Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania yaimarisha tahadhari ya Ebola; Kenya yasema hali inadhibitiwa
Katibu Mkuu wa Afya ya Umma Kenya, Mary Muthoni, amesema mamlaka za afya zimefanikiwa kuwafuatilia karibu asilimia 99 ya watu waliotambuliwa kuwa na mawasiliano na wagonjwa wa Ebola.
Muhtasari
- Iran kwa Marekani: Kubali masharti yetu, Mlango-Bahari wa Hormuz ufunguliwe
- Wahukumiwa miaka 158 jela kwa mauaji ya wasafiri nchini Mexico
- Vituo vya mafuta vyashambuliwa usiku kucha mjini St Petersburg, Urusi
- Tanzania yaimarisha tahadhari dhidi ya Ebola huku visa Kenya vikifikia saba
- Diddy ahamishiwa gereza jingine huku akiendelea kupinga hukumu yake
- Martinez afanyiwa upasuaji baada ya jeraha baya
- Waandamanaji wanaopinga serikali wapambana na polisi Albania
- Wanajeshi wawili wafariki baada ya helikopta kuanguka Saudi Arabia
- Vifo vyathibitishwa kufuatia moto mkubwa karibu na kambi ya jeshi Canada
- Trump asema Marekani itazuia Iran kufufua mpango wake wa nyuklia
- Vurugu na uporaji vyakumba Ufaransa, zaidi ya 1,200 wakamatwa
- Dubois amgaragaza Wardley kwa raundi mbili na kutetea taji lake
- Tetesi za Soka Ulaya Jumapili: Gyokeres ataka kuondoka Arsenal Januari
- Marekani yataka Israel kukomesha vurugu za walowezi Ukingo wa Magharibi
Moja kwa moja
Na Asha Juma.
Iran kwa Marekani: Kubali masharti yetu, Mlango-Bahari wa Hormuz ufunguliwe
Iran imesema pendekezo lake kwa Marekani la kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz ndani ya siku saba bado lipo mezani, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi.
Akizungumza mjini Baghdad wakati wa mkutano wa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Araqchi alisema Iran ilitoa pendekezo hilo katikati ya mwezi Septemba baada ya makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kusambaratika.
Alisema Marekani iliwasilisha maoni yake kuhusu pendekezo hilo, lakini Iran bado inaendelea kuyachambua. Hata hivyo, alisisitiza kuwa njia ya kufunguliwa tena kwa mlango huo wa bahari iko wazi iwapo Marekani itakubali masharti ya Iran.
Miongoni mwa masharti yaliyowekwa na Iran ni:
- Kuondolewa kwa mzingiro wa Marekani dhidi ya bandari zake.
- Kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya mauzo ya mafuta ya Iran.
- Kusitishwa kwa uhasama katika maeneo mbalimbali ya mzozo katika kanda.
Araqchi alisema ikiwa Marekani itakubali masharti hayo, mlango huo muhimu wa bahari unaweza kufunguliwa ndani ya siku sita na mazungumzo kuanza tena siku inayofuata.
Moja ya maeneo makuu ya mkwamo ni msisitizo wa Marekani kutaka suala la mpango wa nyuklia wa Iran kujadiliwa tangu mwanzo wa mazungumzo.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema awali mwezi huu kuwa Iran lazima ipunguze kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kurutubisha uranium ili kukidhi matakwa ya Washington na kuhitimisha vita vya miezi minane kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Tehran inasema hatua ya kwanza inapaswa kuwa kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na kurejesha usalama katika njia hiyo ya kimkakati ya majini.
Kabla ya vita, mlango huo ulikuwa ukipitisha takriban asilimia 20 ya biashara ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) duniani, na hivyo kuwa moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa nishati duniani.
