Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Israel na Lebanon zakubaliana kusitisha mapigano

Hii inafuatia mashambulizi ya Israel kuua watu wasiopungua tisa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano na Hezbollah kufyatua makombora kaskazini mwa Israeli

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Kufuatilia waathiriwa wa Ebola ni changamoto, juhudi zinaendelea kuimarika - WHO

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza Jumatano kwamba juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zinaendelea kuimarika, huku visa 344 vikithibitishwa na vifo 60 kuripotiwa.

    Hata hivyo, changamoto zinaendelea, hasa katika kuongeza uwezo wa kupima na kufuatilia waathiriwa.

    Mlipuko huo unaosababishwa na ugonjwa wa Bundibugyo, umeenea pia katika nchi jirani ya Uganda, ambapo maambukizi 15 yamethibitishwa, ikiwa ni pamoja na kifo kimoja.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisisitiza kwamba wakati hatua inapigwa, mengi zaidi yanahitajika kufanywa, huku asilimia 45 tu ya mawasiliano ya wale waliokutana na waathiriwa ndiyo yanayofuatiliwa kwa sasa.

    Wakati huo huo, Dkt. Tedros Ghebreyesus, ameonya dhidi ya kuwekwa kwa vikwazo vya jumla vya usafiri na baadhi ya nchi kutokana na mlipuko wa unaoendelea wa virusi vya Ebola.

    Marufuku ya kusafiri yaliyowekwa na zaidi ya nchi kumi na mbili yanaathiri uwezo wa Shirika la Afya Ulimwenguni kukabiliana vilivyo na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    Marufuku hiyo ya kusafiri "inatatiza usambazaji na kuzuia mwitikio wa kukabiliana na Ebola," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliambia mkutano wa waandishi wa habari.

    Wito wa Dkt. Tedros unakuja baada ya Idara ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia ya Canada kurejelea tena uamuzi wake wa kusitisha utoaji wa stakabadhi za uhamiaji kwa wakazi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Uganda na Sudan Kusini kwa muda wa siku 90.

    Marekani, Bahrain, Mexico na nchi zingine zimeweka vizuizi vya kusafiri, wakati Canada inatekeleza karantini ya siku 21 kwa wasafiri wote wanaofika kutoka Congo.

    Kando na hayo, WHO imesema inahitaji angalau dola milioni 115 katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ili kukabiliana na dharura hiyo ya kiafya.

    Shirika hilo limeeleza kuwa hadi sasa limefanikiwa kupata takribani asilimia 35 ya fedha zinazohitajika.

    Soma zaidi:

  2. Kura ya Bunge la Ulaya ni utaratibu wa kawaida – Serikali ya Tanzania

    Serikali ya Tanzania imesema kuwa hatua ya kamati mbili za Bunge la Ulaya kupitisha mapendekezo kuhusu mpango wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) ni sehemu ya taratibu za kawaida za kibunge na si uamuzi wa mwisho.

    Katika taarifa yake kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania imesisitiza kuwa uamuzi uliofikiwa Juni 3, 2026 katika ngazi ya kamati hauwezi kutafsiriwa kama msimamo wa mwisho wa EU kuhusu uhusiano wake na nchi hiyo.

    Katika mfumo wa Umoja wa Ulaya, mamlaka ya kiutendaji yapo chini ya Tume ya Ulaya (European Commission), ambayo ndiyo inayosimamia utekelezaji wa sera na uhusiano wa kikanda, lakini yanaweza kuwa na athari katika maamuzi ya mwisho ya maazimio ya Bunge.

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, mapendekezo yaliyopitishwa bado yanapaswa kuwasilishwa na kujadiliwa katika kikao cha Bunge zima la Ulaya lenye zaidi ya wabunge 700, kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa mwisho.

    Tarehe 3 Juni, Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Maendeleo za Bunge la Ulaya zilifanya kura kuhusu mapendekezo yanayohusiana na Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo wa mwaka 2025 kati ya EU na Tanzania. Katika kura hiyo ya ngazi ya kamati, mapendekezo yalipitishwa kwa kura 81 za kuunga mkono, kura 1 ya kupinga na kura 4 za kutokujizuia.

    Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa uhusiano wake na EU bado uko imara na kwamba hatua hiyo ni sehemu ya michakato ya kawaida ya ndani ya Bunge la Ulaya.

    Hata hivyo, moja ya mapendekezo yaliyotolewa yanaweza kuathiri Tanzania endapo yatapitishwa na Bunge zima na baadaye kutekelezwa, ikiwemo uwezekano wa kusitishwa kwa msaada wa euro milioni 156.

    Baadhi ya hoja zilizotajwa katika mjadala kuelekea upigaji huo wa kura zinahusiana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na mwenendo wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

    Hata hivyo, Tanzania imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa uchaguzi wake ulikuwa huru na wa haki, na kwamba masuala ya ndani yanapaswa kushughulikiwa kupitia mifumo ya ndani bila kuingiliwa.

  3. Serikali haitashauriana na Wakenya juu ya kituo cha Ebola cha Marekani Kenya – Waziri wa Afya

    Waziri wa Afya wa Kenya Aden Duale amesema kwenye kikao cha Bunge kuwa Serikali haitashauriana na Wakenya juu ya mpango wa kujenga kituo cha Karantini cha wagonjwa wa Ebola wa Marekani.

    Ugonjwa huu hauhitaji mashauriano kabla ya Wakenya kuambukizwa. Sisi kama serikali tuna wajibu wa kimaadili kuwalinda Wakenya na watu wengine ambao si Wakenya wanaoishi ndani ya mipaka yetu au wanaosafiri ndani ya nchi yetu, amesema Duale.

    Waziri Duale alikuwa ameitwa na Bunge kuelezea utayari wa Kenya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao umelipuka katika nchi ya Kidemokrasi ya Congo.

    Akielezea jinsi ambavyo hali ya ugonjwa huu sio ya kawaida, alisema Sheria ya Afya ya Umma inaipa Wizara ya Afya Kenya jukumu la kuhakikisha usalama kwa umma

    Akizungumzia kituo cha Ebola kilichopendekezwa kujengwa huko kambi ya kijeshi ya Laikipia kwa ushirikiano na Marekani, Duale alisema kitahudumia raia wote ikiwa ni pamoja na Wakenya na ni miongoni mwa vituo vingine 23 vya Ebola ambavyo tayari vimejengwa au vinapangwa kujengwa kote nchini.

    Soma zaidi:

  4. Polisi Zimbabwe waonya kuwa kuchochea vurugu hakutavumiliwa

    Polisi nchini Zimbabwe wamewaonya wananchi dhidi ya kuchochea ghasia na vitisho kwenye mitandao ya kijamii huku mswada wa kuongeza muda wa Rais Emmerson Mnangagwa ukisomwa kwa mara ya pili bungeni, Jumanne.

    Polisi waliweka kizuizi njiani kuelekea bungeni mswada huo ukisomwa kwa mara ya pili katika Bunge la Kitaifa.

    Sheria inayopendekezwa itaongeza mihula ya urais na wabunge kwa miaka miwili na kufutwa kwa kura ya moja kwa moja ya urais kupigwa na umma.

    Waziri wa sheria alitetea mswada huo unaolenga kuongeza muhula wa urais na kufuta kura ya moja kwa moja ya urais akisema italeta utulivu wa kisiasa.

    Wakosoaji wanasema mapendekezo hayo ni kinyume cha sheria na yanadhoofisha demokrasia.

    Kundi la wapiganaji wa zamani wa vita vya ukombozi, mashirika ya kiraia na wananchi wamewasilisha changamoto za kisheria kuzuia mswada huo.

    Hata hivyo inatarajiwa kupitia Mabunge yote mawili ambapo chama tawala cha Zanu PF kinashikilia zaidi ya thuluthi mbili ya wabunge.

    Soma zaidi:

  5. Mapigano yanaendelea mjini Mogadishu kati ya upinzani na vikosi vya serikali

    Mapigano yaliyozuka Jumatano alasiri kati ya vikosi vilivyoungana na upinzani na wanajeshi wa serikali yaliendelea hadi Jumamosi asubuhi katika mji mkuu wa Somalia.

