Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Raúl Castro akabiliwa na mashataka ya uhalifu lakini chanzo cha migogoro kati ya Cuba na Marekani ni nini?
Ajali mbaya ya ndege mbili zilizotokea pwani ya Florida zaidi ya miaka 30 iliyopita ndiyo chanzo cha mashtaka ya uhalifu dhidi ya kiongozi wa zamani wa Cuba Raúl Castro, Marekani imefichua hayo siku ya Jumatano.
Shambulio la jeshi la Cuba dhidi ya ndege za raia lilisababisha moja ya migogoro mikubwa zaidi kati ya Cuba na Marekani, huku athari zake zikiendelea hadi leo.
Ndege za kivita za Cuba zilidungua ndege mbili ndogo - ambazo zilikuwa za kundi la wakimbizi wa Cuba huko Miami - katika njia ya maji kati ya taifa la kisiwa cha Caribbean na jimbo la Florida la Marekani, huku wote wanne waliokuwa ndani ya ndege wakiuawa papo hapo.
Shambulio hilo lilishutumiwa vikali kimataifa, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Raúl Castro, ambaye alikuwa waziri wa jeshi la Cuba wakati huo.
Tukio hilo lilisababisha Marekani kuimarisha vikwazo dhidi ya utawala wa kaka yake Fidel Castro, na kufuta uwezekano wowote wa mazungumzo kati ya Cuba na utawala wa Rais wa Marekani Bill Clinton.
Raúl Castro - kaka yake Fidel Castro - aliachia rasmi urais wa Cuba na uongozi wa Chama cha Kikomunisti mwaka wa 2021, lakini bado anachukuliwa na wengi kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini humo.
Mashtaka ya Castro yanatokea kipindi ambapo kisiwa hicho kinapitia wakati mgumu sana.
Cuba iko kwenye misukosuko ya kiuchumi na nishati kufuatia shinikizo la hivi karibuni kutoka kwa utawala wa Donald Trump na kupoteza uungwaji mkono kutoka Venezuela baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa zamani Nicolás Maduro mnamo mwezi Januari.
Uhaba wa chakula wasababisha wengi kutoroka Cuba
Shambulio hilo la ndege lilitokea wakati wa mgogoro mkubwa wa kiuchumi ulioikumba Cuba miaka ya 1990 baada ya kuanguka kwa mfuasi wake mkuu wa kiuchumi, Umoja wa Kisovieti.
Kisiwa hicho kilitumbukia katika hali mbaya ya kiuchumi, huku kukiwa na kukatika kwa umeme, uhaba wa chakula, na ukosefu wa mafuta.
Mgogoro huo, ambao wengi wanaulinganisha na ule wa sasa, uliwafanya maelfu ya Wakuba kujaribu kuondoka kisiwani humo ili kuungana tena na wanafamilia nchini Marekani.
"Ghafla, kila mtu alianza kutafuta chochote kilichokuwa kikielea kujaribu kufika Florida," mwanahistoria wa Cuba Juan Antonio Blanco, ambaye alikuwa mwanadiplomasia huko Havana wakati tukio hilo linapotokea, aliambia BBC Mundo.
Shirika la 'Brothers to the Rescue' liliibuka haraka huko Miami. Lilianzishwa na wakimbizi wa Cuba na kuongozwa na José Basulto.
Kundi hilo lilianza kuendesha safari za ndege kupitia Mlango-Bahari wa Florida, likitafuta boti zilizokuwa zimewabeba wahamiaji wa Cuba.
"Tulijaribu kuwatafuta, kujua walipo, na kuwafahamisha Walinzi wa Pwani wa Marekani ili waweze kuwaokoa," Basulto, 85, kiongozi wa kundi la Brothers to the Rescue aliiambia BBC Mundo.
Pia walidondosha maji na chakula kwenye maboriti. Lakini, kadiri muda ulivyokuwa unaenda, kundi hilo lilifanya mengi zaidi.
"Waliacha kufanya walichosema walitaka kufanya, ambacho kilikuwa ni kusaidia kuokoa waliokuwa wakisafiri, na wakaanza kuingia katika anga ya Cuba na kudondosha vipeperushi juu ya eneo la Havana," mwanasayansi wa siasa wa Cuba Carlos Alzugaray aliambia BBC Mundo kutoka Havana.
Cuba ilianza kulaani mashambulizi ya anga na kuwaona wanachama wa Brothers to the Rescue kama "magaidi", ikidai kwamba walikuwa tishio kwa usalama wa taifa.
Basulto, ambaye aliongoza baadhi ya operesheni hizo, ana mtazamo tofauti.
"Kwao, ilikuwa ugaidi kwa sababu vipeperushi tulivyodondosha vilikuwa na Azimio la Haki za Binadamu Ulimwenguni, na hilo lilipigwa marufuku nchini Cuba," alisema.
'Niliona moshi wakati ndege ikidunguliwa'
Ndege tatu za Cessna za kundi la Brothers to the Rescue zilipaa kutoka Florida tarehe 24 Februari 1996, kwa ajili ya misheni ya kawaida juu ya mlango-bahari wa Florida.
Kwa kipindi cha dakika sita, mbili kati ya hizo zilidondoshwa na ndege za kivita za Cuba.
Watu wote wanne waliokuwa ndani ya ndege hizo waliuawa: Armando Alejandre Jr, 44, Carlos Alberto Costa, 29, Mario Manuel de la Peña, 24, Pablo Morales, 29. Wote walikuwa raia wa Marekani isipokuwa Pablo Morales, ambaye alikuwa raia wa Cuba.