Soma Zaidi:
Wahukumiwa miaka 158 jela kwa mauaji ya wasafiri nchini Mexico
Jaji wa nchini Mexico amewahukumu wanaume watatu waliopatikana na hatia ya kuwaua ndugu wa Australia, Jake Robinson na Callum Robinson, pamoja na rafiki yao wa Marekani Carter Rhoad, kifungo cha miaka 158 na miezi tisa jela kila mmoja.
Mahakama ilielezwa kuwa ndugu hao pamoja na Rhoad waliuawa mwaka 2024 katika tukio lililoonekana kuwa jaribio la uporaji kwenye ufukwe wa faragha katika jimbo la Baja California, walipokuwa katika safari ya kuteleza kwenye mawimbi.
Mauaji hayo yalizua mshtuko mkubwa duniani, hususan nchini Australia, kwani eneo hilo kwa kawaida huchukuliwa kuwa salama ikilinganishwa na maeneo mengine ya Mexico yanayoshuhudiwa vurugu za mara kwa mara.
Wiki iliyopita, mahakama ilitoa hukumu ya hatia dhidi ya washukiwa hao. Mama wa ndugu hao, Debra Robinson, aliambia mahakama kuwa mauaji ya wanawe "yalinyakua maisha ya baadaye tuliyokuwa tumejiwekea matumaini ya kuyaishi pamoja nao."
Kwa sababu za kisheria, majina kamili ya waliohukumiwa hayakuwekwa wazi. Walitambulishwa tu kama Jesús Gerardo, Irineo Francisco na Ángel Jesús.
Mwezi Novemba mwaka jana, mpenzi wa anayedaiwa kuwa kinara wa kundi hilo, Jesús Gerardo maarufu kama "El Kekas", alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela katika kesi tofauti baada ya kukiri kuhusika katika uporaji huo.
Mahakama pia ilielezwa kuwa miili ya waathiriwa ilipatikana ikiwa imetupwa ndani ya kisima, huku ikiwa na majeraha ya risasi kichwani.
Wakati huo, mauaji hayo yaliwashtua wakazi wa eneo hilo na watalii katika mji wa pwani wa Ensenada, wengi wakishangazwa na jinsi mauaji hayo yalivyotekelezwa kwa urahisi na bila sababu ya msingi.
Vituo vya mafuta vyashambuliwa usiku kucha mjini St Petersburg, Urusi
Mtu mmoja ameuawa na wengine wasiopungua watano kujeruhiwa kufuatia shambulio la usiku kucha lililolenga vituo viwili vya mafuta mjini St Petersburg, Urusi.
Gavana wa eneo hilo, Alexander Beglov, amesema vikosi vya zimamoto vilikuwa vinapambana na moto uliotokea katika Kituo cha Mafuta cha St Petersburg na bohari ya mafuta ya Ruchyi baada ya mashambulizi hayo.
Kituo cha usafirishaji cha kampuni ya Ozon, inayofahamika kama "Amazon ya Urusi", pamoja na kituo cha data kinachomilikiwa na VKontakte (VK), mtandao wa kijamii unaofanana na Facebook nchini Urusi, pia viliripotiwa kushambuliwa.
Hadi sasa, Ukraine haijatoa tamko kuhusu mashambulizi hayo. Hata hivyo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Jumamosi kuwa Urusi imeilenga sekta ya nishati ya nchi yake mara 76 tangu Rais wa Marekani Donald Trump atangaze wiki iliyopita kile alichokiita "usitishaji wa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati".
Ukraine ilikuwa imesitisha mashambulizi yake dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Urusi kwa muda wa siku tatu baada ya tangazo hilo. Kyiv imekuwa ikisema mashambulizi hayo yanalenga kupunguza chanzo kikuu cha mapato kinachofadhili juhudi za vita za Moscow, huku ikiishutumu Urusi kwa kuendelea na mashambulizi yake wakati wa usitishaji huo.
Baadaye, Ukraine ilianza tena mashambulizi yake mapema wiki hii, hatua iliyomkasirisha Trump ambaye alitaka kuwe na makubaliano ya kusitisha mapigano ili kuwezesha utekelezaji wa makubaliano aliyofikia na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu usambazaji wa dizeli.
