Kitendawili cha mgonjwa wa Ebola aliyesafiri kupitia nchi tatu bila kugunduliwa

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Wycliffe Muia
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Mfanyabiashara mmoja kutoka Kenya alisafiri kupitia baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kabla ya kuvuka mipaka ya nchi nyingine mbili bila kugunduliwa kuwa na maamzukizi ya ugonjwa huo.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 40 aligundulika kuwa na Ebola baada ya kulazwa katika hospitali moja jijini Nairobi, na hivyo kuwa mgonjwa wa kwanza kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo nchini Kenya. Alifariki dunia siku mbili baadaye, Oktoba 5.
Kushindwa kubainika kwa maambukizi yake licha ya kupita katika vituo kadhaa vya afya nchini DRC na kufanyiwa ukaguzi wa afya katika viwanja vya ndege vya Uganda na Kenya kumezua maswali kuhusu uimara wa mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa katika ukanda huo wakati wa mlipuko mkubwa wa Ebola.
Mlipuko wa mwaka huu nchini Congo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,000, na kutajwa kuwa miongoni mwa mlipuko mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya ugonjwa huo.
Sasa, Shirika la Afrika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) limefuatilia kwa kina safari na mienendo ya mgonjwa huyo kwa kipindi cha karibu wiki sita, na kubaini mapungufu kadhaa yaliyosababisha maambukizi yake kutogunduliwa mapema.
Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kuwa kulikuwa na fursa nyingi za kubaini ugonjwa wake katika hatua za mwanzo, hatua ambayo ingeweza kusaidia kuzuia watu wengine wengi kugusana na virusi vya Ebola kabla ya kisa hicho kuthibitishwa rasmi.
DR Congo
Simulizi hiyo, iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Dharura wa Africa CDC, Dkt. Wessam Mankoula, inatoa picha ya kina ya safari ya mfanyabiashara huyo, ambaye alisafiri maelfu ya kilomita huku hali yake ya afya ikiendelea kuzorota.
Mwanaume huyo, ambaye jina lake halijawekwa wazi, alikuwa akiishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa miaka saba na alikuwa akisafiri mara kwa mara katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo kwa shughuli zake za kibiashara.
Ingawa bado haijabainika ni lini au wapi hasa aliambukizwa Ebola, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema ugonjwa huo ulikuwa ukiripotiwa katika majimbo yote matatu aliyoyatembelea mwanzoni mwa Oktoba.
Uchunguzi unaonyesha kuwa mwishoni mwa Agosti na mwanzoni mwa Septemba, alikaa kwa muda mrefu katika jimbo la Bas-Uélé, akizuru miji ya Buta, Aketi na Likati, baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakikabiliwa na maambukizi ya Ebola wakati huo.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilithibitisha mlipuko wa Ebola katika mji wa Buta mwezi Agosti, kabla ya mfanyabiashara huyo kuwasili eneo hilo, ingawa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa aliambukizwa virusi hivyo katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Africa CDC, dalili za ugonjwa zilianza kujitokeza mnamo Septemba 15. Alitafuta matibabu na kupewa dawa za antibiotiki kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Hata hivyo, siku mbili baadaye hali yake ilizidi kudhoofika akalazwa katika Kituo cha Afya cha Tongo Etandi kilichopo Bondo, hadi Septemba 19.
Licha ya kuwa na homa na vipele mwilini, wahudumu wa afya walibaini kuwa alikuwa na maambukizi ya ngozi, badala ya Ebola.
Kwa kuwa hakufanyiwa kipimo cha Ebola katika hatua yoyote ya safari yake, ni vigumu kubaini ni lini hasa alipata maambukizi hayo. Japo dalili alizokuwa nazo zinafanana na zile za awali za Ebola, zinaweza pia kuhusishwa na magonjwa mengine yanayopatikana kwa wingi katika eneo hilo, ikiwemo malaria.
Mnamo Septemba 20, alisafiri kwa ndege hadi Kisangani, mji wenye wakazi milioni 1.5 ulioko kando ya Mto Kongo. Alisalia huko kwa zaidi ya siku 10 huku akiendelea kutafuta matibabu.
Haijafahamika ni hospitali au vituo gani vya afya alivyotembelea mjini Kisangani, wala aina ya matibabu aliyopewa. Kisangani ni makao makuu ya mkoa wa Tshopo, ambao kufikia sasa umeripotiwa kuwa na wagonjwa 51 pekee wa Ebola.
Uganda
Hata hivyo, Oktoba 1, zaidi ya wiki mbili tangu aanze kuugua, mfanyabiashara huyo alipanda ndege nyingine ya ndani kuelekea Beni kabla ya kuendelea na safari yake hadi Kasindi, mji wa mpakani unaohudumia shughuli kubwa za biashara kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.
Miji ya Beni na Kasindi iko katika jimbo la Kivu Kaskazini, ambalo limekuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mlipuko wa Ebola nchini DRC, baada ya kurekodi maelfu ya maambukizi na zaidi ya vifo 1,000 vinavyohusishwa na ugonjwa huo.
Hata hivyo, hakukaa kwa muda mrefu katika eneo hilo. Baadaye siku hiyo hiyo alivuka mpaka na kuingia Uganda.