Ndege ya tatu ilifanikiwa kutoroka. Iliongozwa na José Basulto. "Nilitazama kulia na kuona moshi kwa mbali kutoka kwa moja ya ndege iliyodunguliwa," alisema.
"Mara moja nilimtazama Sylvia Iriondo [aliyejitolea katika misheni] na kumwambia, 'sisi ndio tunaofuata.'"
Basulto alisema ndege yake ndiyo "waliyokuwa wakitaka kuidondosha hasa kwa sababu mimi ndiye nilikuwa kiongozi wa kundi hilo".
Makombora kutoka kwa ndege za kivita za Cuba yaliharibu kabisa ndege ndogo za kiraia – kiasi kwamba hakukuwa na ushahidi wowote uliobaki.
Basulto alisisitiza kwamba ndege hizo zilikuwa "katika maji ya kimataifa, kaskazini mwa Havana" ziliposhambuliwa. Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga na Shirika la Marekani lenye makao yake makuu nchini Marekani lilithibitisha hili na kuishutumu Cuba kwa kukiuka sheria za kimataifa.
Lakini serikali ya Cuba imekuwa ikisisitiza kwamba ilidungua ndege hizo ndani ya anga lake.
Mwanahistoria Juan Antonio Blanco alielezea tukio hilo kama "shambulio lililopangwa na Fidel Castro".
"Fidel Castro alijua mapema ni nani angekuwa rubani siku hiyo, ni ndege gani zingekuwa safarini, na njia watakayopita," alisema, akiongeza kwamba huduma za ujasusi za Castro zilikuwa na jasusi ndani ya kundi la Brothers to the Rescue.
Kulingana na Blanco, Fidel Castro alihusika kisiasa na operesheni hiyo, huku Raúl Castro, ambaye wakati huo alikuwa waziri wa majeshi, akiwa ndiye mtekelezaji wake.
Brothers to the Rescue ina rekodi ya wakati huo kwenye tovuti yake, ambapo Raúl Castro, anayedaiwa kuzungumza na waandishi wa habari wa Cuba, anatoa maelezo ya operesheni iliyofanywa chini ya uongozi wake.
Rekodi hiyo ilivuja mwaka wa 2006 na kufika mikononi mwa waandishi wa habari, wataalamu, na maafisa wa zamani wa Cuba waliotoroka na kukimbilia Marekani, ambao walithibitisha ukweli wake.
BBC Mundo haijaweza kuithibitisha kwa kujitegemea.
Kwa nini Cuba ilidondosha ndege hizo?
Sababu zilizofanya serikali ya Fidel Castro iamue kudungua ndege hizo bado ni mada ya kujadiliwa.
Maelezo rasmi ya Cuba - ambayo yanasisitiza kwamba tukio hilo lilitokea katika anga yake - ni kwamba kundi la Brothers to the Rescue walikuwa tishio kwa usalama wa taifa kutokana na mashambulizi yake ya mara kwa mara ya angani.
Lakini tafsiri zingine zinaonyesha hatua zao kilichochewa kisiasa.
Blanco, ambaye wakati huo alishiriki katika njia zisizo rasmi za mawasiliano kati ya Havana na Washington, anaamini kwamba Fidel Castro alijaribu kuzuia uwezekano wa uhusiano wa karibu na Marekani.
Anaeleza kwamba, miezi kadhaa kabla ya shambulio hilo, maafisa wa Cuba na Marekani walikuwa wakichunguza kwa siri uwezekano wa kurejesha uhusiano wa kawaida, kwa kutarajia muhula wa pili wa Bill Clinton.
Mwanahistoria huyo alisema kwamba Castro aliogopa kwamba uhusiano wowote na Marekani ungechochea mageuzi ya kisiasa na kiuchumi katika kisiwa hicho ambayo yangehatarisha mamlaka yake kamili.
"Kudungua ndege hizo kulimfanya Clinton asiweze kuingia katika aina yoyote ya upatanishi baadaye," alisema.
Mgogoro uliosababisha kuzorota kwa uhusiano wa Marekani na Cuba
Tukio hilo lilisababisha mgogoro mkubwa zaidi kati ya Cuba na Marekani tangu Vita Baridi na kuwa mwelekeo wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili hadi karne ya 21.
Bill Clinton alilaani shambulio hilo "kwa maneno makali zaidi," na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani matumizi ya silaha dhidi ya ndege za kiraia angani.
Marekani iliimarisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba kwa kiasi kikubwa, na Havana ilichukulia jibu lao kuwa uchokozi wa kiuchumi na kidiplomasia ambao haujawahi kutokea.
Kipindi hicho, kulingana na mwanahistoria na mwanadiplomasia wa zamani, pia kulikuwa na athari za ndani ya Cuba.
"Ilirudisha sera ya kiimla, ambayo ilikuwa mbaya zaidi," Blanco alisema, akiongeza kuwa ukandamizaji uliongezeka baada ya tukio hilo.
Havana ilikataa kulipa fidia, na familia zao hatimaye zililipwa na serikali ya Marekani kwa kutumia mali zilizozuiliwa za dola milioni 93 za utawala wa Cuba.
Miaka 30 baadaye, kesi hiyo ina uzito mkubwa kiishara ya kisiasa nchini Cuba na miongoni mwa jamii ya wakimbizi wa Cuba.