Kombe la Dunia 2026: Kibarua kinachoikabili FIFA na Marekani kuhakikisaha ushiriki wa Iran

Iran ilifuzu kwa Kombe la Dunia 2026, lakini kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel, ushiriki wao uko mashakani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Iran ilifuzu kwa Kombe la Dunia 2026, lakini kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel, ushiriki wao uko mashakani.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Iran imedokeza kuwa itashiriki michuano ya Kombe la Dunia msimu huu wa joto, lakini imewasilisha msururu wa maombi kwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) na nchi mwenyeji kutokana na mvutano unaozidi kuongezeka kuhusu ushiriki wake katika mashindano hayo.

Shirikisho la Soka la Iran (FFIRI) limesema wazi kwamba nchi hiyo itashiriki Kombe la Dunia, "bila kujitenga na imani, utamaduni na imani zetu," huku likibainisha kuwa Marekani, nchi ambayo watacheza mechi zao, "lazima itilie maanani ombi letu."

Madai haya yalitolewa baada ya rais wa FFIRI Mehdi Taj kuzuiwa kuingia Canada mwezi uliopita kushiriki katika kongamano la FIFA.

Taj alifichua kuwa Iran iliikabidhi FIFA masharti kumi ya ushiriki wake katika Kombe la Dunia litakaloanza Juni 11 nchini Marekani, Mexico na Canada.

Baadhi ya matakwa hayo, ambayo yalichapishwa wikindi hiyo ni pamoja ni sharti la kuhakikisha kwamba wachezaji, makocha, na maafisa wote wanaosafiri na timu wanapata viza zinazofaa, wakiwemo wale waliomaliza utumishi wao wa lazima wa kijeshi katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC).

Kikosi hiki kipo kwenye orodha ya makundi ya kigaidi ya serikali ya Canada na Marekani, na uhusiano wa Taj na IRGC ndio ulimfanya kukataliwa kuingia Canada.

Iran itacheza mechi zake Inglewood na Seattle.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Iran itacheza mechi zake Inglewood na Seattle.

Iran pia inataka kuhakikishiwa timu yake haitatengwa katika taratibu zingine, kama vile bendera yake na wimbo wa taifa kuheshimiwa, pamoja na usalama katika viwanja vya ndege, hoteli na sehemu zingine wakati wa Kombe la Dunia.

Iran katika jukwaa la ulimwengu

Utekelezaji wa baadhi ya masharti bila shaka itakuwa rahisi kwa FIFA zaidi ya mengine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

FIFA inaweza kudhibiti uratibu wa tukio, itifaki rasmi, mapokezi yanayotolewa kwa kwa wajumbe wakati wa shindano.

Lakini masuala kama vile viza, udhibiti wa mpaka na usalama yako chini ya mamlaka ya nchi mwenyeji, Marekani.

Iran itacheza mechi zake katika miji ya Inglewood, California na Seattle.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio tayari amesema wachezaji wa soka wa Iran wanakaribishwa katika mashindano hayo, japo ameonya kuwa watu binafsi walio na uhusiano na jeshi la Mapinduzi ya Kislamu ya Iran IRGC huenda wakakabiliwa na vikwazo vya kuingia nchini Marekani.

Hili linaiacha FIFA katika njia panda ya kusawazisha mambo kati ya kuhakikisha ushiriki wa timu zote zilizofuzu na kushughulikia hali halisi ya kisiasa inayozunguka uhusiano kati ya Tehran na Washington.

Israel na Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran mnamo Februari 28. Iran ilijibu hatua hiyo kwa mashambulizi ya mabomu dhidi ya Israel na washirika wa Marekani katika mataifa ya Ghuba. Tangu wakati huo, mapigano yamekomeshwa kwa kiwango kikubwa chini ya mpango dhaifu wa usitishaji wa mapigano.

Huenda ikawa vigumu kutekeleza maombi mengine ya shirikisho la Soka la Iran.

Maafisa wa Iran wameripotiwa kuwataka waandishi wa habari kuepuka maswali yaliyo nje ya "maswala ya kiufundi ya soka".

Lakini kwa Iran, mstari kati ya soka na siasa mara nyingi haueleweki.

Maswali kuhusu uteuzi wa timu, usaidizi wa umma kwa timu ya taifa, au mazingira yanayozunguka mechi yanaweza kuwa na nyanja za kimichezo na kisiasa kwa wakati mmoja.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kuwa wachezaji watakuwa na dhamana muhimu ya kushiriki katika hafla hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kuwa wachezaji watakuwa na dhamana muhimu ya kushiriki katika hafla hiyo.

