Jinsi Wahouthi wanavyopanua ushawishi wao katika Pembe ya Afrika

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Kundi la Wahouthi wa Yemen, Ansar Allah, limeonekana kuimarika na kupata ushawishi mkubwa zaidi baada ya kutwaa maeneo ya kimkakati karibu na Mlango wa Bab al-Mandab, na mashambulizi yake yaliyolenga maeneo tofauti nchini Saudi Arabia.

Matukio hayo yameashiria maendeleo makubwa katika uwezo wa kijeshi wa kundi hilo katika miaka ya hivi karibuni.

Ripoti iliyotolewa mwishoni mwa mwezi uliopita na The Century Foundation, shirika lisilo la kiserikali la utafiti lenye makao yake New York, imeonyesha kuongezeka kwa uhusiano kati ya kundi la Wahouthi na makundi mengine yenye silaha katika Pembe ya Afrika.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa pia inaashiria kuwepo kwa ubadilishanaji wa silaha na mafunzo kati ya Wahouthi na kundi la Alshabaab nchini Somalia, ambalo lina uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Uhusiano ambao Wahouthi wamejenga katika Pembe ya Afrika umefikia kiwango gani? Je, tutarajie kuundwa kwa muungano wa kikanda wa makundi yenye silaha?

Kutoka ushirikiano wa kimaslahi hadi wa mkakati

Nadwa Al-Dawsari, mtafiti katika Center for Armed Groups na mmoja wa waandishi wa ripoti ya Century Foundation, aliiambia BBC Arabic kwamba uhusiano mwingi wa Wahouthi katika Pembe ya Afrika hapo awali ulikuwa umejikita katika kubadilishana silaha.

"Wahouthi wamekuwa wakitegemea wasafirishaji wa bidhaa za magendo na mitandao ya uhalifu katika Pembe ya Afrika kusafirisha silaha, watu na bidhaa, lakini tumebaini kuwa uhusiano huo umeendelea kwa kiasi kikubwa, hasa kufuatia matukio ya Oktoba 7."

Ushahidi wa wazi zaidi wa kuongezeka kwa uwepo wa Wahouthi katika eneo hilo unatoka Somalia, ambako uhusiano kati ya Ansar Allah na kundi la Al-Shabaab umeimarika kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, kwa mujibu wa ripoti ya Century Foundation pamoja na ripoti ya jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa mwishoni mwa mwaka jana inaonyesha kuwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili umeimarika kwa kiasi kikubwa, ukihusisha usafirishaji wa silaha kwa njia ya magendo na mafunzo ya kiufundi, yakiwemo mafunzo kuhusu mbinu za operesheni, kubadilishana utaalamu wa kijeshi na usafirishaji wa bidhaa zingine.

Ripoti hiyo inaonya kwamba ushirikiano huo unaweza kuwa tishio si tu kwa usalama na utulivu wa Yemen, bali pia kwa eneo zima la Pembe ya Afrika.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ushirikiano huo na Al-Shabaab hauishii katika kunufaishana, bali pia ni sehemu ya mkakati wa Wahouthi wa kupanua ushawishi wao katika eneo hilo.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, mamlaka za Somalia zilikamata silaha na vilipuzi vilivyosafirishwa kimagendo kutoka Yemen.

Raia mmoja wa Somalia anayehusishwa na Al-Shabaab alikiri kushirikiana na Wahouthi na kuwezesha safari za takriban Wasomali 400 kwenda kupokea mafunzo ya kijeshi katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi nchini Yemen.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa Jopo la Wataalamu lilipokea taarifa kutoka kwa vyanzo vya kuaminika kwamba Al-Shabaab ina uwepo wa kiutendaji katika Jimbo la Hadramawt, nchini Yemen.Wasomali katika eneo hilo wanahusika hasa na kununua silaha kutoka kwa wanachama wa Houthi na kuzisafirisha kimagendo hadi Somalia.

Wahouthi na Al-Shabaab wana malengo tofauti na wanafanya shughuli zao katika mazingira tofauti. Makundi hayo mawili pia yanatofautiana kiitikadi; Wahouthi wanafuata tawi la Uislamu wa Kishia, huku wanachama wa Al-Shabaab wakiwa Wasunni.

Je, uhusiano kati yao utaendelea kuwa wa kimkakati na wa kimaslahi, au unaweza kubadilika na kuwa jambo kubwa zaidi?

