Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yasema bado kuna vikwazo kufikia makubaliano na Marekani

Makubaliano yanayojadiliwa yanaripotiwa kuhusisha kuongeza muda wa kusitisha mapigano hadi siku 60, kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz na mpango wa mazungumzo zaidi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Beldeen Waliaula

  1. Iran yasema bado kuna vikwazo kufikia makubaliano na Marekani

    Iran imesema mazungumzo na Marekani yanaendelea licha ya kuwepo kwa “vikwazo” vinavyosababishwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya misimamo ya upande wa Marekani.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesema leo Jumatatu kuwa bado kuna baadhi ya masuala ambayo hayajakamilika, lakini mazungumzo kati ya pande hizo mbili yanaendelea.

    Hata hivyo, ameonya kuwa juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhisho la mgogoro huo zinakabiliwa na “matatizo na vikwazo” vinavyotokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya misimamo pamoja na kauli zinazokinzana kutoka kwa utawala wa Marekani.

    “Mabadiliko ya mara kwa mara ya misimamo na kauli zinazokinzana, ambazo hazihitaji maelezo yangu na unaweza kuziona kwa kutazama tu ujumbe unaotolewa na maafisa wa Marekani, zinaonyesha hali halisi tunayokabiliana nayo na mazingira tunayopaswa kuendesha mchakato wa kidiplomasia,” amesema Baqaei.

    Ameongeza kuwa hali hiyo “kwa kawaida inaleta changamoto na vikwazo vyake” katika mchakato wa mazungumzo ya amani.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Visa vya Ebola nchini Uganda vyaongezeka na kufikia saba

    Uganda imethibitisha visa viwili zaidi vya ugonjwa wa Ebola, Wizara ya Afya ya nchi hiyo imetangaza hii leo, na kufikisha jumla ya visa vilivyoripotiwa kufika saba.

    Visa hivyo viwili vipya ni vya wahudumu wa afya katika kituo binafsi cha matibabu mjini Kampala, na wote ni raia wa Uganda.

    “Wagonjwa wote wawili wamelazwa katika kituo maalum cha matibabu na wanaendelea kupokea matibabu,” Wizara ya afya ya Uganda imesema katika taarifa.

    Uganda ilithibitisha visa vitatu vipya vya Ebola siku ya Jumamosi.

    Mlipuko wa ugonjwa huu uliotokea wilaya ya Ituru nchini DRC ambao unapakana na Uganda.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Ibada za Hija zaanza nchini Saudi Arabia

    Mamilioni ya waumini wa dini ya kiislamu wamewasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija ya mwaka 2026 na tayari wameanza kuelekea eneo la Mina.

    Kulingana na shirika la habari la AFP, kamanda wa Vikosi vya Pasipoti vya Hija vya Saudi Arabia, Saleh bin Saad Al-Murba, alisema Ijumaa kwamba zaidi ya mahujaji milioni 1.5 wamewasili Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija.

    Mamlaka za Saudi Arabia zimesema maandalizi yote ya Hija yamekamilika, huku hatua maalum zikichukuliwa kuwapatia mahujaji huduma hitajika katika miji mitakatifu ya Makka, Mina, Arafat na maeneo mengine matakatifu.

    Taifa hilo limesema limefanya maandalizi makubwa ya kutoa huduma za afya,usafiri, na huduma za kutoa maelekezo kwa lugha mbalimbali.

    Wizara ya Afya ya Saudi Arabia pia imesema kuwa kwa mara ya kwanza mwaka huu, ndege zisizo na rubani zinatumika kutoa huduma za matibabu kwa mahujaji wakati wa ibada ya Hija.

    Tazama picha za mahujaji waliofika Saudi Arabia;

    Pia unaweza kusoma:

  4. Iran yasema haijafikia hatua ya kutia saini makubaliano na Marekani

    Iran imesema wamepiga hatua katika mazungumzo yao na Marekani, “Lakini hakuna dalili ya makubaliano kuafikiwa hivi karibuni”

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Iran, Esmail Baqai, alitoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, kusema kuwa makubaliano yanaweza kuafikiwa hii leo.

