Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Teknolojia 5 zinazombadilisha binadamu kuwa nusu mashine
Mustakabali ambapo binadamu wanaweza kuinua vitu vyenye uzito mkubwa ajabu, kuona gizani na hata kuruka linaweza kuonekana kama hadithi za kisayansi, lakini tayari limeanza kuwa uhalisia.
Watumiaji wa teknolojia hizi mpya wanakuwa mseto wa binadamu na mashine, wakiboresha uwezo wa miili yao ili kufanikisha mambo ambayo hapo awali yalionekana kuwa yasiyowezekana.
Lakini hivi si vifaa vya kinadharia tu; ni teknolojia zinazoibuka ambazo tayari zinapatikana kibiashara au zinatarajiwa kupatikana sokoni katika kipindi cha karibu kijacho.
Paa angani
Kuruka angani kwa muda mrefu kumekuwa ndoto ya binadamu, kuanzia simulizi ya Kigiriki la Icarus hadi magari yanayoruka yaliyooneshwa katika filamu za sayansi ya kubuni kama Blade Runner. Lakini ingawa teknolojia ya kuruka binafsi inaweza kuonekana kama jambo la kufikirika, tayari ipo leo kupitia Gravity Jet Suit.
Ingawa hapo awali watu walitamani kuwa na viatu vya roketi vinavyoweza kuwainua kutoka ardhini, wazo hilo lina changamoto kubwa. Kwa bahati mbaya, viatu hivyo vitakuwa vigumu sana kudhibiti kwa sababu nguvu ya msukumo itatumika mbali na kitovu cha uzito wa mwili wa mtumiaji.
Badala ya kutumia mabawa au rota kama helikopta, Gravity Jet Suit hutumia injini tano za ndege ndogo, kumuwezesha mvaaji kujielekeza kwa urahisi angani. Marubani wanaweza kutulia hewani, kugeuka na hata kuruka umbali mfupi juu ya maji au nchi kavu.
Nguvu kuu ya kuinua mwili hutolewa na injini ya gesi yenye nguvu ya farasi 1,050 (gas turbine) iliyowekwa mgongoni, huku kila mkono ukiwa na injini mbili ndogo za ndege zinazosaidia kudumisha uthabiti na kutoa udhibiti wa mwelekeo wakati wa kuruka.
Mwaka 2021, Jeshi la Wanamaji la Uingereza (Royal Navy) lilijaribu kutumia Gravity Jet Suit katika mazoezi ya kijeshi ili kuchunguza uwezo wake wa kutumika katika operesheni.
Kuona bila kufungua macho
Uwezo wa kuona wa binadamu una mipaka. Bila mwanga, kimsingi hatuwezi kuona.
Miwani ya kuona usiku inayowezesha kuona mawimbi ya mwanga ya infraredi imekuwepo kwa muda mrefu, lakini sasa teknolojia hiyo imepunguzwa ukubwa na kufanywa kuwa rahisi zaidi kutumia.
Wanasayansi nchini China wameunda lenzi za mawasiliano zilizopakwa nanopatikeli zinazofyonza mwanga wa infraredi na kuugeuza kuwa mwanga unaoonekana wa rangi nyekundu, kijani au buluu.
Katika majaribio, lenzi hizo ziliwawezesha watu kuona miale ya mwanga iliyotolewa na LED ya infraredi.
Jambo la kushangaza ni kwamba washiriki waliweza "kuona" miale hiyo vizuri zaidi wakiwa wamefumba macho. Hii ni kwa sababu kope zilizofungwa zilizuia mwanga wa kawaida unaoonekana kuingia machoni, hivyo kupunguza usumbufu na kuruhusu ishara za infraredi zilizobadilishwa kuonekana kwa urahisi zaidi.
Katika siku zijazo, teknolojia hii inaweza kuboreshwa na kutumika kuwasaidia watu wenye upungufu wa kutambua rangi kuona rangi ambazo kwa kawaida ziko nje ya wigo wao wa kuona.
Piga hatua kuelekea wakati ujao
Mifupa ya nje ya mwili (exoskeletons) ni mashine zinazovaliwa mwilini ambazo zimeundwa kuongeza nguvu za asili za binadamu. Unaweza kuzifikiria kama aina ya suti yenye nguvu za mitambo au kama forklift inayovaliwa mwilini.