    Milio ya risasi iliripotiwa katika vitongoji kadhaa huku mapigano yakiendelea, kulingana na wenyeji.

    Rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed, akizungumza wakati wa machafuko hayo, alisema: "Ikiwa rais na wanajeshi wake wanafikiri kwamba tunaogopa au tutatoroka, hatutakimbia."

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, alisema ghasia hizo hazitasitisha maandamano yaliyopangwa katika mji mkuu.

    "Shambulio hili halitasitisha maandamano ya wakaazi wa mji mkuu wanaopinga dhuluma, kulazimishwa kuhama makazi yao, na matumizi mabaya ya mamlaka ya serikali."

    Jeshi la Polisi la Somalia pia limelaani shambulizi katika kituo cha ukaguzi wilaya ya Hawlwadaag, likiwalaumu watu waliotumia silaha.

    "Jeshi la Polisi la Somalia linalaani na kujutia sana shambulio lililofanywa leo na wanamgambo wenye silaha waliovalia barakoa kwenye kizuizi cha polisi katika wilaya ya Hawlwadaag. Wanamgambo hao pia walitumia silaha nzito wakati wa shambulio hilo."

    Kikosi hicho kiliongeza kuwa waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria.

    Machafuko hayo yanatokea huku kukiwa na mvutano mkubwa wa kisiasa na mkwamo wa juhudi za upatanishi zinazohusisha viongozi wa upinzani, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Hassan Ali Khaire na Rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed, pamoja na Rais Hassan Sheikh Mohamud.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Marco Rubio aonya juu ya 'hatari' ya kuongezeka kwa vita vya Ukraine

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuna hatari kubwa ya kuongezeka kwa mvutano katika vita kati ya Urusa na Ukraine.

    Bwana Rubio alieleza kamati ya Bunge kwamba hatari zimeongezeka kutokana na Ukraine kuwa na uwezo zaidi wa kufanya mashambulizi ndani kabisa ya eneo la Urusi.

    Amesisitiza kuwa Marekani iko tayari kuchukua jukumu lolote ili kusaidia kufanikisha amani, ikiamini kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huo, lakini akasema kuwa pande zote mbili bado haziko tayari kufanya makubaliano ya kuachana na vita.

    Aidha, Bwana Rubio ameongeza kuwa Marekani si mpatanishi huru katika mzozo huo, kwa kuwa inaendelea kuiuzia Ukraine silaha na pia kudumisha vikwazo dhidi ya Urusi.

    Soma zaidi:

  7. Wabunge wamgeuka Trump, wapitisha azimio la kuzuia vita dhidi ya Iran

    Bunge la Wawakilishi la Marekani limepitisha azimio la kumzuia Rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran

    Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 215 dhidi ya 208, baada ya wabunge wanne wa Chama anachotoka Trump cha Republican kuungana na wale wa Democrats katika hatua ya nadra ya kupinga hadharani vita hivyo, kati ya Marekani na Iran vilivyoanza mwezi Februari.

    Hata hivyo, azimio hilo bado linahitaji kupitishwa na Bunge la Senate, linalodhibitiwa na Republican. Hata likipitishwa huko, Trump anaweza kutumia mamlaka yake ya kura ya veto kuzuia azimio hilo kuwa sheria, jambo ambalo linahitaji theluthi mbili ya kura katika mabunge yote mawili ili kubatilishwa.

    Wabunge wa Republican Thomas Massie, Brian Fitzpatrick, Tom Barrett na Warren Davidson waliungana na Democrats kuunga mkono azimio hilo. Barrett alisema ni jukumu la Bunge pekee kutangaza vita na kwamba alipiga kura kulingana na dhamiri yake, bila kujali shinikizo lolote la kisiasa.

    Mbunge Gregory Meeks wa Democrats alieleza kura hiyo kama pigo kubwa kwa Trump, akisema vita dhidi ya Iran vimekuwa vya gharama kubwa, havijafanikisha malengo yake yaliyotangazwa na vimeongeza ugumu wa kupata suluhisho la kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Pia alisema Republican wengi wanaanza kusikiliza wapiga kura wao ambao hawataki vita vingine vya muda mrefu Mashariki ya Kati.

    Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana katika siku za karibuni.

    Akizungumza kutoka Ikulu ya White House, Trump alisema mazungumzo ya kumaliza vita yanaendelea vizuri na yanaweza kukamilika mwishoni mwa wiki hii, akiongeza kuwa pande zote ziko karibu kufikia makubaliano ya kumaliza mzozo huo.

  8. Tetesi za soka: Fernandes kusalia United? Jesus wa Arsenal kutua Everton

    Manchester United wameahirisha mazungumzo ya kuongeza mkataba wa nahodha wao na kiungo wa Ureno, Bruno Fernandes, mwenye miaka 31, baada ya kuhakikishiwa kuwa anataka kubaki Old Trafford kwa muda mrefu. (Mirror)

    Real Madrid wanatarajiwa kutoa pauni milioni 17.3 ili kumsajili beki wa kulia wa Inter Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Denzel Dumfries, mwenye miaka 30. (Sky Sports)

    Everton wanamuwania mshambuliaji wa Brazil wa Arsenal, Gabriel Jesus, mwenye umri miaka 29, lakini wanataka mabingwa hao wa Ligi kuu kupunguza bei yao ya pauni milioni 20. (Football Insider)

    Paris Saint-Germain wanataka euro milioni 30 (pauni milioni 25.9) kutoka Juventus kwa ajili ya mshambuliaji wa Ufaransa mwenye miaka 27, Randal Kolo Muani. (La Gazzetta dello Sport)

    Atletico Madrid wanaweza kutumia fedha watakazopata kutokana na mauzo ya mshambuliaji wa Argentina, Julian Alvarez, mwenye miaka 26, kumsajili mshambuliaji wa Marseille na England, Mason Greenwood, mwenye miaka 24. (Fichajes)

    Roma pia wanamfuatilia Mason Greenwood, huku klabu yake ya zamani Manchester United ikitarajiwa kunufaika kupitia kipengele cha asilimia ya mauzo ya baadaye kilichowekwa wakati wa uhamisho wake kwenda Ufaransa. (Teamtalk)

    AC Milan wanamtaka Crysencio Summerville, mwenye umri wa miaka 24, kutoka West Ham United. Winga huyo wa Uholanzi pia anafuatiliwa na Tottenham Hotspur na Aston Villa. (Teamtalk)

  9. Israel na Lebanon zakubaliana kusitisha mapigano Hezbollah ikisitisha mashambulizi

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza katika taarifa kwamba Israel na Lebanon zimekubaliana kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Makubaliano hayo "yanatokana na kukomeshwa kabisa" kwa mashambulizi kutoka kwa kundi lenye silaha la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, miongoni mwa masharti mengine.

    Hii inafuatia mashambulizi ya Israel kuua watu wasiopungua tisa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano na Hezbollah kufyatua makombora kaskazini mwa Israeli, ikiwa majaribu makubwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa hapo awali mwezi Aprili.

    "Nchi zote zilithibitisha tena kwamba mustakabali wa uhusiano kati ya Israeli na Lebanon lazima uamuliwe na serikali mbili huru. Zilikataa jaribio lolote, la serikali yoyote au mhusika yeyote asiye wa serikali, kushikilia siku zijazo za Lebanon," ilisema taarifa hiyo.

    Makubaliano hayo pia yanategemea "kuwahamisha wanajeshi wote wa [Hezbollah]" kutoka eneo ambalo Israeli inadhibiti kusini mwa Lebanon kutoka mto Litani hadi mpakani.

    Nchi hizo mbili zitakutana tena tarehe 22 Juni kufanya mazungumzo zaidi "kwa lengo la kufikia makubaliano kamili". Hezbollah bado haijatoa maoni hadharani kuhusu tangazo hilo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliwaambia waandishi wa habari kabla ya tangazo hilo kwamba alitumai watatoa "mpango wa utekelezaji katika njia ya usalama huko [Lebanon], bila kutegemea Hezbollah".

    Soma zaidi:

  10. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 04/06/2026.