Mambo 7 tuliyojifunza kuhusu EPL hadi sasa

    • Author, Emlyn Begley
    • Nafasi, BBC Sport journalist
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Ligi Kuu England inachukua mapumziko ya karibu wiki tatu wakati timu za taifa zikijiandaa kwa mechi za kimataifa.

Nini hasa tumejifunza katika mechi tano za mwanzo za msimu zilizochezwa na kila timu?

Haya ni mambo saba muhimu.

Arsenal wanafungika

Mabingwa wa Ligi Kuu, Arsenal, walikuwa wanaonekana kama timu ambayo ilikuwa vigumu sana kuizuia katika wiki za mwanzo za msimu.

Ushindi dhidi ya Brighton Jumamosi ungeifanya Arsenal kushinda mechi nane mfululizo katika mashindano yote tangu kuanza kwa msimu, jambo ambalo lingefikia rekodi ya klabu.

Lakini mambo yalibadilika baada ya Arsenal kufungwa 3-0 na Brighton kwenye uwanja wa Amex.

Arsenal walikuwa hawajafungwa mechi ya ligi kwa tofauti ya zaidi ya bao moja tangu Oktoba 2024, lakini safari hii walipoteza kwa tofauti ya mabao matatu.

Hili lilikuwa pia ni kipigo chao kikubwa zaidi katika ligi tangu Mei 2023, walipofungwa 3-0 na hao hao Brighton.

Kocha Mikel Arteta alisema matokeo hayo hayawezi kufuta kile ambacho timu yake imefanya katika wiki sita au saba zilizopita, lakini ni somo kubwa kuhusu kile kinachohitajika ili kushinda katika michezo ya kiwango hicho.

Maresca ameanza vizuri Manchester City

Watu wengi walikuwa wanadhani Manchester City wangepitia kipindi kigumu cha cha kushuka kiwango chao baada ya kocha Pep Guardiola kuondoka baada ya miaka 10.

Mambo hayakuanza vizuri chini ya Enzo Maresca, ambaye alipoteza dhidi ya Arsenal katika mechi ya kufungua msimu ya Community Shield.

Lakini City wameshinda mechi zote tano za Ligi Kuu hadi sasa, pamoja na kushinda mechi saba mfululizo katika mashindano yote.

Ushindi wao wa 5-3 dhidi ya Sunderland Jumapili uliwafanya kuongoza ligi na kuwa na alama tatu mbele ya Arsenal.

Maresca alisema kabla ya mchezo huo alitarajia mechi kuwa ngumu, na kwamba licha ya kufungwa mabao mawili au matatu, timu yake imejifunza mengi katika kipindi cha wiki nane.

Brighton na Brentford zinaendelea kuvutia na kushangaza

Brighton na Brentford, klabu mbili ambazo hazijawahi kushinda kombe kubwa, zimeendelea kufanya vizuri msimu huu.

Brighton walifurahia ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Arsenal na sasa wako nafasi ya tatu kwenye msimamo, alama mbili tu nyuma ya Arsenal.

Brighton pia wameifunga Arsenal nyumbani katika kila msimu katika misimu mitatu iliyopita.

Mchezaji wao nyota Pascal Gross alicheka na kusema "hapana" BBC ilipomuuliza kama Brighton wako kwenye mbio za ubingwa. Lakini katika soka, mambo yasiyotarajiwa yanaweza kutokea.

Brentford wako alama moja tu nyuma ya Brighton katika nafasi ya nne.

Wengi walitabiri Brentford wangepata wakati mgumu baada ya Thomas Frank kuondoka msimu uliopita, lakini kwa sasa wanaonekana kuimarika chini ya Keith Andrews, ambaye awali alikuwa kocha wa mipira ya adhabu.

Brentford hawajafungwa katika mechi tano na ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Chelsea ulikuwa matokeo yao bora zaidi kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa kuanza.

Leeds, ambao wanaendelea kufanya vizuri chini ya Daniel Farke, pia wana alama tisa na wako katika nafasi inayoweza kuwapeleka Ligi ya Mabingwa.

Liverpool na Everton wako nyuma yao kwa tofauti ya mabao.

4. Carrick kakalia kuti kavu?

Miaka saba iliyopita Manchester United walifanya jambo linalofanana na walilofanya sasa, kumteua nyota wa zamani wa klabu ambaye alikuwa amefanya vizuri alipokuwa kocha wa muda, licha ya uzoefu mdogo wa ukocha wa kiwango cha juu.

Mwaka 2019 alikuwa Ole Gunnar Solskjaer, na safari hii ni Michael Carrick.

Lakini msimu huu, baada ya Carrick kupata muda wote wa maandalizi ya msimu wa kuifanyia kazi timu yake, Manchester United wameshinda mchezo mmoja tu wa ligi.

