Moja kwa moja, Mashambulizi ya Iran yamejeruhi takriban wanajeshi 100 ndani ya wiki mbili - Marekani
Jeshi la Marekani lasema limefanya duru nyingine ya mashambulizi dhidi ya Iran ili "kudhoofisha zaidi" uwezo wake wa kushambulia meli katika Lango la Hormuz.
Iran yautaka ulimwengu kutokubali mashambulizi dhidi ya vituo vyake vya nyuklia
Chanzo cha picha, Tasnim news agency
Iran imezitaka mataifa yote duniani kutokubali mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vinavyotumika kwa shughuli za amani, ikisema ulinzi wa miundombinu hiyo ni wajibu wa jumuiya ya kimataifa.
Katika taarifa iliyotolewa na Ujumbe wa Iran katika Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, Tehran imedai kuwa Marekani ilirusha makombora kwenye eneo la ujenzi wa kinu cha nyuklia cha Karun (Darkhovin) asubuhi ya Julai 18.
Iran imeeleza kuwa mradi huo ni "ishara ya hadhi na kujitegemea kisayansi kwa taifa la Iran."
Aidha, imesema licha ya kuwa tayari kuchukua hatua zote zinazohitajika kulinda maslahi yake ya kitaifa na haki zake za kikatiba, kuzuia mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vilivyo chini ya usimamizi wa IAEA na vinavyotumika kwa madhumuni ya amani ni jukumu la jumuiya ya kimataifa.
Hata hivyo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani, CENTCOM, imesema ilishambulia maeneo kadhaa ya kijeshi nchini Iran, yakiwemo vituo vya makombora, droni na mali za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, bila kutaja kinu cha Darkhovin.
Kwa upande wake, IAEA imesema inachunguza taarifa za madai ya kushambuliwa kwa kinu hicho cha nyuklia kinachojengwa, lakini bado haijatoa ripoti huru inayothibitisha tukio hilo.
Fifa yaanzisha uchunguzi dhidi ya Argentina baada ya fainali ya Kombe la Dunia
Chanzo cha picha, Getty Images
Shirikisho la Soka Duniani, Fifa, limeanzisha uchunguzi kuhusu matukio ya vurugu yaliyotokea baada ya fainali ya Kombe la Dunia kati ya Argentina na Uhispania.
Kamati ya Nidhamu ya Fifa imemteua mpelelezi kuchunguza kilichotokea baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya mwisho katika Uwanja wa MetLife, New Jersey.
Iwapo wachezaji au maafisa wa benchi la ufundi watabainika kuhusika na tukio hilo, wanaweza kufungiwa kushiriki mechi, huku Chama cha Soka cha Argentina (AFA) nacho kikikabiliwa na uwezekano wa kutozwa faini.
Baada ya Argentina kufungwa bao 1 kwa 0 na Uhispania, baadhi ya wachezaji na maafisa wa benchi la ufundi wa Argentina walizozana na wachezaji wa Uhispania waliokuwa wakisherehekea ushindi wao.
Nahuel Molina, Leandro Paredes, Thiago Almada na kocha msaidizi Roberto Ayala walionekana kuhusika katika mzozo huo.
Awali, mfumo wa taarifa za Fifa uliripoti kimakosa kuwa Leandro Paredes alipewa kadi nyekundu na mwamuzi Slavko Vinčić baada ya kumshika shingoni Eric García wa Uhispania. Hata hivyo, taarifa hiyo baadaye ilibainika kuwa si sahihi.
Filimbi ya mwisho ilipopulizwa, baadhi ya wachezaji wa Argentina, akiwemo Lionel Messi, walikaa uwanjani wakiwa wamevunjika moyo, huku wengine wakisimama kimya wakishuhudia wachezaji wa Uhispania wakikimbilia uwanjani kusherehekea kutwaa ubingwa.
Rodri, ambaye alikuwa ametolewa wakati wa muda wa nyongeza, alitoka benchi na kuungana na wenzake katika shangwe za ushindi.
