Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi nilivyomtafuta aliyemlaghai mama yangu kimapenzi
"Hawakuwa wajanja kiasi hicho. Hawakuwa werevu kiasi hicho... Hilo lilinishangaza sana."
Carlos Barragán aliposafiri kwenda Nigeria kumtafuta mwanamume aliyemlaghai mama yake kimapenzi, alitarajia kukutana na tapeli mwenye ujuzi mkubwa.
Anwani ya IP ilifichua kuwa barua pepe zilizomlaghai mama yake zilitumwa kutoka Nigeria, na si kutoka kwa mwanajeshi wa Marekani aliyedai kuwa nchini Syria, kama mwanamume huyo alivyodai.
Lakini badala ya kukutana na mhalifu mwenye utaalamu mkubwa, Carlos alijikuta katika safari ya miaka minne ya kutaka kuelewa kuhusu "Yahoo Boys" wa Nigeria — vijana matapeli ambao mara nyingi hawana elimu ya kutosha, hawana fedha na wana fursa chache maishani.
Safari yake hiyo haikubadili tu mtazamo wake kuhusu mwanamume aliyemlaghai mama yake, bali pia ulimfanya aanze kujiuliza kuhusu athari za upweke katika dunia ya kisasa.
Kukutana na Brian
Carlos anamuelezea mama yake kama mwanamke mwenye nguvu na anayejitegemea. Akiwa mtaalamu mwenye elimu ya juu aliyekuwa akiendesha kliniki yake binafsi ya meno, mama yake alionekana kuwa mtu ambaye ingekuwa vigumu kudanganywa. Hivyo, yeye na kaka zake walipatwa na wasiwasi walipoanza kuhisi kwamba huenda mama yao alikuwa ameangukia kwenye mtego wa tapeli.
Lakini barua pepe aliyomtumia mpenzi wake mpya, "Brian," ilitoa dokezo kuhusu sababu iliyomfanya awe katika mazingira ya kudanganywa.
"Nilimtunza mama yangu, kisha nikamtunza dada yangu mdogo, baadaye nikamtunza mume wangu na watoto wangu. Maisha yangu yote nimekuwa nikitunza wengine, na sasa ninataka mtu ambaye anaweza kunitunza."
Miezi kadhaa kabla, Carlos alikuwa amegundua kwamba mama yake, ambaye alikuwa ameachana na mume wake, alikuwa mpweke, hivyo akamhimiza ajiunge na Tinder.
Muda mfupi baadaye, alikutana na Brian kupitia programu tumishi hiyo — Mmarekani mwenye mvuto, aliyekuwa na umri wa kati ya miaka 50 na 60, ambaye alidai kuwa ametumwa nchini Syria.
Kaka mkubwa wa Carlos, ambaye ni mwanajeshi mstaafu, mara moja alitilia shaka jambo hilo.
"Anaonekana kuwa mtu wa ajabu sana. Huenda huu ni utapeli, Mama," alimwambia.
Baada ya hapo, mama yake aliacha kujadili uhusiano huo naye, ingawa mara kwa mara alimwonyesha Carlos barua pepe kutoka kwa Brian.
Barua hizo zilijaa mapenzi na hisia kali. Brian alianza haraka kuzungumzia kuhamia Hispania ili waweze kuishi pamoja, jambo lililomshangaza hata mama yake Carlos.
"Nadhani bado alikuwa na mashaka kidogo," anasema Carlos.
Mzozo ulizuka katika familia Brian aliposema kwamba angetuma dhahabu katika mfumo wa vipande vya dhahabu nyumbani kwao. Lakini ilikuwa pale mama yake aliporudi nyumbani akiwa na pete mbili na kutangaza kwamba hivi karibuni wangeanza kuishi pamoja ndipo Carlos alipoamua kuchukua hatua.
Alipomwonyesha mama yake ushahidi kwamba barua pepe hizo kwa kweli zilikuwa zikitumwa kutoka Lagos, hakusema mengi. Siku chache baadaye, alifuta karibu barua pepe zote. Lakini alikuwa mwenye huzuni.
Kumwona mama yake akihangaika na upweke kulimchochea Carlos kuchukua hatua. Aliamua kusafiri kwenda Nigeria na kumtafuta tapeli huyo.
Biggie, Ikotun na "Yahoo Boys" wake
Kupitia msaidizi wa ndani, Carlos alipata msaada kutoka kwa tapeli mmoja aliyeitwa Biggie, ambaye alikubali kumtambulisha kwa marafiki zake na kumtembeza Ikotun, kitongoji chenye watu wengi huko Lagos, ambako "kila mtu anahangaika kutafuta maisha, kila mtu anajaribu kupata pesa."
Biggie alikuwa na umri wa karibu miaka 30, sawa na Carlos. Alikuwa mwerevu na "mcheshi sana."
Wawili hao walitumia karibu kila saa wakiwa pamoja, na kwa mshangao wake, Carlos alijikuta akimpenda Biggie.
"Niliendelea kujiuliza... mtu kama yeye anawezaje kuwa tapeli anatumia usiku wake akizungumza na watu wapweke mtandaoni?"
Alipokuwa akizungumza na wenyeji, Carlos aligundua kwamba kulikuwa na mtandao mkubwa wa matapeli: mamia ya vijana wanaojulikana kama Yahoo Boys, jina lililotokana na huduma ya barua pepe ya Yahoo ambayo waliitumia katika siku za mwanzo za biashara hiyo.
