Je, huu ndio mwisho wa Rigathi Gachagua katika siasa za Kenya?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rigathi Gachagua
    • Author, Na Laillah Mohammed
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Majaji watatu wa mahakama kuu nchini Kenya Anthony Mrima, Eric Ogola na Freda Mugambi walichukuwa zaidi ya saa kumi Jumatatu ya Juni 8 kutoa uamuazi wao kuhusu hatima ya kisiasa ya aliyekuwa Naibu wa Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua.

Na baada ya kusoma kurasa zaidi ya 300 ya uamuazi huo, watatu hao walionekana kutia msumari moto kwenye kidonda cha Rigathi Gachagua ambaye alikuwa na matumaini makubwa kwamba jina lake lingesafishwa.

Gachagua mwenyewe amesalia kimya na hakufika mahakamani kusikiliza uamuzi wa mahakama na badala yake kuwatuma mawakili wake mahakamani.

Ila alipokuwa kanisani Jumapili Juni 7, kinara huyo wa chama cha DCP alionekana kuashiria kwamba ikiwa dua yake haitapokelewa na malalamishi yake kutupiliwa mbali na mahakama kuu, basi angewaamrisha mawakili wake kujiandaa kuwasilisha kesi mbele ya mahakama ya rufaa.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya Gachagua ana siku 14 za kuwasilisha kesi mbele ya mahakama ya rufaa, na siku zingine 30 za kunakili kesi hiyo. Aidha watakaotajwa kwenye kesi hiyo wanapaswa kujulishwa rasmi kisheria katika siku saba za Gachagua kuwasilisha kesi hiyo mahakamani.

Lakini je, baada ya mahakama kuu kutupilia mbali zaidi ya hoja sita kati ya nane alizowasilisha, mahakama ya juu zaidi ina uwezo wa kubatilisha uamuzi wa makahama kuu?

Rais wa chama cha mawakili nchini Kenya, Charles Kanjama anahisi kwamba , ' pande zote zilizohusika kwenye kesi hii zina masuala mengi ya kisheria ambayo yanaweza kujadiliwa mbele ya mahakama ya rufaa.

Baadhi ya masuala ambayo yalizungumziwa na majaji wa mahakama kuu kwa mfano suala la umma kuhusishwa katika mchakato wa kumtimua madarakani afisa wa umma, iwapo suala hilo lilitekelezwa ipasavyo kwa muibu wa katiba na sheria za nchi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Aidha mahakama iiangazia suala la madai ya Gachagua kwamba umma ulihusishwa kwa maeneo ambayo yaliunga mkono kuondolewa madarakani kwa Gachagua na wala sio maeneo ambayo yalipinga hali hiyo.'

Kulingana na Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Gadys Boss Sholei ambaye alikuwa anahojiwa na runinga ya Citizen nchini Kenya Jumanne asubuhi, 'Mahakama iliangazia kwa kina hoja zote alizowasilisha Gachagua na kusema kwamba alitendewa haki wakati wa kusikizwa kwa kesi yake bungeni ambapo kulikuwa na uwazi.'

Na huku wengi nchini Kenya hasa katika ngome yake ya siasa za 'Mlima Kenya' wakisubiri kusikiliza kauli yake Gachagua kuhusu hatua atakayoichukuwa, wengi wanajiuliza maswali ikiwa huu ndio mwisho wa siasa zake za upinzani nchini Kenya ambao ndio mwanzo wa mkoko kualika maua.

Mchambuzi wa kisiasa Barack Muluka anahisi kwamba Gachagua hawezi kufifia kisiasa kutokana na kile amekitaja kama kujikwaa mahakamani. ' Bado ana ushawishi mkubwa katika eneo la kati la nchi na japo amekabiliwa na changamoto za kushindwa kunyakuwa viti vya ubunge ambavyo viliwachwa wazi na uchaguzi mdogo kuandaliwa, amekuwa na usemi mkubwa katika jamii ya Mlima Kenya na anatikisa ushawishi wa Rais Ruto katika eneo hilo.'

