Iran yaishutumu Marekani kwa kushambulia miundombinu ya kiraia
Iran imeishutumu Marekani kwa kushambulia miundombinu ya kiraia katika wimbi la hivi punde la mashambulizi ya anga tangu mazungumzo ya amani yalipovunjika.
Vyombo vya habari vya serikali na mamlaka za mikoa zinasema kuwa madaraja, kituo cha treni na uwanja wa ndege vilishambuliwa. Kitengo cha BBC Verify kimethibitisha shambulio dhidi ya daraja moja katika mkoa wa Hormozgan.
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) haijatoa orodha ya maeneo yaliyolengwa, lakini imesema mashambulizi hayo yalilenga "kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran".
Rais Donald Trump ametishia kushambulia madaraja na vituo vya kuzalisha umeme vya Iran ili kuishinikiza Tehran kurejea kwenye mazungumzo ya kumaliza vita vilivyoanza tarehe 28 Februari kwa mashambulizi ya Marekani na Israel—hatua iliyochochea Iran kulipiza kisasi dhidi ya Israel na mataifa ya uarabuni ambayo ni washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba.
Kwa usiku sita mfululizo, Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.