Hatua kwa hatua, Carlos alitambua kwamba akiwa na jina bandia na anwani feki ya barua pepe pekee, ilikuwa vigumu sana kumtafuta tapeli aliyemlenga mama yake katika nchi yenye watu zaidi ya milioni 240.
Badala yake, alijikuta akijifunza zaidi kuhusu ulimwengu wa Yahoo Boys.
Kwa sababu Carlos ni mzungu alionekana wazi wazi kila mahali alikokwenda. Anasema watu walidhani ama alikuwa wakala wa FBI au mfanyabiashara Mchina. Walimwita "maga" — neno la mitaani linalomaanisha mtu mjinga au mwepesi wa kudanganywa ambaye ni rahisi kutapeliwa.
Hata hivyo, kupitia utambulisho wa Biggie, aliweza kuzungumza na Yahoo Boys 50.
Mmoja wao alijifanya kuwa mwanamieleka maarufu wa Marekani, Cody Rhodes, na akamshawishi mwanamke mmoja kulipia tiketi 25 za ndege ambazo hazikutumiwa kamwe. Malipo yake ya kwanza yalikuwa euro 300 — kiasi kikubwa kuliko fedha alizowahi kupata katika kipindi cha zaidi ya miezi 18 akifanya kazi kiwandani.
Lakini mafanikio hayakuja kwa urahisi.
"Wanaita 'bombing'," anasema Carlos, "ambayo kimsingi ni kujaribu kuwafikia mamia, au hata maelfu, ya watu."
Carlos pia alianzisha urafiki wa karibu na Yahoo Boy mwingine, Azeez, ambaye alianza kufanya utapeli akiwa na umri wa miaka 14. Alikuwa amehamia Lagos kutoka kijijini kwao na aliishi na mama yake na dada yake mdogo wa mtoto katika nyumba ndogo yenye msongamano.
Azeez alijitambulisha kwa wanaume wa Marekani kama "Vanessa", akitumia picha iliyoibwa ya mwanamke mrembo Mzungu.
Mwanzoni, hakufanikiwa. Kiingereza chake kilikuwa hafifu, na hakuwahi kuwa na mpenzi wala kutembelea Marekani.
"Tunazungumzia wavulana wadogo ambao hawana uelewa mkubwa kuhusu ulimwengu wa Magharibi," anasema Carlos.
Hatimaye, Azeez alipata mafanikio na akapokea dola tano. Alitumia fedha hizo kununua kuku kwenye mgahawa. Ilikuwa mara ya kwanza kabisa kuingia ndani ya jengo lenye kiyoyozi.
Lakini mama yake Azeez na nyanya yake, ambao wote walikuwa wauzaji wa vyakula vya mitaani wasiojua kusoma wala kuandika, walijua kwamba alichokuwa akifanya kilikuwa kibaya. Nyanya yake alimpa sharti la mwisho: aache utapeli au akataliwe na familia.
Tangu wakati huo, hajawahi kufanya tena.
Carlos anasema aliwasili Nigeria akiamini kwamba matapeli hao walikuwa sehemu ya mtandao mkubwa na wa kisasa wa uhalifu. Uhusiano wake na Azeez ulimlazimisha kubadili mtazamo huo.
"Ni rahisi zaidi kuamini kwamba kuna mtandao mkubwa wa wahalifu wenye nguvu Afrika Magharibi unaotudhuru, kuliko kuamini kwamba ni huyu mtu tu mwenye simu yake," anasema.
Pia alishuhudia jinsi vijana wengi wanaofanya utapeli walivyokuwa wahanga wenyewe, huku kujionyesha kwa utajiri wao kukiwavutia wahalifu wenye nguvu zaidi.
Hata hivyo, swali moja lilibaki: vijana hao, ambao baadhi yao walikuwa hawajamaliza hata shule, waliwezaje kuwashawishi watu wazima kama mama yake kuwaamini?
Matapeli hao walimweleza kwamba walikuwa wakitoa kitu ambacho watu wengi wanakikosa: muunganiko wa kihisia na mtu mwingine.
"Walikuwa wakiniambia, 'Unachotakiwa kufanya ni kuwapa umakini.' Ni kuhusu kuwepo kwa ajili yao. Kuwaambia, 'Habari za asubuhi. Unaendeleaje, mpenzi? Ulikula nini mchana?'"
Carlos anasema hitaji hilo hilo la kuwa na uhusiano na mtu mwingine, ambalo mara nyingi linatokana na upweke, pia lilijitokeza mara kwa mara katika mazungumzo yake na wahanga wa utapeli.
"Huu ndio uhalifu wa kusikitisha zaidi duniani kwa sababu hawachukui tu pesa zako," mmoja wa wahanga alimwambia. "Pia wanakumaliza kihisia. Unabaki na pengo kubwa mtu huyo anapotoweka ghafla. Halafu jamii inakuambia wewe ni mjinga na kwamba ni kosa lako."
Carlos ameandika kitabu, The Yahoo Boys, kinachoelezea uzoefu wake.
Makala haya yametokana na kipindi cha Outlook cha BBC World Service, kilichotayarishwa na Vibeke Venema na Julian Siddle.
Maandishi ya Becca Johns na Global Journalism.