa kulikuwa na "makosa" kwa jinsi mpango wa FFE ulivyoshughulikiwa, na kwamba haikuwa nia yake kuwafanya wajumbe wa Baraza la FIFA na mashirikisho wanachama wajisikie wametengwa na mchakato huo.
Shirika hilo pia lilikubali kuwa makosa yalifanyika baada ya taarifa kuhusu pendekezo hilo kuvuja kwa vyombo vya habari, ambapo gazeti la The Times lilikuwa la kwanza kuripoti mpango huo tarehe 28 Julai.
Hata hivyo, FIFA ilisisitiza kuwa haitavumilia mashambulizi dhidi ya uadilifu wake, utawala bora na taratibu zake, na kwamba itachukua hatua zote muhimu kulinda jina na sifa yake.
Mapema siku hiyo, FIFA ilikanusha taarifa ya gazeti la The Times iliyodai kuwa Infantino aliiahidi Morocco kuwa itakuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la Dunia 2030 ili kupata uungwaji mkono.
FIFA ilisema madai hayo ni "ya uongo na yanayopotosha," na kuongeza kuwa uamuzi kuhusu mahali pa kuchezwa fainali ya Kombe la Dunia 2030, ambalo pia litaandaliwa na Hispania na Ureno, utafanywa kwa wakati unaofaa.
Uungwaji mkono wa ndani baada ya kuongezeka kwa ukosoaji
Infantino anatarajia kuwa hatua hii itasaidia kumaliza mjadala kuhusu sakata hili, ambalo linaonekana kuwa kubwa zaidi kuwahi kumkumba katika kipindi chake cha miaka 10 akiwa rais wa FIFA.
Hata hivyo, uungwaji mkono alioupata kutoka kwa viongozi wa FIFA ulifuatia wimbi jingine la ukosoaji mkali dhidi yake.
Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, ambaye nchi yake iliandaa Kombe la Dunia la hivi karibuni pamoja na Marekani na Mexico, alisema hana tena imani na uongozi wa Infantino.
Aliyekuwa nyota wa Barcelona, Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno, Luis Figo, ambaye aliwahi kugombea urais wa FIFA mwaka 2015 dhidi ya mtangulizi wa Infantino, Sepp Blatter, kabla ya kujiondoa, alimtaka Infantino ajiuzulu mara moja.
Figo alisema:
"Infantino ameishusha hadhi ofisi ambayo aliahidi kuiinua."
Aliongeza:
"Ni kuchelewa kuokoa heshima yake, lakini bado si kuchelewa kuuokoa mchezo wa soka."
Hata hivyo, Infantino mwenye umri wa miaka 56 anaonekana kuwa tayari kuwania muhula wa nne wa urais wa FIFA.
Wanaotaka kumpinga wana hadi tarehe 18 Novemba kuwasilisha majina yao, huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika katika Mkutano Mkuu wa FIFA nchini Morocco mwezi Machi 2027.
Mgombea atahitaji kupata kura 106 kati ya wanachama 211 wa FIFA ili kushinda uchaguzi.
Kwa upande mwingine, UEFA huenda ikachukua msimamo tofauti.
Mwishoni mwa wiki, shirikisho hilo la soka la Ulaya lilitangaza kuwa limepoteza imani na uongozi wa Infantino na hata kutishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya FIFA.
Mapema wiki hii, mashirikisho kadhaa wanachama, ikiwemo Wales, huku England ikitarajiwa kufanya hivyo pia, yaliondoa uungwaji mkono wao kwa jitihada za Infantino kugombea muhula mwingine.
FIFA pia ilisema kuwa ingawa "makosa yalifanyika", kila hatua iliyochukuliwa ilizingatia kikamilifu kanuni na taratibu za FIFA. Shirika hilo liliongeza kuwa linaamini matokeo ya mkutano huo yataimarisha utawala bora ndani ya FIFA na kurejesha imani kwa taasisi hiyo.
Hata hivyo, taarifa hizo pamoja na uungwaji mkono wa viongozi wa FIFA zinaonekana kutotosha kupunguza hasira na msimamo mkali wa UEFA.
UEFA inaweza kuchukua hatua gani?
UEFA imekuwa ikijibu haraka kila hatua tangu mpango wa FIFA Forward Enterprise (FFE) wa Gianni Infantino ulipoibuka.
Kuanzia kuupinga mpango huo mara ya kwanza, hadi wakati muhimu ambapo mashirikisho yote 55 wanachama wa UEFA yalitishia kususia mashindano ya FIFA, na baadaye kutoa tamko lililoonekana kama kura ya kutokuwa na imani na uongozi wa Infantino.
Hata hivyo, UEFA inakabiliwa na changamoto kubwa ambayo si rahisi kuishinda.