Mashambulizi ya Iran yamejeruhi takriban wanajeshi 100 ndani ya wiki mbili - Pentagon
Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imesema takriban wanajeshi 100 wa Marekani wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Iran ndani ya kipindi cha wiki mbili zilizopita, hali inayoashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili.
Kwa mujibu wa Pentagon, majeruhi wengi walitokana na mashambulizi yaliyolenga vituo vya kijeshi vya Marekani katika Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, wizara hiyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu aina au ukubwa wa majeraha waliyoyapata wanajeshi hao.
Awali, Pentagon ilithibitisha kuwa wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa katika mashambulizi yaliyoihusisha Iran.
Taarifa hiyo inakuja baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran, IRGC, kutangaza kufanya mashambulizi katika maeneo ya Bahrain, Kuwait na Jordan, ambapo baadhi yake yalisababisha vifo vya wanajeshi watatu wa Marekani.
Mlipuko wa Ebola waenea maeneo mapya mashariki mwa DR Congo
Chanzo cha picha, Getty Images
Mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeenea hadi kanda 47 za afya katika maeneo matano ya Adja, yaliyoko mkoani Ituri.
Takwimu zilizotolewa Julai 19 zinaonyesha kuwa watu 2,423 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo, huku 967 wakifariki dunia, sawa na kiwango cha vifo cha asilimia 39.9.
Katika saa 24 zilizopita pekee, mamlaka zimeripoti maambukizi mapya 79 na vifo 37, vingi vikirekodiwa mkoani Ituri. Maeneo ya Bunia, Nizi, Rwampara na Adja yameripoti idadi kubwa zaidi ya maambukizi mapya.
Mamlaka za afya zinasema zimefanikiwa kuwafuatilia asilimia 81.1 ya watu waliokutana na wagonjwa, ingawa bado kuna mapungufu, hasa katika mkoa wa Haut Uélé.
Mlipuko huo ulitangazwa rasmi Mei 15 na unasababishwa na aina ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo ebolavirus.
Maafisa wa afya wanasema changamoto za kiusalama pamoja na shughuli kubwa za watu na biashara katika mpaka wa DR Congo na Uganda pamoja na Sudan Kusini zinaendelea kutatiza juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.
Wameonya kuwa ufuatiliaji wa karibu na kuimarishwa kwa hatua za kinga ni muhimu ili kuzuia mlipuko huo kuenea zaidi.
Qatar yaishtaki Iran UN kwa kuharibu miundombinu yake
Chanzo cha picha, Getty Images
Qatar imewasilisha barua kwa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja huo ikiilaumu Iran kwa mashambulizi dhidi ya nchi hiyo na kuitaka ilipe fidia kwa uharibifu wote uliosababishwa.
Katika barua hizo, Qatar imesema Iran ilishambulia meli ya mafuta karibu na Mlango wa Hormuz Julai 7, kabla ya kurusha makombora mengine kuelekea nchini humo Julai 12 na Julai 17.
Maafisa wa Qatar wamesema watu watatu, akiwemo mtoto, walijeruhiwa katika shambulio la Julai 12 baada ya vipande vya makombora vilivyolipuka kuangukia maeneo ya makazi.
Qatar imeeleza kuwa mashambulizi hayo ni ukiukaji wa mamlaka yake na uhuru wa taifa, na kwamba yanahatarisha usalama na mamlaka ya nchi hiyo.
Serikali ya Qatar pia imesisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua zozote zinazohitajika kulinda mamlaka yake, usalama wa taifa na raia wake.
Hata hivyo, Iran imesema mashambulizi yake dhidi ya nchi za eneo hilo yanalenga vituo vya kijeshi vya Marekani na wanajeshi wake walioko katika mataifa hayo.
Urusi yasema mashambulizi ya Ukraine yaua raia tisa
Chanzo cha picha, t.me/dsns_telegram
Kaimu gavana wa jimbo la Belgorod nchini Urusi, linalopakana na kaskazini mashariki mwa Ukraine, amesema raia tisa wameuawa katika mashambulizi ya Ukraine ndani ya siku mbili zilizopita.
Alexander Shuvayev amesema pia karibu droni 200 za Ukraine zilidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi katika kipindi hicho.
