Nchi 10 zenye viwango vya chini zaidi vya talaka duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Mamadou Faye
- Nafasi, BBC News Afrique
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kwa sasa, wastani wa kiwango cha talaka duniani, unaopimwa kwa idadi ya talaka kwa kila watu 1,000 kwa mwaka, ni kati ya 1.7 na 1.8. Hata hivyo, baadhi ya nchi zina viwango vilivyo chini sana ya wastani huo, huku nyingine zikiwa karibu kufikia sifuri. India, Sri Lanka na Vietnam ndizo zinazoongoza kwa kuwa na viwango vya chini zaidi vya talaka duniani.
Orodha hii imeandaliwa na WorldAtlas kwa kutumia takwimu kutoka Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Uchumi na Kijamii (UN DESA), Eurostat kwa nchi za Ulaya, Utafiti wa Kitaifa wa Afya ya Familia wa India (NFHS 4 na NFHS 5), pamoja na machapisho ya taasisi za kitaifa za takwimu.
Hata hivyo, kiwango cha chini cha talaka hakimaanishi moja kwa moja kwamba wanandoa katika nchi hizo wana furaha zaidi au ndoa zao ni imara zaidi. Kwa mujibu wa WorldAtlas, mara nyingi hali hiyo hutokana na vikwazo vya kisheria au vya kidini vinavyofanya talaka kuwa ngumu kupatikana, au kutokana na ukweli kwamba wanandoa wengi hutengana bila kufuata taratibu rasmi za kisheria, hivyo kutokujumuishwa katika takwimu za serikali.
1. India (Talaka 0.01 hadi 0.1 kwa kila watu 1,000)

Chanzo cha picha, Getty Images
India inatajwa mara kwa mara kuwa nchi yenye kiwango cha chini zaidi cha talaka duniani.
Nchini humo, sheria za ndoa hutofautiana kulingana na dini ya wanandoa. Kwa mfano, Wahindu husimamiwa na Sheria ya Ndoa ya Wahindu ya mwaka 1955, ndoa za kiraia hutawaliwa na Sheria ya Ndoa Maalumu ya mwaka 1954, huku Waislamu, Wakristo na Waparsi wakifuata sheria zao mahsusi.
Wataalamu wanasema kiwango hicho cha chini kinachangiwa kwa kiasi kikubwa na utamaduni wa ndoa za kupangwa na familia, ambao bado unakubalika na sehemu kubwa ya vijana nchini India. Aidha, ushawishi mkubwa wa familia katika maamuzi ya ndoa kabla ya kufungwa kwake huchangia kudumisha kiwango hicho cha chini cha talaka.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa India mara nyingi huondolewa katika baadhi ya ulinganisho wa kimataifa kutokana na kutokukamilika kwa mfumo wake wa usajili wa talaka za kiraia. Hali hiyo ina maana kuwa takwimu rasmi zinaweza kuwa hazionyeshi kwa usahihi idadi halisi ya talaka nchini humo.
Kwa mujibu wa wachambuzi, kiwango halisi cha talaka huenda kikawa kikubwa zaidi kuliko kinavyoonekana kwenye takwimu rasmi, hususan katika miji mikubwa ambako idadi ya wanandoa wanaotalikiana imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.
2. Sri Lanka (Takriban talaka 0.15 kwa kila watu 1,000)
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, Sri Lanka ndiyo nchi yenye kiwango cha chini zaidi cha talaka kilichosajiliwa duniani.
Nchi hiyo inatumia mifumo mitatu tofauti ya sheria za ndoa kulingana na jamii husika, ambayo ni sheria za kiraia, sheria za kimila za Kandyan na sheria za Kiislamu. Mifumo hiyo inaweka masharti magumu ya kupata talaka, ambayo kwa kawaida hutolewa kwa sababu kama uzinzi, kutelekezwa kwa makusudi au kushindwa kutimiza wajibu wa ndoa.
Aidha, taratibu za mahakamani huchukua muda mrefu na huwa na gharama kubwa. Pamoja na hilo, shinikizo la kijamii la kuendelea kubaki kwenye ndoa lina nguvu katika jamii nyingi nchini humo.
3. Vietnam (Takriban talaka 0.2 kwa kila watu 1,000)
Sheria ya Ndoa na Familia ya Vietnam ya mwaka 2014 inaruhusu wanandoa kupewa talaka hata bila kubainisha kosa la mmoja wao, huku ikiwapa haki sawa mume na mke.
Hata hivyo, maadili yanayotokana na falsafa ya Confucius, ambayo yanasisitiza umuhimu wa familia na heshima kwa wazazi, pamoja na mshikamano mkubwa wa familia katika maeneo ya vijijini, yameendelea kuchangia kiwango cha chini cha talaka.
Katika miji mikubwa kama Ho Chi Minh na Hanoi, hali inaanza kubadilika kutokana na kuongezeka kwa uhuru wa kiuchumi wa wanawake.
4. Guatemala (Takriban talaka 0.2 kwa kila watu 1,000)
Guatemala ndiyo nchi yenye kiwango cha chini zaidi cha talaka katika bara la Amerika.
Hali hiyo inachangiwa na ushawishi mkubwa wa dini za Katoliki na Kiinjili. Pia, sehemu kubwa ya wanandoa huishi pamoja bila kufunga ndoa rasmi, hasa katika maeneo ya vijijini na miongoni mwa jamii za Wamaya.
Kutokana na hali hiyo, wanapotengana, matukio hayo hayaingii katika takwimu rasmi za talaka.
5. Tajikistan (Takriban talaka 0.3 kwa kila watu 1,000)