    “Ni kweli kusema kwamba tumeafikia makubaliano kuhusu masuala muhimu yaliyokuwa yakijadiliwa, lakini kusema kuwa hii ina maanisha tuko karibu kutia Saini makubaliano hayo si kweli” alisema Baqai.

    Makubaliano yaliyoafikiwa kufikia sasa, yanasemekana kuwa, kuongezwa kwa muda usitishaji mapigano hadi siku 60, kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz na mpango wa nyuklia wa Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Spika wa Senegal ajiuzulu, siku mbili tu baada ya waziri mkuu kufutwa kazi

    Spika wa bunge la Senegal, El Malick Ndiaye, amejiuzulu, siku mbili tu baada ya rais wa taifa hilo kumfuta kazi Waziri mkuu, Ousmane Sonko.

    Ndiaye alisema hapo jana kuwa kuondoka katika wadhfa wake, ni uamuzi wake binafasi na amezingatia maslahi ya taifa.

    Spika huyo ni miongoni mwa wanachama wa chama cha PASTEF kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri mkuu Ousmane Sonko, na kina kinaongoza kuwa na wawakilishi wengi bungeni.

    Kuondoka kwa Ndiaye, kunazidisha msukosuko wa kisiasa ambao tayari unatokokota katika taifa hil na Afrika Magharibi.

    Kulingana na wachambuzi, huenda rais wa Senegal Diomaye Faye, akapata wakati mgumu kuingoza taifa hilo na kupitisha sheria, kutoka na wengi wa wawikilishi wa bunge kuwa wanachama wa PASTEF.

    Rais Faye alimfuta kazi Waziri mkuu Ousmane Sonko siku ya Ijumaaa, baada ya miezi kadhaa ya mvutano baina ya viongozi hao wawili.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Marekani, Iran huenda zikafikia makubaliano leo - Rubio

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa wapatanishi wa Marekani na Iran wana kile alichokiita “mapendekezo madhubuti mezani”, na kwamba makubaliano kati ya nchi hizo mbili yanaweza kufikiwa leo Jumatatu.

    “Bado tuko katika mchakato wa mazungumzo,” Rubio amesema akiwa katika ziara nchini India.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kusema kuwa amewaagiza wapatanishi kutoharakisha kufikia makubaliano, licha ya kuwa hapo awali alikuwa ameashiria kuwa mwafaka ulikuwa karibu kupatikana.

    Makubaliano yanayojadiliwa yanaripotiwa kujumuisha kuongezwa kwa muda wa usitishaji mapigano kwa siku 60, kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz na mpango wa kuendelea na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano hayo yalisababisha bei za mafuta kushuka kwa kiasi kikubwa huku masoko ya hisa ya Asia yakipanda siku ya Jumatatu.

    Akizungumza mjini Delhi, Rubio alisema:

    “Bado tuko katika hatua ya mazungumzo. Tulidhani huenda tungepata taarifa muhimu jana usiku, lakini pengine leo.”

    Aliongeza kuwa kuna msingi imara wa makubaliano kuhusu kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya majini inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa inayouzwa duniani, na ambayo imekuwa ikizuiwa na Iran.

    Hata hivyo, Rubio alionya dhidi ya kutoa hitimisho la haraka, akisema kuwa bado inachukua muda kupata majibu kutoka Iran.

    Wakati huo huo, kwa mujibu wa CBS News, mashirika ya kijasusi ya Marekani yanaamini kuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, ambaye alijeruhiwa katika shambulio la Israel siku ya kwanza ya vita, yuko katika eneo lisilojulikana. Ripoti hiyo inaeleza kuwa hali hiyo imefanya mawasiliano kati yake na wajumbe wake kuwa magumu na hivyo kupunguza kasi ya mazungumzo na Marekani.

    Mwishoni mwa wiki, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema kuwa pande hizo mbili ziko “karibu sana na pia mbali sana” na kufikia makubaliano.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, makubaliano yanayojadiliwa kwa sasa si suluhisho la mwisho, bali yanaacha baadhi ya masuala magumu zaidi yaamuliwe katika mazungumzo ya baadaye.