Taarifa hiyo inakuja wakati Umoja wa Mataifa ukisema idadi ya raia waliouawa katika vita kati ya Urusi na Ukraine imeongezeka kwa zaidi ya theluthi moja katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.
Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu nchini Ukraine amesema wamehesabu zaidi ya raia 1,400 kutoka Urusi na Ukraine waliopoteza maisha tangu mwanzoni mwa mwaka.
Wakati huo huo, mapigano kati ya pande hizo mbili yanaendelea.
Jeshi la Anga la Ukraine limesema Urusi ilishambulia nchi hiyo usiku wa kuamkia leo kwa kutumia droni 58, huku 46 zikidunguliwa.
Kwa upande wake, Urusi imesema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilidungua droni 209 za Ukraine katika mashambulizi ya usiku kucha.
Marekani yashutumu China kwa kumjeruhi baharia wa Ufilipino
Chanzo cha picha, Screengrab
Marekani imeishutumu China kwa kile ilichodai imemjeruhi mwanamaji wa Ufilipino wakati wa tukio lililotokea katika Bahari ya China Kusini, eneo linalogombaniwa na mataifa kadhaa.
Katika taarifa yake, Washington imesema hatua ya China ni "ukiukaji wa wazi" na haiwezi kukubalika.
Jeshi la Ufilipino limesema mwanamaji huyo alipigwa kichwani kwa fimbo na maafisa wa ulinzi wa baharini wa China siku ya Jumapili walipokaribia meli ya kijeshi ya Ufilipino iliyokuwa ikifanya operesheni ya usalama.
Hata hivyo, China imekanusha tuhuma hizo na kudai kuwa mzozo huo ulianza baada ya mwanamaji wa Ufilipino kumshambulia afisa wa ulinzi wa baharini wa China.
Baada ya tukio hilo, Beijing ilimwita mwakilishi wa Ufilipino nchini China kwa mazungumzo yaliyofanyika Jumatatu.
China na Ufilipino zimekuwa zikivutana mara kwa mara kuhusu umiliki wa maeneo ya Bahari ya China Kusini, huku Beijing ikidai umiliki wa sehemu kubwa ya bahari hiyo.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, yuko Manila kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN.
Rubio amesema yuko tayari kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, baada ya mkutano huo.
Meli ya kivita ya Urusi yafanya majaribio ya makombora karibu na pwani ya Uingereza
Chanzo cha picha, Getty Images
Meli ya kivita ya Urusi imefanya mazoezi ya kurusha makombora katika maji ya kimataifa, takribani kilomita 74 kusini mwa mji wa Plymouth nchini Uingereza, huku ikifuatiliwa kwa karibu na Jeshi la Wanamaji la Uingereza.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Uingereza amesema meli ya kivita ya HMS Tyne ilisimamia shughuli hiyo na inaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya meli hiyo ya Urusi.
Meli hiyo ya Urusi, Neustrashimy, pia ilifuatiliwa na ndege ya kijeshi ya Ufaransa. Kwa mujibu wa taarifa ambazo BBC imezipata, ndege hiyo iliwasiliana kwa njia ya redio na meli hiyo ikiitaka ifafanue shughuli zake.
BBC pia imeelezwa kuwa kabla ya kuanza mazoezi ya kurusha makombora, Neustrashimy iliijulisha HMS Tyne kwamba ilikuwa ikijiandaa kufanya majaribio hayo na kuishauri ihamie umbali salama. Meli ya Uingereza ilikubali ombi hilo.
Mazoezi hayo yalifanyika katika maji ya kimataifa na yalidumu kwa takribani dakika 30.
Tukio hilo limejiri saa chache baada ya Andy Burnham kuapishwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.
Mwezi uliopita, vikosi maalumu vya Jeshi la Wanamaji la Uingereza vilikamata meli ya mafuta ya Urusi iliyokuwa ikifanya shughuli katika Mfereji wa Kiingereza, ikiwa ni mara ya kwanza kwa jeshi hilo kuchukua hatua kama hiyo.