Chanzo cha picha, Getty Images
Tajikistan, nchi yenye Waislamu wengi katika Asia ya Kati, ina viwango vya chini vya talaka kutokana na mfumo wa kijamii unaozingatia maadili ya kifamilia.
Shinikizo kutoka kwa jamii na umuhimu unaowekwa kwenye heshima ya familia huwafanya wengi, hasa wanawake, kusita kuomba talaka.
6. Bosnia na Herzegovina (Takriban talaka 0.3 kwa kila watu 1,000)
Bosnia na Herzegovina ni miongoni mwa nchi za Ulaya zenye kiwango cha chini cha talaka.
Nchi hiyo ina mchanganyiko wa jamii za Kiislamu, Kiorthodoksi na Kikatoliki, huku maadili ya jadi kuhusu familia yakiendelea kuwa na ushawishi mkubwa, hasa nje ya miji mikubwa.
7. Chile (Takriban talaka 0.7 kwa kila watu 1,000)

Chanzo cha picha, Getty Images
Chile ilikuwa miongoni mwa nchi za mwisho katika bara la Amerika kuruhusu talaka kisheria mwaka 2004.
Kabla ya hapo, wanandoa waliweza tu kufuta ndoa kupitia taratibu maalumu za kisheria ambazo mara nyingi zilikuwa ghali.
Ingawa Katiba ya Chile bado inaipa familia nafasi ya msingi katika jamii na ushawishi wa Kanisa Katoliki pamoja na madhehebu ya Kiinjili unaendelea kuwa mkubwa, kiwango cha talaka kinaongezeka taratibu kadiri ndoa zilizofungwa baada ya mwaka 2004 zinavyoendelea kudumu kwa muda mrefu.
8. Malta (Takriban talaka 0.6 kwa kila watu 1,000)
Malta ilikuwa nchi ya mwisho katika Umoja wa Ulaya kuhalalisha talaka mwaka 2011, baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na asilimia 53 ya wapiga kura.
Kabla ya hapo, wanandoa waliweza tu kutengana kisheria au kufuta ndoa kwa misingi ya kidini.
Hata sasa, sheria ya Malta inawataka wanandoa kutengana kwa angalau miaka minne kabla ya kupewa talaka, muda ambao ni mrefu zaidi katika Umoja wa Ulaya. Hali hiyo imechangia nchi hiyo kuwa na kiwango cha chini zaidi cha talaka ndani ya umoja huo.
9. Peru (Takriban talaka 0.6 kwa kila watu 1,000)

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchini Peru, ushawishi wa Kanisa Katoliki pamoja na idadi kubwa ya wanandoa wanaoishi pamoja bila ndoa rasmi umechangia kiwango cha chini cha talaka zinazotambuliwa kisheria.
Hali kama hiyo pia inaonekana katika baadhi ya nchi nyingine za Amerika Kusini.
10. Ireland (Takriban talaka 0.7 kwa kila watu 1,000)
Ireland ilihalalisha talaka mwaka 1996 baada ya kura ya maoni iliyopitishwa kwa tofauti ndogo ya asilimia 50.3.
Mwaka 2019, kura nyingine ya maoni ilipunguza muda wa lazima wa kutengana kabla ya talaka kutoka miaka minne kati ya mitano iliyotangulia hadi miaka miwili kati ya mitatu.
Ni kati ya asilimia 12 na 15 pekee ya ndoa nchini Ireland huishia kwenye talaka, kiwango ambacho ni cha chini zaidi kuliko wastani wa asilimia 35 hadi 45 katika nchi nyingi za Ulaya Magharibi.
Wataalamu wanaeleza tofauti hiyo inachangiwa na kuchelewa kuhalalishwa kwa talaka, ushawishi unaoendelea wa Kanisa Katoliki, gharama na ugumu wa taratibu za talaka, pamoja na watu wengi kuoa au kuolewa wakiwa na umri mkubwa zaidi.
Takwimu hizi zinaashiria nini?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa WorldAtlas, kuna sababu tatu kuu zinazojitokeza katika nchi nyingi zenye viwango vya chini vya talaka.
Kwanza ni uwepo wa vikwazo vikubwa vya kitamaduni au kidini, kama ilivyo India, Sri Lanka, Guatemala, Chile na Peru.
Pili ni nchi ambazo zimeruhusu talaka kisheria katika kipindi cha hivi karibuni, kama Malta mwaka 2011, Chile mwaka 2004 na Ireland mwaka 1996.
Tatu ni kuongezeka kwa idadi ya wanandoa wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa rasmi. Wanandoa hao wanapotengana, matukio hayo hayaingii katika takwimu rasmi za talaka, kama ilivyo Guatemala, Peru na kwa kiasi fulani Mexico.
Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa kiwango cha chini cha talaka hakipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ndoa katika nchi hizo zina mafanikio zaidi. Wakati mwingine kinaweza kuficha hali nyingine kama kutengana bila kufuata taratibu rasmi, ukatili wa majumbani usioripotiwa, au wanandoa wanaoendelea kuishi pamoja kutokana na shinikizo la kijamii au kisheria badala ya hiari yao wenyewe.















