Kenya yathibitisha mgonjwa wa pili wa Ebola
Mgonjwa huyo mwenye miaka 39 ni jamaa wa karibu wa kisa cha kwanza cha Ebola nchini, alisema Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt. Patrick Amoth.
Muhtasari
- Kenya yapandisha bei za mafuta
- Kenya yathibitisha mgonjwa wa pili wa Ebola
- Chad na Ufaransa zatia saini azimio la ushirikiano wa ulinzi
- Urusi yamkamata mwandishi wa habari wa Japan kwa tuhuma za ujasusi
- Meli yazama lango la Hormuz baada ya kugonga bomu la majini - ripoti
- Saudi Arabia yabatilisha hukumu ya kifo dhidi ya raia wa Sri Lanka
- Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kubwa wiki moja kabla ya uchaguzi wa Israel
- Kiongozi wa genge aliyepanga mauaji ya rapa Tupac Shakur ahukumiwa kifungo cha miaka 40 jela
- Mashambulizi ya Urusi yamepiga kiwanda muhimu cha umeme huko Kyiv, Zelensky asema
- Makombora yazuiliwa karibu na Riyadh baada ya Saudi Arabia kushambulia ghala la mafuta la Yemen
- Roboti yakamatwa na polisi wa Ujerumani baada ya kudaiwa kumpapasa msichana mdogoTrump:
- Huenda tumezidi kuwaua viongozi wa Iran
- Papa agunduliwa na saratani ya mapafu lakini upasuaji umefanikiwa, Vatican yasema
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi & Ambia Hirsi
Kenya yapandisha bei za mafuta

Chanzo cha picha, AFP
Wakenya wanatarajiwa kukabiliana na ongezeko la gharama za mafuta baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) kutangaza nyongeza ya bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Katika marekebisho mapya ya bei yatakayotumika kuanzia Oktoba hadi Novemba, bei ya petroli imeongezeka kwa shilingi 12.93 kwa lita, dizeli kwa shilingi 9.90 kwa lita, huku mafuta ya taa yakiongezeka kwa shilingi 28.49 kwa lita.
EPRA imesema ongezeko hilo limetokana na kupanda kwa gharama za uagizaji mafuta kutoka nje, jambo ambalo limeongeza gharama za bidhaa za petroli zinazoingia nchini.
Hatua hiyo inatarajiwa kuwaathiri madereva, waendeshaji wa magari ya usafiri wa umma na biashara zinazotegemea mafuta katika shughuli zao za kila siku.
Ongezeko la bei ya dizeli linaweza kuwa na athari kubwa zaidi katika uchumi, kwani mafuta hayo hutumiwa na malori, mabasi na magari mengine ya biashara. Hali hiyo inaweza kuongeza gharama za usafirishaji na usambazaji wa bidhaa, na hivyo kuchangia kupanda kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali.
Vita vya Maneno DRC: Kamerhe amshutumu Kabila kwa 'kuunga mkono uasi'

Chanzo cha picha, Bunge la Congo
Maelezo ya picha, Picha ya maktaba ya Spika wa zamani wa Bunge la DR- Congo Vital Kamerhe Mshirika wa karibu wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Félix Tshisekedi, amemkosoa vikali rais wa zamani Joseph Kabila baada ya kutangazwa kuwa kiongozi wa muungano mpya wa kisiasa na kijeshi, akisema hatua hiyo inapingana na msimamo wake wa kutaka amani nchini.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X mapema Jumatano, Vital Kamerhe, ambaye ni mshirika mkuu wa Tshisekedi na aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, alisema haiwezekani kudai kutetea amani huku ukiunga mkono au kuongoza vuguvugu lenye mkondo wa kijeshi.
Kamerhe pia alimtaka Kabila kuwajibika kwa urithi wa utawala wake wa miaka 18, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kupewa tathmini kwa misingi ya matokeo ya uongozi wao.