Ingawa wengi wetu tunavihusisha na filamu ya kisayansi ya kubuni Aliens, vifaa hivi tayari vinatumika katika maisha halisi leo.
Vihisishi (sensa) vilivyowekwa kwenye eksoskeletoni hufuatilia mienendo ya mwili wa mtumiaji na kuamsha mota zilizopo kwenye viungo mbalimbali vya kifaa hicho ili kutoa nguvu ya ziada.
Eksoskeletoni tayari zimewasaidia baadhi ya watu wenye ulemavu kutembea bila msaada wa mtu mwingine, na sasa zinaboreshwa ili kuwasaidia wafanyakazi wa maghala kuinua na kusafirisha mizigo mizito kwa usalama zaidi.
Teknolojia hii pia inaanza kupata matumizi katika maisha ya kila siku. Kwa mfano, inaweza kuwasaidia watu kutembea umbali mrefu zaidi wakati wa matembezi ya milimani, kupunguza uchovu wa misuli, au kupanda ngazi ambazo kwa kawaida zingekuwa changamoto kutokana na umri, majeraha au hali za kiafya.
Wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha London (University College London - UCL) hivi karibuni wameunda kifaa kinachovaliwa kama glavu kinachompa mtumiaji kidole gumba cha ziada cha roboti.
Hili linaweza kuonekana kama jambo lisilo la lazima, kwani watu wengi tayari wana vidole gumba viwili. Hata hivyo, majaribio yameonyesha kwamba uwezo wa ziada wa kutumia vidole kwa ustadi unaotolewa na gumba la tatu humwezesha mtu kufanya baadhi ya kazi kwa mkono mmoja ambazo kwa kawaida huhitaji mikono miwili.
Mienendo ya gumba hilo la tatu hudhibitiwa na vihisishi (sensa) vilivyowekwa chini ya vidole vya miguu ya mtumiaji. Kwa kubonyeza au kusogeza vidole vya miguu kwa njia tofauti, mtumiaji anaweza kuelekeza jinsi gumba hilo linavyosogea na kushika vitu.
Licha ya kwamba kidole cha tatu cha ziada si sehemu ya maumbile ya kawaida ya mwili wa binadamu, katika majaribio watu wengi waliweza kujifunza kukitumia kwa haraka. Kati ya karibu watu 600 walioshiriki katika majaribio hayo, ni watu wanne tu ambao walishindwa kukitumia.
Dhibiti vitu kwa kutumia mawazo yako
Muunganisho ya ubongo na kompyuta (Brain-Computer Interfaces - BCI) ni teknolojia zinazochipuka zinazowawezesha watu kudhibiti kompyuta na vifaa vingine kwa kutumia mawazo yao.
Kwa kupandikiza safu ya elektrodi ndogo sana ndani ya ubongo, ishara za neva zinazohusishwa na harakati za viungo vya mwili zinaweza kutambuliwa na kutafsiriwa na kompyuta. Badala ya kutuma amri kwa misuli, ishara hizo hutumiwa kuendesha vifaa vya nje kama mkono wa roboti au kiti cha magurudumu.
Teknolojia hii haijahusu tu kuboresha uwezo wa kutumia kompyuta. Inaweza pia kuwapa watu wenye magonjwa yanayosababisha kudhoofika kwa mfumo wa neva uwezo wa kudhibiti mazingira yao kwa uhakika zaidi na kwa kujitegemea.
Hadi sasa, teknolojia hii imewawezesha baadhi ya watu waliojeruhiwa uti wa mgongo kudhibiti kishale cha kompyuta kwa kufikiria tu kuhusu kusogeza mkono au mkono wao uliopooza. Kwa njia hiyo, wanaweza kuwasiliana na kutumia vifaa vya kidijitali bila kufanya harakati za kimwili.
Hatua inayofuata katika maendeleo ya vifaa hivi ni kuwezesha udhibiti sahihi zaidi wa viungo vya roboti. Wanasayansi wanaamini kwamba siku moja teknolojia ya BCI inaweza kuwasaidia wagonjwa wenye kudhoofika kwa misuli na matatizo mengine ya mfumo wa neva kurejesha kwa kiwango kikubwa, au hata kikamilifu, uwezo wao wa kufanya harakati za mwili.