Ingawa Ukraine imewahi kuishambulia St Petersburg hapo awali, maeneo yaliyo karibu zaidi na mpaka wa Ukraine ndiyo ambayo kwa kawaida hukumbwa na mashambulizi mara nyingi zaidi. Kituo cha Mafuta cha St Petersburg kilishambuliwa mara ya mwisho mwezi Julai.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ilidungua zaidi ya ndege zisizo na rubani 1,000 za Ukraine katika anga ya Urusi katika usiku wa kuamkia Jumapili.
Soma Pia:
Tanzania yaimarisha tahadhari ya Ebola; Kenya yasema imechukua hatua za kudhibiti ugonjwa huo
Tanzania yaimarisha tahadhari dhidi ya Ebola huku Kenya ikisema imeimarisha hatua za kudhibiti ugonjwa huo
Serikali ya Tanzania imeimarisha hatua za kujikinga dhidi ya Ebola, huku Wizara ya Afya ya Kenya ikisema imechukua hatua za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Wizara ya Afya ya Tanzania imetoa mwongozo mpya wa usafiri kufuatia mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kisa cha kwanza kilichothibitishwa nchini Kenya cha mgonjwa aliyekuwa amesafiri kutoka DRC kupitia Uganda.
Katibu Mkuu wa Afya ya Umma Kenya, Mary Muthoni, amesema mamlaka za afya zimefanikiwa kuwafuatilia karibu asilimia 99 ya watu waliotambuliwa kuwa na mawasiliano na wagonjwa wa Ebola.
Katika mwongozo huo wa tarehe 17 Oktoba 2026, Wizara ya Afya ya Tanzania imesema wasafiri wote wanaoingia nchini humo wanapaswa kujaza fomu ya tamko la afya kupitia mfumo wa AfyaMsafiri kabla ya safari au wanapowasili nchini.
Wasafiri hao pia watakaguliwa katika viingilio vyote vya nchi, vikiwemo viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu. Uchunguzi huo utajumuisha kupima joto la mwili.
Aidha, wasafiri watakaotambuliwa kuwa katika kundi la hatari kubwa watafuatiliwa kwa siku 21 kupitia ujumbe wa simu au njia nyingine za mawasiliano ili kufuatilia hali zao za afya.
Hatua hizo zinalenga kusaidia kutambua mapema dalili zinazoweza kuashiria maambukizi na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Nchini Kenya, visa vinne vipya vilitangazwa tarehe 17 Oktoba, vikijumuisha wahudumu watatu wa afya waliomhudumia mgonjwa wa kwanza na ndugu mmoja wa kiume wa mgonjwa huyo aliyefariki dunia. Visa hivyo vilifanya jumla ya visa vilivyothibitishwa kufikia saba.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka za afya, wagonjwa hao wote wanne walikuwa tayari wamewekwa karantini walipoanza kuonyesha dalili na baadaye kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo.
Wagonjwa hao wanapatiwa matibabu ya kusaidia mwili kukabiliana na ugonjwa huo.
Mgonjwa wa kwanza alikuwa raia wa Kenya aliyekuwa akiishi nchini DRC. Alisafiri kupitia Uganda na kuwasili Nairobi tarehe 3 Oktoba. Alifariki dunia tarehe 5 Oktoba baada ya kulazwa hospitalini.
Kufikia tarehe 17 Oktoba 2026, watu 128 kati ya 130 waliotambuliwa kuwa na mawasiliano na wagonjwa walikuwa wamefikiwa na kufuatiliwa na mamlaka za afya, huku juhudi zikiendelea kuwatafuta watu wawili waliobaki.
Visa vipya vilithibitishwa miongoni mwa watu waliokuwa tayari wamewekwa karantini. Hata hivyo, mamlaka za afya zinaendelea kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa ili kubaini maambukizi mengine yanayoweza kujitokeza.