Akiweka wazi kumuunga mkono Rais Tshisekedi, Kamerhe alitoa wito wa umoja wa kitaifa, mazungumzo na kukataliwa kwa uasi kama njia ya kufikia madaraka. Alisema amani, mshikamano wa kitaifa na kulindwa kwa mamlaka ya nchi vinapaswa kutangulizwa mbele ya maslahi ya kisiasa.
Kauli hiyo imekuja siku mbili baada ya Kabila kutangazwa kuwa kiongozi wa Front for the Refoundation of the Nation (FRN), muungano mpya uliozinduliwa mjini Goma, mashariki mwa DRC. Muungano huo umetangaza dhamira ya kuiondoa serikali ya sasa kwa kutumia mbinu zote zinazowezekana, ikiwemo nguvu za kijeshi.
Hatua hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa Kabila kuhusishwa waziwazi na vuguvugu lenye silaha linaloshirikiana na waasi wa M23.
Jumanne, Rais wa Seneti, Jean-Michel Sama Lukonde, naye alimshutumu Kabila kwa kuongoza kile alichokiita vuguvugu la kisiasa na kijeshi. Alisema hatua hiyo inaonekana kuthibitisha madai ya muda mrefu ya Rais Tshisekedi kwamba mtangulizi wake ana uhusiano na makundi ya waasi yanayofanya shughuli zao mashariki mwa nchi.
Sama Lukonde alisema wakati Tshisekedi akiendelea na juhudi za kurejesha amani ya kudumu, Kabila amejiweka katika nafasi inayopingana na matarajio ya wananchi wa Kongo.
Wakati huo huo, Baraza la Kitaifa la Ufuatiliaji wa Makubaliano na Mchakato wa Uchaguzi (CNSA) limetoa wito wa mazungumzo ya kitaifa na kujizuia kutumia nguvu.
Katika taarifa yake ya Oktoba 13, baraza hilo lilisema DRC inakabiliwa na uchaguzi muhimu kati ya amani na vita, pamoja na umoja wa kitaifa na mgawanyiko. CNSA liliwataka wadau wote wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya taifa, kukataa vurugu na kushiriki mazungumzo ya pamoja ili kulinda utulivu, mamlaka na umoja wa nchi.
Mpaka sasa, serikali ya DRC na Ikulu ya Rais hawajatoa tamko rasmi kuhusu kutangazwa kwa Kabila kuwa kiongozi wa FRN. Kabila mwenyewe pia hajajibu hadharani ukosoaji uliotolewa na Kamerhe na Sama Lukonde.
Maelezo zaidi:
Kenya yathibitisha mgonjwa wa pili wa Ebola

Chanzo cha picha, EPA
Kenya imethibitisha kisa cha pili cha ugonjwa wa Ebola aina ya Bundibugyo, huku mamlaka za afya zikieleza kuwa mgonjwa huyo alikuwa tayari amewekwa karantini na kufuatiliwa kila siku kabla ya kuanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dkt. Patrick Amoth, alisema mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 39 ni mwanafamilia wa karibu wa mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa kuwa na Ebola nchini. Alianza kuonyesha dalili mnamo Oktoba 13 na mara moja akatengwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Vipimo vilivyofanywa katika Maabara ya Kitaifa ya Marejeleo ya Virusi na maabara ya KEMRI-CDC vilithibitisha kuwa ameambukizwa virusi vya Ebola.
Kufikia sasa, visa viwili vya Ebola vimethibitishwa nchini Kenya, na ugonjwa huo umesababisha kifo cha mtu mmoja.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kubainika kwa maambukizi hayo katika hatua za awali kunadhihirisha mafanikio ya hatua zilizowekwa za karantini na ufuatiliaji wa watu waliowahi kukaribiana na wagonjwa. Mgonjwa huyo anaendelea kupata huduma za matibabu chini ya uangalizi maalumu katika kituo cha afya kilichoteuliwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa Ebola.
