Wananchi washambulia timu ya mazishi DRC, hofu ya Ebola kuenea yaongezeka

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zimeeleza wasiwasi mkubwa baada ya wakazi wa eneo la Katana katika jimbo la Kivu Kusini kushambulia timu maalum ya mazishi ya waathirika wa Ebola.
Tukio hilo lilitokea Jumatatu na kulazimisha wahudumu wa afya kuacha jeneza walilokuwa wakilisafirisha kutokana vurugu hizo.
Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya afya, mwili wa marehemu uliendelea kushughulikiwa na wananchi wa kawaida baada ya timu hiyo kuondoka. Hatua hiyo inatajwa kuwa hatari kubwa kwa sababu miili ya waathirika wa Ebola inaweza kuendelea kusambaza maambukizi ikiwa haitashughulikiwa kwa kufuata taratibu maalum za afya.
Tukio hilo limeongeza changamoto katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa aina ya Bundibugyo ya Ebola, huku kukiwa na taarifa za mashambulizi mengine dhidi ya wahudumu wa afya na timu za mazishi katika maeneo tofauti. Katika mji wa Bunia, jimbo la Ituri, watu kadhaa walijeruhiwa baada ya wakazi kushambulia timu ya wahudumu wa afya kwenye makaburi.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ukosefu wa imani kutoka kwa baadhi ya wananchi na upinzani dhidi ya hatua za kudhibiti ugonjwa huo vinaendelea kuathiri mapambano dhidi ya Ebola. Baadhi ya familia zimekuwa zikipinga taarifa rasmi za sababu za vifo vya ndugu zao, jambo linalochochea migogoro na wahudumu wa afya.
Tangu mlipuko huu wa 17 wa Ebola nchini DRC kutangazwa Mei 15, jumla ya wagonjwa 363 wamethibitishwa kuambukizwa huku watu 62 wakifariki dunia. Maambukizi yameendelea kuongezeka katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, hali inayoongeza hofu ya kuenea zaidi kwa ugonjwa huo ikiwa hatua za kudhibiti maambukizi hazitaheshimiwa kikamilifu.



