Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Nilivutwa kwenye mtego': Mwanahabari asimulia kukamatwa Urusi
- Author, Tiffany Wertheimer
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mwandishi wa Habari wa Marekani Evan Gershkovich amesema alitambua kuwa alikuwa amewekewa mtego na Urusi wakati maafisa wa FSB walipomkamata na kumtuhumu kuwa jasusi.
Katika mahojiano na kipindi cha Today cha Radio 4, Gershkovich alieleza wakati alipotambua kuwa alikuwa "amevutwa kwenye mtego" baada ya wanaume waliovaa barakoa kumzingira katika mkahawa mwaka 2023 na kumkamata.
"Sihojiwi, siteswi... Ninatuhumiwa kwa ujasusi," alisema, akieleza hisia za afueni alizopata: "Wamenitega na kutengeneza kesi hii ili niwe mateka mwenye thamani - chombo katika mchezo mkubwa zaidi."
Gershkovich, ambaye sasa ana umri wa miaka 34, alihukumiwa kifungo cha miaka 16 jela, lakini aliachiliwa baada ya kukaa gerezani kwa miezi 16, katika mabadilishano makubwa ya wafungwa.
Gershkovich alikuwa akiishi Urusi tangu mwaka 2017, na alikuwa mwandishi wa masuala ya kimataifa wa Wall Street Journal mjini Moscow alipokamatwa. Sasa anaishi Berlin, Ujerumani. Yeye pamoja na mwajiri wake wameendelea kusisitiza kuwa mashtaka dhidi yake yalikuwa ya uongo.
Siku aliyokamatwa, Gershkovich alikuwa Yekaterinburg - takriban kilomita 1,600 mashariki mwa Moscow - akikutana na mtu aliyedhani alikuwa chanzo cha habari kwa ajili ya taarifa aliyokuwa akiandaa.
Walikuwa wamekaa katika ukumbi wa chakula uliokuwa karibu tupu, wakati "kundi la takriban wanaume sita waliovaa barakoa waliingia na kusema, 'Nadhani tuliweka nafasi ya meza hiyo.'"
Gershkovich alisema ilikuwa kauli ya ajabu, lakini baadaye aligundua kuwa ilikuwa mbinu nzuri kwa sababu "inakufanya ushindwe kusogea."
Wanaume hao wawili waliinuka na Gershkovich akaambiwa kuwa amekamatwa na FSB, chombo cha usalama wa ndani cha Urusi chenye nguvu na kinachojulikana kwa ukali.
"Ni wakati huo unapogundua kuwa jambo hili ni zito sana... Unapohusisha FSB, unajua kuwa limepangwa."
Gershkovich alijiuliza kuhusu mwanaume aliyekuwa amekutana naye. Alimwona akitoweka katikati ya umati.
Muda mfupi baada ya kukamatwa, mwanahabari huyo alisema aligundua kuwa ukweli kwamba hakuwa akihojiwa wala kuteswa - mbinu zinazodaiwa kutumiwa mara kwa mara na vyombo vya usalama vya Urusi dhidi ya majasusi - huenda ulimaanisha kwamba alikuwa akichukuliwa zaidi kama bidhaa ya kubadilishana, badala ya adui halisi wa serikali.
"Nilipata wakati wa ajabu - hisia za afueni zilinijaa," alisema. "Niligundua kuwa hawakunitendei kama jasusi wa kweli. Wamenitega na kutengeneza kesi hii ili niwe mateka mwenye thamani, chombo katika mchezo mkubwa zaidi. Hiyo inamaanisha itachukua muda, lakini sitakaa hapa kwa miaka 12 hadi 20."
Ufahamu huo ulimsaidia kubaki "mtulivu na mwenye nidhamu gerezani", lakini pia ulimpa namna ya kipekee ya kutabiri kile ambacho kingetokea baadaye - na moja ya makadirio yake ilikuwa kwamba angehusishwa katika mabadilishano ya wafungwa.
"Nilidhani jambo hilo lingekuwa kubwa sana, kwamba lingezua taharuki duniani kote. Yaani, ni mwandishi wa kimataifa wa Wall Street Journal," alisema - na alikuwa sahihi.
Mashirika ya habari duniani kote yaliripoti kuhusu kesi hiyo, picha yake ikaonekana kwenye bango kubwa katika Times Square, na Rais wa wakati huo wa Marekani, Joe Biden, alisema kuwa "hakuna jambo lililopewa kipaumbele zaidi" kuliko kumrudisha Gershkovich nyumbani.