Maafisa wa afya wameeleza kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha ugonjwa huo umeenea katika jamii, huku visa vyote viwili vikihusishwa na mlolongo mmoja wa maambukizi.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, watu 128 waliotambuliwa kuwa walikaribiana na mgonjwa wa kwanza wameorodheshwa kwa ajili ya ufuatiliaji, na 113 kati yao tayari wamepatikana. Kati ya hao, watu 108 wako karantini nchini Kenya na wanafanyiwa uchunguzi wa afya kila siku kwa kipindi cha siku 21.
Watu wengine watano wako nje ya Kenya, na mamlaka husika za afya katika nchi wanakoishi zimejulishwa kupitia mifumo ya kimataifa ya ufuatiliaji wa magonjwa.
Wakati huohuo, juhudi zinaendelea kuwatafuta watu waliobaki kwenye orodha ya waliohusiana na mgonjwa wa kwanza pamoja na kuwabaini wale ambao huenda walikutana na mgonjwa wa pili baada ya kuanza kuonyesha dalili.
Wizara ya Afya imewataka wananchi kubaki watulivu lakini waendelee kuwa waangalifu, ikisisitiza kwamba Ebola huambukizwa kupitia kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa, na si kupitia hewani.
Aidha, Kenya haijatangaza vikwazo vyovyote vya usafiri, biashara au mikusanyiko ya umma kufuatia visa hivyo vya Ebola.
Maelezo zaidi:
Chad na Ufaransa zatia saini azimio la ushirikiano wa ulinzi
Chad na Ufaransa zimetia saini azimio la nia la kuimarisha ushirikiano wao katika sekta ya ulinzi, karibu miaka miwili baada ya N'Djamena kusitisha makubaliano ya kijeshi yaliyokuwa yamekuwepo kwa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Hati hiyo ilisainiwa na mawaziri wanaosimamia majeshi wa mataifa hayo mawili katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Élysée, Jumanne. Hafla hiyo ilifanyika sambamba na ziara ya kikazi ya Rais wa Chad, Mahamat Déby, nchini Ufaransa, ambapo yeye na Rais Emmanuel Macron walishuhudia utiaji saini wa mpango huo wa pamoja.
Ingawa maelezo kamili ya azimio hilo hayajawekwa wazi, Ikulu ya Chad imesema litasaidia kuimarisha uwezo wa nchi hiyo katika viwanda vya ulinzi. Kwa upande wake, Rais Macron alieleza hatua hiyo kuwa ni mwanzo wa sura mpya ya kurasimisha na kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi kati ya mataifa hayo mawili, katika mazingira ya uhusiano ulioboreshwa.
Macron alisema ushirikiano huo mpya unajengwa juu ya msingi wa kuheshimiana na maslahi ya pamoja.
Mnamo Novemba 2024, Chad ilisitisha makubaliano ya kihistoria ya ulinzi na Ufaransa, hatua iliyosababisha kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa kutoka nchini humo. Ingawa N'Djamena ilisisitiza kuwa uamuzi huo usingeathiri ushirikiano katika sekta nyingine, wachambuzi wengi waliutafsiri kama mabadiliko makubwa katika uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, azimio la sasa halihusiani na kurejeshwa kwa majeshi ya Ufaransa nchini Chad wala halifanyi kazi kama makubaliano mapya ya kijeshi. Badala yake, linaweka msingi wa kuendeleza ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama.
Tangu mwanzoni mwa mwaka 2026, Paris na N'Djamena zimekuwa zikichukua hatua za kurejesha na kuimarisha uhusiano wao, huku marais Macron na Déby wakikutana mara tatu ndani ya kipindi cha chini ya miezi kumi.
Chad ilikuwa ngome ya mwisho ya Ufaransa katika eneo la Sahel baada ya Mali, Niger na Burkina Faso, ambazo zilivunja au kupunguza kwa kiasi kikubwa uhusiano wao na washirika wa Magharibi kufuatia mapinduzi ya kijeshi.