Aidha, mwezi Juni, wanandoa wa Uingereza waliokuwa wakisafiri kwa boti yao katika maji ya kimataifa karibu na Kisiwa cha Wight walikutana na meli ya kivita ya Urusi Admiral Grigorovich. Meli hiyo ilifyatua risasi za onyo baada ya kueleza kuwa boti yao ilikuwa ikifanya kile ilichokiita "maneva hatari", madai ambayo wanandoa hao walikanusha.
Meli za kivita za Urusi hupita mara kwa mara katika maji ya kimataifa ya Mfereji wa Kiingereza, huku vikosi vya wanamaji vya Uingereza au Ufaransa vikizifuatilia kwa karibu hadi zinapoondoka eneo hilo.
Uganda imetangaza kanuni mpya kwa mabasi ya shule baada ya vifo vya wanafunzi
Chanzo cha picha, Reuters
Uganda imetangaza kanuni mpya kwa mabasi ya shule kufuatia vifo vya zaidi ya watoto ishirini katika ajali ya barabarani wiki iliyopita.
Serikali inasema magari yote yanayosafirisha wanafunzi yatakuwa na rangi moja maalum.
Madereva wa mabasi ya shule watahitaji pia vibali maalum na vitambulisho kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi.
Ajali hiyo ya Alhamisi ilikuwa miongoni mwa ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Uganda hivi karibuni.
Tukio hilo limesababisha kusimamishwa kwa safari zote za shule hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Trump aitoza Canada ushuru wa asilimia 50, Carney aahidi kuimarisha mazungumzo ya biashara
Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa mbalimbali zinazoagizwa kutoka Canada, akisema hatua hiyo ni kulipiza kisasi kutokana na kile alichokiita "kutendewa isivyo sawa" kwa magari, bidhaa za maziwa na vileo vya Marekani.
Bidhaa za matumizi ya kila siku kama vile divai na fimbo za mchezo wa hoki, pamoja na bidhaa za viwandani kama saruji, ni miongoni mwa bidhaa zitakazotozwa ushuru huo.
Hata hivyo, baadhi ya bidhaa muhimu zitaondolewa kwenye ushuru huo, zikiwemo nishati, madini muhimu na samaki.
Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, amesema nchi yake iko tayari "kuongeza kasi" ya mazungumzo ya biashara na Marekani katika wiki zijazo.
Ikulu ya White House imesema ushuru huo utaanza kutekelezwa baada ya siku 30. Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa mvutano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili jirani za Amerika Kaskazini.
Canada ilikuwa miongoni mwa nchi chache zilizojibu ushuru wa Trump mwaka 2025 kwa kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya takribani dola bilioni 30 za Canada (C$30bn).
Baadaye, Carney aliondoa baadhi ya ushuru huo lakini akaendelea kutoza ushuru kwa magari, chuma na alumini kutoka Marekani.
Mapema mwaka huu, Mahakama Kuu ya Marekani iliamua kuwa ushuru mwingi ambao Trump aliweka kwa kutumia mamlaka ya dharura ulikuwa umeanzishwa kinyume cha sheria.
Ushuru mpya utatozwa kwa bidhaa zote zinazohusika, bila kujali kama zilikuwa zimejumuishwa katika makubaliano ya biashara huria kati ya Canada, Marekani na Mexico (USMCA).
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X, Mark Carney alisema:"Hii ni hatua ya hivi karibuni katika mfululizo wa hatua za upande mmoja za Marekani kuhusu biashara, ambazo zilianza kwa Marekani kuweka ushuru unaokiuka moja kwa moja Makubaliano ya Canada, Marekani na Mexico (USMCA)."
IRGC inasema iliishambulia na kuharibu ndege ya Marekani aina ya F-15 Jordan
Chanzo cha picha, IRNA
Idara ya Uhusiano wa Umma ya IRGC inasema kuwa, ikiendeleza mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya rada na mifumo ya ulinzi ya Marekani katika eneo hilo, imeharibu ndege ya Marekani aina ya F-15 iliyokuwa katika ghala lake.
IRGC inasema kuwa mfumo wa rada ya ulinzi dhidi ya makombora pia ulilengwa.
Katika siku za hivi karibuni, Iran imekuwa ikilenga maeneo nchini Jordan mara kwa mara.