Tangu Infantino alipobatilisha mpango wake wa FFE, ni Concacaf pekee kati ya mashirikisho ya mabara iliyomkosoa waziwazi rais huyo wa FIFA. Lakini tofauti na UEFA, Concacaf haikufikia hatua ya kutangaza kuwa imepoteza imani naye.
Ingawa Shirikisho la Soka la Asia (AFC) pia lilipinga mpango wa FFE, halijatoa tamko la pamoja tangu Infantino alipouondoa rasmi mpango huo.
UEFA ina ushawishi mkubwa katika soka la dunia, lakini haiwezi kumng'oa Infantino madarakani peke yake. Inahitaji kuungwa mkono na mashirikisho mengine kutoka mabara mbalimbali.
Nje ya Ulaya, hadi sasa ni Jordan pekee kati ya nchi chache wanachama 211 wa FIFA ambazo hazikusaini barua ya kumuunga mkono Infantino kugombea tena, iliyomtaka aondoke madarakani hadharani.
Kwa upande mwingine, orodha ya nchi zinazomuunga mkono Infantino ni ndefu zaidi, hasa kutoka katika ngome yake ya kisiasa ya Asia na Afrika.
Katika siku za karibuni, Misri, Morocco, Niger, Mauritania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ufilipino zote zimetangaza kumuunga mkono Infantino.
Nchi hizi zimekuwa zikinufaika na ufadhili kupitia mpango wa FIFA Forward, ambao ndio uliotangulia FFE, na kila moja hupokea takriban dola milioni 8 za Marekani katika kila kipindi cha miaka mitatu.
Kwa hiyo, UEFA italazimika kuwashawishi wanachama hao kwamba mgombea mwingine wa urais wa FIFA anaweza kuendeleza programu za ufadhili kama hizo, lakini kwa uwazi zaidi, uwajibikaji mkubwa na mageuzi ya utawala.
Hata hivyo, kwa sasa Infantino anaonekana kuwa tayari ameimarisha uaminifu kwa nchi nyingi, jambo linalofanya iwe vigumu kwa UEFA kubadili mwelekeo wa uchaguzi ujao.
Infantino anawezaje kurejesha imani?
Mizozo mingine yote ya hivi karibuni haikuweza kumtikisa Gianni Infantino kisiasa, kuanzia namna Saudi Arabia ilivyopata haki za kuandaa Kombe la Dunia la mwaka 2034, hadi tuzo ya FIFA Peace Prize aliyopewa Rais wa Marekani Donald Trump, pamoja na suala la mshambuliaji Folarin Balogun kuepuka adhabu ya kusimamishwa wakati wa Kombe la Dunia.
Hata hivyo, safari hii hali ilikuwa tofauti. Jaribio la kuuza sehemu ya haki za kibiashara na tiketi za mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi lilionekana kuvuka mipaka kwa viongozi wengi wa soka.
Sababu haikuwa tu jinsi mpango huo ulivyoonekana mbele ya umma, bali pia kwa sababu uliandaliwa kwa siri bila kuwashirikisha viongozi wengine waandamizi wa FIFA. Zaidi ya hayo, mmoja wa walionufaika na mpango huo angekuwa Joshua Kushner, ambaye ni kaka wa Jared Kushner, mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump.
Kutokana na hali hiyo, Infantino sasa analazimika kurekebisha uhusiano wake si tu na mashirikisho 211 wanachama wa FIFA, bali pia na viongozi wake wa karibu ndani ya shirika hilo.
Carlos Cordeiro, mshauri mkuu wa Infantino kuhusu mkakati wa kimataifa na utawala bora, alijiuzulu kutokana na mpango huo.
Viongozi wengine walioukosoa mpango huo hawakujiuzulu, akiwemo Katibu Mkuu Mattias Grafstrom, mkuu wa maendeleo ya soka duniani Arsène Wenger, pamoja na Afisa Mkuu wa Uendeshaji Kevin Lamour.
Inaaminika pia kuwa kuna viongozi wengine ndani ya FIFA ambao hawakutoa maoni yao hadharani, licha ya kuwa na wasiwasi kuhusu mpango huo.
Mbali na kurejesha uhusiano, Infantino huenda atalazimika kuanzisha au kupendekeza mageuzi ya utawala ndani ya FIFA.
Mageuzi hayo yanaweza kujumuisha kuweka mifumo madhubuti ya ukaguzi na uwajibikaji ili kuhakikisha mpango kama huu hauwezi tena kuandaliwa au kuwasilishwa kwa siri bila ushirikishwaji wa viongozi husika.
Aidha, anaweza kuamua kuachana na baadhi ya mapendekezo yenye utata, kama vile wazo la kupanua Kombe la Dunia hadi timu 64, au kufungua zaidi matumizi ya akiba ya fedha za FIFA ili kuongeza uwazi na kujenga upya imani ya wanachama.
Hatua kama hizo zinaweza kumsaidia Infantino kupunguza shinikizo analokumbana nalo na kurejesha imani ya wadau wa soka duniani.