    Miongoni mwa masuala hayo ni muda na kiwango cha kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran, kuachiliwa kwa fedha za Iran zilizozuiwa nje ya nchi, pamoja na matakwa ya Washington ya kuizuia Iran kuendeleza shughuli zake za nyuklia.

    Soma zaidi:

  7. Bei ya mafuta yashuka kutokana na matumaini ya makubaliano kati ya Marekani na Iran

    Bei za mafuta duniani zimeshuka kwa kiwango kikubwa huku masoko ya hisa ya Asia yakipanda, kufuatia matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano ambayo yanaweza kumaliza vita kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, akiwa katika ziara nchini India, amesema kuwa wapatanishi wana “mapendekezo madhubuti mezani” na kwamba makubaliano ya kumaliza mzozo huo yanaweza kufikiwa Jumatatu.

    Asubuhi ya Jumatatu, mafuta ghafi ya Brent, ambayo ni kigezo kikuu cha bei za mafuta duniani, yalishuka kwa asilimia 5.5 hadi dola 97.90 kwa pipa, huku mafuta ghafi yanayouzwa nchini Marekani yakishuka kwa asilimia 5.9 hadi dola 90.93 kwa pipa.

    Awali, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema kuwa makubaliano hayo yatajumuisha kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, ingawa hakutoa maelezo zaidi.

    Kwa upande wake, Iran imesema kuwa misimamo ya Tehran na Washington imekuwa ikikaribiana katika kipindi cha wiki iliyopita.

    Mlango Bahari wa Hormuz, ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) inayouzwa duniani, umekuwa ukikumbwa na vikwazo vya usafiri tangu kuanza kwa mzozo huo mnamo Februari 28.

    “Bado mazungumzo yanaendelea. Tulitarajia huenda tungepata taarifa muhimu jana usiku, lakini pengine zitapatikana leo,” amesema Rubio akiwa mjini Delhi.

    Kauli yake imekuja baada ya Trump kusema kuwa amewaagiza wapatanishi wa Marekani kutoharakisha kufikia makubaliano, licha ya kuwa hapo awali alikuwa ameashiria kuwa mwafaka ulikuwa karibu kupatikana.

    Soma zaidi:

  8. Lissu afika Mahakama Kuu kusikiliza shauri la kesi ya mali za CHADEMA

    Mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha CHADEMA, Tundu Lissu, amewasili katika Mahakama Kuu, Masijala ya Dar es Salaam, ambako shauri lake litaanza kusikilizwa leo Mei 25, 2026.

    Kesi hiyo inahusu ombi lake la kutaka kuunganishwa katika shauri linalohusu mali za chama hicho, lililofunguliwa na Saidi Issa Mohamed pamoja na wenzake wawili.

    Shauri hilo linatarajiwa kuamua iwapo Lissu ataruhusiwa kuwa sehemu ya mchakato wa kesi inayohusiana na mgogoro wa mali za chama hicho cha upinzani.

    Soma zaidi:

  9. Papa kutoa waraka mkubwa kuhusu akili unde (AI)

    Papa Leo XIV anatarajiwa Jumatatu ya leo kutoa waraka wake uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu kuhusu akili unde (AI), katika juhudi za kushughulikia changamoto za kimaadili na kijamii zinazotokana na maendeleo ya haraka ya teknolojia hiyo duniani.

    Papa huyo raia wa Marekani atahudhuria hafla ya uzinduzi wa waraka huo uitwao “Magnifica Humanitas” (Ubinadamu wa Ajabu) katika mji wa Vatican, hatua inayoelezwa kuwa ya kwanza ya aina yake katika Kanisa Katoliki.

    Katika hafla hiyo atajiunga na maafisa wa Vatican pamoja na wataalamu wa teknolojia, akiwemo mmoja wa waasisi wa kampuni ya Marekani ya Anthropic, kampuni inayochukuliwa kuwa mchezaji muhimu katika sekta ya akili mnemba inayokua kwa kasi.