Jana, gazeti la New York Times liliripoti, likimnukuu afisa wa jeshi la Marekani, kwamba makumi ya askari walijeruhiwa na helikopta kadhaa kuharibiwa katika mashambulio ya Iran dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan wiki iliyopita.
Masaa machache yaliyopita, Pentagon ilithibitisha kuwa Iran imejeruhi karibu wanajeshi 100 wa Marekani katika kipindi cha wiki mbili zilizopita cha mashambulio dhidi ya kambi za Marekani katika eneo hilo.
Mashambulio ya Iran ya tarehe 17 Julai dhidi ya Jordan pia yalisababisha vifo vya askari wa Marekani.
Habari za hivi punde, IRGC: Idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani waliuawa katika mashambulizi Jordan
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi IRGC linasema idadi kadhaa ya wanajeshi wa Marekani waliuawa katika mashambulizi yake katika eneo la Rukban nchini Jordan.
Katika taarifa nambari 40, IRGC ilisema kwamba katika "Wimbi 24 la Operesheni Nasr 2," ilishambulia "mahali ambapo vikosi vya jeshi la Marekani viliwekwa" katika mkoa wa Rukban wa Jordan, na kuua "idadi" yao.
Marekani haijajibu.
Kwa mujibu wa jeshi la Marekani, wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa katika mashambulizi ya makombora ya balistiki ya Iran na ndege zisizo na rubani huko Jordan tarehe 17 Julai.
Mahakama kutoa hukumu kuhusu kesi ya biashara ya watoto wachanga Indonesia
Mahakama nchini Indonesia inatarajiwa kutoa hukumu leo katika kesi inayohusu mtandao unaodaiwa kujihusisha na ununuzi na uuzaji wa watoto wachanga kwa ajili ya kuasiliwa.
Kesi hiyo, ambayo ilifichuliwa kwa mara ya kwanza mwaka jana, imeishtua Indonesia na Singapore, pamoja na wazazi waliowaasili watoto hao ambao sasa wanahofia kuwa huenda watoto wao walikuwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu.
Jumla ya watu 19, wanawake 18 na mwanaume mmoja wanashtakiwa katika jimbo la Java Magharibi kwa madai ya kusafirisha watoto wachanga kinyume cha sheria na kughushi nyaraka ili kufanya uhamisho wa watoto hao uonekane kuwa ni mchakato halali wa kuasili.
Kati ya watoto wachanga 34 wanaodaiwa kuhusika katika mtandao huo, takribani 20 walikuwa wakipelekwa Singapore.
Wakati wa kesi mapema mwaka huu, ilibainika kuwa takribani watoto 12 walikuwa tayari wameingia nchini Singapore.
Washtakiwa wameeleza kuwa hawakujua kuwa walichokuwa wakifanya kilikuwa kinyume cha sheria na walidai waliamini kuwa walikuwa “wakisaidia familia” kupata watoto.
Waendesha mashtaka wameiomba mahakama iwahukumu washtakiwa kifungo cha miaka kati ya mitano na kumi jela.
CBS: Pentagon yaripoti karibu wanajeshi 100 wa Marekani wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Iran ndani ya wiki mbili zilizopita
Chanzo cha picha, US Central Command
Maafisa wa Marekani wameiambia CBS News kwamba karibu wanajeshi 100 wa Marekani wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi kadhaa ya anga yaliyofanywa na Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani katika Mashariki ya Kati mwezi huu.
Sean Parnell, msemaji mkuu wa Idara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), alithibitisha takwimu hizo katika taarifa kwa CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani. Alisema kuwa kufikia tarehe 7 Julai 2026, karibu watu 100 walikuwa wamepata majeraha ya viwango mbalimbali, huku asilimia 96 yao wakirejea kazini.
"Wameonesha azma ya kurejea uwanjani.
Majeraha mengi yaliyopatikana yalikuwa mtikisiko mdogo wa ubongo," msemaji wa Pentagon alisema.
Taarifa hizi zinakuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran umeongezeka kufuatia kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa miezi kadhaa.
