Kuanzia miaka 83 hadi 15,000: Wanyama wanaoishi muda mrefu zaidi duniani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuanzia panya fuko hadi papa wa Greenland, hawa hapa ni viumbe wenye muda wa kuishi mrefu usio wa kawaida.

Dhana ya muda inaweza kuwa na utata kidogo. Kwa mfano, Einstein alieleza jinsi muda ulivyo wa kiasi, na jinsi vitu vinavyoupitia kwa namna tofauti kulingana na kasi ya mwendo wao. Hili ni jambo linalohitaji kutafakari kwa kina ili kulielewa.

Hata hivyo, wanyama wengi duniani wamefanikiwa kuishi muda mrefu zaidi ya ule unaotarajiwa kwa kawaida, wakiishi maisha marefu ya ajabu na kuvunja rekodi zinazotarajiwa. Lakini ni mnyama yupi anayeishi muda mrefu zaidi duniani?

Wanasayansi wametumia miaka mingi kutafuta siri za maisha marefu, na spishi nyingi zilizo kwenye orodha hii zinaweza kutoa mwongozo kuhusu jinsi tunavyoweza kuishi maisha yenye afya bora na marefu zaidi hapo baadaye.

Basi, ungana nasi tunapoangazia baadhi ya viumbe wanaoishi muda mrefu zaidi duniani.

Mamalia wa nchi kavu anayeishi muda mrefu zaidi – Binadamu

.

Chanzo cha picha, Pascal Parrot/Sygma/Getty Images

Jeanne Calment, anayetambuliwa kama mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani kuwahi kurekodiwa, aliishi maisha ya ajabu ya miaka 122 na siku 164. Alizaliwa Arles, Ufaransa, mnamo mwaka 1875 na alijulikana kwa kudai kuwa alikutana na Vincent Van Gogh, ingawa hakumzungumzia kwa namna ya kuvutia au ya kusifu.

Calment alihusisha maisha yake marefu na kutokuwa na msongo wa mawazo pamoja na kuwa na uwezo wa kufurahia maisha na kucheka. Hakufanya jitihada zozote maalum za kudumisha mtindo wa maisha yenye afya, hata alivuta sigara baada ya kila mlo, kabla ya kuacha hatimaye akiwa na umri wa miaka 117.

Alifariki dunia mwaka 1997, akiwa amewapita umri binti yake pekee na mjukuu wake, ambao wote walifariki wakiwa na umri mdogo zaidi.

Kiumbe wa majini anayeishi muda mrefu zaidi – Sponji ya kioo

.

Chanzo cha picha, National Marine Sanctuaries/Wikipedia

Spongi za kioo ni miongoni mwa viumbe hai wenye maisha marefu zaidi duniani. Licha ya muonekano wao dhaifu, inakadiriwa kuwa zinaweza kuishi hadi miaka 15,000. Na ingawa ni nadra kiasi, zinaweza kupatikana katika kila bahari duniani, kwa kawaida katika kina cha zaidi ya mita 450.

Kinachozifanya ziwe za kipekee ni uwezo wake wa kutoa misukumo ya umeme katika miili yake. Sehemu zake zinazofanana na mijeledi midogo (nywele ndogo zinazonasa bakteria waliomo majini) huacha kusogea zinapohisi hatari. Hata hivyo, tofauti na aina nyingine za spongi za baharini, spongi za kioo hazijikunji wala kubadili umbo zinapochochewa.

.

Chanzo cha picha, Nimesh Madhavan/Wikipedia

Ndege aliyeishi muda mrefu zaidi katika rekodi ni Cookie, jogoo dume wa aina ya *pink cockatoo* (au *Major Mitchell's cockatoo* - *Cacatua leadbeateri*), aliyeishi katika Bustani ya Wanyama ya Brookfield jijini Chicago, Marekani.

Mnamo mwaka wa 2014, Cookie alitambuliwa na Guinness World Records kama kasuku mwenye umri mkubwa zaidi duniani. Wakati huo, alikuwa na umri wa miaka 81 na alikuwa amestaafishwa kutoka kwenye maonyesho ya hadhara ili kulinda afya yake. Kwa masikitiko, alifariki dunia mwaka wa 2016 akiwa na umri mkubwa wa miaka 83.

Cha kushangaza ni kwamba, Cookie aliishi muda mrefu zaidi kwa miaka 52 kuliko ndege mwingine yeyote wa aina hiyo aliyeshika nafasi ya pili kwa kuishi muda mrefu.

Panya anayeishi muda mrefu zaidi – Panya-fuko asiye na manyoya

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Puku-fuko asiye na manyoya, ni panya wa ajabu kwelikweli. Ana uwezo mkubwa wa kustahimili mazingira kiasi kwamba anaweza kuishi kwa dakika 18 bila oksijeni, na pia ana kinga dhidi ya aina nyingi za saratani. Sababu nyingine inayochangia maisha yake marefu ni kwamba huishi ndani kabisa ya mashimo ya chini ya ardhi, jambo linalomaanisha kuwa ana maadui wachache wa asili wanaomwinda.