    Anthropic kwa sasa iko katika mgogoro wa kisheria na jeshi la Marekani baada ya kukataa kubadilisha sera yake inayokataza matumizi ya mfumo wake wa Claude katika vita vya kujiendesha kiotomatiki vinavyoweza kusababisha vifo au ufuatiliaji wa watu kwa wingi.

    Papa Leo XIV amekuwa akikosoa mbio za kuendeleza AI katika sekta ya kijeshi, akisema kuwa “kukabidhi maamuzi ya uhai na kifo cha binadamu kwa mashine” ni “mzunguko hatari unaoharibu maadili ya binadamu”.

    Tangu achaguliwe mwaka mmoja uliopita kama Papa wa kwanza kutoka Marekani, amekuwa akionya mara kwa mara kuhusu hatari za AI, ikiwemo kile alichokiita “kuongezeka kwa uhalisia bandia unaochukua nafasi ya uhalisia halisi wa maisha ya binadamu.”

  10. Shambulio kubwa la Urusi dhidi ya Ukraine laua watu wanne na kujeruhi makumi

    Urusi imefanya mashambulizi makubwa na ya maangamizi dhidi ya Ukraine usiku wa kuamkia Jumamosi, ikirusha mamia ya droni na makombora kadhaa.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amesema mji mkuu Kyiv ndio ulikuwa shabaha kuu, ingawa maeneo mengine pia yalilengwa, huku takribani watu 100 wakijeruhiwa.

    Watu wanne waliuawa katika mji mkuu na maeneo ya karibu, huku milipuko ikisikika usiku kucha.

    Mamia ya majengo ya makazi, shule, nyumba ya opera na jumba la makumbusho yaliharibiwa.

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kuwa ilitumia kombora la hypersonic aina ya Oreshnik katika mashambulizi hayo, ambayo ilieleza kuwa ni kujibu “mashambulizi ya Ukraine dhidi ya miundombinu ya kiraia”. Hata hivyo, jeshi la Ukraine limekanusha kulenga raia.

    Mapema Jumatatu, miundombinu ya nishati iliharibiwa katika shambulio la makombora katika eneo la Belgorod nchini Urusi linalopakana na Ukraine, ikiwa ni pamoja na mji wa Belgorod, kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax likinukuu mamlaka za eneo hilo.

    Hakukuwa na vifo vilivyoripotiwa, lakini huduma za umeme na maji zilikatika, taarifa hiyo ilisema.

    Eneo la Yaroslavl nchini Urusi, kaskazini mashariki mwa Moscow, pia lililengwa na mashambulizi ya droni, gavana wake Mikhail Yevrayev alisema kupitia Telegram.

    Rais wa Urusi Vladimir Putin alianzisha uvamizi mkubwa dhidi ya Ukraine Februari 2022.

    Jeshi la Ukraine limesema pia lilifanya shambulio katika eneo la Starobilsk lililoko mashariki mwa Ukraine linalodhibitiwa na Urusi usiku wa Ijumaa, likieleza kuwa lililenga kitengo maalum cha kijeshi cha droni cha Urusi.

    Viongozi wa Ulaya wamelaani mashambulizi hayo ya Urusi yaliyofanyika mapema Jumapili, yakija baada ya onyo la Zelensky kwamba Urusi ilikuwa inapanga mashambulizi mapya na huenda ilijiandaa kutumia kombora la Oreshnik.

    Inaripotiwa kuwa kombora hilo husafiri kwa kasi zaidi ya mara 10 ya sauti, ni vigumu kulizuia, na lina uwezo wa kubeba vichwa vya kawaida na vya nyuklia.

    Soma zaidi:

  11. Zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa ni Ebola vimegundulika DR Congo - WHO

    Zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa kuwa Ebola, ikiwemo visa 101 vilivyothibitishwa, vimegunduliwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, siku ya Jumapili.