Hatua za Tanzania zinakuja wakati nchi za Afrika Mashariki zikiongeza ufuatiliaji wa afya katika mipaka na maeneo mengine ya kuingilia ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo kutoka nchi zilizoathirika.
Wizara ya Afya ya Kenya imewataka wananchi kuwa watulivu lakini waendelee kuchukua tahadhari na kufuata miongozo ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya Ebola.
Soma Zaidi:
Martinez afanyiwa upasuaji baada ya jeraha baya
Kipa wa Chelsea, Emiliano Martinez, amesema atarejea uwanjani ndani ya wiki chache baada ya kufanyiwa upasuaji kufuatia jeraha alilopata katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Everton Jumamosi.
Kipa huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 34 anaripotiwa kuvunjika taya baada ya kugongana kichwa na beki wa Everton, Jarrad Branthwaite, katika kipindi cha pili cha mchezo huo.
Martinez alipatiwa matibabu kwa dakika nane uwanjani kabla ya kutolewa kwa machela na kukimbizwa hospitalini. Baadaye, kocha wa Chelsea, Xabi Alonso, alithibitisha kuwa pia alipata mtikisiko wa ubongo.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii akiwa hospitalini, Martinez alisema:
"Asanteni kwa jumbe zenu zote. Upasuaji umefanikiwa. La muhimu zaidi ni kwamba tumeshinda na tumemaliza mchezo bila kuruhusu bao. Nitarejea ndani ya wiki chache."
Kutokana na jeraha hilo, kipa kijana Mike Penders aliyemrithi katika mchezo huo huenda akalinda lango la Chelsea katika mechi zijazo dhidi ya Tottenham Hotspur, Manchester United na Liverpool.
Akizungumzia Penders, Alonso alisema: "Mike ana ujasiri na haogopi majukumu makubwa. Tunamuamini kabisa. Alifanya vizuri alipoingia na yuko tayari wakati wowote timu inapomhitaji."
Pia unaweza kusoma:
Diddy ahamishiwa gereza jingine huku akiendelea kupinga hukumu yake
Mwanamuziki na mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Sean "Diddy" Combs, amehamishwa kutoka gereza la jimbo la New Jersey kwenda gereza la usalama wa chini la Pennsylvania, huku akiendelea na juhudi za kupinga hukumu yake mahakamani.
Diddy, mwenye umri wa miaka 56, anatumikia kifungo cha miezi 50 jela na amewasilisha rufaa akitaka kuachiliwa pamoja na kubatilishwa kwa hatia zake zinazohusiana na makosa ya ukahaba.
Mamlaka za magereza nchini Marekani hazikutoa sababu rasmi ya uhamisho huo, zikieleza kuwa ni suala linalohusu usalama na faragha ya mfungwa.
Uhamisho huo umefanyika wiki chache baada ya kuibuka kwa taarifa zilizodai kuwa Diddy alikuwa akipata upendeleo gerezani, ikiwemo madai ya upatikanaji wa simu za mkononi na bidhaa nyingine zilizopigwa marufuku.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, amewahi pia kuchukuliwa hatua za kinidhamu gerezani, jambo ambalo lilisukuma mbele tarehe yake ya kuachiliwa.
Pia unaweza kusoma:
Waandamanaji wanaopinga serikali wapambana na polisi Albania
Waandamanaji wanaoipinga serikali nchini Albania walipambana vikali na polisi wa kutuliza ghasia katikati mwa mji mkuu Tirana Jumamosi, huku maandamano yakiingia siku ya tano mfululizo.
Waandamanaji waliovaa barakoa, wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule za upili na vyuo vikuu, walirusha mawe na mabomu ya petroli dhidi ya polisi waliokuwa wakilinda Wizara ya Elimu, moja ya maeneo yanayolengwa na waandamanaji.
