Mwanamume ashtakiwa Uingereza kwa kushirikiana na Iran kijasusi

Mwanamume mmmoja aliye na umri wa miaka 39 ameshtakiwa nchini Uingereza kwa kushirikiana na idara ya ujasusi ya Iran.
Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa. Wahid Abri, mkaazi wa Liverpool, alikamatwa siku ya Jumatano (Julai 15) kufuatia uchunguzi wa polisi wa kupambana na ugaidi uliofanyika Birmingham, na kupelekwa katika kituo cha polisi huko West Midlands.
Maafisa wa polisi walifanya upekuzi katika maeneo kadhaa huko Birmingham na Liverpool kama sehemu ya uchunguzi wao.
Bw. Abri ameshtakiwa kwa kushirikiana na idara ya ujasusi ya kigeni chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya Uingereza ya mwaka 2023 na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.
"Katika miaka ya hivi karibuni, kiwango cha shughuli zetu za uchunguzi wa usalama wa taifa kimeimarishwa kwa kiasi kikubwa," alisema Helen Flanagan, mkuu wa kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi jijini London.
"Kesi hii ni mfano mwingine wa juhudi zetu za kuzuia shughuli zenye utata zinazohusishwa na idara za ujasusi za kigeni," aliongeza.
Bi. Flanagan pia alisema: "Mtu mmoja tayari ameshtakiwa lakini hatuwezi kutoa maelezo zaidi kuhusu mashtaka hayo. Hata hivyo, ningependa kuuhakikishia umma kwamba hakuna tishio la moja kwa moja dhidi ya raia, kundi lolote katika jamii au mtu yeyote ambalo limebainishwa katika uchunguzi huu."






























