FIFA yakosoa kampeni ya kutaka Infantino ajiuzulu

Chanzo cha picha, Getty Images
FIFA imekosoa vikali kile ilichokiita juhudi zinazoendelea za kuidhoofisha taasisi hiyo pamoja na rais wake, Gianni Infantino. Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti zilizomuhusisha Infantino na madai kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi, ambayo FIFA imesema ni madai yasiyo na msingi na ya uongo.
Infantino pia anakabiliwa na shinikizo kutoka UEFA na baadhi ya vyama vya soka barani Ulaya kufuatia mpango wake uliositishwa wa FIFA Forward Enterprise, uliolenga kuanzisha kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na tiketi za FIFA, huku sehemu ya kampuni hiyo ikiuzwa kwa mwekezaji binafsi.
Rais wa Shirikisho la Soka la Norway, Lise Klaveness, ametaka Infantino ajiuzulu, huku UEFA ikisema bado iko tayari kususia baadhi ya matukio ya FIFA ikiwa haitapewa uhakikisho kwamba mpango huo hautafufuliwa.
FIFA imemtetea Infantino ikisema alichaguliwa kidemokrasia na vyama wanachama na anaendelea kuhudumu kwa mamlaka waliompa. Shirikisho hilo limeonya kwamba wanaopinga uongozi wake wanapaswa kutumia taratibu rasmi za kidemokrasia za FIFA badala ya madai au taarifa potofu.
Upinzani dhidi ya Infantino unatoka zaidi Ulaya, huku Mexico, Conmebol na CAF zikimuunga mkono. CAF, inayowakilisha nchi 54 za Afrika, imesema inaunga mkono Infantino kwa kauli moja.






