Polisi walijibu kwa kutumia magari ya kunyunyizia maji na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Pia kuna ripoti kwamba risasi za mpira zilitumika kwa mara ya kwanza.
Maandamano yaliyoanza majira ya joto sasa yamegeuka kuwa harakati kubwa dhidi ya serikali, huku waandamanaji wakimtaka Waziri Mkuu Edi Rama kujiuzulu kufuatia madai ya ufisadi yanayohusishwa na utawala wake.
Waandamanaji wengi katikati mwa Tirana walivaa barakoa za kujikinga na gesi au kufunika nyuso zao, huku watu wa kujitolea wakigawa sindano za maji ya chumvi kwa ajili ya kusafisha macho na kupunguza athari za gesi ya kutoa machozi iliyokuwa ikitanda mitaani.
Miluzi na milipuko ya mabomu ya petroli ilisikiwa mara kwa mara siku nzima ya Jumamosi.
Mchana, maandamano yalielekea zaidi katika ofisi ya Waziri Mkuu Edi Rama kwenye barabara kuu ya jiji, ambapo umati wa watu uliongezeka na kufikia idadi kubwa zaidi kuliko siku zilizotangulia.
Polisi wa kutuliza ghasia walikabiliwa na mashambulizi ya mawe na fataki kutoka kwa waandamanaji, huku wakijibu kwa kurusha makopo mengi ya gesi ya kutoa machozi. Baadhi ya makopo hayo yaliangukia mbali ndani ya umati na kusababisha taharuki.
Wakiwa na hasira kutokana na matumizi ya gesi hiyo, waandamanaji walikuwa wakisubiri moshi utoweke kabla ya kuendelea tena na mashambulizi yao.
Moshi mweusi kutoka kwa gari lililokuwa likiungua na ving'ora vya magari ya polisi na ambulansi vilitawala mazingira ya jiji hilo mchana kutwa.
Jioni ilipoingia, vikosi maalum vya polisi vilitumwa kuimarisha operesheni za kudhibiti ghasia.
Watu wengi kutoka pande zote mbili wamejeruhiwa. Hadi sasa, watu 80 wamefunguliwa mashtaka ya kuhusika katika ghasia, huku mamia wengine wakikamatwa au kuchunguzwa na mamlaka.
Soma Pia:
Vifo vyathibitishwa kufuatia moto mkubwa karibu na kambi ya jeshi Canada
Moto mkubwa uliotokea karibu na kambi ya jeshi katika jimbo la Alberta nchini Canada umeua na kujeruhi watu kadhaa, Waziri wa Ulinzi amesema, ingawa hajathibitisha idadi kamili ya waliofariki au kujeruhiwa.
Jeshi la Canada limekuwa likishirikiana na mamlaka za eneo hilo kudhibiti moto huo na kuchunguza chanzo chake. Waziri wa Ulinzi David McGuinty amesema hali bado ni tete na operesheni zinaendelea.
Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, ameandika kwenye mtandao wa X kwamba tukio hilo kubwa lililosababisha moto mkubwa ni la kusikitisha, akiongeza kuwa mawazo yake yako kwa wote walioathirika.
Moto huo ulizuka katika Kambi ya Jeshi ya Wainwright, mojawapo ya vituo vikubwa zaidi vya mafunzo ya kijeshi nchini Canada.
Wanajeshi wawili wafariki baada ya helikopta kuanguka Saudi Arabia
Helikopta ya upelelezi aina ya AH-6i imeanguka katika eneo la Najran, kusini mwa Saudi Arabia, kutokana na hitilafu ya kiufundi, na kusababisha vifo vya wafanyakazi wake wawili, msemaji wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, Meja Jenerali Turki al-Maliki, amesema.
Katika taarifa yake, al-Maliki amesema helikopta hiyo ilianguka katika eneo lililo chini ya mamlaka ya Wizara ya Walinzi wa Taifa wa Saudi Arabia.
Eneo la Najran limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, huku mapigano kati ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia na kundi hilo la Yemen yakizidi kushika kasi.
