Wakati mila za mazishi zinapokutana na tishio la Ebola

    • Author, Robert Kiptoo
    • Akiripoti kutoka, BBC Bunia
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeendelea kushuhudia simanzi na majonzi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Maambukizi ya sasa yamesababishwa na aina adimu ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ambayo husababisha vifo kwa takribani robo ya watu wanaoambukizwa.

Ebola huambukizwa kupitia kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa, ikiwemo damu, mkojo, matapishi, shahawa na maziwa ya mama.

Kutokana na urahisi wa virusi hivyo kusambaa, ni lazima taratibu kali za afya zifuatwe ili kuzuia maambukizi zaidi. Miongoni mwa hatua muhimu zaidi ni kuhakikisha mazishi salama na yanayozingatia kanuni za afya ya umma.

Hata hivyo, kuhakikisha kuwa waliofariki kutokana na ebola wanazikwa kwa uangalifu zaidi imekuwa changamoto kwa wahudumu wa afya.

Kisa? Familia nyingi zinavamia vituo vya matibabu vinavyohudumia wagonjwa wa ebola kudai miili ya ndugu zao waliofariki dunia wakawapatie heshima za mwisho kimila.

Katika maeneo kama Rwampara na Mongbwalu, hali ya wasiwasi imekithiri zaidi.

Mara kadhaa wakaazi wamevamia vituo vya afya na hata kuviteketeza kwa moto baada ya kuzuiwa kuchukua miili ya jamaa zao kwa ajili ya mazishi ya kijadi.

Kwa jamii nyingi za eneo hilo, mazishi si tukio la kawaida. Ni sehemu muhimu ya utamaduni na heshima kwa marehemu. Kifo huonekana kama mwanzo wa safari nyingine, na safari hiyo inapaswa kuambatana na taratibu maalumu za kijamii na kiroho.

Kwa mujibu wa wataalamu wa anthropolojia, katika tamaduni nyingi za Kiafrika familia hukaa karibu na mwili wa marehemu, huuosha, huugusa na kuaga kwa njia mbalimbali za kitamaduni kabla ya mazishi kufanyika.

Lakini tangu mlipuko wa Ebola mila na desturi imelazimika kubadilika.

Mwili wa marehemu kuwa chanzo cha maambukizi

Julienne Anoko, mwanaanthropolojia wa Shirika la Afya Duniani (WHO), anasema kwa kawaida waombolezaji huwavalisha marehemu mavazi mazuri, huku taratibu za mazishi zikidumu kwa siku kadhaa.

Anaeleza kuwa jamii nyingi katika jimbo la Ituri huamini kuwa marehemu anapaswa kuonekana katika hali yake bora zaidi kwa kuwa anakuwa "anasafiri kutoka ulimwengu huu kwenda ulimwengu mwingine, ulimwengu wa mababu".

"Wanawake huvalishwa gauni za harusi na kupambwa kwa vipodozi. Watu huimba na kusherehekea maisha ya marehemu kwa sababu wanaamini ni safari mpya, si mwisho wa maisha," ameiambia BBC.

Hata hivyo, mtu anayefariki kutokana na Ebola hulazimika kuwekwa mara moja kwenye mfuko maalumu usiovuja majimaji ya mwili kabla ya kuzikwa, ili kuzuia kuenea kwa maambukizi.

Lakini Ugonjwa wa Ebola sasa umebadilisha mambo mengi. Hata katika kifo virusi vya Ebola vinasalia kuwa hatari. Na mwili ambao jamii nyingi hapa Mashariki mwa Congo, wanaidhamini sasa imegeuka na kuwa Chombo hatari zaidi cha kusambaza virusi vya ebola.

Lakini ili kuzuia maambukizi zaidi ya ebola, Familia nyingi zinanyimwa nafasi yao muhimu ya mwisho ya kuwaaga jamaa wao.

