Soko la mitumba linavyoathiri sekta ya mavazi Afrika Mashariki

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Alfred Lasteck
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Kitu cha kwanza kinachowavutia wanunuzi wanapoingia katika Soko la mitumba la Ilala katika jiji kuu la kibiashara la Tanzania, Dar es Salaa, si bei tu, wala si ubora wa bidhaa, upekee wa nguo na chapa zilizowekwa kwenye mavazi
Ukifika unaona fulana, kaptula, suruali za 'jeans', gauni yenye michoro ya maua yanayoning'inia kwenye vibanda vya muda. Hapo zinaonekana chapa za wabunifu kutoka Ulaya, Uchina na Marekani zikiwa zimechanganyika na jezi za michezo na makoti yaliyosafiri maelfu ya kilomita kabla ya kufika nchini Tanzania.
Inapofika majira ya saa nne za asubuhi, njia nyembamba za soko huwa zimejaa watu, wafanyabiashara hupaza sauti kutangaza bei za nguo huku wakichuana na kelele za pikipiki 'bodaboda' zinazopita karibu.
Wanunuzi hupitia mafungu ya nguo moja baada ya jingine wakitumaini kupata bidhaa nzuri kabla haijanyakuliwa na mtafutaji mwingine.
Mchambuzi wa uchumi kutoka jijini Dar es Salaam, Alvin Alex anasema, "Kwa mfanyabiashara wa Ilala, Dar es Salaam ni biashara, kwa mnunuzi wa kawaida ni nafuu ya maisha, kwa mbunifu wa mavazi wa ndani inaweza ikawa njia ya kumuharibia biashara yake kutokana na wingi wa nguo hizo. Suala hili linaibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa uchumi wa nchi."
Ingawa Tanzania inatoza ushuru wa 35% kwa nguo zilizotumika yaani mitumba, soko kubwa la mitumba la Ilala bado hufurika wateja wanaotafuta nguo za bei nafuu.
Biashara hiyo, ni moja ambayo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zifikie ukomo na nchi wanachama kuchukua mwelekeo mwingine ikiwemo kuzalisha nguo zake.
Mnamo 2015, wanachama sita wa EAC wa wakati huo - Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, na Uganda walitangaza kwamba wote wataweka ushuru wa juu sana na hatimaye kupiga marufuku uagizaji wa mitumba.
Lakini Marekani, msafirishaji mkuu wa nguo za mitumba, ilisema hatua hizo zitakiuka makubaliano ya biashara huria na kutishia kuziondoa nchi za EAC kwenye Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika (Agoa).
Makubaliano ya Agoa, ni urasimishaji wa kibiashara kimataifa unaoruhusu mataifa kadhaa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara kusafirisha maelfu ya bidhaa bila ushuru kwa Marekani.
Mitumba si suala la uchaguzi wa mtindo wa maisha

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa wengi ni hitaji muhimu isipokuwa kwa idadi inayoongezeka ya wazalishaji wa ndani, wabunifu wa mavazi na wachumi, nguo hizo zinaleta changamoto kadhaa.
Hapa ni onyo kwamba ndoto ya Tanzania ya kujenga sekta imara na shindani ya nguo na mavazi huenda ikawa inapotea chini ya mzigo wa nguo zinazoagizwa kutoka nje.
"Katika duka langu, bei ya chini kabisa ya gauni ni shilingi za kitanzania 50,000 (dola za kimarekani 20)," anasema Elizabeth Paul, mmiliki wa duka la mitindo ya mavazi la Kuya Creations lililopo jijini Dar es Salaam.
Kuya anasema kuwa wengi ushangazwa na biashara yake huku baadhi wakihoji iwapo inamlipa ipasavyo.
Anasema, "Watu wananiambia, Kwa shilingi 50,000 wanaweza kupata magauni 10 ya mitumba, kwa hiyo ngoja waendele kujikita kununua huko badala ya kununua nguo kwangu."
Kwa wengi ni hesabu rahisi inayofanywa maelfu kufika kwenye masoko ya mitumba kila mara na kila siku kote nchini Tanzania.
Kwa watumiaji wanaokabiliwa na gharama kubwa za maisha, mitumba inatoa nafuu na uchaguzi mpana wa mavazi lakini kwa wazalishaji wa mavazi wa ndani, ni ngumu watumiai wengi kuwafikia.
Amina Hassan, mkazi wa Mwanza anasema, " Nguo za mitumba ni za kiwango na bei nafuu, nimeishi nikitumia toka mdogo mpaka sasa nini miaka zaidi ya 30."
Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa pamba barani Afrika. Maelfu ya wakulima hulima zao hilo katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya mavazi yanayovaliwa na Watanzania huagizwa kutoka nje ama kama nguo za mitumba kutoka nchi za Magharibi au kama nguo mpya za bei nafuu kutoka Asia hususani China na Uturuki.
Baadhi ya wadau wa sekta hiyo wanaamini hali hii inaifanya Tanzania kuuza malighafi zake huku ikinunua bidhaa zilizokwisha tengenezwa, jambo linalopunguza fursa za ajira na ukuaji wa viwanda vya ndani.
Hali mbaya kote, si uchumi pekee
Katika Soko la Ilala kama ilivyo masoko mengine Tanzania, wanunuzi huzungumzia kwa msisitizo sababu zinazowafanya wachague mitumba.
"Nguo nyingi zina ubora mzuri. Zinadumu kwa muda mrefu," anasema Najma Issa huku akikagua magauni yaliyopo kwenye eneo lenye watu wengi.
Juma Awadh mwenye umri wa miaka 22 anakubaliana naye, akisema, "Mimi hununua mitumba kwa sababu ya ubora wake na pia zinaonekana za kipekee kutokana na nyingi kuwa na chapa tofauti zenye kutambulika ulimwenguni"
Maoni yao yanaonyesha kwa nini jitihada za kupunguza uingizaji wa mitumba zimekuwa zikikumbana na ugumu mara kwa mara.
Licha ya Tanzania kuweka ushuru wa asilimia 35 kwa nguo za mitumba zinazoagizwa kutoka nje, mahitaji ya bidhaa hizo bado ni makubwa.
Mitumba msingi wa maisha ya watu

