Mahakama yaagiza Lissu ajibiwe ndani ya siku 7

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imetoa siku saba kwa wajibu maombi katika kesi inayohusisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ili kujibu maombi yake ya kutaka kuunganishwa katika shauri la mgawanyo wa mali ndani ya chama hicho.

Kesi hiyo namba 8323 inaendelea kusikilizwa mbele ya Jaji David Ngunyale.

Shauri hilo limefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA, Said Mohamed, pamoja na wajumbe wawili wa bodi ya wadhamini wa CHADEMA Zanzibar, Ahmed Rashid na Maulida Komu ambaye sasa ni marehemu. Walalamikaji hao wanapinga mgawanyo wa mali unaohusiana na chama hicho kati ya Tanzania bara na Zanzibar.

Awali Tundu Lissu aliomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo akidai ana maslahi ya moja kwa moja katika shauri hilo. Hata hivyo, mahakama ilikataa ombi hilo awali, kabla ya sasa kufungua tena maombi mapya ya kuunganishwa.

Leo Jaji Ngunyale amesikiliza hoja kutoka pande zote mbili na kutoa maelekezo kwamba wajibu maombi wote wawasilishe viapo kinzani ndani ya siku saba. Awali, wajibu maombi namba moja mpaka tatu ambao ndio waliofungua kesi ya msingi dhidi ya Katibu mkuu na bodi ya wadhamini CHADEMA, walikuwa wameomba siku 14 wakidai hawajapokea nyaraka za kesi, lakini ombi hilo lilikataliwa baada ya kupingwa na Katibu mkuu na bodi ya wadhamini CHADEMA ambao ni wajibu maombi namba nne na tano.

Wakili wa upande wa wajibu maombi hao ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dk. Rugemeleza Nshala, alipinga ombi la kupewa muda mrefu, hali iliyosababisha mahakama kupunguza muda hadi siku saba kama ilivyoamuliwa.

Lissu pia aliiomba mahakama kesi hiyo isikilizwe kwa uwazi kutokana na kile alichokiita kuwa ina maslahi ya umma. Pande zote zilipoulizwa na mahakama, hazikupinga ombi hilo, na hivyo Jaji Ngunyale akasema atatoa uamuzi Juni 2, 2026.

Kesi hiyo itatajwa tena Juni 2, ambapo mahakama itatoa maelekezo ya namna itakavyoendelea kusikilizwa. Wakati huo huo, uamuzi wa msingi kuhusu kama mahakama ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo unatarajiwa kutolewa Mei 28, 2026.

Wakili wa upande wa wadaiwa aliieleza mahakama kuwa kuna pingamizi la awali linalodai kesi hiyo ni batili kwa kushindwa kubainisha kwa uwazi muda wa kuanza kwa madai ya ubaguzi na mgawanyo wa mali kati ya CHADEMA Tanzania Bara na CHADEMA Zanzibar.

Hatima ya kesi hiyo sasa ya Lissu kuunganishwa inategemea uamuzi wa Mei 28, 2026, ambao utabainisha kama shauri hilo litaendelea kusikilizwa au litafutwa kabisa mahakamani kutokana na madai ya ubatili yaliyowasilishwa na wadaiwa.