Mwanahabari huyo aliamini kuwa yote hayo yalikuwa sehemu ya mpango wa Moscow - kuwa na mfungwa maarufu ambaye ingeweza kumbadilisha na mmoja wa watu wake - na mtu huyo alikuwa Vadim Krasikov, muuaji aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha nchini Ujerumani.
"Kwa maana fulani, [Moscow] ilifanikiwa kwa sababu hakukuwa na vikwazo vilivyowekwa. Kwa hiyo, ukiangalia kwa mtazamo wa kimkakati, walicheza mchezo huo kwa ustadi sana."
Gershkovich alishikiliwa katika gereza maarufu la Lefortovo mjini Moscow, ambalo kwa miaka mingi limewahi kuwashikilia baadhi ya wafungwa mashuhuri zaidi nchini humo, wakiwemo wafungwa wa kisiasa na wapinzani wa serikali. Wakati wa kipindi cha Great Terror chini ya utawala wa Joseph Stalin katika miaka ya 1930, mateso na mauaji vilikuwa vya kawaida katika gereza hilo.
Alieleza hali hiyo kama "uzoefu wa kutengwa sana", akiwa katika nafasi ndogo sana.
"Hilo linakuchosha kisaikolojia," Gershkovich alisema, lakini akaongeza kuwa alitendewa kwa kiasi kizuri: "Niliruhusiwa kulala, chakula kilikuwa sawa."
Picha za Gershkovich akitabasamu kuelekea kamera wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake mjini Moscow zilisambazwa duniani kote - na alisema hilo lilifanywa kwa makusudi, kama njia ya kuonyesha kuwa alikuwa salama.
"Nilitaka kuwaonyesha watu aina hii ya msimamo wa kutokata tamaa... Tunajua kwamba hii ni kesi iliyotengenezwa, kwa hiyo ikiwa huu ni mchezo wa kuigiza, tusiwaruhusu [Moscow] kuuendesha kwa namna wanayotaka."
Lakini alisisitiza kuwa si kila mtu anayefungwa katika gereza la Urusi hutendewa kama yeye:
"Baadhi ya watu... wanateswa. Wanavunjwa utu wao, wananyimwa chakula, wananyimwa maji ya moto ya kuoga, wanaambiwa kwamba hawatawahi tena kuziona familia zao. Mimi nilitendewa kwa namna tofauti kabisa."
Gershkovich alilinganisha uzoefu wake na kesi ya mwanahabari wa Ukraine Viktoriia Roshchyna, aliyefariki akiwa chini ya ulinzi wa Urusi mwaka 2024 akiwa na umri wa miaka 27. Miezi kadhaa baadaye, mwili wake uliporejeshwa hatimaye, uliripotiwa kuwa na dalili za mateso na baadhi ya viungo vyake vilikuwa vimeondolewa.
Gershkovich alijua kuhusu mpango wa mabadilishano ya wafungwa wiki tatu kabla haujatekelezwa - kipindi alichokieleza kuwa "cha kutesa sana", kwa sababu "sasa kila siku ilionekana kuwa ndefu kwa maumivu."
Hatimaye, mabadilishano hayo yalifanyika tarehe 1 Agosti 2024, na ulikuwa wakati wa "furaha tupu". Lakini baadaye "furaha hupungua, msisimko hushuka, na unakabiliwa na ukweli kwamba sasa lazima urudi kwenye maisha ya kawaida."
Gershkovich alisema kipindi hicho kilikuwa kigumu na wakati mwingine kilimlemea. Hakuwa akilala, alipata mashambulizi ya hofu akiwa katika mikusanyiko mikubwa ya watu na alikuwa na hasira za haraka kwa sababu alikuwa akijaribu kuzuia hisia zake.
Ameonana na wataalamu wa tiba wanaobobea katika tatizo la msongo wa mawazo baada ya tukio la kutisha (PTSD), na alisema pia kuandika kitabu kuhusu yaliyompata kulimsaidia.
Na je, atarudi tena Urusi?
Gershkovich ana historia ndefu na nchi hiyo - wazazi wake walihamia Marekani kutoka Umoja wa Kisovieti katika miaka ya 1970. Alikulia katika familia iliyozungumza Kirusi, akiwa na jina la Kirusi, alihamia Urusi akiwa na umri wa miaka 25 na akapata marafiki wengi huko, akiwemo mpenzi wake wa Kirusi.
"Ningependa kurudi siku moja, lakini nadhani itabidi tusubiri tuone kitakachotokea baada ya [Rais wa Urusi Vladimir] Putin. Na haijulikani kabisa kama serikali itakayofuata itakuwa bora zaidi."
Imetafsiriwa na Faidha Ngaga