Chanzo cha picha, Getty Images
Biashara ya nguo inaendesha maisha ya maelfu ya watu.
Waagizaji, wasafirishaji, wauzaji wa jumla, wafanyabiashara wa masokoni, mafundi wa kushona na wenye maduka madogo madogo katika maeneo ya biashara hutegemea sekta hii kujipatia kipato.
Wanaounga mkono biashara ya mitumba waliiambia BBC kuwa kuzuia uagizaji wake kutawaumiza zaidi Watanzania wa kawaida kuliko itakavyosaidia wazalishaji wa ndani.
Mtafiti wa biashara ya nguo za mitumba duniani, Dkt Andrew Brooks anasema, "Biashara ya rejareja inatengeneza fursa kidogo zaidi za ajira kwenye uchumi wowote ule, tofauti na kwa sekta ya uzalishaji masoko na usambazaji…
"…ukiwa unafanya kazi ya kuagiza bidhaa na kuziuza tu, mchango wako katika uchumi wa taifa unakuwa mdogo sana," anaeleza.
Ni ipi suluhu ya changamoto hizo?
Kwa miaka mingi, serikali zimekuwa zikihamasisha viwanda kama njia ya kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kukuza mauzo ya nje. Serikali imekuwa ikiongeza tozo za bidha zinazotoka nje ili kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya bidhaa za ndani.
Hata hivyo, wazalishaji wa mavazi nchini wanasema wanakabiliwa na ushindani kutoka pande mbili kwa wakati mmoja, mitumba kutoka nje na nguo mpya za bei nafuu zinazoingia kutoka nchi kama China na Uturuki.
Kwa wengi wao, swali si tena kama Tanzania inapaswa kupunguza uingizaji wa mitumba. Swali ni kama nchi inaweza kujenga uwezo wa kutosha wa uzalishaji ili kuziba pengo litakaloachwa na bidhaa hizo.
Je vifaa vya uchakataji suluhisho?
Wataalamu wa uchumi wanasema suluhisho la kudumu litahitaji zaidi kwenye ushuru wa forodha na si kuzuia uagizaji tu wa mitumba
Tayari kwa mwaka wa fedha wa 2026/27, Serikali ya Tanzania imeeleza kuweka mzaingira bora ya uwekezaji katika viwanda vya nguo, unafuu wa kuingiza mitambo ya kisasa ya ushonaji, mafunzo ya ufundi, upatikanaji wa mitaji nafuu kupitia mifuko mbalimbali ya Serikali ikiwemo ya Halmashauri, umeme wa uhakika na ushirikiano imara kati ya wakulima wa pamba na wazalishaji wa mavazi.
"Serikali ioendelee kuongeza nguvu kuhakikisha viwanda vya ushonaji vinakuwa, wakulima wa pamba wanauza ndani. Hakika watu watanunua vya ndani kuliko vile vinavyotoka nje," anasema mbunifu wa mavazi, Heri Anderson anayefanya shughuli zake jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania.
Hali ikoje masoko mengine ya EAC