Sherehe za mazishi zilivyobadilika

Maria Munoz Bertrand, mratibu wa dharura za afya ya umma katika Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC), anasema juhudi zinaendelea kufanywa ili kuzingatia mahitaji ya familia za waathiriwa huku usalama wa afya ukipewa kipaumbele.

Katika jimbo la Ituri, hatua hizo zinajumuisha matumizi ya majeneza, ambapo mwili uliowekwa kwenye mfuko maalumu wa kuzuia kuvuja kwa majimaji huwekwa ndani ya jeneza. Jeneza hilo huwa na sehemu ndogo za uwazi pembeni ili kuwawezesha waombolezaji kumwona marehemu bila kuhatarisha afya zao.

Mabadiliko mengine yamefanywa kwenye mifuko ya kuhifadhia miili, ambayo sasa imewekewa sehemu ya juu yenye uwazi ili uso wa marehemu uonekane.

"Tunahitaji kuwa karibu sana na jamii, kushirikiana nazo kwa ukaribu na kuhakikisha zinaelewa kinachoendelea, zinapata taarifa sahihi na zinatoa ridhaa yao," anasema Munoz Bertrand.

Kwa nini jamii zinapinga taratibu za afya?

Kwa wakazi wengi wa mashariki mwa Congo, kutomzika mpendwa wao kwa mujibu wa mila ni sawa na kumvunjia heshima.

Imani hizi zimefanya baadhi ya familia kuendelea kushinikiza kurejeshewa miili ya marehemu hata pale ambapo kuna hatari ya kueneza maambukizi.

Changamoto hiyo imeongezwa na kusambaa kwa taarifa za kupotosha kuhusu Ebola. Baadhi ya watu wanaamini kuwa ugonjwa huo haupo au kwamba ukweli kuhusu maambukizi unafichwa.

Kutokana na hali hiyo, wahudumu wa afya wamekuwa wakituhumiwa kuwa mawakala wa mataifa ya Magharibi na mara nyingine wamekuwa walengwa wa mashambulizi kutoka kwa wananchi wenye hasira.

Katika baadhi ya matukio, maafisa wa kujitolea wanaoshiriki mazishi salama ya waathiriwa wa Ebola wamefukuzwa makaburini au kushambuliwa, huku familia zikichukua miili ya marehemu na kuirejesha nyumbani kwa ajili ya kufanyiwa tambiko na ibada za kiafrika kinyume kabisa na ushauri wa madaktari.

Kanisa nalo lakabiliwa na maamuzi magumu

Kanisa Katoliki, ambalo waumini wake wengi wameathiriwa na ebola, linasema limejikuta katika nafasi ngumu kati ya kuheshimu mila za jamii na kulinda afya za waumini.

''Jukumu letu limekuwa kutoa mwongozo wa kiimani huku tukihamasisha waumini kufuata masharti ya afya yaliyowekwa ili kuzuia maambukizi zaidi'', anasema Padre X ni msaidizi wa baba Paroko katika kanisa la Noterdamme mjini Bunia.

Kutokana na hatari ya maambukizi, baadhi ya shughuli za kidini na sakramenti zimelazimika kusitishwa au kufanywa kwa tahadhari kubwa.

Sayansi dhidi ya mila

Katika mashariki mwa Congo, vita dhidi ya Ebola si suala la matibabu pekee. Ni mapambano yanayohusisha imani, utamaduni na sayansi.

Wataalamu wa afya wanaamini kuwa mafanikio ya kudhibiti ugonjwa huo yatategemea uwezo wa jamii kuelewa kwamba katika mazingira ya mlipuko wa Ebola, kuepuka kugusa mwili wa mpendwa aliyefariki si kukosa upendo, bali ni hatua ya kuwalinda walio hai.

Kwa wengi, huo ni uamuzi mgumu. Lakini katika eneo ambalo Ebola imeendelea kuua, viongozi wa afya wanaonya kuwa ili kuokoa maisha zaidi, baadhi ya mila za kale zitalazimika kuendana na mahitaji ya kisasa ya afya ya umma.