Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Simba imeamka au utawala wa Yanga unafika mwisho?
Simba SC imeondoa ukame wa zaidi ya miaka mitatu bila kuifunga Yanga SC katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye dabi ya Kariakoo iliyochezwa Oktoba 10, 2026, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ushindi huo umehitimisha kipindi kirefu ambacho Saimba imekuwa 'ikisasambuliwa dhidi ya watani wao wa jadi, huku kila dabi wanapochapwa inaendelea kuongeza presha kwa Simba na mashabiki wake.
Lakini uzito wa ushindi huo wa jana unaonekana zaidi ukiangalia historia ya ushindani wa timu hizo katika miaka ya hivi karibuni. Kabla ya mchezo wa jana Simba iliifunga Yanga mara ya mwisho katika ligi kuu ilikuwa Aprili 16, 2023, kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Kibu Denis na Henock Inonga, ambao tayari wameondoka klabuni hapo. Tangu wakati huo, Yanga ilikuwa imeendelea kujenga taswira ya timu yenye uwezo wa kuizuia Simba kupata ushindi katika mechi ambazo mara nyingi huwa na umuhimu mkubwa zaidi ya alama tatu.
Kwa ushindi wa jana Je, Simba imeanza kurejesha makali yake, au Yanga inaweza kuendelea kutawala licha ya kipigo hicho? Na je, ushindi huu unaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko ya muda mrefu au utabaki kuwa kisasi cha mchezo mmoja?
Simba ilionyesha nini tofauti katika ushindi wa jana?
Yanga ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya tano kupitia mshambuliaji wake Peter Shalulile, baada ya shambulizi lililomuhusisha Maxi Nzengeli. Yanga ilikwenda mapumzikoni ikiwa mbele kwa bao 1-0, lakini kipindi cha pili kilibadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo.
Simba ilisawazisha kupitia Neo Maema dakika ya 68, kabla ya Elie Mpanzu kufunga bao la ushindi dakika ya 71. Katika kipindi cha dakika tatu, Simba ilitoka nyuma na kuongoza mchezo. Kwa timu iliyokuwa imekaa muda mrefu bila kuwafunga watani zao, kufunga bao la kuongoza nyuma kwa kuruhusu bao la mapema kulikuwa na umuhimu wa kiufundi na kisaikolojia.
Zaidi ya mabao hayo, Simba ilionyesha uwezo wa wasogelea zaidi wapinzani wao. Takwimu za mchezo zilizoripotiwa na Pan Africa Football zinaonyesha kuwa Simba ilikuwa na asilimia 62 ya umiliki wa mpira na ilipiga mashuti 15, sita yakilenga lango, huku Yanga ikipiga mashuti saba, moja likilenga lango.
Hata hivyo, ni muhimu kuangalia ushindi huo kwa upana zaidi ya mchezo mmoja. Simba haikushinda kwa sababu tu Yanga ilishindwa kutumia nafasi zake ama kutengeza nafasi nyingi, bali ilihitaji pia kuonyesha uwezo wa kuhimili presha, kurekebisha makosa ya kipindi cha kwanza na kutumia nafasi muhimu.
Hayo ndiyo mambo ambayo itahitaji kuyadumisha katika mechi zijazo ili kuthibitisha kuwa ushindi huo ni sehemu ya mabadiliko ya kiwango, badala ya tukio la mara moja.
Ushindi wa Simba ni mwanzo wa mabadiliko au kisasi tu?
Kwa upande wa Simba, ushindi huu umeondoa mzigo wa muda mrefu wa kutopata ushindi wa ligi dhidi ya Yanga. Kuanzia Aprili 16, 2023 hadi Oktoba 10, 2026, Simba ilikuwa imekaa miaka mitatu, miezi mitano na siku 24 bila kuifunga Yanga katika ligi. Kwa hiyo, matokeo ya jana yana thamani kubwa kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki, ambao wamekuwa wakisubiri kuona timu yao iiondoa mwenendo huo mbovu.