Katika taarifa yake kwa BBC News Arabic, Profesa Stig Jarl Hansen, profesa wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Norwegian na mwandishi wa kitabu Al-Shabaab in Somalia: History and Ideology of an Armed Islamist Movement, anasema,

"Kwa kuzingatia tofauti za kiitikadi, ikiwemo uwezekano kwamba uhusiano wa aina hii unaweza kuwafanya waajiriwa wapya katika safu za Al-Shabaab kuachana na kundi hilo, nadhani uhusiano huu una msingi wa manufaa na maslahi."

Hansen anaongeza kuwa "Huenda kukawa na baadhi ya viongozi ndani ya kundi la Al-Shabaab waliotaka kutumia utaalamu wa Wahouthi katika kutengeneza ndege zisizo na rubani.

Al-Shabaab kufikia sasa imeweza kujipatia fedha nyingi, jambo ambalo huenda limewavutia Wahouthi.

Hata hivyo, Al-Dossari anaamini kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili unaweza, katika siku zijazo,kuunda muungano mmoja, na huenda ikawa vigumu kumaliza mzozo wa Yemen na Somalia.

Somalia imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa kivita kwa karibu miongo miwili kati ya serikali ya Mogadishu na kundi la Al-Shabaab.

Kuenea zaidi katika eneo la Bahari ya Shamu

Somalia si nchi pekee katika Pembe ya Afrika ambayo imewavutia Wahouthi.

Ripoti ya Century Foundation pia inataja Djibouti, Sudan na Eritrea kama nchi nyingine ambazo shughuli na uwepo wa Wahouthi unaongezeka, na kuna mazingira yanayoweza kuiwezesha kundi hilo kupanua ushawishi wake katika siku zijazo.

Jiografia inaweza kueleza kwa nini Wahouthi wana nia ya kutafuta vyanzo mbalimbali vya malighafi na vifaa vinavyotumika kutengeneza silaha zao, hasa nchini Djibouti, ambayo iko kwenye lango la kusini la Bahari ya Shamu, mkabala na Yemen, na ina moja ya bandari muhimu zaidi katika eneo hilo, Bandari ya Djibouti, inayotazama Mlango wa Bab al-Mandab.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa bandari hiyo imekuwa kitovu cha shughuli za usafirishaji wa bidhaa za magendo zinazohusishwa na Wahouthi, ambao hutumia miundombinu iliyopo ya kibiashara na mitandao halali ya usafirishaji, kupata vifaa na sehemu mbalimbali wanazohitaji, ambazo baadaye husafirishwa hadi Yemen.

Katika muktadha huo, Al-Zubaidi, ambaye yuko karibu na kundi la Wahouthi, anaamini kuwa Bandari ya Djibouti iko chini ya utaratibu wa Umoja wa Mataifa wa ukaguzi na uthibitishaji. Anahoji jinsi kundi hilo linavyoweza kutuhumiwa kusafirisha mizigo kimagendo kupitia bandari hiyo, ikizingatiwa kwamba Marekani na Saudi Arabia wameshika doria na wanaendelea kufuatilia shughuli zinazoendelea bandarini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wahouthi walianza kuunga mkono jeshi la Sudan katika mapambano yake dhidi ya Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) ,katikati ya mwaka 2024, wakidaiwa kuwapatia silaha kwa niaba ya Iran.

Ripoti hiyo, ikinukuu vyanzo mbalimbali, inaonyesha kuwepo kwa wanachama wa Houthi katika Port Sudan, ambayo wanaitumia kama kituo cha shughuli za vifaa na fedha, pamoja na usafirishaji wa silaha na watu kuvuka Bahari ya Shamu katika pande zote mbili.

Ingawa ushahidi unaounga mkono madai hayo unaongezeka, ripoti hiyo inasema bado haijathibitisha madai hayo kwa ukamilifu.

Ripoti ya Century Foundation inadokeza kwamba huenda Wahouthi wanajenga upya uhusiano wao na Eritrea kwa msaada wa Iran, na huenda wakaitumia kama njia ya kupitisha silaha zinazoelekezwa Yemen. Hata hivyo, ushahidi unaopatikana hadharani bado haujathibitisha kwa uhakika shughuli katika maeneo yanayodaiwa kutumika kwa usafirishaji wa kimagendo.

Al-Dossari anasema ukosefu wa ushahidi haupaswi "kutufanya tufumbe macho dhidi ya kile tunachokiona katika Pembe ya Afrika."