    Haya yanajiri baada ya wakazi wenye hasira katika mji ulio katika kitovu cha mlipuko wa Ebola mashariki mwa Kongo kushambulia na kuchoma hema lililokuwa sehemu ya kituo cha afya kinachotibu wagonjwa wa virusi hivyo, wahudumu wa afya wamesema Jumamosi. Tukio hilo lilikuwa la pili la aina hiyo katika eneo hilo ndani ya wiki moja.

    Kwa mujibu wa taarifa za awali, hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulio hilo, lakini wagonjwa walipokimbia ili kuepuka moto huo, watu 18 wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola walitoroka katika kituo hicho na hadi sasa hawajulikani walipo, alisema mkurugenzi wa hospitali ya eneo hilo.

    Wakazi hao wenye hasira walifika katika kliniki iliyopo katika mji wa Mongbwalu usiku wa Ijumaa na kuchoma moto hema lililokuwa limewekwa kwa ajili ya wagonjwa wanaoshukiwa na waliothibitishwa kuwa na Ebola, lililokuwa likiendeshwa na shirika la misaada la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), alisema Dk. Richard Lokudi, mkurugenzi wa hospitali ya Mongbwalu, akizungumza na shirika la habari la Associated Press.

    “Tunalilaani vikali tukio hili, kwani limesababisha hofu miongoni mwa wahudumu na pia kusababisha kutoroka kwa watu 18 wanaoshukiwa kuambukizwa katika jamii,” alisema.

    Siku ya Alhamisi, kituo kingine cha matibabu katika mji wa Rwampara kilichomwa moto baada ya ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua mwili wa mwanafamilia wao aliyeshukiwa kufariki kutokana na Ebola.

    Soma zaidi:

  12. Mshukiwa wa shambulio karibu na Ikulu ya Marekani atambuliwa

    Siku moja baada ya milio ya risasi kusikika karibu na Ikulu ya Marekani na maafisa wa usalama kutangaza kuwa mshukiwa alipigwa risasi na kuuawa na maafisa wa siri waliokuwa kazini, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti utambulisho na historia ya mtu huyo.

    Kwa mujibu wa CBS, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani, mshukiwa aliyetekeleza shambulio hilo ametambuliwa kuwa Nasser Best, mwenye umri wa miaka 21, ambaye alikuwa akifahamika kwa vyombo vya sheria na alikuwa na historia ya matatizo ya afya ya akili.

    Milio ya risasi ilisikika muda mfupi baada ya saa kumi na mbili jioni kwa saa za Washington siku ya Jumamosi, hali iliyowalazimu waandishi wa habari waliokuwa wakirusha matangazo nje ya Ikulu ya Marekani kujilaza chini na kukimbilia ndani ya jengo hilo kwa usalama.

    Maafisa wa Ujasusi wa Marekani waliokuwa wakilinda eneo hilo walijibu mashambulizi hayo kwa kufyatua risasi na kumlenga mshukiwa.

    Baada ya tukio hilo, mshukiwa alikimbizwa hospitalini lakini baadaye alitangazwa kufariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata.

    Mtu mmoja aliyekuwa karibu na eneo la tukio pia alijeruhiwa, ingawa maafisa wa idara ya upelelezi hawakutoa taarifa zaidi kuhusu hali yake. Hakuna afisa wa usalama aliyeripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo.

    Vyanzo vinavyofahamu uchunguzi huo vimesema mshukiwa alitumia bastola aina ya revolver kutekeleza shambulio hilo.

    Chanzo kimoja kilichozungumza na CBS kuhusu uchunguzi huo kilisema kuwa Nasser Best aliwahi kujaribu kuingia katika Ikulu ya Marekani mwezi Julai 2025, na baadaye alipelekwa katika kituo cha afya ya akili baada ya kukamatwa na maafisa wa usalama karibu na jengo hilo.

    Kwa mujibu wa taarifa hizo, alikuwa akiishi mjini Washington, D.C., kwa miezi 18 iliyopita.

    Soma zaidi:

  13. Asilimia 95 ya makubaliano kati ya Iran na Marekani imekamilika - Fox News

    Shirika la habari la Marekani, Fox News, limeripoti kuwa maafisa waserikali wametangaza kwamba asilimia 95 ya masharti ya makubaliano yanayojadiliwa kati ya Tehran na Washington tayari yamekamilishwa.