Alama zao tano baada ya mechi tano ni alama ndogo zaidi kuzipata katika hatua kama hii ya msimu wa Ligi Kuu.

Wanaingia kwenye mapumziko ya mechi za kimataifa baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Fulham, huku wakihitaji bao la kusawazisha la Matheus Cunha katika dakika za za mwisho ya mchezo ili kuizuia Fulham kupata ushindi wao wa kwanza wa msimu.

Baada ya Fulham kupata bao la kujifunga la Lisandro Martinez, nahodha wa zamani wa United, Gary Neville, alisema kupitia Sky Sports kwamba katika miaka yake yote ya kuishuhudia Manchester United, hizo zilikuwa dakika 15 mbaya zaidi alizowahi kuziona.

Manchester United watakuwa na karibu wiki tatu za kutafakari hali hiyo kabla ya kuikaribisha Tottenham Oktoba 10.

5. Timu zilizopanda daraja si za kubezwa

Mwaka 2024 na 2025, timu zote tatu zilizopanda daraja kuja Ligi Kuu kutoka Championship zilishuka tena moja kwa moja kurudi zilikotoka, nyingi zikiwa na alama chache sana.

Lakini mwenendo huo uliishia msimu uliopita, wakati Sunderland ilimaliza nafasi ya saba na kufuzu kucheza Ulaya, huku Leeds ikimaliza nafasi ya 14. Ni Burnley pekee iliyoshuka daraja.

Wiki za mwanzo za msimu huu zinaonyesha huenda tukashuhudia hali kama hiyo tena.

Hull City wako nafasi ya nane baada ya mechi tano, huku kipigo cha 2-1 dhidi ya Newcastle kikiwa ndiyo mara yao ya kwanza kufungwa.

Ipswich wako nafasi ya 11.

Coventry, baada ya kufungwa mechi zao nne za mwanzo bila kufunga bao, waliifunga Nottingham Forest 1-0 na sasa wako kwenye eneo la kushuka daraja kwa tofauti ya mabao pekee.

Spurs bado hali tete

Tottenham walimaliza nafasi ya 17 katika misimu miwili iliyopita, ikiwa ni nafasi zao za chini zaidi tangu walipokuwa kwenye daraja la pili msimu wa 1977-78.

Lakini matarajio yaliongezeka baada ya klabu hiyo kutumia fedha nyingi katika usajili wa majira ya kiangazi.

Spurs walitumia pauni milioni 302 kununua wachezaqi wapya na kusajili wa wachezaji wengine wawili kwa mkopo.

Safu ya ulinzi na kiungo ilifanyiwa mabadiliko makubwa, huku pia wakiongeza mawinga wapya.

Lakini sasa wana mshambuliaji mmoja tu mwenye uzoefu wa Ligi Kuu, Dominic Solanke, ambaye amefunga mabao 12 tu katika Ligi Kuu katika zaidi ya miaka miwili tangu ajiunge na klabu hiyo.

Mchambuzi wa TNT na aliyekuwa mchezaji wa England, Joe Cole, alisema Tottenham wamelipa fedha nyingi zaidi kwa kila mchezaji waliyemsajili msimu huu lakini hali bado tete.

Kipigo cha 3-2 dhidi ya Aston Villa Jumamosi kiliwaacha Spurs wakisalia katika nafasi ya 19 kabla ya mapumziko, licha ya kufunga mabao yao mawili ya kwanza ya msimu kwenye ligi.

Kocha Roberto de Zerbi alisema timu yake inapaswa kuonyesha kitu zaidi ya kile wanachoonyesha kwa sasa.

7. Chelsea ni waburudishaji

Watu wengi walikuwa na hamu ya kuona Xabi Alonso angefanya nini katika msimu wake wa kwanza akiwa Chelsea.

Kocha huyo wa Hispania aliwahi kuiongoza Bayer Leverkusen kushinda mataji mawili makubwa bila kufungwa msimu wa 2023-24.

Chelsea pia walifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chao msimu huu.

Walimsajili kiungo mshambuliaji Morgan Rogers kwa pauni milioni 117 na pia kipa Emiliano Martinez kutoka Aston Villa.

Katika mechi zao tano za ligi, Chelsea wamehusika katika mabao 22, huku wakiwa wameruhusu mabao mengi zaidi (12) kuliko waliyofunga wao (10) na wako nafasi ya 10.

Na hiyo haijumuishi hata ushindi wao wa 6-3 dhidi ya Leeds katika Carabao Cup.

Kwa mashabiki wasiohusika na timu hiyo, mechi za Chelsea zimekuwa burudani kubwa. Lakini huenda hali hiyo isiwe hivyo kwa mashabiki wa Chelsea au uongozi wa klabu.