Msemaji wa kijeshi wa Houthi, Yahya Saree, aliandika kwenye mtandao wa X kuwa kundi hilo lilidungua helikopta ya kivita aina ya Apache karibu na Najran wakati ikidaiwa kufanya operesheni dhidi ya maeneo ya Houthi mpakani.
Hata hivyo, al-Maliki alipinga madai hayo, akichapisha picha ya helikopta kadhaa za Apache na kusema: "Mnadai mmeidungua, lakini itarudi uwanjani hivi karibuni."
Soma Pia:
Trump asema Marekani itazuia Iran kufufua mpango wake wa nyuklia
Rais wa Marekani Donald Trump amesema tena siku ya Jumamosi, wakati wa hotuba ya kampeni katika jimbo la Kentucky, kwamba suala la Iran litapatiwa suluhu hivi karibuni na bei za mafuta zitarejea katika hali ya kawaida.
"Hatutaki kurejea kila baada ya miaka miwili. Tunataka kumaliza kazi hiyo kabisa," Trump alisema.
"Iran ilipaswa kushambuliwa kwa sababu ilikuwa ikiendeleza silaha za nyuklia," Trump aliongeza.
Iran imekuwa ikikanusha mara kwa mara madai kwamba inajaribu kupata au kutengeneza silaha za nyuklia.
Trump aliongeza kuwa "tunahitaji kuhakikisha kwamba uwezo wa nyuklia wa Iran haujengwi upya, na hilo ndilo tunalolifanyia kazi hivi sasa."
Pia unaweza kusoma:
Vurugu na uporaji vyakumba Ufaransa, zaidi ya 1,200 wakamatwa
Vurugu zilizuka katika maeneo mbalimbali nchini Ufaransa Jumamosi wakati wa siku nyingine ya maandamano dhidi ya changamoto zinazokabili mfumo wa elimu na kupanda kwa gharama ya maisha.
Zaidi ya watu 1,200 walikamatwa wakati wa maandamano hayo ambayo serikali ya Ufaransa ilielezea kuwa ni "ongezeko la kiwango cha vurugu", huku takribani watu 550,000 wakishiriki maandamanoni kote nchini.
Mjini Paris, makabiliano makali yaliendelea hadi jioni kati ya waandamanaji na polisi wa kutuliza ghasia, ambao walitumia gesi ya kutoa machozi na magari ya kunyunyizia maji kutawanya umati wa watu.
Majengo kadhaa yalichomwa moto katika mji mkuu huo na maeneo mengine, yakiwemo ya mji wa Limoges, ambapo moto mkubwa katika jengo la halmashauri ya mji ulisababisha sehemu ya paa kuporomoka.
Pia kulishuhudiwa matukio ya uporaji katika miji kadhaa, huku uharibifu mkubwa ukiripotiwa katika majengo ya halmashauri na biashara mbalimbali.
Waziri Mkuu Sébastien Lecornu alisema maafisa wa polisi wapatao 150 walijeruhiwa
Mjini Paris, maandamano makubwa yalionekana kuwa ya amani kwa kiasi kikubwa wakati wa mchana. Kundi la vijana lililiambia BBC kuwa wao ni "wapenda amani" na kwamba "wanajaribu kuleta mabadiliko, lakini hakuna kinachobadilika."
Hata hivyo, kadri siku ilivyoendelea, baadhi ya makundi yalichoma mioto barabarani na kuwasha moto magari, ikiwemo katika maeneo maarufu katikati mwa jiji kama Place de la République.
Maduka yalivamiwa na kuporwa, angalau mgahawa mmoja uliteketezwa kwa moto, na BBC ilishuhudia mapigano yakizuka kati ya baadhi ya makundi yaliyokuwa kwenye maandamano hayo.
Polisi wa kutuliza ghasia walionekana wakilikimbilia kundi moja la waandamanaji katikati mwa Paris na kuwapiga baadhi yao kwa marungu.