Jeshi la Marekani limekuwa likifanya mashambulizi dhidi ya Iran kila usiku kwa siku 10 mfululizo, likisema kuwa lengo la operesheni hiyo ni kuzuia mashambulizi ya Iran dhidi ya meli za kibiashara.
Kwa upande wake, Iran imekuwa ikishambulia maslahi ya Marekani na kambi zake zilizoko Jordan, Kuwait, Bahrain, pamoja na maeneo mengine ya washirika wa Marekani katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa Pentagon na kauli za Donald Trump, mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua wanne hadi sasa: watu wawili waliuawa na mmoja bado hajulikani alipo kufuatia shambulio la Iran nchini Jordan, huku mtu mmoja akifariki kaskazini mwa Iraq alipokuwa akijaribu kuharibu mabaki ya vilipuzi ambavyo havikulipuka baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani ya Iran.
Rais Samia azindua ujenzi wa reli ya kisasa Tabora–Kigoma, mradi wa dola bilioni 2.4
Chanzo cha picha, Ikulu Mawasiliano
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilomita 506, mradi ambao serikali inasema utakuwa kiungo muhimu katika kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kipande hicho cha reli, chenye thamani ya takribani shilingi trilioni 6.23 (sawa na dola za Marekani bilioni 2.4), kitaiunganisha Kigoma na mtandao wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam, hatua inayolenga kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwenda Burundi na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa serikali, reli hiyo itakapokamilika, safari ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma itachukua takribani saa saba hadi nane, ikilinganishwa na takribani saa 40 zinazotumika sasa kupitia reli ya kati ya kawaida.
Serikali pia inasema usafirishaji wa mizigo kwenda mashariki mwa DRC utakuwa wa haraka zaidi kuliko usafiri wa malori, ambao kwa sasa unaweza kuchukua kati ya siku nne na saba kutegemeana na eneo la mwisho la mzigo na hali ya barabara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia alisema uwekezaji katika miundombinu ya uchukuzi unalenga kuiunganisha Tanzania na masoko ya kikanda.
"Kijiografia, nchi yetu ni lango la biashara kwa nchi jirani zinazotuzunguka. Kwa msingi huo, kila tunapojenga reli, viwanja vya ndege, bandari au barabara, hatuunganishi mikoa yetu pekee, bali tunaiunganisha pia nchi yetu na fursa za masoko ya Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Kusini mwa Afrika."
Serikali inasema mradi huo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 15,000 wakati wa ujenzi na kuchochea uwekezaji, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika mikoa ya Tabora na Kigoma.
Changamoto za utekelezaji
Pamoja na matarajio hayo, upanuzi wa mtandao wa SGR nchini umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa fedha. Baadhi ya vipande vya reli vimeendelea kwa kasi, huku vingine vikichelewa kutokana na changamoto za ufadhili na utekelezaji.
Kwa mujibu wa serikali, ujenzi wa kipande cha Tabora–Kigoma umefikia zaidi ya asilimia 10 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 48, sawa na miaka minne, ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, wadau wa sekta ya uchukuzi wataendelea kufuatilia iwapo ratiba hiyo itaweza kutekelezwa, ikizingatiwa changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya miradi mingine ya SGR, zikiwemo gharama za ujenzi, upatikanaji wa fedha na uratibu wa miundombinu mingine kama bandari na usafiri wa majini.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi.
"Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika reli ya kisasa ya SGR, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini kwa lengo la kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi unaounganisha maeneo ya uzalishaji, masoko ya ndani na nchi jirani.
Uwekezaji huu unaendelea kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji, biashara na huduma za ugavi katika Afrika Mashariki na Kati."
Ushindani wa njia za biashara
Mradi huo unatekelezwa wakati ushindani wa njia za biashara katika Afrika Mashariki na Kati ukiendelea kuongezeka.
Tanzania inalenga kuimarisha nafasi ya Central Corridor, inayotumia Bandari ya Dar es Salaam, huku ikishindana na Northern Corridor inayopitia Bandari ya Mombasa nchini Kenya, pamoja na Lobito Corridor inayounganisha Angola, Zambia na DRC kwa lengo la kuvutia biashara ya madini.