    Katika vipindi vyake vya habari na uchambuzi vilivyorushwa Jumapili, Fox News ilijadili maendeleo ya mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Iran, huku wachambuzi na wageni mbalimbali wakieleza kuwa pande hizo mbili zimepiga hatua katika masuala muhimu, yakiwemo kuongeza muda wa usitishaji mapigano, kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz na kuondolewa kwa vikwazo vya kijeshi vya majini dhidi ya Iran.

    Hata hivyo, FOX News pia iliangazia wasiwasi uliopo miongoni mwa baadhi ya wanasiasa na wadau wa kisiasa nchini Marekani kuhusu misimamo ya serikali ya Iran, kwa kuonyesha matamshi ya hivi karibuni ya Mohsen Rezaei, aliyewahi kuwa kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

    Katika kauli yake ya karibuni, Rezaei alionya kuwa Iran inaweza kujiondoa katika Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) ikiwa hali ya sasa itaendelea bila mabadiliko.

    Kauli hiyo imeongeza uzito wa mjadala kuhusu mustakabali wa mazungumzo hayo, wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu kwa mzozo uliopo kati ya Iran na Marekani.

    Soma zaidi:

  14. Mwanaanga wa China kuishi mwaka mzima anga za juu huku Beijing ikijipanga kuelekea Mwezini

    China imezindua safari mpya ya anga za juu inayojumuisha watu watatu kuelekea kituo chake cha anga cha Tiangong Space Station, ambapo mmoja wa wanaanga hao atatumia mwaka mzima akiwa katika mzunguko wa Dunia.

    Hatua hiyo inachukuliwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya mpango wa Beijing wa kupeleka binadamu Mwezini ifikapo mwaka 2030.

    Misheni hiyo, inayojulikana kama Shenzhou-23, imezinduliwa siku ya Jumapili kwa kutumia roketi ya Long March 2F kutoka kituo cha kurushia vyombo vya anga cha Jiuquan kilichopo katika Jangwa la Gobi, kaskazini magharibi mwa China.

    Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, China imewekeza mabilioni ya dola katika sekta ya anga huku ikilenga kujiimarisha kama moja ya mataifa yanayoongoza katika uchunguzi wa anga za juu.

    Tangu mwaka 2021, misheni za Shenzhou zimekuwa zikituma wanaanga watatu kwa wakati mmoja katika kituo cha Tiangong kwa safari za takribani miezi sita. Hata hivyo, safari hii itakuwa ya kipekee kwa kuwa itashuhudia mwanaanga mmoja akibaki angani kwa muda wa mwaka mzima kwa mara ya kwanza katika historia ya mpango wa anga wa China.

    Miongoni mwa wanaanga walioko katika misheni hiyo ni Li Jiaying mwenye umri wa miaka 43, ambaye amekuwa mwanaanga wa kwanza kutoka Hong Kong kushiriki katika safari ya anga. Kabla ya kujiunga na mpango wa anga wa China, Li aliwahi kufanya kazi katika jeshi la polisi la Hong Kong.

    Wanachama wengine wa misheni hio ni Zhu Yangzhu, mhandisi wa anga mwenye umri wa miaka 39, na Zhang Zhiyuan, mwenye umri wa miaka 39 na aliyekuwa rubani wa Jeshi la Anga la China. Kwa wote wawili, hii ni safari yao ya kwanza kwenda angani.

    Wakiwa katika kituo cha Tiangong, wanaanga hao wanatarajiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kisayansi inayohusu sayansi ya maisha, sayansi ya vifaa, fizikia ya vimiminika na tiba.

    Jaribio muhimu zaidi katika misheni ya Shenzhou 23 ni kufuatilia athari za kukaa kwa muda mrefu katika mazingira yenye mvutano mdogo wa nguvu za uvutano yaani gravity. Utafiti huo unalenga kusaidia maandalizi ya safari za baadaye za kuelekea Mwezini na hata sayari ya Mirihi.