Ingawa si jambo geni Ufaransa kushuhudia maandamano na machafuko ya mara kwa mara, wimbi hili la hivi sasa linakuja wakati taifa hilo likielekea katika kipindi cha sintofahamu ya kisiasa.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, anatarajiwa kuondoka madarakani mwaka ujao, huku kura za maoni zikionyesha kuwa uchaguzi wa urais wa Aprili unaweza kugeuka kuwa pambano kati ya kiongozi wa chama cha National Rally, Marine Le Pen, na Jean-Luc Mélenchon wa chama cha mrengo mkali wa kushoto cha La France Insoumise.
Soma Pia:
Dubois amgaragaza Wardley kwa raundi mbili na kutetea taji lake
Daniel Dubois ameendelea kuthibitisha hadhi yake kama bondia bora wa uzani wa juu nchini Uingereza baada ya kumshinda Fabio Wardley kwa mtoano katika raundi ya pili na kutetea taji lake la WBO mjini London.
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 29 alimwangusha Wardley kwa ngumi ya kulia ya moja kwa moja ndani ya sekunde 20 za kwanza za pambano lao la marudiano lililokuwa likisubiriwa kwa hamu katika ukumbi wa O2 Arena, kabla ya kuendelea kumshambulia bila huruma.
Wardley alinusurika raundi ya kwanza lakini alizidiwa na mashambulizi mengine makali katika raundi ya pili, hali iliyolazimisha kona yake kutupa taulo kuashiria kujisalimisha.
Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa mtoano kwa Dubois dhidi ya Wardley, miezi mitano tu baada ya kumng'oa mpinzani wake huyo wa Uingereza katika pambano la kusisimua la raundi 11 huko Manchester.
Safari hii hakukuwa na ushindani mkubwa kwa bingwa huyo, ambaye alitawala pambano tangu mwanzo hadi mwisho na kuongeza rekodi yake ya ushindi wa kulipwa kuwa 24, kati ya hiyo 23 akiwa ameshinda kwa mtoano, huku akiwa na vipigo vitatu pekee.
"Fabio ni bondia mzuri, lakini huu ni wakati wangu na enzi yangu. Nilikuja nikiwa na dhamira kubwa tangu mwanzo," alisema Dubois.
Kwa upande wake, Wardley mwenye umri wa miaka 31 alikubali kipigo chake cha pili katika mapambano 23 ya kulipwa.
"Daima nimekuwa nikijaribu kujipima dhidi ya wapinzani bora zaidi. Hakuna aibu kupoteza unapopambana na walio bora kabisa," alisema.
Wardley amekuwa bondia anayependwa na wengi kutokana na haiba yake ya kuvutia pamoja na utulivu wake wa kipekee. Alipoingia ulingoni, alionekana mwenye kujiamini na mwenye lengo thabiti, akichukua muda wake jukwaani huku fataki zikilipuka mbele yake. Tofauti na tabasamu lake la kawaida, safari hii uso wake ulionyesha umakini mkubwa na dhamira ya kupata ushindi.