Chanzo cha picha, Getty Images
Muongo mmoja uliopita, Jumuiya ya EAC ilidai kuwa uwepo wa nguo nyingi za mitumba na hivyo ikalazimika kuweka marufuku katika nchi wanachama wake. Lakini baada ya kukabiliwa vikali na Marekani,ambaye ni moja ya nchi anayeleta mitumba mingi Afrika Mashariki, pendekezo hilo lilisambaratika lakini sasa mjadala umeibuka tena.
Uganda, nchi ambayo rais wake, Yoweri Museveni aliwahi kukosoa nguo za mitumba kuwa zinatoka kwa "watu waliokufa" weupe, imeanzisha ushuru wa ziada wa 30% kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje katika jitihada za kukuza sekta ya nguo za ndani na kulinda mazingira.
Joel Okalany, mbunifu wa mavazi nchini Uganda ambaye chapa yake ya Ekikumba Fusion anasema kuwa Afrika Mashariki haijajiandaa kwa ajili ya kutokomeza mitumba.
"Ukweli ni kwamba, bado hatupo tayari kwa utengenezaji wetu wa nguo kuanza," alisema.
Kwa mujibu wa kituo cha Utafiti wa Sera ya Uchumi kinachofadhiliwa na serikali kilichopatikana mwaka 2024, katika nchi jirani ya Uganda, nguo za mitumba ndizo nguo zinazotafutwa zaidi, zikifuatiwa na nguo mpya zilizoagizwa kutoka nje na kwa uchachee nguo zinazotengenezwa nchini,
Ushuru mpya wa kimazingira wa 30% kwa nguo zilizotumika unakuja juu ya ushuru uliopo wa 35% na 18% ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Kwa mujibu wa muswada wa fedha wa mwaka wa fedha unaoisha 2025/26 wa Uganda, Ushuru wa 30% kwa nguo zilizochakaa unanuiwa kupunguza uharibifu wa mazingira wakati wa kukuza uzalishaji wa ndani.
Tangazo hilo halikuwaendea vyema wafanyabiashara wa mitumba wa Uganda kama vile Aaron Sekky.
"Sikubaliani na hili, kwa sababu huu lazima uwe uchumi huria, biashara ya mitumba "inasaidia watu wengi", " Sekky anasema.
Kenya yakwama

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Serikali ya Kenya ilijaribu kubadilisha jinsi inavyotoza ushuru nguo zilizotumika, ikisema mfumo wake uliopendekezwa utarahisisha mambo kwa waagizaji kutoka nje. Lakini kufuatia msukosuko kutoka kwa Wakenya waliokuwa na wasiwasi kwamba ingesababisha kupanda kwa bei, pendekezo hilo liliondolewa haraka kutoka kwa Mswada wa Fedha wa mwaka 2025/26.
"Tunashindana kuuza dhidi ya nguo za mitumba, lakini hatuwezi kushindana kwa bei, kwanini tusiwe huru kufanya biashara?" anasema Zia Bett, mwanzilishi wa chapa ya Kikenya ya nguo za wanawake Zia Africa.
Katika jitihada za kusaidia watengenezaji wa nguo za nyumbani, Kenya tayari inatoza ushuru wa forodha wa 30% kwa uagizaji wa nguo zilizokwishatumika - 5% zaidi ya gharama ya kusafirisha nguo mpya.
Kulingana na jukwaa la data la biashara la Observatory of Economic Complexity (OEC), Kenya kwa sasa ndiyo inayoongoza barani Afrika kwa kuingiza nguo za mitumba.
Taifa hilo lilipokea karibu tani 180,000 za nguo zilizotumika mwaka 2022 - ongezeko la 76% ya kiasi kilichoagizwa kutoka nje mwaka wa 2013, ni kwa mujibu wa data ya biashara ya Umoja wa Mataifa
Hakuna data rasmi kuhusu idadi ya watu wanaofanya kazi katika sekta hii lakini kulingana na utafiti ulioidhinishwa na Muungano wa Mitumba Consortium Association of Kenya (MCAK), hadi watu milioni 4.9 kote Afrika Mashariki wanategemea biashara ya nguo zilizotumika kufanya kazi.
Lisa Kibutu, mjumbe wa bodi ya Baraza la Mitindo la Kenya, anasema kazi nyingi zinazohusisha mitumba ni majukumu ya "mkono kwa mdomo" ambayo hayaruhusu ukuaji na uhamaji wa kijamii.
Hata hivyo, anaamini pia mavazi yaliyotumika yanatoa huduma muhimu nchini Kenya.
"Nilipoondoka Kenya katika miaka ya 80, ungeona watu maskini bila mavazi. Hivi sasa hata mtu maskini ana mavazi ya heshima," Kibutu, ambaye hapo awali alifanya kazi Marekani kwa wabunifu kama Giorgio Armani na Eileen Fisher, anasema