Baadhi ya wabunge ambao wanashirikiana na Gachagua katika muungano wa kisiasa wa UNITED OPPISITION maarufu Serikali kivuli, wamekashifu uamuzi wa mahakama na kusisitiza kwamba walihisi mkono wa seikali kuu katika uamuzi wa mahakama kuu.

Mwanasiasa Miguna Miguna aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamiiwa wa X, kwamba ; ' Kuondolewa madarakani kwa Rigathi Gachagua kulifanyika kinyume na sheria, hakukuwa na uwazi, haki na kikubwa ni kwamba mchakato mzima ulichochewa na kusambaratika kwa uhusiano kati ya Gachagua na Ruto.

Mahakama kuu ingepaswa kufutilia mbali kuondolewa madarakani kwa Gachagua.'

.

Chanzo cha picha, Kenya Parliament

Maelezo ya picha, Mbunge Mwengi Mutuse Eckomas

Gachagua alijipata vipi katika kikaango alicho ndani kwa sasa?

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alitimuliwa na Bunge la Kenya mnamo Oktoba 2024, na kuwa naibu wa kwanza wa rais katika historia ya nchi hiyo kuondolewa afisini kupitia mchakato huo.

Kuondolewa huko kwa kihistoria kulitokana na msururu wa madai ya kisiasa, kikatiba na kiuchumi. Hoja ya kuondolewa kwake iliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Eckomas Mwengi Mutuse na kuidhinishwa kwa wingi na Bunge, ilieleza kwa kina sababu 11 za kutimuliwa kwake. Hatahivyo Bunge la Seneti lilikubali mashtaka matano kati ya hayo. Mashtaka hayo yaliorodhesha kumhujumu Rais William Ruto na kutenda kinyume na sera za serikali, kuchochea mivutano ya kikabila kupitia matamshi ya mgawanyiko na kudhalilisha hadharani Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS)

Takriban wabunge 281 katika Bunge la Kitaifa walipiga kura kupitisha hoja ya mashtaka 11 ya kuondolewa kwake. Baadaye bunge la Seneti lilifanya kesi ya siku mbili ambapo Gachagua alikana kuwa na hatia. Kesi hiyo ilisitishwa kwa muda baada ya Gachagua kuugua, lakini iliendelea tena. Baraza la Seneti hatimaye lilipiga kura ya kumtia hatiani kwa mashtaka matano, na kumaliza rasmi muda wake. Baada ya kuondolewa kwake, Kithure Kindiki aliteuliwa na kuapishwa kama Naibu Rais mpya wa Kenya.

Kipi kitarajiwe sasa baada ya mahakama kuzamisha maombi yake ?

Kisiasa, Gachagua bado ana uwezo wa kushirikiana na viongozi wenzake katika mchakato mzima wa uchaguzi Mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2027.

Akizungumza katika mazishi mjini Ol Kalau mwezi jana, Katibu Mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna alimtaka Gachagua kuweka yaliyopita kando na kuungana na wenzake kwa ajili ya kupambana na Rais Williama Ruto.

'Najuwa kwamba sote hapa tuko na mambo ambayo yalifayika awali na hatukuwa tunaelewana wakati huo, lakini nimemueleza rafiki yangu Gachagua hapa kwamba njia bora zaidi ya kushindana na Ruto ni kwa kushikana pamoja na kumteua kiongozi mmoja ambaye tutamuunga mkono.

Sote tukipigania hiki kiti, atatumaliza mapema sana asubuhi.,' alisema Seneta Sifuna.

Miezi tisa iliyopita, Gachagua alitangaza wazi na rasmi azma yake ya kuwania Urais, na kumuondoa aliyekuwa Bosi wake William Ruto ambaye amedai mara kwa mara kwamba uongozi wake ni mbaya na unawaumiza raia na kufinya uchumi wa nchi.