Urusi yamkamata mwandishi wa habari wa Japan kwa tuhuma za ujasusi

Chanzo cha picha, TASS
Mamlaka za Urusi zimemkamata mwandishi wa habari wa Japan, Yuki Imai, kwa tuhuma za ujasusi, zikidai kuwa alikusanya taarifa zinazohusu uwezo wa ulinzi wa Moscow kwa niaba ya Tokyo.
Imai, ambaye anafanya kazi katika gazeti la Hokkaido Shimbun, alikamatwa katika eneo la Sakhalin, mashariki mwa Urusi, siku moja kabla ya ratiba yake ya kuondoka nchini humo. Baadaye alisafirishwa kwa ndege hadi Moscow, ambako mahakama iliamuru azuiliwe rumande akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake.
Serikali ya Japan imesema inatafuta maelezo zaidi kuhusu tukio hilo na haijaweza kuwasiliana na mwandishi huyo tangu alipokamatwa.
Kukamatwa kwake kunajiri wakati uhusiano kati ya Urusi na Japan ukiendelea kuzorota, hasa baada ya Rais Vladimir Putin kutembelea Visiwa vya Kuril vinavyogombaniwa na mataifa hayo mawili mwezi Agosti.
Kwa mujibu wa mamlaka za Urusi, Imai alidaiwa kufanya kazi kwa maelekezo ya idara ya ujasusi ya Japan na kukusanya taarifa kuhusu watu wanaohusika katika kile Moscow inachokiita "operesheni maalum ya kijeshi" katika Visiwa vya Kuril.
Visiwa vya Kuril viko kati ya kisiwa cha Hokkaido nchini Japan na Rasi ya Kamchatka nchini Urusi. Ingawa vinasimamiwa na Urusi, Japan inadai umiliki wa visiwa vinne vya kusini mwa eneo hilo, ambavyo inayataja kama "Maeneo ya Kaskazini".
Shirika la usalama la Urusi (FSB) lilichapisha video inayowaonyesha maafisa waliovalia barakoa wakimkamata mtu katika chumba cha hoteli kabla ya kumsafirisha hadi Moscow. Video hiyo baadaye ilimuonyesha akiwa ndani ya kizimba mahakamani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax, Imai ataendelea kuzuiliwa hadi Desemba 12 kabla ya kuanza kwa kesi yake. Serikali ya Japan haijatoa tamko la kina kuhusu tuhuma zinazomkabili mwandishi huyo.
Pia unaweza kusoma:
Meli yazama lango la Hormuz baada ya kugonga bomu la majini - ripoti

Chanzo cha picha, NurPhoto/Getty images
Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) linasema meli moja ya mizigo imezama kusini mwa Lango la Hormuz baada ya kugonga bomu la majini ilipokuwa ikipita katika njia ambayo haijaiidhinishwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha uhusiano wa umma cha jeshi hilo, meli hiyo ilikiuka taratibu za usafiri wa majini kwa kujaribu kutumia njia ambayo haijaidhinishwa na ambayo ilitajwa kuwa hatari kwa meli zinazopita katika eneo hilo.
IRGC ilisema mgongano huo ulisababisha moto mkubwa ulioteketeza sehemu kubwa ya meli hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba zaidi ya makontena 2,500 na ilizama mapema Jumatano kutokana na uharibifu mkubwa uliosababishwa na moto huo.
Hata hivyo, taasisi nyingine zinazofuatilia usalama wa usafiri wa majini katika Lango la Hormuz bado hazijatoa taarifa kuhusu tukio hilo wala kuthibitisha iwapo kuna wafanyakazi waliopoteza maisha au kujeruhiwa.
