AFCON U-17: Tanzania kuandika historia leo?

S

Chanzo cha picha, CAF

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Jioni ya leo macho ya Watanzania yataelekezwa jijini Rabat, Morocco, ambako Serengeti Boys watashuka dimbani kuikabili Senegal katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17). Ni mechi inayoweza kuandika historia mpya kwa taifa ambalo tangu lianzishwe halijawahi kutwaa kombe lolote la Afrika kwa timu zake za soka, kuanzia vilabu mpaka timu zote za taifa.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo, Tanzania imefika hatua ya fainali na sasa ina dakika 90 kutwaa taji la Afrika. Mafanikio hayo tayari yameiweka Serengeti Boys katika vitabu vya historia, lakini ushindi leo unaweza kuifanya Tanzania kuingia katika sura mpya kabisa ya maendeleo ya soka.

Ingawa ushindi wa Serengeti Boys hauwezi kufuta maumivu ya waliopoteza wapendwa wao, unaweza kupoza kidogo kwa muda kupitia furaha kwa mamilioni ya Watanzania wanaotafuta jambo la kuwaunganisha katika wakati huu.

Disemba 2025 kaka zao, Taifa Stars (timu ya wakubwa ya Tanzania), ilijitahidi kusuuza mioyo ya watanzania kwa kufika 16 bora kwenye mashindano ya AFCON , kwa mara ya kwanza, kutwaa kombe wa Serengeti boys, ni zaidi ya kombe na taji la Afrika kwa watanzania.

Safari ya Tanzania kuingia fainali

S

Chanzo cha picha, CECAFA

Safari ya Tanzania katika michuano hiyo imeelezwa kuwa ya kuvutia kutokana na uimara, nidhamu na uwezo wa kupambana katika nyakati ngumu.

Katika hatua ya makundi, Serengeti Boys walimaliza kinara wa Kundi C kwa pointi sita baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Msumbiji na Angola kabla ya kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Uganda. Matokeo hayo yaliwapa nafasi ya kusonga mbele huku wakionyesha dalili za kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kushtua wengi katika mashindano hayo.

Robo fainali dhidi ya Algeria ndiyo iliyoonyesha kwa mara ya kwanza uimara wa kiakili wa vijana hao. Katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa, Tanzania ilitoka sare ya mabao 3-3 ndani ya dakika 90 kabla ya kushinda kwa penalti 4-3. Ulikuwa mchezo uliohitaji utulivu, uvumilivu na kuamini mpaka sekunde za mwisho.

Hatua ya nusu fainali dhidi ya Misri ilifuata mkondo huohuo. Baada ya sare ya bila kufungana ndani ya muda wa kawaida, Serengeti Boys walionyesha tena utulivu mkubwa katika mikwaju ya penalti na kuibuka na ushindi wa 4-3, matokeo yaliyowapeleka kwenye fainali yao ya kwanza kabisa katika historia.

Kilichowafikisha hapa si bahati, ni mfumo wa timu, nidhamu ya ulinzi, kujituma kwa kila mchezaji na uwezo wa kusimama imara wakati wa presha kubwa.

"Hongereni Tanzania, mmecheza soka zuri, mchezo mzuri, matumani yangu tutaonana punde kwenye kombe la dunia", anasema Arsene Wenger, kocha wa zamani wa Arsenal, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Maendeleo ya soka duniani wa FIFA nafasi anayoishilia tangu mwaka 2019.

Ufundi na jitihada kuamua mshindi leo

S

Chanzo cha picha, cecafa

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mchezo wa leo unakutanisha mitazamo miwili tofauti ya soka. Tanzania imefika hapa kupitia jitihada za kitimu, nidhamu ya kujilinda na mashambulizi ya kushtukiza, wakati Senegal imekuwa ikitumia nguvu za mwili, kasi, ufundi na kukabilia juu kwa wapinzani wake.