Uganda iliimarisha udhibiti wa mipaka yake na Congo muda mfupi baada ya mlipuko wa Ebola kuanza mwezi Mei. Nchi hiyo imekuwa na uzoefu wa kukabiliana na milipuko kadhaa ya ugonjwa huo, ikitegemea mifumo ya ufuatiliaji wa wagonjwa, utafutaji wa waliokutana nao na utengaji wa visa vinavyoshukiwa.
Ingawa Uganda iliripoti visa kadhaa vya Ebola mapema mwaka huu, hasa miongoni mwa wasafiri waliowasili kutoka DRC, ilitangazwa kuwa haina maambukizi ya ugonjwa huo mwezi Agosti.
Hata hivyo, mpaka kati ya nchi hizo mbili ni mpana ulio na miundombinu duni, jambo linalowapa changamoto maafisa wa afya na usalama kufuatilia harakati za wasafiri na kudhibiti kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza.
Mpaka sasa, bado haijabainika kama mfanyabiashara huyo alipitia kituo rasmi cha ukaguzi wa afya alipovuka mpaka wa Congo na kuingia Uganda.

Chanzo cha picha, EPA
Baada ya hapo, alisafiri kwa barabara hadi Kampala kabla ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, ambako alipanda ndege kwenda Nairobi mnamo Oktoba 3.
Maafisa wa Uganda walisema uchunguzi wa afya uliofanyika uwanjani hapo haukubaini dalili zozote za hatari, huku joto la mwili wake likionekana kuwa katika kiwango cha kawaida.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema kisa hicho kimeibua maswali kuhusu ufanisi wa kutegemea vipimo vya joto pekee na taarifa za kiafya zinazotolewa na wasafiri katika kubaini wagonjwa wa magonjwa hatari ya kuambukiza.
Kwa mujibu wa Dkt. Wessam Mankoula, wachunguzi bado wanachunguza iwapo dawa alizokuwa akitumia zilichangia kupunguza joto la mwili wake na hivyo kuficha dalili za ugonjwa huo wakati wa ukaguzi.
Aliongeza kuwa pia kuna uwezekano kwamba wakati alipopitia vituo vya ukaguzi hakuwa na homa, jambo ambalo lingeifanya kuwa vigumu kwa maafisa wa afya kubaini maambukizi yake.
Kenya
Pia hakutambuliwa kama mgonjwa anayeshukiwa kuwa na virusi vya Ebola alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi. Kutoka uwanjani, alipelekwa moja kwa moja hospitalini baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa huo, zikiwemo homa, maumivu ya mwili, maumivu ya koo na kutokwa damu.
Vipimo vya maabara vilivyofanyika baadaye vilithibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa virusi vya Ebola vya aina ya Bundibugyo, aina iliyokuwa ikisababisha mlipuko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Baada ya utambuzi huo, alitengwa kwa uangalizi maalumu wa matibabu, lakini hali yake iliendelea kuzorota. Alifariki dunia Oktoba 5 na kuzikwa siku iliyofuata chini ya taratibu kali za kuzuia maambukizi.
Kisa hicho kimeibua maswali makubwa kuhusu jinsi mgonjwa aliyekuwa na dalili za Ebola alivyoweza kuvuka mipaka ya nchi tatu na kupitia mifumo kadhaa ya uchunguzi wa afya bila kutambuliwa.
Serikali ya Kenya imesema watu 66 waliokuwa wametangamana na mgonjwa huyo wametambuliwa na wanaendelea kufuatiliwa, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likionya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka kadri uchunguzi unavyoendelea nchini Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kisa hicho pia kimezua wasiwasi kuhusu hatua zilizochukuliwa katika matibabu yake, hasa baada ya kuibuka kwa maswali kuhusu namna alivyohudumiwa kabla ya kugundulika kuwa na Ebola.
Hata hivyo, Wizara ya Afya ya Kenya imesema imeimarisha hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa huo. Kwa mujibu wa wizara hiyo, zaidi ya wasafiri 652,000 wamefanyiwa uchunguzi wa afya, karibu wahudumu 5,000 wa afya wamepatiwa mafunzo maalumu, na vituo vitano vya matibabu vimetengwa kwa ajili ya kushughulikia visa vya Ebola.
Ebola huambukizwa kupitia mgusano wa moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa na ambaye tayari ameanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo, au kupitia vifaa vilivyochafuliwa na virusi hivyo.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ugonjwa huo unaweza kuchukua kati ya siku mbili na 21 kabla ya dalili kujitokeza, jambo linalofanya ufuatiliaji wa waliokutana na mgonjwa kuwa muhimu katika kuzuia maambukizi zaidi.
CDC advice
Mankoula amewataka wasafiri wanaohisi kuwa na dalili za Ebola kuripoti hali zao mapema na kutafuta matibabu, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kuokoa maisha na kusaidia kudhibiti maambukizi.
"Kuripoti dalili mapema kunasaidia kujilinda na kuzuia ugonjwa kusambaa kwa wengine," alisema.
Wakati huo huo, WHO imeonya kuwa unyanyapaa na taarifa potofu kuhusu Ebola huwafanya baadhi ya watu kuficha dalili au kuchelewa kutafuta matibabu, hali inayochangia kuenea kwa ugonjwa huo. Shirika hilo limesema linaongeza juhudi za kuelimisha jamii, hasa nchini DRC ambako baadhi ya wahudumu wa afya wamewahi kushambuliwa na watu wanaopinga uwepo wa Ebola.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi
