Maelezo zaidi:
Saudi Arabia yabatilisha hukumu ya kifo dhidi ya raia wa Sri Lanka

Chanzo cha picha, Human Rights Watch
Mahakama Kuu ya Saudi Arabia imebatilisha hukumu ya kifo iliyokuwa imetolewa dhidi ya mfanyakazi mhamiaji kutoka Sri Lanka, Anojan Sivarasa, baada ya kupatikana na hatia ya kukufuru kwa kumtusi Mtume Muhammad kupitia maoni aliyochapisha kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Arun Hemachandra, alitangaza uamuzi huo akisema mahakama hiyo ilifuta hukumu hiyo siku ya Jumatano. Aliishuku mamlaka na timu za kisheria za mataifa yote mawili kwa juhudi zao katika kushughulikia kesi hiyo.
Sivarasa, mwenye umri wa miaka 27, alihukumiwa kifo mwezi Septemba baada ya mahakama ya rufaa nchini Saudi Arabia kumtia hatiani kwa kosa hilo. Kesi hiyo ilizua mshtuko mkubwa nchini Sri Lanka na kusababisha juhudi za kidiplomasia za kuomba msamaha.
Chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na mjadala mkali uliozuka kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa Juni, baada ya kusambaa kwa video ikimuonyesha kijana mmoja Muislamu akimpiga teke mbwa aliyekuwa akiwafuata mahujaji wa Kihindu. Mjadala huo ulisababisha mabishano ya kidini mtandaoni.
Katika mabadilishano hayo ya ujumbe, mtumiaji mmoja alitoa kauli za kumdhalilisha mungu wa Kihindu, jambo lililomfanya Sivarasa kujibu kwa lugha ya Kitamil kwa maneno yaliyomkashifu Mtume Muhammad.
Ingawa baadaye alifuta maoni hayo na kuchapisha video ya kuomba radhi, picha ya skrini ya ujumbe huo ilifikishwa kwa mwajiri wake na maafisa wa Saudi Arabia, hatua iliyosababisha kukamatwa kwake mwezi Julai.
Haijabainika ikiwa atachukuliwa hatua nyingine za kisheria au kama Sivarasa ataendelea kuzuiliwa, na kwa muda gani. Awali, Mahakama ya Jinai ya Al-Ahsa ilikuwa imemhukumu kifungo cha miaka mitano gerezani pamoja na faini ya riyal milioni tatu za Saudi Arabia.
Soma pia:
Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kubwa wiki moja kabla ya uchaguzi wa Israel

Chanzo cha picha, EPA
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amethibitisha kwamba mkuu wa shirika la ujasusi la Misri alikuwa Israeli kabla ya mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 2023, lakini alisisitiza tena kwamba hakukutana na Kamil Meja Jenerali Abbas Kamel, afisa mstaafu wa kijeshi wa Misri ambaye anahudumu kama mshauri wa rais na mratibu wa vyombo vya usalama.
Netanyahu alikanusha madai kwamba hakuchukua hatua kutokana na maonyo ya Kamil kuhusu uwezekano wa mashambulizi.
Katika mahojiano ya televisheni, Netanyahu alisema hakujua ni nani aliyezungumza na Kamil, lakini kwamba kila mtu aliyehusika alikuwa akijaribu kuepuka lawama na kumlinda mtu huyo kutokana na jukumu.
Huku ikiwa imesalia wiki moja kabla ya uchaguzi wa Israel, na wiki moja baada ya maadhimisho ya shambulio la Oktoba 7, Netanyahu anakabiliwa na shinikizo linaloongezeka huku wanasiasa wakimtaka kuelezea ni vipi ujasusi ulishindwa kuzuia Hamas yaliyosababisha vifo vya Waisrael.
Unaweza pia kusoma:
Kiongozi wa genge aliyepanga mauaji ya rapa Tupac Shakur ahukumiwa kifungo cha miaka 40 jela

Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi wa zamani wa genge Duane "Keffe D" Davis alihukumiwa Jumanne kifungo cha miaka 40 jela kwa mauaji ya rapa wa Marekani Tupac Shakur miongo mitatu iliyopita.