Aidha aliongezea kuwa,

"Kuna somo tulilojifunza kutokana na mzozo wa Yemen, nalo ni kwamba Wahouthi hawapaswi kupuuzwa kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi wa kutosha. Nakumbuka kwamba muongo mmoja uliopita kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu kiwango cha msaada wa Iran kwa Wahouthi, na kwa kiasi fulani mjadala huo ulitokana na ukosefu wa ushahidi madhubuti. Kufikia wakati ushahidi ulipokuwa wa kutosha kuthibitisha hilo, Wahouthi walikuwa tayari wamejenga uwezo mkubwa wa kijeshi, uhusiano wao na Iran ulikuwa umeimarika, na imekuwa vigumu zaidi kukabiliana nao."

Je, tutarajie kuundwa kwa muungano wa kikanda?

Ripoti ya Century Foundation inasema kuongezeka kwa uwepo wa Wahouthi katika Pembe ya Afrika, kando ya Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, kunaashiria juhudi zilizofanywa na Iran na kundi la Hezbollah la Lebanon mwanzoni mwa karne hii za kuunda mitandao ya makundi yenye silaha Mashariki ya Kati.

Mtandao huo baadaye ulijulikana kama Axis of Resistance. Ripoti hiyo inaeleza kwamba Wahouthi wanajaribu kuimarisha nafasi yao kama kituo kipya cha mhimili huo.

Hata hivyo, Profesa Hansen anaamini kwamba kuelezea uhusiano wa sasa kama dalili ya kuibuka kwa mtandao mpana wa kikanda wa makundi yenye silaha ni "kutia chumvi kwa kiasi kikubwa." Anaongezea kwamba "shughuli za Wahouthi barani Afrika bado ni chache, na ni ndogo zaidi ikilinganishwa na shughuli za Iran."

Jukumu la Iran linaifanya hali hiyo kuwa tata zaidi. Kuna muungano wa karibu kati ya Tehran na Wahouthi, ambao wamenufaika na msaada wa kijeshi kutoka Iran, lakini pia wameimarika katika kutengeneza mifumo yao wenyewe ya silaha.

Uhusiano wao na Tehran haimaanishi kwamba Iran inawadhibiti kikamilifu. Hansen anasema:

"Wahouthi ni washirika wa Wa Iran, lakini si vibaraka wa Tehran. Ina maana Wahouthi wanaweza kuiunga mkono Iran, mradi msaada huo usiwagharimu sana."

Hivyo basi, swali linabaki, Je, kuna dalili zozote zinazoonyesha kwamba uhusiano wa Wahouthi na makundi yenye silaha katika Pembe ya Afrika unabadilika na kuwa mtandao wa kikanda unaoweza kudumu na kuendelea kukua?

Abdul Ghani al-Zubaidi anaelezea uhusiano kuwa uhusiano huo bado ni mdogo

"Tunatamani tungekuwa na mafanikio ya kiusalama, kisiasa au kiuchumi na nchi yoyote inayopakana na Bahari ya Shamu au iliyo karibu nasi, lakini nadhani Wahouthi kwa sasa wanafikiria jinsi ya kupata chakula na silaha, na kwa sasa tuko katika hali ya vita."

Al-Dossari anasema itakuwa vigumu kubaini ni kwa kiwango gani uhusiano huo utaendelea kwa sababu huenda utaendelea kufanyika kwa usiri.

Anasema dalili za kujua uwepo wa Wahouthi Pembe ya Afrika inaweza kujumuisha Al-Shabaab au makundi mengine yenye silaha kutumia ndege zisizo na rubani au silaha katika Pembe ya Afrika zinazoonyesha matumizi ya teknolojia ya Wahouthi au Iran; kufanya mashambulizi ya baharini au vitendo vya uharamia katika Ghuba ya Aden na magharibi mwa Bahari ya Hindi kwa njia ya kisasa zaidi au iliyoratibiwa, kuwepo kwa Wahouthi kwa kiwango kikubwa zaidi nchini Somalia, au shughuli za usafirishaji wa magendo, mafunzo na vifaa kuwa za kisasa zaidi na zenye uratibu mkubwa.

Iwapo uhusiano huo utaimarika, Al-Dossari anasema, vitisho kwa usalama wa usafiri wa baharini katika Mlango wa Bab al-Mandab na Ghuba ya Aden vinaweza kuenea zaidi na kuwa na uwezo mkubwa wa kubadilika, na hivyo kuwa vigumu zaidi kutambua, kubaini chanzo chake au kuvizuia.