"Nimechagua kutokuwa na watoto"- Wanawake Nigeria wapinga nadharia kuwa lazima uwe mama

Susan Imaibehe Ekpoh, ni mmoja wa marubani wachache wanawake nchini Nigeria. Anaishi mjini Abuja.
Azma yake ya kutaka kuwa rubani ilianza akiwa mtoto, alipokuwa na umri wa miaka nane alipata fursa ya kuingia kwenye sehemu ya rubani ndani ya ndege, na ikampa hamasa ya yeye kuwa rubani.
Baadaye, Susan alitimiza ndoto yake ya kuwa rubani. Kama rubani wa safari za kibiashara, kazi yake inahitaji awe anapatikana masaa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki.
Wakati yupo kazini, umakini wake wote umeelekezwa kwenye kazi.
Macho ya Susan yanang'aa anapotuelezea uzoefu wake. "Kuendesha ndege kama mwanamke ni moja ya mambo mazuri yaliyowahi kutokea katika maisha yangu. Ninapenda, ila kuna changamoto na msongo wa mawazo. Kuendesha ndege hukufanya kuiona dunia kwa mtazamo tofauti, ni moja ya mambo ninayoyapenda."
Lakini ingawa alipata kazi katika sekta ambayo imejaa wanaume, uamuzi wake wa kutokuwa na watoto unamtofautisha hata zaidi.
Katika jamii nyingi za Nigeria,thamani ya mwanamke bado inahusishwa na uwezo wake wa kuoleka na kuzaa, ila kwa sasa wanawake wengi nchini Nigeria wanachagua kutokuwa na watoto, si kwa sababu ya kushindwa kujifungua, bali kwa hiari yao wenyewe.
Susan, akiwa na umri wa miaka thelathini, anaona uzazi kama moja ya kazi ngumu zaidi duniani.
Anafafanua kuwa uamuzi wake haujachochewa na kazi yake, kwani kuna marubani wengi wanawake ambao wana watoto, ila uamuzi wake umetokana na mchanganyiko wa sababu mbalimbali.
"Sio tukio moja lililonifanya kusema sitaki kuwa na watoto. Ni jinsi maisha yangu yalivyo, maamuzi niliyoyafanya, maisha ninayotaka kuishi, na kwa muda, nimeelewa kuwa mtoto hawawezi kuwa katika safari ya maisha yangu."

Chanzo cha picha, Susan Ekpoh
Ingawa Susan anaungwa mkono na familia yake, anadai kuwa uamuzi wake haujamuathiri katika kuwa na mahusiano ya kimapenzi.
"Naamini huwezi kumlazimisha mtu kufanya kitu ambacho hakitaki,hivyo ndivyo chuki huanza. Siwezi kuwa na mpenzi anayetaka mtoto akidhani nitabadilisha mawazo yangu baadaye."
"Ikija katika suala la ushirikiano na ndoa, niko tayari kwa hilo, lakini sijasimamisha maisha yangu nikisubiri hilo lifanyike. Ikiwa Mungu anataka lifanyike, itakuwa jambo jema zaidi. Ikiwa sitapata mtu anayeendana na malengo yangu, bado nitaishi kwa furaha" anasema Susan.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jennifer anafanya kazi katika kampuni ya FinTech iliyoko Lagos.
Uamuzi wake wa kutokuwa na watoto unachochewa zaidi na hali aliyopitia akiwa binti wa kwanza wa familia, lakini pia na changamoto za kijamii na kiuchumi.
"Nilikulia katika familia yenye changamoto nyingi. Niliona shangazi zangu, mama yangu, na majukumu aliokuwa nayo kama binti wa kwanza. Niliiambia nafsi yangu kwamba sinauhakika kama ningependa kuwa na mtoto."
Jennifer, ambaye mama yake bado anajaribu kumshawishi abadilishe uamuzi wake, anasema anafahamu kuhusu upweke ambao uamuzi huu unaweza kumletea na athari zake katika mahusiano yake ya kimapenzi.
"Mama yangu huniambia, 'Nani atakutunza utakapokuwa mzee?'
"Nilikuwa na waza sana, lakini nilipoanza kutumia mitandao ya kijamii kujadili uamuzi wangu, nilikutana na wanawake wengine ambao walichukua uamuzi huo huo, na walikuwa na umri wa miaka 50 au 60 na wamefanikiwa na wanaishi vizuri, niliiambia nafsi yangu kwamba nitafanikiwa pia, mradi nikipanga maisha yangu vizuri."