Hili lilidhihirika katika Kombe la Asia la Wanawake nchini Australia mwezi Machi, wakati wachezaji kadhaa wa Iran walipojaribu kutafuta hifadhi, na kusababisha mzozo mkali wa kidiplomasia. Wanachama saba wa timu hiyo walipata viza kwa kwa maslahi ya kibinadamu wakiwa Australia, lakini watano walibadili nia na kurejea Iran.

Kocha wa timu ya taifa ya wanaume ya Iran, Amir Ghalenoei, hivi majuzi alikiri kwamba mzozo wa kisiasa unaweza kugubika baadhi ya mechi za Iran katika Kombe la Dunia.

Licha ya mvutano huo, kwa sasa hakuna dalili zozote zinazoonyesha Iran ina nia ya kujitoa kwenye michuano hiyo.

Matukio ya hivi majuzi yanajikita kwenye mazungumzo yanayozidi kuwa magumu kati ya FIFA, Tehran, na mamlaka za Marekani kuhusu hali inayozunguka ushiriki wa Iran katika Kombe kubwa la Dunia katika historia.

Kutokuwepo kwenye michuano mingine ya Kombe la Dunia

Iran imeweka wazi kuwa itashiriki michuano hiyo - japo wakati mashambulizi ya Marekani na Israel yalipoanza, ilikuwa imeonyesha kwamba haitashiriki - na FIFA inaunga mkono ushiriki wake, lakini katika historia ya Kombe la Dunia kumekuwa na matukio maalum ambapo timu zimekataa kushiriki au hazijaruhusiwa kutokana na migogoro ya silaha au masuala ya kijamii.

Kwa Kombe la Dunia la 1938, timu kama Argentina na Uruguay zilikataa kushiriki kwa sababu FIFA ilikuwa imeahidi haki za mwenyeji kwa nchi ya Amerika Kusini, lakini hatimaye ikawapa Ufaransa.

Kwa Kombe la Dunia la 1950, India ilifanikiwa kufuzu - kwa sababu ya kujiondoa kwa timu zingine kwenye mechi za mchujo - lakini ilikataa kushiriki kwa sababu hawakuzingatia Kombe la Dunia kuwa mashindano yenye thamani ya kusafari mwendo mrefu kama huo.

Afrika Kusini ilifurushwa kwenye shirikisho la soka duniani FIFA kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi katika miaka ya 1970. Ilirudishwa tena mnamo 1992.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Afrika Kusini ilifurushwa kwenye shirikisho la soka duniani FIFA kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi katika miaka ya 1970. Ilirudishwa tena mnamo 1992.

Kwa Kombe la Dunia la 1966, nchi zote za Kiafrika ziliamua kususia hafla hiyo kwa sababu zilipewa nafasi ya nusu tu katika dimba hilo: timu iliyoshinda mechi ya kufuzu kwa bara ililazimika kukabiliana na timu ya Asia.

Migogoro ya silaha pia imekuwa na athari kwenye historia ya mashindano haya.

Kesi ya hivi punde zaidi niile ya Urusi, ambayo kwa sababu ya uvamizi wake nchini Ukraine mnamo 2022, ilizuiwa kushiriki katika mashindano ya FIFA au UEFA (Umoja wa Vyama vya Soka vya Ulaya).

Mnamo 1992, kwa sababu ya uungwaji mkono wa Jamhuri ya Shirikisho ya Yugoslavia (ambayo baadaye ilijulikana kama Serbia na Montenegro) kwa mzozo wa Bosnia-Herzegovina, nchi hiyo iliwekewa vikwazoi na haikuweza kushiriki katika mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la 1994 nchini Marekani.

Kesi nyingine sawa na hiyo ni ile ya Afrika Kusini, ambayo iliondolewa katika michuano ya Kombe la Dunia kwa takriban miaka 30 kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi. Ilizuiwa kwa mduda mnamo 1961, na hatimaye mwaka 1976 ikawa nchi ya kwanza kupigwa marufuku na FIFA kwa mauaji mabaya ya Soweto, ambapo watu 176 walifariki, wengi wao wakiwa wanafunzi wa Kiafrika.

Taarifa ya ziada na Pooria Jafereh, BBC World Service.