    Shirika la Anga la China limesema kuwa mwanaanga atakayechaguliwa kubaki angani kwa mwaka mmoja atatangazwa baadaye kulingana na maendeleo ya misheni hiyo.

    Mtaalamu wa unajimu na profesa katika Chuo Kikuu cha Macquarie nchini Australia, Richard de Grijs, amesema changamoto kuu za safari za muda mrefu angani ni pamoja na kupungua kwa msongamano wa mifupa, kudhoofika kwa misuli, kuathiriwa na mionzi ya anga, matatizo ya usingizi pamoja na uchovu wa kisaikolojia na kitabia.

    Ameongeza kuwa mifumo ya uhakika ya kuchakata maji na hewa, pamoja na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya mbali na Dunia, ni mambo muhimu yatakayochangia mafanikio ya safari za muda mrefu za anga katika siku zijazo.

    Soma zaidi:

  15. Katika Picha: Jinsi Arsenali ilivyosherehea kukabidhiwa rasmi kombe la EPL 2026

    Ilikuwa siku ya kipekee kwa kocha Mikel Arteta kuifurahia. Akiwa mbele ya mmiliki wa klabu, Stan Kroenke, ambaye alishuhudia mchezo huo akiwa uwanjani katika moja ya ziara zake nadra za kuifuatilia timu ana kwa ana, Arsenal walisherehekea ubingwa wao wa kwanza wa ligi tangu mwaka 2004 baada ya kuichapa kwa urahisi Crystal Palace.

    Arsenal walithibitisha ubora wao kwa ushindi huo muhimu, huku Crystal Palace wakionekana kuwa na mawazo zaidi kuelekea fainali yao ya michuano ya Ulaya inayowasubiri. Ushindi huo ulihitimisha safari ndefu ya kusaka taji la ligi na kuwapa Mashabiki wa Arsenal sababu ya kushangilia baada ya kusubiri kwa zaidi ya miongo miwili.

  16. Trump: Nimewaagiza wapatanishi kutoharakisha kufikia makubaliano na Iran

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema amewaagiza wapatanishi wa Marekani “kutoharakisha kufikia makubaliano” na Iran, baada ya hapo awali kuashiria kuwa pande hizo zilikuwa karibu kufikia mwafaka.

    Makubaliano yanayojadiliwa yanaripotiwa kujumuisha kuongezwa kwa usitishaji mapigano kwa siku 60, kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz, pamoja na mpango wa kuendelea na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema mazungumzo yanaendelea kwa “mtazamo chanya”, lakini akasisitiza kuwa:

    “Pande zote mbili zinapaswa kuchukua muda wao na kuhakikisha kila jambo linafanyika kwa usahihi.”

    Siku ya Jumamosi, Trump alisema kuwa makubaliano hayo yalikuwa “kwa kiasi kikubwa yamejadiliwa”, hali iliyozua matarajio kwamba tangazo rasmi lingeweza kutolewa wakati wowote.

    Kwa upande wake, maafisa wa Iran pia wameashiria kuwepo kwa maendeleo katika mazungumzo hayo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema kuwa pande hizo mbili ziko:

    “Karibu sana sio mbali sana” kufikia makubaliano.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, makubaliano yanayojadiliwa kwa sasa si suluhisho la mwisho, bali yanaacha baadhi ya masuala magumu zaidi yaamuliwe katika mazungumzo ya baadaye.

    Masuala hayo ni pamoja na matakwa ya Iran ya kuondolewa vikwazo vya kiuchumi, kurejeshewa fedha zake zilizozuiwa nje ya nchi, pamoja na shinikizo la Washington kwa Iran kupunguza shughuli zake za nyuklia.

    Ripoti hizo pia zinasema kuwa mapendekezo ya makubaliano hayo yamezua mgawanyiko ndani ya Chama cha Republican, huku baadhi ya wanachama wakidai kuwa masharti yake yanaipa Iran nafuu kubwa kupita kiasi.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo ya Jumatatu ya tarehe 25 mwezi Mei 2026.