"sina majuto"
Kwa Destiny Udeh, mwenye umri wa miaka 41 ambaye ameolewa, suala lililochochea uamuzi wake ni tofauti kabisa.
Anasema kwa muda mrefu alikuwa akijiuliza umuhimu wa kuwa na watoto, baada ya kupoteza ujauzito wake, na kupoteza mtoto mwingine baada ya kujifungua,hapo ndipo alipata ujasiri wa kutangaza kuwa hataki tena kuwa na mtoto.
"Mwaka wa 2021, nilipata ujauzito. Nakumbuka nilipojua, nilishawishiwa kuwa na mtoto. Baada ya kujifungua, mtoto mwenyewe alifariki, hapo ndipo niliamua kuwaambia marafiki zangu,familia na mume wangu kuwa sitaki kuwa na mtoto tena"
Destiny anaelezea kwamba mumewe, mama yake, na familia ya mume wake wanamuunga mkono katika uamuzi wake, ingawa baadhi ya familia na marafiki hawajakubali na wanaendelea kumshinikiza apate mtoto.
"Kabla sijaolewa, tulikubaliana na mume wangu kuwa sio lazima kuwa na watoto. Kwa hivyo, nilipoamua kutokuwa na watoto, aliniuliza kama ninauhakika na uamuzi huo"
"Nimezingatia faida na hasara za kuwa na mtoto. Nimechunguza mitazamo mingi ambayo jamii imeeneza, kutufanya tuamini kwamba kuwa na mtoto ni jukumu la mwanamke. Na nimeamua kutokuwa na watoto. Ninajiandaa kustaafu kwa sasa, nina watu wengi wanaonipenda na ninawapenda pia, kwa hivyo nina furaha na sina majuto."
Destiny haogopi kuzungumza kuhusu maamuzi yake na safari yake kwenye mitandao ya kijamii.
"Ninafurahi kuwa na uwezo wa kuishi maisha yangu kikamilifu. Nimefumbua macho ya wanawake wengine kwa kuwaonyesha kuwa inawezekana kujichagua wao wenyewe na kuwa na furaha, na hilo linaniridhisha."

Chanzo cha picha, Destiny Udeh
"Hakuna njia sahihi ya kuwa mwanamke"
Kwa Dkt Abiola Akiyode-Afolabi, mwanzilishi wa shirika la Women Advocates Research and Doc Center (WARDC), anasema kuwa, suala la kutokuwa na watoto linazungumziwa sana, kwasababu nyakati zimebadilika, na ni tofauti na vizazi vya awali.
"Tunashuhudia ongezeko la idadi ya wanawake wanaofanikiwa katika nyanja mbalimbali ambazo kwa kawaida huhusishwa na wanaume, jambo ambalo halikuwezekana miaka michache iliyopita. Tunashuhudia kuibuka kwa kizazi cha wanawake walio na elimu ya juu na wanaojitegemea kifedha. Kwao, ndoa na watoto si suala la lazima, na mitandao ya kijamii imechangia katika mabadiliko haya."
Akiyode Afolabi anaongeza kwamba mabadiliko haya yana changamoto zake.
Ingawa wanawake wasiotaka watoto bado ni wachache, bado wanakumbana na ubaguzi kuwa wao ni wabinafsi,hawajakamilika,wamejuruhiwa kwa namna fulani na hawana huruma
Kulingana na shirika la UNICEF, takriban watoto milioni saba huzaliwa kila mwaka nchini Nigeria, jambo linalofanya nchi hiyo kuwa mchangiaji mkubwa katika ongezeko la idadi ya watu duniani.
Kwa Mwanafsi Maymunah Kadiri, wazo kwamba wanawake wasiokuwa na watoto ni wenye ubinafsi na hawakamiliki ni mtazamo wa zamani.
"Kuwa mwanamke haufafanuliwi tu kwa uzazi, na thamani yake,au uwezo wa kupata mtoto"