Utafiti umeonyesha kuwa hatari ya puku-fuko hawa kufa haiongezeki kadiri wanavyozeeka kwa kasi ileile inayotokea kwa mamalia wengine. Shukrani kwa sifa za kipekee za kijenetiki, seli zao hujigawanya kwa usahihi zaidi na zina uwezekano mdogo wa kuharibika. Mnamo mwaka wa 2020, iliripotiwa kuwa puku-fuko mmoja dume alifikisha umri wa miaka 37, jambo linalomfanya kuwa panya anayeishi muda mrefu zaidi duniani.

Kiumbe kisicho na uti wa mgongo kinachoishi muda mrefu zaidi –quahog wa baharini

.

Chanzo cha picha, Bangor University

Chaza wa aina ya *quahog wa baharini* ndio viumbe hai wanaoishi muda mrefu zaidi duniani. Mmoja wao, aliyepatikana karibu na pwani ya Iceland mwaka wa 2006, aligunduliwa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Bangor kuwa na umri wa ajabu wa miaka 507.

Alipewa jina la 'Ming' na waandishi wa habari, wakirejelea nasaba ya Ming iliyokuwa ikitawala China wakati chaza huyo alipozaliwa. Hata hivyo, nchini Iceland, chaza huyo anajulikana kama 'Hafrun' jina la kike linalomaanisha 'siri ya bahari'.

Umri wa chaza wa aina hii unaweza kubainishwa kwa njia inayofanana sana na ile inayotumika kwa miti. Kila mwaka, mstari hutokea kwenye ganda la chaza huyo, hivyo, kuhesabu mistari hiyo hubainisha umri wake.

Kobe anayeishi muda mrefu zaidi – Kobe mkubwa wa Aldabra

.

Chanzo cha picha, Deshakalyan Chowdhury/AFP/Getty Images

Aina ya kobe wanaoishi muda mrefu zaidi duniani ni kobe mkubwa wa Aldabra. Kobe mkongwe zaidi alikuwa dume aliyeitwa Adwaita, inakadiriwa kuwa alikuwa na umri wa miaka 255 alipofariki katika Bustani ya Wanyama ya Alipore, jijini Kolkata, India, mwaka wa 2006. Inaaminika kuwa Adwaita alianguliwa mwaka wa 1750 na aliishi maisha ya upweke katika bustani hiyo ya wanyama kwa zaidi ya miaka 100.

Kama jina lake linavyoashiria, kobe mkubwa wa Aldabra anatoka katika kisiwa cha pete (atoll) cha Aldabra nchini Seychelles, ambapo kuna takriban kobe 100,000 wa aina hiyo. Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya kobe waliokusanyika mahali pamoja duniani.

Samaki anayeishi muda mrefu zaidi – Papa wa Greenland

.

Chanzo cha picha, Alamy

Papa wa Greenland ndiye spishi ya papa anayeishi muda mrefu zaidi duniani. Hata hivyo, kwa sababu anajitofautisha sana na papa wengine, ni vigumu zaidi kubaini umri wake. Papa wengi wengine huwa na mistari ya ukuaji kwenye miiba ya mapezi yao, sawa na jinsi mti unavyokuwa na pete za ukuaji. Hata hivyo, papa wa Greenland hana tishu ngumu mwilini mwake na haukuwi na mistari hiyo.

Njia pekee ya kukadiria kwa usahihi umri wa papa huyu ni kwa kutumia mbinu ya kubaini umri kupitia kaboni , ambayo si kipimo sahihi sana. Kwa kutumia mbinu hii, wanasayansi walifanikiwa kubaini kuwa papa mmoja jike alikuwa na umri wa kati ya miaka 252 na 512.

Maji baridi wanayoishi huenda yakasababisha michakato ya mwili wao, kwenda polepole sana, jambo hili linaweza kuelezea kwa nini wanaishi muda mrefu na pia kwa nini huogelea kwa mwendo wa taratibu.

Mbwa aliyeishi muda mrefu zaidi – Bobi

.

Chanzo cha picha, Patricia De Melo Moreira/ AFP/Getty Images

Bobi, mbwa wa aina ya Rafeiro do Alentejo, alifikisha umri wa ajabu wa miaka 31 kabla ya kufariki dunia mnamo Oktoba 2023. Mapema mwaka huo huo, umri wake ulithibitishwa na Guinness World Records kama mbwa aliyeishi muda mrefu zaidi kuwahi kutokea, akivunja rekodi ya awali ya miaka 29 na miezi 5. Hata hivyo, tangu wakati huo kumekuwa na madai kwamba huenda umri huo si sahihi.

Mbwa wa aina ya Rafeiro do Alentejo wana asili ya Ureno na wanajulikana kwa utulivu na uwezo mkubwa wa kulinda. Hii ni aina ya mbwa wakubwa wenye vichwa vikubwa na manyoya mengi mazito yanayowasaidia kuhifadhi joto mwilini.