Vita kubwa vinatarajiwa kuwa katika eneo la kiungo ambako Senegal itajaribu kutawala mchezo kupitia nguvu na kasi ya kurejesha mpira haraka. Tanzania kwa upande wake itahitaji kuwa makini katika kupitisha mipira na kutumia vyema nafasi chache itakazozipata. Kwa sababu kwa uwezo wa Senegal, inatarajiwa watatawala sehemu kubwa ya mchezo.

Makipa wanaweza pia kuwa watu muhimu zaidi katika mchezo huu. Tanzania imefaidika mara kadhaa na uimara wa kipa wake katika mechi za mtoano, huku Senegal ikiwa na Assane Sarr ambaye amekuwa miongoni mwa nyota wa mashindano haya kutokana na uwezo wake wa kuokoa michomo mingi ikiwemo penati na kuipa timu yake uhai katika nyakati ngumu.

Wachezaji wanne wanaotarajiwa kuvuta macho ya mashabiki ni Dismas Athanasi Shida wa Tanzania ambaye tayari amefunga mabao matatu katika mashindano haya, Issa Chole pamoja na Razaki Mbelegendi ambaye amekuwa injini muhimu katika eneo la kiungo. Shida ndiye mchezaji mdogo zaidi kwenye mashindano hayo akiwa na miaka 14.

Kwa upande wa Senegal, macho mengi yatakuwa kwa kipa Assane Sarr pamoja na kiungo mshambuliaji Souleymane Commissaire Faye ambaye amekuwa mhimili muhimu wa mashambulizi ya timu hiyo.

Kwa ubora ambao timu zote mbili zimeonyesha hadi sasa, tofauti inaweza kupatikana kupitia maamuzi madogo sana. Kona moja, pasi moja ya mwisho, okoa moja muhimu au kosa moja la kujihami vinaweza kuamua hatma ya ubingwa wa Afrika kwa vijana wa chini ya miaka 17.

Ushindi una maana gani kwa Tanzania?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Iwapo Serengeti Boys watafanikiwa kuifunga Senegal usiku wa leo, watakuwa wameandika moja ya sura muhimu zaidi katika historia ya michezo Tanzania.

Hakuna timu ya taifa ya Tanzania iliyowahi kutwaa ubingwa wa AFCON katika ngazi yoyote. Taifa Stars, timu ya wakubwa ilifuka hatua ya 16 bora AFCON iliyomalizika hivi karibuni, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo. Hivyo ushindi wa leo utakuwa wa kwanza wa aina yake na utaifanya Serengeti Boys kuwa kizazi kilichovunja 'mkosi' ambao umedumu tangu taifa hilo lizaliwa mwaka 1961.

Mafanikio hayo yatakuwa pia ushahidi kuwa uwekezaji katika maendeleo ya soka la vijana unaanza kuzaa matunda. Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitafuta msingi wa kuzalisha kizazi kitakachokuja kuibeba Taifa Stars katika mashindano makubwa ya baadaye. Kizazi hiki kinaonekana kuwa mwanzo wa safari hiyo, na lengo la nchi hiyo kufuzu michuano ya kombe la dunia mwaka 2030.

Serikali tayari imeonyesha namna inavyothamini mafanikio ya timu hiyo. Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alitangaza zawadi ya shilingi milioni 500 baada ya Serengeti Boys kufuzu fainali. Serikali pia imeahidi kuwapatia viwanja katika mji wa Suluhu New City mkoani Morogoro wachezaji wote wa timu hiyo iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika. Wamepewa ndege na Serekali itakayowarudisha Dar es Salaam.

Mbali na hilo, Serengeti Boys tayari wameihakikishia Tanzania nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA U-17 nchini Qatar kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, kufuzu Kombe la Dunia pamoja na kutwaa ubingwa wa Afrika kutafanya mwaka 2026 kuwa miongoni mwa miaka ya kukumbukwa zaidi katika historia ya soka la taifa.

Ndiyo maana mchezo wa leo ni zaidi ya fainali ya soka una maana kubwa zaidi kwa nchi hiyo. Ni kombe, hamasa, fedha, uwezekaji, maisha na tabasamu katika kipindi ambacho Watanzania wengi wanahitaji habari njema za kuwaunganisha na kuwafurahisha.