Mwezi uliopita, jopo la majaji lilimkuta Davis na hatia ya kosa moja la mauaji kwa kutumia silaha hatari katika kifo cha rapa na muigizaji huyo aliyekuwa nyota wa wakati huo.
Shakur alifariki kwa kupigwa risasi akiwa njiani huko Las Vegas mnamo Septemba 7, 1996.
Timu ya utetezi ya Davis ilitangaza kwamba itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Hukumu ya "Keffe D" Davis, 63, ilikuwa ya kwanza katika kesi ambayo haijatatuliwa ambayo imewavutia mashabiki wa hip-hop kwa karibu miaka 30.
Waendesha mashtaka walidai kwamba ingawa Davis hakufyatua risasi mwenyewe, alikuwa kiongozi wa kundi lililofanya mauaji hayo. Alikiri katika kumbukumbu zake kwamba ndiye aliyetoa silaha iliyotumika katika uhalifu huo.
Jambo hili la mwisho lilikuwa muhimu katika kesi hiyo, kwani katika kumbukumbu zake alikiri mara kwa mara na hadharani kuwa alikuwa ndani ya gari la Cadillac jeupe ambamo risasi zilifyatuliwa.
Unaweza pia kusoma:
Mashambulizi ya Urusi yawaacha watu 600,000 bila umeme nchini Ukraine, Zelensky asema

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Wazima moto wakifanya kazi katika eneo la jengo la ghorofa lililoharibiwa na shambulio la kombora la Urusi Rais Volodymyr Zelensky amesema watu wasiopungua 600,000 kote Ukraine sasa hawana umeme baada ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi usiku kucha.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kituo muhimu cha nishati kinachosambaza joto na umeme Kyiv kimeshambuliwa katika shambulio la makombora ya balestiki ya Urusi.
Darnytska CHP-4, au CHPP-4, na jengo la makazi vilipigwa katika shambulizi ambalo rais alisema halikuja bila "onyo la mapema kutoka kwa washirika wetu".
Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amesema watu wawili wameuawa na 21 kujeruhiwa katika shambulio la kombora kwenye jengo la ghorofa Jumanne jioni. Alisema "vituo kadhaa vya nishati" mjini Kyiv vimepigwa bila kutoa maelezo zaidi.
Kyiv imeripoti mashambulizi mengi ya Urusi tangu Rais wa Marekani Donald Trump aliposema makubaliano ya kusitisha mapigano ya nishati yalifikiwa na Urusi na Ukraine siku mbili zilizopita.
Mapema Jumatano, Klitschko alisema "mashambulizi makubwa ya makombora" yalianguka kwa nguvu katika sehemu za Kyiv.
Maafisa wa Kyiv wamewahimiza wakazi kukaa katika nyumba zao baada ya kutangaza tahadhari kutokana na "tishio la makombora".
Kufuatia mashambulizi ya Jumanne, Zelensky alisema: "Ukraine iliunga mkono usitishaji mapigano ya nishati, lakini Urusi inalenga kiwanda kingine cha umeme na maisha ya watu wetu."
"Hili si jambo la haki kabisa: wanapoharibu miundombinu yetu ya nishati, na Ukraine haipokei hata maonyo ya mapema kuhusu uzinduzi wa makombora ya masafa marefu," aliongeza.
Unaweza pia kusoma:
Makombora yazuiliwa karibu na Riyadh baada ya Saudi Arabia kushambulia ghala la mafuta la Yemen

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Kampuni ya Petroli ya Yemen inayoongozwa na Wahouthi iliwahakikishia wakazi wa Sanaa kwamba ina mafuta ya kutosha Makombora na ndege zisizo na rubani vimezuiliwa Riyadh baada ya mapigano ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen kushambulia kituo cha mafuta karibu na mji mkuu unaodhibitiwa na Wahouthi, Sanaa, msemaji wake anasema.