Simba inahitaji kuendelea kushinda mechi nyingine za ligi, kudumisha kiwango chake na kuonyesha kuwa inaweza kushindana kwa ubingwa hadi mwisho wa msimu. Historia ya soka inaonyesha kuwa ushindi wa dabi unaweza kuongeza kujiamini na kuleta msukumo, lakini hauhakikishi ubingwa wala hauondoi moja kwa moja changamoto za timu katika msimu mzima.
Kwa Yanga, kipigo hiki ni jaribio la namna itakavyojibu mapigo baada ya kupoteza mchezo huo mkubwa dhidi ya watani zao. Timu hiyo ilitwaa ubingwa msimu uliopita kwa alama mbili mbele ya Simba iliyomaliza na pointi 73, na hivyo kuonyesha kuwa ushindani wa timu hizo katika ligi haukuwa wa upande mmoja kabisa.
Ingawa Yanga imekuwa na mafanikio makubwa ya ubingwa katika miaka ya karibuni, tofauti ndogo ya alama katika msimu uliopita inaonyesha kuwa Simba nayo imeendelea kuwa mshindani wa karibu na inaimarika. Hivyo alama tatu za jana zinaweza kuwa na athari kubwa kwenye msimamo wa ligi itakapofikia tamati.
Simba imeamka au utawala wa Yanga unafika mwisho?
Kuelewa uzito wa swali hili kunahitaji kuangalia historia ya mataji na mechi zinazoikutanisha timu hizo.
Mechi ya jana ilikuwa ya 117, kwa timu hizi kukutana katika Ligi Kuu tangu mwaka 1965 na kati ya hizo, Yanga imeshinda 42 na SIMBA ikishinda 33, ukijumlisha na ushindi wea jana. Michezo 42, ilimalizika kwa sare Katika mechi hizo yamefungwa jumla ya mabao 235, ambapo Yanga imefunga 126, na Simba ikifunga mabao 109.
Kwenye upande wa ubingwa, Yanga imetwaa ubingwa mara tano mfululizo kuanzia 2021/22 hadi 2025/26, na kufikisha mataji 32 ya ligi. Huo ni mfululizo unaoonyesha uthabiti wa kikosi na benchi la ufundi kwa misimu kadhaa. Simba, ambayo mara ya mwisho ilitwaa ubingwa msimu wa 2020/21, inahitaji kufanya zaidi ya kuifunga Yanga ili kuondoa pengo hilo la mafanikio ya hivi karibuni.
Hata hivyo, historia pia inaonyesha kuwa utawala katika soka si wa kudumu. Simba yenyewe iliwahi kutwaa mataji matano mfululizo kati ya 1976 na 1980. Yanga nayo imefikia rekodi hiyo ilipoitwaa ubingwa msimu uliopita. Hilo linaweka ushindani wa timu hizo katika muktadha mpana ambapo mafanikio ya muda mrefu yanahitaji timu kuendelea kujijenga, kuboresha kikosi na kuwa na uwezo wa kushindana msimu baada ya msimu.
Kwa uapnde wa Simba, changamoto sasa ni kugeuza ushindi wa jana kuwa mwendelezo wa matokeo mazuri. Kwa upande wa Yanga, ni kuthibitisha kuwa inaweza kuendelea kuwa timu ya kutisha katika dabi na katika mbio za ubingwa licha ya kupoteza mchezo huu.
Ni ngumu kusema mopja kwa moja kuwa Yanga imerudi kuwa kibonde kwa kipigo kimoja, kama ambavyo ushindi huo wa jana hauwezi kuthibitisha kuwa Simba imerejesha utawala wake.
Ila jambo kubwa lililo wazi ni kwamba Simba imeondoa ukame wake wa muda mrefu dhidi ya Yanga katika ligi na kuifanya dabi ya Kariakoo kuwa na sura mpya ya ushindani, ambao ulianza kuonekana ni upinzani wa kawaida. Lakini kama utawala wa Yanga unafika mwisho, au Simba imerejesha makali yake, hilo litafahamika mwishoni mwa msimu atakapotangazwa bingwa, na pia baada ya mchezo wa mzunguko wa pili utakapopigwa tena.