Pia unaweza kusoma:
Tetesi za Soka Ulaya Jumapili: Gyokeres ataka kuondoka Arsenal Januari
Mshambulizi wa Sweden, Viktor Gyokeres, mwenye umri wa miaka 28, anaripotiwa kuwa tayari kushinikiza kuondoka Arsenal wakati wa dirisha la usajili la Januari kutokana na kukosa muda wa kutosha wa kucheza. (TeamTalk)
Liverpool wanaendelea kumfuatilia kiungo wa Borussia Dortmund, Felix Nmecha, 26, endapo watashindwa kufanikisha usajili wa kiungo Alex Scott, 23, kutoka Bournemouth. (CaughtOffside)
AC Milan wanajiandaa kumpatia kiungo wa kati wa Ufaransa, Adrien Rabiot, mkataba mpya utakaomuweka klabuni humo hadi mwaka 2030 kufuatia mwanzo wake mzuri wa msimu. (Corriere dello Sport - in Italian)
Kocha wa Chelsea, Xabi Alonso, anatazamia kuimarisha kikosi chake katika dirisha la usajili la Januari kwa kuwasajili wachezaji wawili kutoka Barcelona: beki wa Ufaransa Jules Kounde, 27, na kiungo wa Uholanzi Frenkie de Jong, mwenye umri wa miaka 29. (Football365)
Chelsea pia wanamfuatilia winga wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Marekani chini ya umri wa miaka 17, Mathis Albert, 17, ambaye hadi sasa ameichezea klabu hiyo ya Ujerumani mechi moja pekee. (FootballTransfers)
Beki wa AS Roma na Brazil, Wesley, 23, amevutia Arsenal, Manchester United na Newcastle. (SportWitness)
Beki wa zamani wa Brighton, Solly March, 32, anatarajiwa kujiunga na klabu ya Charlton inayoshiriki Championship kwa uhamisho wa bure. Mwingereza huyo amekuwa bila klabu tangu alipoachiliwa na Brighton mwezi Julai. (Football Insider)
Kiungo wa IFK Goteborg,17, Oliver Mansson, amevutia Arsenal na Chelsea. (TeamTalk)
Arsenal na Manchester United zimeondoa uwezekano wa kumwania beki wa kushoto wa Sporting na Uruguay, Maxi Araujo, 26. (Sport Witness)
Chelsea wako kwenye mazungumzo ya hatua za mwisho kumsajili winga wa Morocco, Gessime Yassine, mwenye umri wa miaka 20, kutoka klabu ya Strasbourg. (Ekrem Konur)
Soma Zaidi:
Marekani yataka Israel kukomesha vurugu za walowezi Ukingo wa Magharibi
Marekani imeitaka Israel kuchukua hatua zaidi kuzuia mashambulizi yanayotekelezwa na walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema.
"Tunasikitishwa sana na picha hizo na kile tunachokiona," Rubio alisema. "Tumewaomba Waisraeli, na tunaendelea kuwaomba, wakabiliane vikali na vitendo hivyo."
Kauli yake ilitolewa baada ya kusambazwa kwa video zinazoonyesha watu kadhaa wakimshambulia Heidi Levine, mwandishi wa picha raia wa Marekani anayefanyia kazi gazeti la Washington Post. Levine alikuwa mmoja wa watu wasiopungua wawili waliojeruhiwa katika tukio la Ijumaa, wakati walowezi wa Kiyahudi walipowashambulia raia wa Kipalestina.
Wanadiplomasia wa Ulaya pamoja na meya mmoja wa Ufaransa pia waliripotiwa kushambuliwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji.
Ubelgiji imelaani shambulio hilo lililomlenga balozi wake mkuu pamoja na wanadiplomasia wengine, na kuitaka Israel kuwafikisha mbele ya sheria waliohusika na tukio hilo.
Jeshi la Israel (IDF) pia lililaani kile lilichokiita "kitendo kikubwa cha vurugu" na kusema kuwa linaendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilitia shaka simulizi kuhusu yaliyotokea na kudai kuwa huenda tukio hilo ni sehemu ya "kampeni iliyoratibiwa ya kuchafua sifa ya Israel."
Rubio alisema Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio lililohusisha shambulio dhidi ya Levine. Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kupanda ndege kuelekea Uzbekistan, alisema anatarajia kupata taarifa kutoka Ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem ifikapo Jumapili.
Kwa mujibu wa Yesh Din, kundi la Israel linalofuatilia shughuli za walowezi, walowezi katika Ukingo wa Magharibi wamehusika katika mashambulizi yasiyopungua 170 dhidi ya Wapalestina tangu Septemba 27, kipindi kilichoanza karibu na msimu wa kila mwaka wa uvunaji wa mizeituni.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Mimi ni Asha Juma.