Meja Jenerali Turki al-Maliki amesema makombora kadhaa yaliyolenga mji mkuu wa Saudi Arabia na miji mingine yalizuiliwa baada ya muungano huo kufanya shambulio kwenye kituo cha al-Sabaha cha Kampuni ya Mafuta ya Yemen Jumanne usiku.
Wahouthi walionya kwamba wangelenga uwanja wa ndege na kiwanda cha kusafisha mafuta cha Aramco katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, na makao makuu ya Aramco katika mji wa mashariki wa Dammam.
Baadaye Al-Maliki alisema makombora yanayolenga miji ikiwemo Dammam yamezuiliwa, huku vipande vya makombora vikianguka katika eneo la makazi huko Dhahran.
Jengo la utawala la Armaco huko Dhahran pia lililengwa, na kusababisha "moto mdogo", Wizara ya Nishati ya Saudi Arabia ilisema katika taarifa.
Hakuna majeruhi walioripotiwa, taarifa hiyo ilisema.
Ilikuja huku baraza la mawaziri la Saudi Arabia, linaloongozwa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman, likisema kundi hilo linaloungwa mkono na Iran "litabeba matokeo" ya mashambulizi yake ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo dhidi ya ufalme huo.
Unaweza pia kusoma:
Roboti yakamatwa na polisi wa Ujerumani baada ya kudaiwa kumpapasa msichana mdogo

Chanzo cha picha, North Rhine Westphalia Police Cologn
Polisi wa Ujerumani wameanzisha uchunguzi dhidi ya vijana wawili wanaotuhumiwa kudhibiti roboti inayodaiwa kumpapasa msichana wa miaka 16.
Polisi mjini Cologne wameikama roboti hiyo yenye rangi nyekundu na dhahabu ambayo inadaiwa kumshika makalio msichana huyo na kumsukuma kabla ya kupiga kelele na kuondoka.
Polisi wa Rhine Kaskazini Westphalia walisema mmiliki wa roboti hiyo mwenye umri wa miaka 16 na mwenzake, 19, wanaaminika kutangaza tukio hilo moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii na kutoa maoni yao kuhusu tukio hilo.
Kulingana na taarifa ya polisi kwenye Facebook, kifaa hicho chenye urefu wa sentimita 120 (futi 3.9) kilimkaribia msichana huyo kutoka nyuma alipokuwa na marafiki zake karibu na saa sita usiku kwa saa za huko siku ya Jumamosi.
Polisi walisema msichana huyo alikuwa mbele ya duka la vyakula vya haraka karibu na katikati ya jiji wakati tukio hilo lilipotokea.
Huduma za dharura ziliarifiwa, na roboti na kijana pamoja na roboti hiyo walipatikana umbali mfupi baadaye. Roboti hiyo iligunduliwa nyuma ya gari, ambapo mvulana alikuwa ameiweka, polisi walisema.
Picha iliyotolewa na polisi ilionyesha roboti hiyo ikiwa imevaa masharubu meusi, mnyororo wa rangi ya dhahabu na fulana nyeupe.
Pamoja na roboti hiyo, polisi walikamata simu mbili za mkononi za washukiwa. Wanajaribu kubaini kama kuna mtu alikuwa akidhibiti mienendo ya roboti hiyo kimakusudi wakati wa tukio hilo.
Unaweza pia kusoma:
Trump: Huenda tumezidi kuwaua viongozi wa Iran

Chanzo cha picha, Alex Wong/Getty Image
Katika hotuba yake katika mkutano wa kampeni, Donald Trump alizungumzia kuhusu "kupindukia" katika kuwalenga viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya siku arobaini.
Rais wa Marekani aliwaambia wafuasi wake katika mkutano wa kampeni huko Ohio jana usiku: "Labda tumevuka mipaka na viongozi wa Iran kwa sababu hatujui tena tunashughulika na nani."
Uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani utafanyika katika wiki ya kwanza ya Novemba.
