Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Arsenal yatwaa ubingwa EPL
Baada ya miaka 22 ya kusubiri, hatimaye Arsenal wamerejea rasmi kileleni mwa soka la England baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2025/26.
Ubingwa huo umethibitishwa usiku wa Jumanne kufuatia Manchester City kutoka sare ya 1-1 na Bournemouth, matokeo yaliyoifanya City kubaki na pointi 78 ambazo haiwezi tena kuifikia Arsenal yenye alama 82 kileleni mwa msimamo.
Jumatatu, Arsenal waliweka mazingira mazuri ya kutwaa taji hilo baada ya kuichapa Burnley bao 1-0 katika Uwanja wa Emirates, ushindi uliowafanya kusogea karibu zaidi na ubingwa huo waliokuwa wakiusaka kwa zaidi ya miongo miwili.
Mafanikio hayo yanaweka mwisho wa miaka mitatu mfululizo ambayo Arsenal walikuwa wakimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Manchester City, huku kocha Mikel Arteta akifanikiwa kuirejesha klabu hiyo kwenye enzi zake za mafanikio makubwa.
Arsenal sasa watakabidhiwa rasmi kombe lao katika mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Crystal Palace, wakati Manchester City wakihitimisha ratiba yao kwa mchezo dhidi ya Aston Villa.
Hata hivyo, safari ya mafanikio kwa Arsenal bado haijafikia mwisho. Mei 30, vijana hao wa Arteta watakuwa na nafasi nyingine ya kuandika historia watakapocheza dhidi ya PSG katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakisaka taji lao la kwanza kabisa la michuano hiyo.
Wakati Arsenal wakisherehekea ubingwa huo wa kihistoria, Manchester City wanamuaga kocha wao Pep Guardiola anayetarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu baada ya miaka 10 ya mafanikio makubwa, akiwa ameipa klabu hiyo jumla ya mataji 20 yakiwemo FA Cup na Carabao Cup ya msimu huu.