Moja kwa moja, Israel na Lebanon zakubaliana kusitisha mapigano

Hii inafuatia mashambulizi ya Israel kuua watu wasiopungua tisa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano na Hezbollah kufyatua makombora kaskazini mwa Israeli

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. WHO yaonya marufuku ya kusafiri inaathiri uwezo wa kukabiliana na Ebola

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Ghebreyesus, ameonya dhidi ya kuwekwa kwa vikwazo vya jumla vya usafiri na baadhi ya nchi kutokana na mlipuko wa unaoendelea wa virusi vya Ebola.

    Marufuku ya kusafiri yaliyowekwa na zaidi ya nchi kumi na mbili yanaathiri uwezo wa Shirika la Afya Ulimwenguni kukabiliana vilivyo na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    Marufuku hiyo ya kusafiri "inatatiza usambazaji na kuzuia mwitikio wa kukabiliana na Ebola," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliambia mkutano wa waandishi wa habari.

    Wito wa Dkt. Tedros unakuja baada ya Idara ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia ya Canada kurejelea tena uamuzi wake wa kusitisha utoaji wa stakabadhi za uhamiaji kwa wakazi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Uganda na Sudan Kusini kwa muda wa siku 90.

    Marekani, Bahrain, Mexico na nchi zingine zimeweka vizuizi vya kusafiri, wakati Canada inatekeleza karantini ya siku 21 kwa wasafiri wote wanaofika kutoka Congo.

    Kando na hayo, WHO imesema inahitaji angalau dola milioni 115 katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ili kukabiliana na dharura hiyo ya kiafya.

    Shirika hilo limeeleza kuwa hadi sasa limefanikiwa kupata takribani asilimia 35 ya fedha zinazohitajika.

    Soma zaidi:

  2. Marco Rubio aonya juu ya 'hatari' ya kuongezeka kwa vita vya Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuna hatari kubwa ya kuongezeka kwa mvutano katika vita kati ya Urusa na Ukraine.

    Bwana Rubio alieleza kamati ya Bunge kwamba hatari zimeongezeka kutokana na Ukraine kuwa na uwezo zaidi wa kufanya mashambulizi ndani kabisa ya eneo la Urusi.

    Amesisitiza kuwa Marekani iko tayari kuchukua jukumu lolote ili kusaidia kufanikisha amani, ikiamini kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huo, lakini akasema kuwa pande zote mbili bado haziko tayari kufanya makubaliano ya kuachana na vita.

    Aidha, Bwana Rubio ameongeza kuwa Marekani si mpatanishi huru katika mzozo huo, kwa kuwa inaendelea kuiuzia Ukraine silaha na pia kudumisha vikwazo dhidi ya Urusi.

    Soma zaidi:

  3. Wabunge wamgeuka Trump, wapitisha azimio la kuzuia vita dhidi ya Iran

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bunge la Wawakilishi la Marekani limepitisha azimio la kumzuia Rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran

    Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 215 dhidi ya 208, baada ya wabunge wanne wa Chama anachotoka Trump cha Republican kuungana na wale wa Democrats katika hatua ya nadra ya kupinga hadharani vita hivyo, kati ya Marekani na Iran vilivyoanza mwezi Februari.

    Hata hivyo, azimio hilo bado linahitaji kupitishwa na Bunge la Senate, linalodhibitiwa na Republican. Hata likipitishwa huko, Trump anaweza kutumia mamlaka yake ya kura ya veto kuzuia azimio hilo kuwa sheria, jambo ambalo linahitaji theluthi mbili ya kura katika mabunge yote mawili ili kubatilishwa.

    Wabunge wa Republican Thomas Massie, Brian Fitzpatrick, Tom Barrett na Warren Davidson waliungana na Democrats kuunga mkono azimio hilo. Barrett alisema ni jukumu la Bunge pekee kutangaza vita na kwamba alipiga kura kulingana na dhamiri yake, bila kujali shinikizo lolote la kisiasa.

    Mbunge Gregory Meeks wa Democrats alieleza kura hiyo kama pigo kubwa kwa Trump, akisema vita dhidi ya Iran vimekuwa vya gharama kubwa, havijafanikisha malengo yake yaliyotangazwa na vimeongeza ugumu wa kupata suluhisho la kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Pia alisema Republican wengi wanaanza kusikiliza wapiga kura wao ambao hawataki vita vingine vya muda mrefu Mashariki ya Kati.

    Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana katika siku za karibuni.

    Akizungumza kutoka Ikulu ya White House, Trump alisema mazungumzo ya kumaliza vita yanaendelea vizuri na yanaweza kukamilika mwishoni mwa wiki hii, akiongeza kuwa pande zote ziko karibu kufikia makubaliano ya kumaliza mzozo huo.

  4. Tetesi za soka: Fernandes kusalia United? Jesus wa Arsenal kutua Everton

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Manchester United wameahirisha mazungumzo ya kuongeza mkataba wa nahodha wao na kiungo wa Ureno, Bruno Fernandes, mwenye miaka 31, baada ya kuhakikishiwa kuwa anataka kubaki Old Trafford kwa muda mrefu. (Mirror)

    Real Madrid wanatarajiwa kutoa pauni milioni 17.3 ili kumsajili beki wa kulia wa Inter Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Denzel Dumfries, mwenye miaka 30. (Sky Sports)

    Everton wanamuwania mshambuliaji wa Brazil wa Arsenal, Gabriel Jesus, mwenye umri miaka 29, lakini wanataka mabingwa hao wa Ligi kuu kupunguza bei yao ya pauni milioni 20. (Football Insider)

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Paris Saint-Germain wanataka euro milioni 30 (pauni milioni 25.9) kutoka Juventus kwa ajili ya mshambuliaji wa Ufaransa mwenye miaka 27, Randal Kolo Muani. (La Gazzetta dello Sport)

    Atletico Madrid wanaweza kutumia fedha watakazopata kutokana na mauzo ya mshambuliaji wa Argentina, Julian Alvarez, mwenye miaka 26, kumsajili mshambuliaji wa Marseille na England, Mason Greenwood, mwenye miaka 24. (Fichajes)

    Roma pia wanamfuatilia Mason Greenwood, huku klabu yake ya zamani Manchester United ikitarajiwa kunufaika kupitia kipengele cha asilimia ya mauzo ya baadaye kilichowekwa wakati wa uhamisho wake kwenda Ufaransa. (Teamtalk)

    AC Milan wanamtaka Crysencio Summerville, mwenye umri wa miaka 24, kutoka West Ham United. Winga huyo wa Uholanzi pia anafuatiliwa na Tottenham Hotspur na Aston Villa. (Teamtalk)

  5. Israel na Lebanon zakubaliana kusitisha mapigano Hezbollah ikisitisha mashambulizi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza katika taarifa kwamba Israel na Lebanon zimekubaliana kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Makubaliano hayo "yanatokana na kukomeshwa kabisa" kwa mashambulizi kutoka kwa kundi lenye silaha la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, miongoni mwa masharti mengine.

    Hii inafuatia mashambulizi ya Israel kuua watu wasiopungua tisa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano na Hezbollah kufyatua makombora kaskazini mwa Israeli, ikiwa majaribu makubwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa hapo awali mwezi Aprili.

    "Nchi zote zilithibitisha tena kwamba mustakabali wa uhusiano kati ya Israeli na Lebanon lazima uamuliwe na serikali mbili huru. Zilikataa jaribio lolote, la serikali yoyote au mhusika yeyote asiye wa serikali, kushikilia siku zijazo za Lebanon," ilisema taarifa hiyo.

    Makubaliano hayo pia yanategemea "kuwahamisha wanajeshi wote wa [Hezbollah]" kutoka eneo ambalo Israeli inadhibiti kusini mwa Lebanon kutoka mto Litani hadi mpakani.

    Nchi hizo mbili zitakutana tena tarehe 22 Juni kufanya mazungumzo zaidi "kwa lengo la kufikia makubaliano kamili". Hezbollah bado haijatoa maoni hadharani kuhusu tangazo hilo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliwaambia waandishi wa habari kabla ya tangazo hilo kwamba alitumai watatoa "mpango wa utekelezaji katika njia ya usalama huko [Lebanon], bila kutegemea Hezbollah".

    Soma zaidi:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 04/06/2026.