Bw. Trump alikuwa akiwazungumzia viongozi wa zamani na maafisa wakuu katika Jamhuri ya Kiislamu ambao waliuawa katika vita kati ya Israeli na Marekani dhidi ya Iran.
Ali Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wakati huo, pamoja na makamanda kadhaa wakuu wa kijeshi, kama vile Mkuu wa majeshi na Waziri wa ulinzi, na maafisa wa kisiasa wa ngazi za juu, akiwemo Katibu wa baraza la ulinzi wa wakati huo, waliuawa siku ya kwanza ya vita mnamo Machi 29, 2018.
Bw. Trump anaamini kwamba kuuawa kwa viongozi kadhaa wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu kumezidisha ugumu wa juhudi za kuwatambua wale ambao Marekani inapaswa kujadiliana nao.
Hapo awali alisema kwamba mashambulizi ya Marekani na Israel yalisababisha "mabadiliko ya utawala" nchini Iran na alikuwa amerudia mara kadhaa kwamba Marekani inawasiliana na "viongozi wapya wa Iran."
Saa chache mapema, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alikuwa ameiambia Reuters katika taarifa kama hizo kwamba Marekani bado haina uhakika kuhusu jinsi maamuzi yalivyokuwa yakifanywa katika ngazi za uongozi wa Iran, na kulingana naye, utaratibu wa kufanya maamuzi nchini Iran haukuwa wazi kwa Marekani.
Unaweza pia kusoma:
Papa agunduliwa na saratani ya mapafu lakini upasuaji umefanikiwa, Vatican yasema

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Papa Leo alifika katika Hospitali ya Gemelli ya Roma kabla ya upasuaji wake Jumanne Papa Leo XIV amegunduliwa kuwa na saratani ya mapafu lakini alifanyiwa upasuaji uliofanikiwa kuondoa sehemu ya chini ya pafu lake la kulia, Vatican imesema katika jarida la kimatibabu.
Papa mwenye umri wa miaka 71 alifanyiwa upasuaji wa dakika 90 siku ya Jumanne katika Hospitali ya Gemelli ya Rome na baadaye akagundulika kuwa na ugonjwa wa mapafu unaoitwa adenocarcinoma.
"Operesheni ilifanikiwa na hakukuwa na matatizo yoyote," Vatican ilisema. "Baada ya upasuaji, Papa aliamka kawaida na akarudi chumbani mwake baada ya kipindi kifupi cha uchunguzi chumbani," iliongeza.
Uvimbe huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza wakati wa kile ambacho Vatican imekielezea kama "uchunguzi wa kawaida". Papa anatarajiwa kubaki hospitalini kwa takriban wiki moja.
Hapo awali, umati mkubwa wa watu ulisubiri kwa saa nyingi nje ya hospitali kwa ajili ya Papa.
Walishangilia kwa salamu na matakwa kheri alipopita, huku akipunga mkono na kutabasamu kupitia dirisha la nyuma la gari lake.
Kisha akakutana na wafanyakazi wa hospitali kwenye ngazi za hospitali. "pole," mmoja wao alisikitika, ambapo Papa alitabasamu na kuinua mabega. "Tuko hapa kwa ajili yako," alimhakikishia.
Katika taarifa yake, Vatican ilisema sehemu yote ya chini ya pafu la kulia la Papa iliondolewa "ili kuhakikisha matibabu yanafanyika ipasavyo".
Chanzo cha habari cha Vatican kiliambia shirika la habari la Agence France-Presse kwamba vipimo zaidi vinafanyika ili kuona kama kulikuwa na ishara yoyote kwamba saratani ilikuwa imeenea.
Ni Papa Leo XIV mwenyewe ambaye Jumapili alitangaza habari za operesheni yake kwa ulimwengu, akizungumza kutoka kwenye roshani katika Uwanja wa St Peter baada ya kutoa baraka ya kawaida.
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ya leo Jumatano tarehe 14.10.2026, shukran kwa kuwa nasi.



