Iwapo reli ya Tabora–Kigoma itakamilika kwa wakati na kuunganishwa kikamilifu na bandari pamoja na usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika, inaweza kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango muhimu la biashara kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kiongozi sugu wa genge la dawa za kulevya Ismael Zambada ahukumiwa kifungo cha maisha jela nchini Marekani
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Zambada akiwekwa chini ya ulinzi mnamo Julai 2024
Jaji wa Marekani ameamua kuwa Ismael "El Mayo" Zambada, mmoja wa watu mashuhuri na hatari zaidi katika magenge ya dawa za kulevya nchini Mexico, atatumikia kifungo cha maisha gerezani; uamuzi huu umetolewa miaka miwili baada ya kiongozi huyo mkuu kushawishiwa kuja Marekani kupitia operesheni maalum na ya siri iliyopangwa kwa ustadi.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 76, ambaye alianzisha Genge la Sinaloa (Sinaloa Cartel) pamoja na Joaquin "El Chapo" Guzmán, aliomba radhi mahakamani na pia akaamriwa kulipa dola bilioni 15 (pauni bilioni 11).
Mnamo mwaka wa 2024, mtoto wa El Chapo alimshawishi Zambada kuamini kuwa walikuwa wakisafiri kwenda kaskazini mwa Mexico kukagua viwanja vya ndege vya siri, lakini badala yake ndege yao ilitua Texas ambapo alikamatwa.
Mwaka jana, Zambada alifikia makubaliano na upande wa mashtaka na kukiri makosa ya kusafirisha dawa za kulevya na kula njama, ili kuepuka adhabu ya kifo. Siku ya Jumatatu, Jaji wa Wilaya ya Marekani Brian Cogan alitoa hukumu dhidi ya Zambada katika kikao cha mahakama ya shirikisho huko Brooklyn.
Kukiri kwake hatia kulileta adhabu ya lazima ya kifungo cha maisha gerezani. Zambada alizungumza kupitia mkalimani wa lugha ya Kihispania wakati wa kikao hicho. Alisema anaomba radhi "kwa madhara niliyosababisha na kwa mfano mbaya nilioonyesha" na akatoa wito kwa vizazi vijavyo "kuchagua njia tofauti".
"Kama kuna jambo moja ninaloweza kusema lenye thamani leo, ni hili: ni lazima vurugu na uhalifu wa kikatili vikome," alisema kiongozi huyo wa zamani wa genge la dawa za kulevya.
Marekani yafanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran, Trump aonya kuhusu kulipiza kisasi kufuatia vifo vya wanajeshi
Chanzo cha picha, US Central Command / X
Jeshi la Marekani linasema limefanya duru nyingine ya mashambulizi dhidi ya Iran ili "kudhoofisha zaidi" uwezo wake wa kushambulia meli katika mlango bahari wa Hormuz.
Mashambulizi hayo—ambayo ni ya usiku wa kumi mfululizo—yanakuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuiadhibu Iran kufuatia vifo vya wanajeshi wa Marekani.
Awali, Trump alisema Iran ilishambuliwa "vikali sana" usiku uliotangulia "kwa heshima" ya wanajeshi watatu wa Marekani waliouawa hivi karibuni—wawili nchini Jordan na mmoja nchini Iraq.
Kufuatia wimbi hilo la hivi karibuni, Iran ilisema ilishambulia meli mbili za mafuta katika njia hiyo ya maji, pamoja na vifaa vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, IRNA.
Rais Masoud Pezeshkian alisema Iran sasa inapambana katika "vita kamili" na Marekani. Wakati huo huo, Tehran ilisema ujumbe wa kidiplomasia bado unaendelea kati ya pande zote mbili kupitia wapatanishi, licha ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema kwenye mtandao wa X kwamba mashambulizi ya hivi karibuni yalilenga "vituo vya amri ya kijeshi, uwezo wa majini, maeneo ya kurushia makombora na ndege zisizo na rubani, pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga" ya Iran.
Meli za kibiashara zimeendelea kupita katika Lango la Hormuz, Centcom ilisema.
Natumai hujambo na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja