Mambo yanayoifanya Iran ya sasa kuwa tofauti kabisa na ilivyokuwa awali

Mambo matano yanayoifanya Iran ya sasa kuwa tofauti kabisa na ilivyokuwa awali
    • Author, Paul Adams
    • Nafasi, Diplomatic correspondent
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati Rais wa Marekani, Donald Trump, alipoweka saini kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano na Iran katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika kwenye Jumba la Versailles nchini Ufaransa mwezi uliopita, wengi waliona tukio hilo kuwa na kejeli ya kihistoria.

Mwenyeji wa hafla hiyo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, huenda alitaka kuhakikisha makubaliano hayo yanakamilishwa kabla ya Trump kubadili msimamo wake. Inawezekana pia aliamini kuwa uzuri na fahari ya ukumbi maarufu wa Hall of Mirrors ungemvutia mgeni wake.

Hata hivyo, uchaguzi wa eneo hilo uliibua mara moja kumbukumbu za Mkataba wa Versailles wa mwaka 1919, ambao ulibadilisha kwa kiasi kikubwa ramani ya kisiasa ya Ulaya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ingawa mkataba huo uliweka msingi wa amani kwa muda, masharti yake magumu dhidi ya Ujerumani yalichochea hasira na chuki zilizochangia kuzuka kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia karibu miaka 20 baadaye.

Swali linalojitokeza sasa ni kama makubaliano haya mapya kati ya Iran na Marekani, licha ya kuwa tofauti kwa namna nyingi, yanaweza siku moja kuonekana kuwa na athari kubwa za kihistoria kama zile za Mkataba wa Versailles.

Takriban wiki tatu baada ya kutiwa saini, usitishaji huo wa mapigano bado unaonekana kushikiliwa, ingawa kwa hali ya tahadhari kubwa. Hata hivyo, baada ya matukio kadhaa ya mapigano madogo ndani na karibu na Mlango wa Hormuz, pamoja na ukweli kwamba chanzo kikuu cha mvutano huo bado hakijapatiwa suluhisho la kudumu, hali ya Mashariki ya Kati inaendelea kuwa tete.

Iran katika kipindi cha mpito

Wakati huo huo, Iran inapitia mojawapo ya vipindi muhimu zaidi katika historia yake ya kisasa.

Nchi hiyo inaendelea kuomboleza kifo cha aliyekuwa Kiongozi Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei, ambapo taarifa hii inadai aliuawa zaidi ya miezi minne iliyopita katika mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel yaliyoanzisha vita na kuangamiza sehemu kubwa ya uongozi wa juu wa Tehran.

Mabadiliko hayo yanaashiria mwisho wa enzi ya viongozi wa kizazi cha Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 na kuibuka kwa kizazi kipya cha viongozi wenye mtazamo tofauti kuhusu mustakabali wa taifa hilo.

Swali kubwa ni ikiwa Marekani na Israel, kwa kuyaondoa madarakani baadhi ya makada wa zamani wa Iran, wamefungua mlango wa kupatikana kwa viongozi wenye misimamo mikali zaidi au viongozi wenye uwezo mkubwa wa kuimarisha taifa hilo.

Vita vilivyobadili mwelekeo wa siasa za kikanda

Kwa mujibu wa Profesa Vali Nasr wa Johns Hopkins School of Advanced International Studies, vita hivi vinaweza kuwa na athari kubwa kuliko inavyodhaniwa.

"Vita vya kiwango hiki kwa kawaida hubadilisha kabisa kanuni za mchezo wa kisiasa. Ninaamini ndivyo vitakavyofanya katika Mashariki ya Kati," anasema.

Kabla ya vita, Iran ilikuwa tayari imeathiriwa na vikwazo vya kiuchumi vya muda mrefu pamoja na changamoto nyingine za ndani. Programu yake ya nyuklia ilikuwa imepata uharibifu mkubwa, huku mtandao wake wa washirika wa kikanda, maarufu kama Axis of Resistance, ukiwa umedhoofishwa kwa kiasi kikubwa.

Nchini Syria, utawala wa Bashar al-Assad ulikuwa umeondolewa madarakani. Nchini Lebanon, Hezbollah ilipoteza viongozi kadhaa waandamizi na sehemu muhimu ya uwezo wake wa kijeshi. Hamas katika Gaza ilikabiliwa na operesheni kubwa za kijeshi za Israel, huku waasi wa Houthi nchini Yemen pia wakilengwa na mashambulizi ya Marekani, Uingereza na Israel.

Kutokana na hali hiyo, wengi waliamini Iran ilikuwa dhaifu zaidi kuliko wakati wowote tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Je, Tehran ilinufaika na vita?

Licha ya matarajio ya baadhi ya wachambuzi kwamba mfumo wa utawala wa Iran ungeanguka, hilo halikutokea.

Badala yake, simulizi hii inaeleza kuwa Iran iliweza kusalia imara, kwa kiasi fulani kutokana na uwezo wake wa kutishia kufunga Mlango wa Hormuz, ambao ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.

Profesa Nasr anaamini kwamba badala ya kuanguka, Tehran huenda hata imenufaika kisiasa.

"Kizazi kipya kabisa kimechukua uongozi. Kilisimamia vita, na sasa kinaongoza pia kipindi cha amani," anasema.

Kwa maoni yake, viongozi hawa wapya hawatawaliwi na fikra za kimapinduzi kama watangulizi wao, bali wanazingatia zaidi kulinda maslahi ya dola na kufanya maamuzi ya haraka yanayolenga kuimarisha taifa.

Miongoni mwa sura mpya za uongozi ni Kiongozi Mkuu mpya Mojtaba Khamenei, Spika wa Bunge Mohammad Bagher Ghalibaf na Kamanda Mkuu wa IRGC Ahmad Vahidi.

Mchambuzi Sanam Vakil wa Chatham House anasema kuondoka kwa Ali Khamenei kumefungua mlango wa mageuzi ambayo kwa muda mrefu yalikwamishwa na mfumo wa zamani wa uongozi.

Uhusiano mpya na majirani wa Ghuba

Majibu ya Iran katika kipindi cha vita yalizua maswali kuhusu usalama wa mataifa ya Ghuba yanayotegemea ulinzi wa Marekani.

Ali Vaez wa International Crisis Group anasema baadhi ya nchi hizo sasa zinaanza kujiuliza ikiwa uwepo wa vituo vya kijeshi vya Marekani unazifanya ziwe salama zaidi au unazigeuza kuwa shabaha za mashambulizi.

Kutokana na hali hiyo, kuna ishara kuwa baadhi ya mataifa ya Ghuba yanafikiria kuboresha tena uhusiano wao na Tehran, ingawa bado yanategemea kwa kiasi kikubwa dhamana ya usalama kutoka Washington.

Vaez anaeleza kuwa huu unaweza kuwa "wakati wa mpito" ambao unaweza kufungua fursa za kujenga mahusiano mapya kati ya maadui wa zamani.

Je, wananchi wa Iran watanufaika?

Licha ya mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea, bado haijulikani iwapo wananchi wa Iran watanufaika moja kwa moja.

Ingawa kuna dalili ndogo za kulegezwa kwa baadhi ya vikwazo vya kijamii, wataalamu wengi wanaamini kuwa kipaumbele kikuu cha utawala mpya kitasalia kuwa kulinda mamlaka yake na kudhibiti upinzani wa ndani.

Hata hivyo, kuna ishara za mabadiliko ya polepole katika jamii. Utekelezaji wa sheria kali za hijabu umepungua katika maeneo mengi, huku baadhi ya shughuli zilizokuwa zikifanyika kwa siri hapo awali zikionekana kuvumiliwa zaidi.

Kwa mujibu wa Nasr, hatua hizo zinaonyesha juhudi za serikali kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za dola baada ya kipindi kigumu cha vita na maandamano.

Mustakabali usiojulikana

Kwa sasa, Iran ipo katika kipindi nyeti cha mpito kinachoweza kuamua mwelekeo wake wa kisiasa, kijamii na kidiplomasia kwa miongo ijayo.

Ingawa nchi bado inaongozwa kwa kiasi kikubwa na wasomi wanaohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), kuna matarajio kwamba kizazi kipya cha viongozi kitalazimika kuandaa mkataba mpya wa kijamii unaokidhi matarajio ya wananchi na changamoto za dunia ya kisasa.

Wakati huo huo, Tehran imeanza tena mawasiliano ya kidiplomasia na Washington. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, mchakato huo unaweza hatimaye kuzaa kile alichokiita "uhusiano uliobadilika kimsingi" kati ya mataifa hayo mawili.

Iwapo matumaini hayo yatageuka kuwa uhalisia, au yatabaki kuwa sehemu nyingine ya historia ndefu ya mivutano kati ya Marekani na Iran, ni jambo ambalo wakati pekee ndio utaweza kulijibu.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi